SASA ni ruksa kujadili hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa miaka 48 iliyopita, Aprili 26, 1964.
Hili limewekwa wazi na Mwenyekiti wa Tume ya kuratibu Maoni juu ya Katiba mpya, Jaji Joseph Sinde Warioba hivi karibuni.
Awali na mwanzoni kabisa mwa mchakato huu, na kusema kweli tangu kuasisiwa kwake; wananchi hawakuruhusiwa kujadili Muungano. Kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na mtu kujaribu kukanyaga mahali patakatifu umevaa viatu. Wengi iliwagharimu nafasi zao za kisiasa na hata kiuchumi.
Ruksa hii imefungua mafuriko tele ya mawazo mbalimbali juu ya Muungano. Wapo wanaotaka Muungano upitiwe upya kwa kuzingatia madhumuni sahihi ya kuanzishwa kwake na kwa mazingira ya sasa; wapo pia wanaotaka muundo wa serikali tatu badala ya muundo wa serikali mbili wa sasa; na wapo pia wahafidhina wa siasa za utengano wanaotaka uvunjwe.
Yote haya ni sehemu ya demokrasia chini ya dhana ya uhuru wa mawazo. Ingekuwa enzi za demokrasia ya chama kimoja, wote hao wangeishia Keko.
Kuzuka kwa mawazo kinzani juu ya Muungano ni uthibitisho wa kutosha kwamba Muungano wetu si shwari tangu mwanzo; na kwamba ukimya wa wananchi juu yake ulibeba hofu, ghadhabu na kiu ya haki ya maoni iliyopokwa, na ambayo sasa imezaa kishindo chenye mwangwi mkubwa.
Muungano wowote wa kisiasa unaofikiwa bila ridhaa ya wananchi siku zote ni wenye mitafaruku, kero na uhasama, na hivyo hauwezi kudumu mara waasisi wake wanapoondoka madarakani; ila unaweza kuokolewa tu kwa kusikiliza hoja za wananchi na kwa kurekebisha kasoro zilizokithiri.
Tumeshuhudia na kujionea jinsi muungano wa siku nyingi, kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini ulivyogubikwa na mitafaruku, ikiwa ni pamoja na hoja tata juu ya uhalali wa Wabunge wa Bunge la Muungano kutoka Ireland ya Kaskazini kupigia kura bungeni mambo yasiyoihusu Ireland Kaskazini. Ni sawa tu na hapa kwetu juu ya uhalali wa Wabunge kutoka Zanzibar kupigia kura mambo yanayohusu Tanzania Bara au Tanganyika.
Kuna hoja pia juu ya Wazanzibari kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara; au Wazanzibari kushika nafasi za uongozi katika Serikali ya Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, wakati Watanzania Bara hawaruhusiwi kugusa mambo hayo Visiwani.
Kwa nini tunaendelea kuwa na Wazanzibari na Watanzania Bara, wakati wote hao ni Watanzania ndani ya nchi moja? Je, Zanzibar ni nchi au Taifa kiasi cha kuwa na watu wenye utaifa wa Zanzibar – Wazanzibari; au Watanzania Bara nao wana Taifa lao, Taifa la Watanzania Bara?
Nimesema, muungano unaopatikana kwa shuruti na shinikizo kwa wanachama una hatari ya kukataliwa na kuvunjika siku zote, tena kwa aibu.
Kushindwa kwa Shirikisho la Afrika ya Kati (CAF) miaka ya 1960, Muungano wa Nchi za Kiarabu (UAR) na Muungano wa Ethiopia – Eritrea ulioanzishwa mwaka 1952, ni mifano hai ya Muungano iliyokufa kwa kukosa ridhaa ya wananchi, kama ambavyo kujitenga kwa Sudan Kusini na Sudan Kaskazini kunavyothibitisha jinsi muungano unaosimamiwa kidikteta unavyoweza kuvunjika hima.
Kitendawili cha uhiari wa Muungano
Mengi yameandikwa juu ya chimbuko la Muungano wetu; lakini kwa sehemu kubwa kwa kupotoshwa. Wapotoshaji wakubwa ni wale wanaodai ulifikiwa kwa hiari, wakati ukweli ulipatikana kwa shinikizo la mataifa makubwa ya Magharibi katika jitihada za kuzima kuenea kwa Ukomunisti Afrika Mashariki, wakati huo Zanzibar kilikuwa kitovu cha kuenea kwa itikadi hiyo.
Zaidi ya hilo, hofu ya Karume ya kupinduliwa na wanaharakati wa siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx Visiwani, ilimfanya aombe msaada wa Askari 300 kutoka Tanganyika kumlinda na kuimarisha utawala wake na hivyo akawa tayari mateka wa Tanganyika kwa maamuzi yaliyofuata.
Na pale juhudi za Mwalimu Nyerere za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (likihusisha Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar) – EAF, zilipogonga mwamba (kama ambavyo juhudi za kuunda Shirikisho la Afrika ya Kati, likihusisha, Nyasaland, Rhodesia Kaskazini na Rhodesia Kusini zilivyogonga mwamba kwa sababu zile zile za EAF), aligeukia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa msaada mkubwa wa nchi za Magharibi, siku nne tu tangu kugonga mwamba; na Muungano ukazaliwa siku 100 tu baadaye, katikati ya malumbano makali kati ya Mataifa ya Magharibi na Mataifa ya nchi za Kikomunisti za Mashariki, zikiwamo Urusi, China na Ujerumani Magharibi.
Wanaobisha hili, waeleze kwa nini Zanzibar ilibatizwa jina la “Cuba ya Afrika” enzi hizo za vita baridi? Kwa nini Marekani na Uingereza ziliandaa majeshi kuivamia Zanzibar kama Muungano usingefikiwa?
Si hivyo tu; inafahamika pia kwamba pale Karume alipoonyesha kutokuwa na hiari ya haraka kuunda Muungano na Tanganyika, Nyerere alitishia kuondoa askari wake Visiwani kumwacha Karume bila ulinzi ili apinduliwe na mahasimu wake wa kisiasa Visiwani, wakiwamo viongozi wenzake wa Baraza la Mapinduzi.
Hakuna ushahidi kuonyesha kwamba Watanganyika na Wazanzibari walihusishwa kufikia Muungano wa Tanzania. Wala hakuna ushahidi kuonyesha kwamba Bunge la Zanzibar, maarufu kama Baraza la Mapinduzi, liliridhia Mkataba wa Muungano wala kutunga sheria kuhalalisha kutumika kwa mkataba huo kwenye ardhi ya Zanzibar.
Sisemi kwamba kwa mapungufu hayo ya kikatiba na kisheria, Muungano ubatilishwe; la hasha; hilo litakuwa ni jambo la kijinga kubatilisha taasisi iliyodumu kwa miaka 48 kwa mema na mabaya.
Ninachosema hapa ni kuwa Muungano ujadiliwe kwa kuendeleza na kuimarisha yale mema yote ya Muungano, na kwa kuzingatia muundo wa Muungano uliokusudiwa ili kukomesha kero zisizo za lazima.
Na katika kufanya hivyo, tuzingatie na tuishi kwa matakwa ya Mkataba wa Muungano kwa yaliyokusudiwa kwenye Mkataba huo wa Kimataifa. Tunajua, ni mambo 11 tu yaliyokusudiwa kuwa kwenye Serikali na Katiba ya Muungano; lakini hadi Katiba ya kudumu ikitungwa mwaka 1977, mambo ya Muungano yalikuwa yemefika 17, ambapo sita yaliongezwa kinyemela na kinyume cha Mkataba wa Muungano.
Mambo hayo 11 yaliyotajwa kwenye ibara ya nne ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) na kuridhiwa kwa Sheria ya Bunge Namba 22 ya 1964 (Acts of Union) chini ya kifungu cha tano cha Sheria hiyo hayabadiliki (unalterable) na hivyo kwamba marekebisho yenye kuongeza mambo ya Muungano chini ya kifungu hicho ni haramu na batili.
Vivyo hivyo, kitendo cha Bunge cha kujitanua na kujitwalia mamlaka ya kurekebisha Mambo ya Muungano kwa kuvuka uwezo wake, kinadhalilisha msingi mzima wa Muungano. Hiki ndicho kinachoitwa “ubabe” wa kisiasa unaotibua na kuchefua Muungano. Huo ndio mwanzo wa kuchezea Muungano. Hili ndilo chimbuko la hasira, kero na uhasama wa kisiasa ndani ya Muungano ambalo Mchakato wa Katiba wa sasa lazima ulijadili ili kuokoa Muungano.
Hapa nisisitize tu kwamba, Mkataba wa Muungano ndiyo Katiba ya Muungano; kwa maana ikitokea kwamba kuna mgongano kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Mkataba wa Muungano au kati ya Mkataba wa Muungano na Katiba ya Zanzibar, Mkataba wa Muungano utashinda (shall prevail) kwa turufu yake.
Maoni yangu ni kuwa wote wanaodhani kwamba kujadili Muungano ni dhambi au kwamba kutojadili Muungano ni kuusalimisha, ni wapofu wa kisiasa, kidemokrasia na kikatiba. Hao ndio wafichao ugonjwa alivyosema Mwalimu Nyerere, kwamba kilio ndicho pekee kitakachowaumbua.
Hatari ya Muungano kuvunjika
Kuna kila dalili kuonyesha kwamba Muungano uko hatarini kusambaratika kama hatutachukua hatua za haraka na za makusudi. Hatari hiyo inatokana na sababu kuu mbili: kwanza, ni kukosekana kwa nahodha au manahodha wa kuongoza Muungano kwa utamaduni (wa kidikteta) na kwa mtizamo wa madhumuni ya kuanzishwa kwake.
Kuondoka kwa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume, kama manahodha wa meli ya Muungano kwa muundo waliofikiria wao na kutumika kwa nguvu na udikteta mkubwa, kumefanya meli ya Muungano kuyumba.
Yaliyoupata Muungano wa Ethiopia – Eritrea hadi kuvunjika kufuatia kung’olewa madarakani kwa Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia, yanaweza kuukumba pia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu Zanzibar kwa Tanganyika ni sawa na ilivyokuwa Eritrea kwa Ethiopia, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Pili, kuna usiri mpya na mkubwa zaidi miongoni mwa Wazanzibari (dhidi ya) kwa Muungano unaoashiria chuki, uhasama na kuchoshwa na Muungano.
Tunachofahamu, Muungano kwa Wazanzibari umeweza kushinikizwa na kudumu kutokana tu na siasa zao za chuki miongoni mwao wenyewe (divide and rule) tangu enzi za harakati za Uhuru mwaka 1957 hadi kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) miaka miwili iliyopita.
Lakini sasa Wazanzibari wanaweza wakahoji na kujadili Muungano kwa umoja na kwa sauti moja kwa kulindwa na Katiba ya nchi yao na Bunge (Baraza la Wawakilishi) lao lisiloweza kuingiliwa na chombo chochote au taasisi yoyote ya Muungano.
Wakati huo huo, wananchi nao wanadai na kutaka kuonyeshwa Mkataba wa Muungano; wanataka kujua ni aina gani ya Muungano uliokusudiwa, na kwa nini kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa misingi na matakwa ya Muungano?
Majibu tuliyozoea kuwapa wananchi, kwamba nakala za Mkataba huo zilipotea na kuwashauri wakaulizie Umoja wa Mataifa ambao una nakala, ni ya kihayawani na yatazidi kuongeza kero za Muungano.
Tatu, misingi yote mitatu iliyofanya Muungano ufanye kazi imeporomoka; hivi sasa kunatakiwa tathmini mpya. Msingi wa kwanza ulikuwa ni Vita Baridi kati ya Mataifa ya Magharibi na Mataifa ya Mashariki vilivyokamiana kumalizana kwa kugombea nchi za dunia ya tatu.
Msingi wa pili ni mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa uliozaa rais dikteta, maarufu kama “rais beberu” (imperial presidency) asiyeambilika.
Rais aliweza kurekebisha na kuchezea matakwa ya Muungano kwa amri yake (decree) na Bunge la chama kimoja likaridhia bila kuhoji.
Yeyote aliyehoji Muungano aliwajibishwa kwa viwango mbalimbali. Mfano ni Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, aliyevuliwa nyadhifa zote za uongozi wa Serikali na chama mwaka 1984, alipotumia haki yake ya Kikatiba, kutaka kujua Muundo sahihi wa Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano.
Jumbe, kwa kutumia ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, aliandaa Hati kupeleka Shauri kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba kutaka itoe ufafanuzi ni aina gani ya Muungano uliofikiwa kati ya Tanganyika na Zanzibar na mgawanyo wa madaraka kati ya nchi hizo mbili ndani ya Muungano.
Kazi pekee ya Mahakama hiyo ni kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake, na kutoa uamuzi wa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Msingi wa tatu ulioporomoka ni Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea lililosimamiwa na Serikali ya chama kimoja na ambalo lilipigwa dhoruba na Azimio la Zanzibar mwaka 1992. Na ingawa Azimio na Siasa hii haikuwa na nguvu sana Zanzibar, lakini kikatiba ilijenga Umoja wa Kitaifa na kuondoa dhana ya watu kuhoji hoji mambo mengi ya kiserikali na kiuongozi, lakini leo mambo ni tofauti ambapo matakwa ya Haki za Binadamu, Haki za Kisiasa na za kiraia na kuwapo kwa Asasi huru za Kiraia [Civil Society], kunafanya mfumo wowote unaobana jamii uhojike na kuzua changamoto na vuguvugu za mabadiliko.
Maoni ya Wasomaji
Mimi naona wazanzibar
Mimi naona wazanzibar hawautaki Muungano hat kidogo kwa hiyo naona tuwaache waendelee na mafuta yao na sisi tuendelee na almasi yetu.
Mihangwa,
Mihangwa,
usituletee za kuleta bwana. Watanganyika tumechoka kuwabeba Wazanzibari. Muungano wa kuwabembeleza Wazanzibari ifike mahali Watanganyika tuseme INATOSHA. Tumewahonga kila kitu, ikiwemo umeme bure, ardhi, nafasi za biashara,Uraisi, Umakamu,Uwaziri Mkuu, lakini hawaridhiki. They keep coming for more. Mwisho watasema kila Mtanganyika achukuliwe UTUMWA na Mzanzibari. TUMECHOKAAA. Hatutaki muungano wa aina yoyote ile, hata wa mkataba. IMETOSHA!!
siasa za kudanganywa sasa iwe
siasa za kudanganywa sasa iwe mwisho kwa kupitia katiba hii mpya iweke wazi mwanzo na mwisho wa kitu hiki kinachoitwa muungano,wote tunajua kuwa hamna muungano unaolazimishwa na WAAMUZI WA MWISHO NI WANANCHI NA MAAMUZI YAO YAHESHIMIWE,TUKISEMA NDIO NA WENGINE WAKISEMA HAPANA BASI IWEMWISHO WA MJADALA HUU
Hongera sana, Bwana ,Mihangwa
Hongera sana, Bwana ,Mihangwa kwa makala nzuri yenye kueleweka.
Yeyote ambaye anajifanya kutoielewa makala hii, basi huyo ana matatizo ya akili.
Mchangiaji namba 2, inaonekana anatumia kichwa chake kuoteshea na kukuzia nywele tu, na sio kufikiria! Pole zake sana.
Mtanzania mwenzangu, Ndugu
Mtanzania mwenzangu, Ndugu Mihangwa, yawezekana una lengo jema la kutotaka Muungano kuvunjwa. Hilo nakupa heko, kwa sababu kwa hakika ilipaswa Muungano uwe kati ya mambo ambayo hayana mjadala - yeyote - kiwe ni chama tofauti cha siasa au mtu tofauti - anapoingia madarakani alipaswa awe anajua kuwa kati ya maeneo yasiyohitaji kuuliza mara mbili kama yawepo au yasiwepo ni Muungano. Lakini sasa umesema kwa usahihi kuwa, hayo yangewezekana kama pande zote mbili za nchi zilizoungana zingeona ipo "legitimacy" ya kuendelea kuumbatia - na kuwa jazba, chuki, husda,"uhayawani" na "uhafidhina" wa kutaka kuvunjwa Muungano - visingekuwepo. Natofautiana nawe unapoamua ku-generalize kuwa upinzani wowote dhidi ya Muungano na kutaka Zanzibar "iwe huru" ni "uhafidhina" - naona matumizi ya neno hilo yako "value-ladden" mno na yanataka kuwepo mtazamo kuwa wasemao "Muungano ujadiliwe tu kuona namna gani "utaboreshwa" ili pande zote zenye mitazamo tofauti kuuhusu ziweze kuwa accomodated" basi hao ni wa mrengo wa kati (moderates) - hivyo sauti zao ndizo za "busara" zaidi, "hazina uhayawani" au "ulevi" wa kutaka Muungano uvunjike.Ingekuwa hali halisi iliyopo sasa ni hiyo "ideal" unayoitaka wewe, ya kutokuwepo jazba na upotoshaji huo mkubwa uliojitokeza hasa Zanzibar - ningekubaliana nawe kuwa asemaye Muungano uvunjike kweli ni mhafidhina - na huyo isingekuwa rahisi kusikiliza tena "sauti za busara" na tafakuri.
