Tundu Lissu achaguliwa kwa kishindo TLS

MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Tundu Lissu, amechaguliwa na wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuwa rais wao kwa takriban asilimia 88 ya kura.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki ameshinda kinyang'anyiro hicho katika staili ya aina yake, ikizingatiwa kwamba uchaguzi huo umekuwa kivituo kwa wengi baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa onyo kwa wanachama hao wa TLS kujihadhari na wagombea wenye mrengo dhahiri wa kisiasa.

Mbali na Rais Dk. Magufuli, hata Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Harisson Mwakyembe naye alipata kutoa kauli kuhusu kuonya wanachama hao kuhusu uchaguzi wao kuingiliwa na wanasiasa. Katika kauli yake, Dk. Mwakyembe alifikia hatua ya kutishia kikufuta chama hicho endapo kingeendelea kukumbatia baadhi ya wagombea wanasiasa.

Hata hivyo, kwa sasa ushindi wa Tundu Lissu ni pigo kwa Rais Magufuli pamoja na waziri wake Dk. Mwakyembe, ni dhahiri sasa mawakili wameamua kwenda kinyume na mitazamo au ushawishi wa viongozi hao ambao ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa viongozi wapya wa TLS leo hii, Tundu Lissu alishinda kwa kupata kura 1411, kati ya 1682 zilizopigwa. Katika uchaguzi huo pia Godwin Ngwilimi ameshinda nafasi ya makamu wa rais TLS. Ngwilizi amewahi kuwa mmoja wa wanasheria katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

 

One thought on “Tundu Lissu achaguliwa kwa kishindo TLS”

 1. kaite Kaitike says:

  Hizi kofia nyingi hazina "conflicts of interests'?

  Moja, mbunge, Mhimili wa kutunga sheria.

  Mbili, wakili mtetezi: Mhimili wa Mahakama?

  Tatu, Rais wa Chama cha Wanasheria, ambacho ni technical kwa kutoa ushauri bila upendeleo ikiwa ni pamoja na maslahi ya wanasheria.

   

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *