HII ndio makala yangu ya mwisho ninayoiandika kwa mwaka huu wa 2011, na hivyo niianze kwa kuwatakieni nyote heri ya mwaka mpya wa 2012.
Nina hakika kila Mtanzania, hivi sasa, atakuwa anafanya tafakuri ya kina na kuutathmini mwaka wa 2011 ulivyokuwa kwake kabla ya kujiandaa kupambana tena kwa mwaka mpya ujao wa 2012.
Hata mimi ninapoandika tafakuri hii ya mwisho kwa mwaka 2011, najikuta nikijiuliza iwapo haya niliyokuwa nikiyaandika kwa miezi 12 yote ya mwaka huu tunaouaga, yamesababisha mtazamo wowote mpya wa kifikra kwa yeyote au ndio zile Waingereza wanazoweza kuziita ‘inconsequential writtings’ (tafakuri jadidi zisizo na maana).
Vyovyote vile; hii inanikumbusha sms ya msomaji wangu mmoja aliyonitumia wiki iliyopita. Msomaji huyo alinipongeza kwa makala zangu mbili zilizopita kuhusu Rwanda – makala zilizowashauri watawala wetu kuiga mambo mazuri mawili au matatu hivi kutoka kwa Rais Kagame.
Lakini baada ya kunipongeza, msomaji huyo alisema kwamba napoteza bure muda wangu kutoa ushauri wowote kwa watawala wetu; kwani si tu kwamba hawaambiliki, lakini pia hawana muda kusoma magazeti na kujua hisia za wananchi wanaowaongoza kama si kuwatawala.
Baada ya kuisoma sms hiyo, nilitafakari kama kweli napoteza muda wangu kuandika safu hii. Nilijiuliza kama kuna sababu yoyote ya kuendelea kuandika safu hii kwa mwaka mpya wa 2012.
Jibu nililolipata ni kwamba sababu ipo ya kuendelea kuandika; nayo ni kwamba katika nchi ambayo hakuna mjadala wa kitaifa (national dialogue) makala moja moja za wanasafu kama hii, zinasaidia kuziba ombwe lililopo hata kama utaziita ‘inconsequential writtings’.
Ni lazima niandike, na ni lazima tuendelee kuandika ili kuchochea mijadala yenye kina na fikra mpya kuhusu masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa nchi yetu. Kama hatuna muafaka wa kitaifa kuhusu masuala hayo; angalau basi tujadiliane wenyewe kwa wenyewe na kuulizana ni wapi watawala wetu wanatupeleka!
Lakini kuna sababu nyingine muhimu inayonichochea kuendelea kuandika hata kama watawala wetu hawajali haya tunayoyaandika. Naandika ili kuweka rekodi kwa ajili ya vizazi vijavyo ambavyo nina hakika vitakuja kutulaumu kwa jinsi tulivyorithishwa nchi nzuri lakini tukaiharibu na kuwaachia nchi ‘tasa’.
Kwa mfano; watakapokuja kuona kulikokuwa na hazina ya madini sasa kumebaki mashimo matupu na maendeleo yoyote makubwa hawayaoni, si tu watatushangaa, lakini watatukana kwamba sisi si babu zao. Watasema hawawezi kuwa na mababu waliokuwa wajinga kiasi hicho.
Kwa hiyo; tunaandika hivi sasa ili wajukuu wetu watakapokuja kufanya tafiti zao miaka ijayo, wafahamu kwamba si Watanzania wote walioafiki (zama hizo) kutoa migodi yetu yote kwa wawekezaji wa kigeni ambao wamechuma na kujiondokea zao wakituachia mashimo.
Kule Mererani mkataba wa Tanzanite One unatarajiwa kumalizika Februari mwakani, na sasa wawekezaji hao wa kigeni wapo katika pilikapilika za kusombasomba tanzanite za mwisho mwisho kabla hawajaondoka na kutuachia mashimo.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi wananchi wa Mererani kwamba mkataba huo wa mwekezaji utakapomalizika, vitalu hivyo vitagawiwa kwa wachimbaji wadogo.
Sina hakika kama hilo litatekelezwa; lakini hata kama litatekelezwa, nina hakika wachimbaji hao wadogo watakuta tanzanite zote zilishasombwa na wawekezaji hao wa kigeni, na wao ‘wamerithi’ mashimo tu!
Ndiyo maana ninasema kwamba ni lazima kumbukumbu ziwekwe kwamba wapo Watanzania walioandika na kupinga kutwaliwa kwa migodi yetu na wawekezaji wa kigeni lakini hawakusikilizwa na waliokuwa watawala wao. Hili ndilo linalonitia moyo kuendelea kuandika.
Nikirejea kwenye suala la kuukaribisha mwaka mpya wa 2012, napenda kuwasisitizia wasomaji wangu kwamba utakuwa mwaka wa machungu kiuchumi, na hivyo ni vyema wakajiandaa kufunga mikanda. Picha ya uchumi wa dunia kwa mwaka 2012 na hasa wa Ulaya si nzuri. Huo ndio ukweli.