Lakini, kwa hakika, mimi nafikiri hoja zilizoibuka hivi karibuni, hususan kutokea Bara za LET ZANZIBAR GO! Siyo hoja za kihafidhina - ni hoja za kiuhalisia (realism) ambazo zimetokana na kupikika na kukubalika kwanza, hususan Visiwani, kwa hizo siasa za siri kuwa Zanzibar inanyonywa na kunyanyaswa, na sasa inahitaji kupewa "uhuru"zaidi. Hayo yameanzia na kushika kasi huko Zanzibar, Wabara hata hawakuwa wamesema lololote. Hadi sasa ilipofikia kwenye dhahama za huo unaoitwa "uamusho" na kutendwa makosa ya jinai ya kuchoma makanisa na baa (jamani yanahusiana nini na Muungano kuwepo au kutokuwepo hayo - lakini si ndo kilele cha chuki kuwa Wabara "ondokeni mtuachie Zanzibar" yetu??!) - Kwa dunia ya leo yenye utumiaji wa nguvu wa kila namna wa watu na vikundi vyenye imani zao (sasa ndo za kihafidhina) - vitendo hivyo vingestahili hata kuitwa "ugaidi" - manaake vinatia hofu kwa watu wa aina fulani ....na mfumo wa uchukuliwaji hatua za kisheria nao unaonekana kuwa ni wa "window dressing" zaidi sababu wenye mamlaka na jukumu la kusisimamia sheria Zanzibar nao pia ni kama sympathy wanayo juu ya utendaji makosa uliofanyika - walitenda wanajulikana, lakini kama hawawi swift kuchukua hatua; hayo yote si inapaswa tukubali kuwa ni viashiria vya matatizo makubwa yajayo kama hatutafuti mzizi wa fitina na kutibu ugonjwa? Kama hatukubaliani mapema nini cha muhimu kwetu - sote - kama Watanzania, tutakuwa ni mbuni afichaye kichwa mchangani, kumbe mwili mzima uko juu..
Ni wazi viashiria hivyo sasa vimejidhihiri kwa vitendo, baada ya Wazanzibari kufikia kuunda Serikali ya umoja wa Kitaifa. Chuki iliyokuwa imewatenga sasa imekuwa muungano - wanatafuta lipi tena la kuunganishia nguvu zao - of course - hebu tujadilia Muundo wa Muungano - lakini kwa hakika - hebu tujadili "Uhuru wa Zanzibar".... Lakini hiyo nayo si jipya - lilianza kidogokidogo kwa viashiria vingine. naoodhesha vichache hapa chini.
Wimbo wa Taifa la Zanzibar. Mtu asipofikiria sana atasema - aaah, kwani Zanzibar kuwa na wimbo wa Taifa kuna madhara gani? Kama mtu atauliza hilo, nami nitauliza kuwa na wimbo wa Taifa wa bara kuna madhara gani? Sema hatuhitaji wimbo wa taifa wa Bara - tunao wimbo wa Taifa wa Tanzania unatosha - ndo wengi tunaoujua kwa hakika - pamoja na "Tazama Ramani"... Niseme tu, ulipoombwa wimbo wa taifa wa Zanzibar ikasemwa - kwani kuna shida gani? Hewallah. Wimbo wa Taifa wa Zanzibar ukaanza rasmi, ukawa mbadili wa Wimbo wa Taifa (Mungu Ibariki Tanzania... Mungu Ibariki Afrika). Ukafundishwa skuli, na sasa ndio unaoimbwa kila asubuhi kabla ya watoto kuanza masomo yao skuli. Nani asiyeelewa kuwa, ili uzalendo na utaifa vidumu, lazima viimarishwe kupitia mfumo wa ilimu? Watoto wa leo si ndiyo watu wazima na watoa maamuzi kesho? Lakini watoto Zanzibar kama "pledge of allegiance" wanayoijua ni ya Taifa la Zanzibar; wala siyo kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano - hivyo ziwepo mbili - kesho wasipoutambua Muungano utawauliza nini tena???
