Makala
Tunaweza kuwa kama Nyerere, angalau tunaweza kujaribu
Jenerali Ulimwengu
Toleo la 209
26 Oct 2011

BAADA ya kujadili (katika makala ya wiki jana) ni kwa nini Mwalimu Nyerere anawatia hofu watawala wetu kiasi kwamba wamebaki wanamung’unya maneno pasipo na uwezo wa kutamka wazi kile wanachokiamini juu ya Mzee huyu, napenda kusema ni faida gani tungepata iwapo tungejisemea ukweli tunaouhisi katika nafsi zetu.

Nasema ni muhimu kuusema ukweli uliomo ndani yetu ili tuelewe ni nini tunataka, nini hatutaki, na ni njia gani itatusaidia kupata tunachotaka na kutuepusha na tusichokitaka.

Haiwezekani kupiga hatua kwenda kokote kama tutaendelea hivi hivi bila watu kuambizana kwa uwazi misimamo yao na kuichakata ili kupata muafaka kutokana na kupambanisha hoja.

Tumejifunza kutoka kwa mwanafalsa Goerg W. F. Hegel kwamba mchakato wa maendeleo huanza na wazo-awali (thesis) ambalo huzua wazo-kinzani (antithesis) na haya mawili yanapokutana na kupambana ndipo huzaliwa wazo-daraja(Synthesis) ambalo linakuwa limetokana na mkinzano baina ya wazo-awali na wazo-kinzani. (Naomba radhi kwa tafsiri yangu isiyo rasmi; nia ni kubainisha mchakato wa utungaji wa wazo. Nalitumia neno ‘daraja’ kwa maana ya nyenzo inayotuvusha kwenda ng’ambo ya juu).

Na hili wazo-daraja nalo huanza safari yake kwa kuwa wazo-awali katika ngazi nyingine, ya juu, tayari kupokea wazo-kinzani jipya, na kwa mara nyingine tena mawazo haya husuguana na kukinzana na kuendelea kuzaa mawazo mapya. Kwa jinsi hii dunia inasonga mbele, na kila mara mzunguko wa mikinzano hii unapofikia mwisho, mzunguko mwingine huanza, kila mara jamii husika ikiimarika, ikipanda na kuwa bora zaidi.

Baadhi ya mikinzano hiyo inaweza ikazaa zahma, mitafaruku na hata vita. Mbegu ya wazo iliyopandikizwa katika michakato ya ‘kidialektiki’ huwa mithili ya mimba changa inayotunga ndani ya tumbo la uzazi na kukua taratibu hadi inapopevuka, ikawa inadai kuzaliwa. Kama zitafanyika jitihada za kuizuia isizaliwe, mimba hiyo inaweza kuwa na madhara makubwa kwa aliyeibeba. Hivyo, uamuzi hufanywa wa kumzalisha kwa kumpasua.

Historia inatupa mifano mingi ya mimba zilizotunga ndani ya jamii, mataifa na himaya, halafu zikakumbwa na ugumu wa kuzaliwa, na mwisho wake mazingira ya uzazi wake yakawa na madhara makubwa yaliyosababisha machungu ya muda mrefu baadaye. Mifumo mikongwe inapong’ang’ania mawazo mgando yaliyopitwa na wakati, na ikalazimisha, kwa nguvu za dola na hila mbalimbali, kuzuia kuzaliwa kwa mtoto, hatima yake ni zahma.

Tunaweza kuchukua mifano miwili au mitatu ya karne za hivi karibuni, mifano ambayo inabainisha mimba zilizokabiliana na ugumu wa upevu wa mimba usiopata mwanya wa kutokea. Wakati Waingereza wakiitikia mwito wa Oliver Cromwell aliyekuwa akiongoza majeshi ya Bunge la Uingereza dhidi ya mfalme Charles l (1642) ilikuwa tayari ni karne nne tangu kusainiwa kwa Magna Carta (1215) baina ya mfalme Yohana wa Uingereza na mabwenyenye wa himaya yake waliomtaka awatambue kama wabia wake na si wapagazi wake, na hivyo awakasimie madaraka ya kutawala maeneo yao.