Sina hakika Rais Kikwete atawaambia nini Watanzania katika salamu zake za mwaka mpya; lakini labda nimkumbushe tu kile ambacho Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Christine Lagarde, alichokisema, wiki iliyopita, alipotembelea Afrika kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo.
Christine Legarde aliwataka viongozi wa Afrika kuanza kuchukua tahadhari, kwa sababu ya kusambaratika kwa uchumi wa Ulaya kulikosababishwa na kutetereka kwa sarafu ya Euro. Alisema kuwa hali itakuwa mbaya kwa mwaka 2012, na hivyo ni vyema wakuu wa nchi za Afrika wakaanza kuchukua hatua za kujihami.
Sina hakika kama watawala wetu waliichukulia kwa uzito kauli hiyo ya bosi huyo wa IMF lakini sitashangaa kwao ikawa business as usual. Vyovyote vile; nawasihi wasomaji wangu waanze kuchukua hatua za kujihami – waanze kubana matumizi.
Nasema hivyo, kwa sababu, hata kabla athari za kusambaratika huko kwa uchumi wa Ulaya hazijatufikia, tayari mambo yameshaanza kuwa magumu kwetu. Kilo ya nyama sasa ni Sh. 7,000, sukari 4,000, ada zimepanda karibu shule zote, lita ya petroli kuna sehemu hapa nchini imeanza kuuzwa kwa Sh. 4,000.
Mfumuko wa bei sasa ni asilimia 20 na yawezekana kabisa ukafikia asilimia 30, Juni mwakani. Wakati huo huo nakisi katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012 imeshaanza kuwasumbua watawala wetu kiasi kwamba sasa hata kuwalipa tu mishahara watumishi wake ni shughuli kubwa!
Pamoja na hali hii ambayo kila mmojawetu anaiona na imeshaanza kutuathiri, bado kwenye salamu zake za mwaka mpya Bwana Mkubwa (Rais) anaweza kusema kwamba hatutatetereka kiuchumi kutokana na hali hiyo ya Ulaya.
Kama akituambia hivyo, itakuwa si mara ya kwanza kutupa matumaini feki. Alitueleza hivyo hivyo mwaka 2008 wakati wa anguko la uchumi wa dunia, lakini baadaye akalazimika kukiri mwenyewe kwamba tumeathirika.
Ndiyo maana nawatahadharisha mapema wasomaji wangu kwamba tusidanganyike; kwani mwaka 2012 utakuwa ni mwaka wa machungu kweli kweli. Ni vyema wakajiandaa kufunga mikanda. Na hizo ndizo salamu zangu za mwaka mpya.
Machungu yetu yatakuwa pengine maradufu ya machungu ya wenzetu wengine katika dunia ya tatu, kwa sababu sisi hatuna manahodha imara wa kukiongoza chombo kivuke dhoruba hii hatari.
Msomi mmoja alipata kusema kwamba tatizo la nchi zetu za Kiafrika si ukosefu wa madini au ukosefu wa gesi na mafuta au ukosefu wa ardhi au ukosefu wa rasilimali watu; bali ni ukosefu wa viongozi!
Tafakari.
Maoni ya Wasomaji
Wewe Johnson unaandika ukweli
Wewe Johnson unaandika ukweli. Mfumuko wa bei umekuwa mkubwa mno, nadhani hutujawahi kuwa na mfumuko wa asimilia 20 tangu tupate uhuru, shilingi ndiyo hiyo inazidi kudodo!! Wakati wewe unasema ukweli huo mwandishi mwingine wa malaka, Bwana Mjengwa anasema uchumi unazidi kupaa!! Hivi huo uchumi wa kupaa wa Mjengwa ni kwa watu wangapi? Watanzania wangapi wa Kijijini wataweza kununua sukari ya kilo Shilingi 4,000. Mazao yao sasa itakuwa kazi kusafirisha maana bei ya usafiri itakuwa kubwa mno kwa kuwa mafuta yanazidi kupanda Bei.
Nadhani waandishi wengine wanaandikia ushabiki na si kuandika uhalisia.
heri ya kuukaribisha mwaka
heri ya kuukaribisha mwaka mpya.
mungu akuongoze hasa pale unapoandika makala za kuinua hamasa za vijana ambao hawana muda wa kusoma magazeti au habari za kimaendeleo kwenye mitandao.
nashauri muandae makongamano, semina na ushindani hasa mashuleni na vyuoni ili kuhamasisha watu katika kusoma magazeti hasa tahariri kwani watanzania wengi tumebakia kwenye ushabiki wa mapokeo hasa kuangalia filam, michezo na mitandao ya kijamii ambapo wengi wetu hatuna elim na namna sahihi ya kutumia vitu hvyo