Haya, eneo jingine ni la bendera. Kukawa na shinikizo - Zanzibar ipepeze bendera yake yenyewe ... Ikasemwa hewallah! Leo hiyo inapepea - na narudia tena ikiwemo mashuleni - pledge of allegiance huenda sambamba na wimbo wa Taifa - utasema tena hata mkijadiliana - ikubalike nini sasa wakati kiashiria cha allegiance ni katika Uzanzibari? Siyo Jamhuri ya Muungano? Siyo kwa sababu nalazimisha, lakini kwa kuwa utaifa na uzalendo ni dhana - siyo kitu cha kushikika (tangible) - huwezi kulazimisha watu kama hawataki kuweka allegiance yao katika Muungano.
Eneo jingine, mgawanyo wa mapato...Ni hoja inayorudi leo hadi kesho. Je, ni asilimia 4.5 au 5%? Au ni 10% au 40% au ni 50%? Lakini swala kuu hasa - ni % ya mapato yapi? Kwa sababu mapato na mchango utokanao na watu 43 milioni huwezi kulinganisha na watu 2%! Bado sijasema, nafasi za uongozi na ajira, nk. Hivyo uwiano huo uanzie na kuishia wapi?? Lakini bado matusi ya "ukoloni", "unyonyaji" nk yanaendelea! Si kutoka Bara, ni kutoka Zanzibar.
Kwangu mimi Mtanzania naamini kuwa mjadala pekee utakaotaka kutatua "kero" ambazo zinaonekana zimejipika kila pembe ya huo Muungano, ili ukubalike pande zote - utapaswa uzingatie utowaji haki kwa kila upande - haki haiko katika kuimeza Zanzibar iwe mkoa au wilaya kwa sababu ni wazi Wazanzibari wameshatusisitizia kuwa wanataka HADHI YAO YA UTAIFA ndani au nje ya Muungano itambulike kwa wazi zaidi na kwa kila mtu kuwa ni huru - lakini bado hawawi wazi huo uhuru ufike wapi - je, wawe na hati zao za kusafiria za Zanzibar? Wawe na Jeshi lao rasmi la ulinzi? Wawe na nini zaidi?
Naamini utakubaliana nami kuwa, vyovyote itakavyokuwa, hitajio la "uhuru zaidi" japokuwa wala halihitaji ugomvi na kuchukizana kama Wazanzibari ndo wanachokitaka, litakuwa limefikia huko ambako wewe katika makala yako unaogopa na unapendekeza tusifike: kuvunja Muungano. Lakini kama Wazanzibari ndo hicho wakitakacho, sisi ni nani mpaka tuwazuie? Hatuhitaji katika hili tufikie kwenda vitani kama Chechnya, Ireland Kaskazini, au Basque huko Hispania - nasema hatuhitaji kwa sababu madhara ya vita ni chuki na visasi kwa vizazi vingi zaidi vijavyo - licha ya kujirudisha nyuma kiuchumi.
Pendekezo langu, hao wanaotaka kupata Zanzibar huru yao - waruhusiwe kutengeneza muswada na kuupeleka Baraza la Wawakilishi upitishwe na Baraza hilo, na bila shaka, ukija Bunge la Jamhuri itakuwa rahisi kupata theluthi mbili zinazohitajika - uhuru huo... Itakuwa imekihalalisha kile ambacho sasa watu wanapigapiga kelele za chini chini ambazo zingine hazieleweki hata maana yake ni nini - mara Mzee Moyo aseme eti kuwepo Muungano wa Mkataba - ni upi tena wakati Mkataba ni Katiba? Kuna Muungano wa Kihisia hapa? Kwa nini hasemi tu Zanzibar Moja na Tanzania Moja zote huru zinawezekana tukajua moja - na kuamua sasa tujadilia ya maana zaidi kwa maendeleo ya Watanzania kuliko kupoteza masaa mengi na fikra juu ya kitu kisichokuwa na tija kwa walio wengi isipokuwa wachache wanaoona watafaidika wao na jamii zao kwa kuwepo Zanzibar Huru? Si wapewwe? ..............Siyo jazba, ni uhalisia.
Maulidi Kitulya wa Muziwanda