KWA wale ambao bado hawajafahamu tatizo lilipo, ngoja niwaambie taarifa za sasa hivi karibuni kabisa. Katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza Ngazi ya Tisa Bora iliyomalizika mkoani Morogoro hivi karibuni, timu mbili tu kati ya tisa ndizo zilizokuwa za kiraia.
Timu hizo ni Transit Camp ya Dar es Salaam na Mbeya City Council ya Mbeya. Nyingine zote zilikuwa ni timu zilizo chini ya vyombo vya dola – Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Magereza.
Timu hizo ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga, Mlale JKT ya Ruvuma, Tanzania Prisons ya Mbeya, Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.
Mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, timu tatu zimefanikiwa kupanda daraja na zitacheza Ligi Kuu ya Tanzania msimu ujao. Timu hizo ni Prisons, Polisi Morogoro na Mgambo Shooting. Zote hizo ni timu zinazomilikiwa na majeshi.
Zikiingia Ligi Kuu zitaungana na timu za Oljoro JKT, JKT Ruvu na Ruvu Shooting ambazo zipo kwenye ligi hiyo tayari. Kwa bahati mbaya, Polisi Dodoma ambayo ilikuwa kwenye ligi hiyo, imeshuka daraja tayari.
Kwenye Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu, kulikuwa na timu nne za majeshi ambazo ni Oljoro, Ruvu, JKT na Polisi. Kwa matokeo haya ya ligi daraja la kwanza, maana yake ni kwamba Ligi Kuu itakuwa na timu sita za majeshi msimu ujao. Hii maana yake ni kuwa asilimia 43 ya timu za Ligi Kuu msimu ujao zitakuwa za majeshi!
Niseme mapema kwamba mimi sina matatizo yoyote na timu hizi za majeshi. Kwanza ninazishukuru kwa sababu zimewapa ajira vijana wengi ambao kama isingekuwa fursa hizo, huenda wengine wangekuwa na maisha mabaya sana hivi sasa.
Tatizo lililopo hapa ni ukweli kwamba katika mashindano ya aina iwayo yote ile, si vizuri kushindanisha watu ambao wana maslahi yanayofanana au wenye mahusiano ya aina moja au nyingine.
Timu zote hizi za jeshi zina bosi mmoja ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Kama siku moja yatafanyika maamuzi kwamba ni lazima Tanzania iwakilishwe na timu ya jeshi, kuna uwezekano mkubwa timu hizi zikapanga njama hizo.
Na njama hizi zinaweza kupangwa na taasisi yoyote ile ambayo ingekuwa na timu nyingi kwenye ushindani wa aina yoyote ile achilia mbali mpira. Inawezekana vyombo vyetu vina uadilifu lakini ni lazima tujipange kuzuia mianya ya aina yoyote inayoweza kuleta upangaji wa matokeo.
Kwa kawaida, bingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania hupatikana kwa wastani wa pointi 56 hivi. Kama una timu sita za majeshi, maana yake ni kwamba zinaweza kuamua kugawa pointi kwa mojawapo ya timu hizo na itakuwa na uhakika wa pointi 30 hata kabla ligi haijaanza!
Hili ni jambo ambalo haliwezi likaachwa liendelee namna hii.
Nchini Hispania kwa mfano, kwenye Ligi Daraja la Kwanza la nchi hiyo timu za Real Madrid na Barcelona huchezesha timu zao B kwenye michuano hiyo. Hata hivyo, hata kama timu hizo zitafanikiwa kuongoza ligi, huwa hazipandi daraja kwa vile kuna Real na Barca ambazo ziko huko tayari.
Hii yote iliwekwa ili kuzuia aina yoyote ile ya upangaji wa matokeo. Ni lazima na hapa kwetu tulione hili katika mapana yake. Na isiishie tu kwenye timu za jeshi. Hata makampuni ya sukari nayo yakiwa na timu nyingi kwenye ligi tutapaswa kupiga kelele pia.
Hata hivyo, ni muhimu kuangalia ni kwa vipi soka halichezwi tena mitaani kwetu na mashuleni. Duniani kote, soka limeendelezwa na timu zinazotokana na wananchi wenyewe na si serikali au taasisi.
Je, ni kwa sababu tumeuza viwanja vyote vya kuchezea? Je ni kwa sababu walimu pekee wa kulea vipaji wako kwenye majeshi yetu pekee? Je, ni kwa sababu soka umekuwa mchezo aghali kiasi kwamba timu za uraiani haziwezi tena kumudu gharama zake?
Kama tutaendelea kuruhusu taasisi moja kuhodhi aina zote za michezo, tujue kwamba tunaruhusu michezo kufa kifo cha kibudu. Michezo ni kwa wote.
Ni lazima sisi kama Taifa tukae chini na kuangalia ni namna gani tutarudisha michezo kwa wananchi ili ichezwe mitaani kwetu. Hakuna haja ya kutupa lawama kwa yeyote yule. Tuangalie tulipojikwaa na kutafuta suluhisho la kudumu.
La sivyo, muda si mrefu tutaanza kwenda kutazama soka kwenye kambi za majeshi yetu… Na hili linakuja
Tunakwenda Olimpiki kufanya nini?
Toa maoni yako