Madai ya msingi ya mabwanyenye hawa yalikuwa kwamba mfalme atambue kwamba bila wao yeye hana nguvu yoyote, na kama asiporidhia matakwa ya mabwanyenye hao, wao wasingeendelea kutekeleza majukumu ambayo ni muhimu kwa utawala wa mfalme huyo, kama vile kukusanya kodi kutoka kwa watwana waliokuwa katika vihimaya vyao, na pia kuwakusanya watwana hao na kuwaongoza vitani kama wapiganaji bei-nafuu (chakula cha mizinga) wa mfalme kila mara anapokabiliwa na vita dhidi ya mfalme wa Ufaransa.

Mfalme Yohana asingeweza kujua wakati ule, lakini mimba ilikwisha kuanza kumea ndani ya tumbo la uzazi la utawala wa Uingereza na ilibidi aliyeibeba ajiandae kujifungua. Lakini hili halikuwa kwa muda wa karne nne, kipindi ambamo masharti aliyokuwa ameyakubali mfalme Yohana shingo upande yalipuuzwa kidogo kidogo mpaka makubaliano ya 1215 yakawa hayana nguvu tena. Aliyekuja kubeba uzito wote wa kihistoria alikuwa ni mfalme Charles ambaye alilazimika kupambana na majeshi ya Bunge, na mwisho aliposhindwa vitani, akakamatwa, akashitakiwa, akakutwa na hatia, akakatwa kichwa, na Uingereza ikawa jamhuri kwa muda.

Laiti kama wafalme na malikia wa Uingereza wangejua kwamba Magna Carta ilikuwa ni mwanzo wa mimba kutunga na kwamba mwisho wa siku mimba hiyo ilibidi izaliwe, labda yasingetokea hayo yaliyompata mfalme Charles.

Wafaransa walikuwa na historia kama hiyo ya binamu zao wa Uingereza, watawala wao, wafalme na mabwanyenye wa himaya yao wakidharau mbegu ya ubepari iliyokuwa imeanza kumea ndani ya mifumo ya utawala. Hatimaye ni mfalme Louis XVI na malikia wake, Marie-Antoinette kukatwa vichwa huku maelfu ya raia Wafaransa wakishangilia kama walioko kwenye onyesho(1789).

Urusi nayo ilipatwa na mkasa kama huo (1917) Mfalme wa mwisho wa nchi hiyo, Nicholas ll, alipouawa na familia yake yote kufyekwa kwa sababu mfalme alikuwa ameziba masikio na kufumba macho, akawa hawezi tena kusikia wala kuona mambo ambayo kwa watu wengine wengi yalikuwa bayana, hususan kuendelea kupanda kwa ghadhabu za wafanyakazi na matabaka mengine yaliyokuwa yameelemewa na ugumu wa maisha, vita na kunyonywa na matajiri wao. Nicholas naye alishindwa kusoma ishara za nyakati na kuyasikia mapigo ya moyo ya kiumbe kilichomo tumboni kikitafuta upenyo wa kutokea.

Sababu mojawapo inayowafanya watawala wetu, hasa barani Afrika na nchini humu, wasisikie mapigo ya mimba na kichanga kinachotaka kiachiliwe kitoke ni kutosemezana, kutojadili masuala muhimu, kujidai hakuna lolote la kutia wasiwasi, kusema kila kitu ni shwari wakati hata eneo moja si shwari, kudanganyana waziwazi wakati wote wakijua wanadanganyana, kupigana makofi mazito mgongoni (Komred) huku waking’ong’ana nyuso zikiwa hazitazamani. Ni unafiki unaowamaliza.

Katika makala yangu ya wiki jana nilisema kwamba watawala wetu na viongozi wa siasa, kama hawa nao wapo, wanapata hofu kumjadili Mwalimu na kujadili maisha yake, misimamo yake, maandiko yake na matamko yake na kuangalia ni yapi mema na tuyaige, na tubaini ni yapi tunadhani hayakuwa sahihi (au hata kama yalikuwa sahihi wakati ule, siyo sahihi hii leo) ili tuyaepuke au tuyafanyie marekebisho yapasayo ili tuweze kuyatumia katika mazingira mapya.

Lakini inavyoelekea hakuna aliye tayari kuyazungumzia haya kwa dhati kutokana na sababu nilizozieleza katika makala hiyo. Wote wanapiga blah blah bila kusema lolote linaloweza kutusaidia kwenda mbele. Ama ni sifa za moja kwa moja zinazomfanya Mzee wetu aonekane kama malaika (wakati hakuwa malaika), au ni ukimya unaozaa pengo linalozibwa kwa maneno mengi yasiyokuwa na uzito wa kimaudhui.

Baadhi ya maneno hayo ni yale yanaosema kwamba haiwezekani kumpata kiongozi mwingine kama Mwalimu. Ebo! Kwani yeye alitokana na majini? Nini kinatufanya tuamini kwamba hatuwezi kumpata Nyerere mwingine, wakati tunajua kwamba alizaliwa na mwanamke kama watu wengine, alikulia kijijini kama wanavyokuwa Watanzania wengi bado, aliishi na kufanya kazi miongoni mwetu, na tulimwona, na tunajua hakuwa na pembe wala mkia? Na hususan, wakati huu tunapohitaji watu kama yeye?

Tunatakiwa tuseme kwamba tutakuwa kama yeye, angalau tutajitahidi kuwa kama yeye, kila mmoja kwa namna yake. Kwanza, tujifunze kujenga hoja juu ya kile tunachokitaka au tusichokitaka. Ujengaji hoja hukuzwa kwa kuwa na taarifa na kisha kuzifanyia kazi kwa kutumia ubongo. Mwalimu alilifanya hili kwa umahiri mkubwa kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa, na utashi pia, wa kusaka maarifa na kuyachakata kichwani mwake. Nasi tunaweza angalau kujaribu.

Tutakuwa tofauti kwani hatuwezi kuwa sote tu sawa, na wala si vyema kuwa hivyo. Kwa mfano ni wachache wanaweza kujisomea kama alivyojisomea Mwalimu, kupenda vitabu, majarida na machapisho mengine. Lakini tunaweza kujaribu, tukasoma angalau kidogo, hususan sasa ambapo tovuti inaturahisishia mambo. Kwa hiyo kwa watu wa kiwango fulani cha maisha hatuna sababu ya kusema kwamba hatuwezi kupata taarifa.

Lakini muhimu zaidi ni kuzitumia taarifa tunazozipata kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wetu kwa kuwawezesha kupambana na maadui watatu wa jadi: umasikini, maradhi na ujinga. Na kazi hii hatuwezi kuifanya iwapo hatusemezani, kila mtu amekaa na lake moyoni, ni wachache wanathubutu kusema wanachokiamini, na wengi tunasubiri mkumbo ujitokeze ndipo tuufuate.

Wale manyani watatu katika ile sanamu wanaweza kuwa kielelezo mwafaka. Kila mmoja katumia viganja vya mikono kujizuia kuwasiliana na yeyote.Mmoja kafumba macho, mwingine kaziba masikio na wa tatu kafunga mdomo.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Jenerali Ulimwengu
ulimwengu@jenerali.com
www.jenerali.com

Jenerali  Ulimwengu ni Mwanajopo la Wataalam la Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Maoni ya Wasomaji

Tatizo si uwezo wa kuthubutu kumkosoa nyerere, tatizo ni ukiukwaji wa miiko ya maadili. Huyu Mzee wetu alisema kwa uzoefu wake Ikulu si mahali pa kukimbilia, mathalinhakusemea urai tu bali uongozi wote kwa ujumla, pamoja na hayo watu wanatumia pesa nyingi kupata uongozi, mambo yanapokwenda vibaya hakuna aliye tayari kujiuzuru ili kutoa nafasi kwa wenye mawazo mapya waweze kuingia pale aliposhindwa. Tunapokosa uzalendo huu tukataka kung'gang'ania hata pale tunaposhindwa kutimiza wajibu wetu ni dhahili kuwa katu hatuwezi kumkosoa au kumuunga mkono mwalimu. tukimkosoa tutaulizwa mbona hatuna njia mbadala, na tukumuunga mkono tutaulizwa mbona hatufuati maadlili ya uongozi?
 
kwa hiyo nyerere anabaki kuwa kipimo ambacho wapenda madaraka hawapendi kukitumia hata kidogo

Toa maoni yako