Michezo
Tusiwalaumu Yanga, ni mikataba yetu ya ki-Mangungu!
Chesi Mpilipili
Toleo la 202
7 Sep 2011

SIKU tatu kabla ya Ligi Kuu ya soka ya Vodacom kuanza kutimua vumbi, klabu ya Villa Squad ya Magomeni Mapipa, Dar es Salaam,  ilitoa taarifa kuwa ilikuwa kwenye hatihati ya kushindwa kupeleka timu Mwanza kwa ajili ya mchezo wa kufungua dimba baina yake na Toto Afrika kutokana na ukata uliokuwa unaikabili.

Nilitegemea kuwa hata kama timu hiyo isingepata chochote kutoka TFF, basi, angalau shirikisho hilo la mpira ambalo moja ya majukumu yake makuu nchini ni kuendeleza mpira wa miguu, lingefanya kila jitihada ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inafika Mwanza; hata kama ni kwa kuiombea mkopo mahali kisha kulipana kwenye makato ya mechi zinazofuata.

Sivyo ilivyokuwa. Badala ya kutoa msaada Shirikisho hilo ndio kwanza likaichimbia mkwara klabu hiyo kwamba iwapo ingediriki kutopeleka timu Mwanza, basi, ingekuwa imejishusha yenyewe kutoka Ligi Kuu.

Mkwara huu ulikuwa na maana kuwa Villa ingeweza kushuka daraja bila hata pengine kucheza mechi moja Ligi Kuu kwa sababu tu haikuwa na nauli ya kuifikisha kwenye kituo cha mechi yake ya kwanza!

TFF, kupitia msemaji wao, wakafafanua kuwa lilikuwa ni jukumu la kila timu kufanya mipango yake ya usafiri ili kufika kwenye vituo vya mechi bila kusubiri fedha zinazotoka kwa mdhamini!

Nilidhani kuwa kuna mtu mwingine baki ambaye TFF ilipaswa kumchimbia mkwara, lakini sio Villa ambayo ilikuwa ilikuwa inawakilisha juhudi, jasho na damu la wakazi wa Magomeni waliojitolea kwa hali na mali kuifikisha hapo ilipo.

Inaeleweka wazi kuwa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ni Kampuni ya simu za kiganjani ya Vodacom.

Ninaamini kwamba miongoni mwa mambo muhimu kabisa ambayo tunategemea kuwa yamo kwenye mkataba wa TFF na Vodacom wa kudhamini Ligi hiyo, ni muda wa kutoa nauli na pesa za maandalizi kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Kwa hali ya kawaida kabisa, tunaamini kuwa mkataba wa TFF na Vodacom umeweka wazi kabisa muda wa mdhamini kutoa fedha za nauli na vifaa kwa ajili ya kutoa nafasi kwa timu kutengeneza bajeti zao.

Tunadhani kuwa badala ya TFF kuikemea Villa Squad na kuitishia kushushwa daraja iwapo isingefika Mwanza, ilipaswa kuangalia mkataba wake na Vodacom unasemaje linapokuja suala la malipo ya awali kwa timu zinazoshiriki Ligi kuu.

Vodacom kutoa pesa ya nauli ikiwezekana hata wiki mbili kabla ya michuano hio kuanza ili kuzipa nafuu timu ambazo zinawakilisha hali halisi ya mtanzania wa kawaida. Mlalahoi.

Villa inawakilisha kizazi cha timu kama vile Ashanti, Manyema na kadhalika ambazo kupanda kwao daraja hutegemea michango ya Watanzania wa kawaida wanayoikusanya siku za mechi zao kwa kuweka bakuli nje na kwenye kona za mitaa ambayo klabu zao zimo.

Timu hizi zilizojaa vipaji lukuki zinapopanda daraja na kufika ligi kuu hutegemea angalau kupata unafuu kwenye gharama za kujiendesha kutokana na fedha zinazopaswa kutolewa na mdhamini wa ligi hiyo.

Inapotokea mdhamini wa ligi akachelewa kutoa fedha mapema kwa ajili ya maandalizi na usafiri wa kuvifikisha vilabu kwenye vituo vyao vya mechi, ni wazi kuwa maandalizi ya klabu hizi ndogo hutetereka.

TFF haipaswi kuvitisha vilabu hivi na kushushwa daraja vilabu na badala yake shirikisho hilo linapaswa kumbana mdhamini kwa kuchelewesha mkwanja kwa vilabu.

Hii ni mbali na TFF kuvipatia mkopo vilabu hivyo ili kuweza kufika kwenye vituo vya mechi zao mapema iwezekanavyo pale inapolazimu. Ndio maana mojawapo ya kukuza soka hiyo.

Hakukuwa na sababu yoyote TFF kukimbilia kuwatisha Villa kwamba itashushwa daraja iwapo ingeshindwa kufika Mwanza kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi huku ikijua fika kosa liko wapi.

Kazi kubwa ya TFF ni kukuza kandanda na huwezi kukuza kandanda kwa kutishia nyau vilabu vidogo ambavyo vimetoka jasho la damu ili kucheza Ligi kuu.

Badala ya kuitishia Villa kushuka daraja, TFF ilitakiwa kuwa na moja, mkakati mbadala wa kuhakikisha kuwa timu hiyo inafika Mwanza na pili, kumshikia bango mdhamini wa Ligi kuu kutekeleza yale yanayompasa kabla Ligi haijaanza kwa mujibu wa mkataba.

Tatizo la mikataba mingi tunayoingia na wadhamini ama wafadhili ni ile ya kuona tunafanyiwa hisani sana na watu hao na kwa maana hiyo mwisho wa siku mikataba hiyo kuandikwa kwa namna ambayo inawafaidisha zaidi wao kuliko sisi wenyewe.

Ndio maana hata inapotokea mdhamini ama muwekezaji tuliye ingia naye mkataba amechemsha mahali badala ya kumbana ili atimize wajibu wake kama mkataba unavyosema tunakimbilia kuwabana wananchi wetu wenyewe huku tukijua wazi kuwa hawana kosa lolote.

Angalau Yanga wameliona hili; ndio maana kwa kisingizio cha kukataa logo nyekundu ya mdhamini wa ligi wamekataa kutumia jezi za mdhamini huyo pengine wakitaka mkataba wake na TFF uangaliwe upya ili kuhakikisha kuwa timu zinafaidika nao kuliko ilivyo sasa.

Nimeshangazwa mno na jinsi mdhamini huyo alivyokimbilia haraka haraka kubadilisha rangi ya nembo yake kwenye jezi za Yanga ili tu Yanga wavae jezi za mdhamini.

Kwa haraka haraka hii ya kukubaliana na Yanga, ninapata picha kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba mdhamini huyo wa Ligi kuu yetu anapata faida kubwa zaidi kutokana na mkataba wake na TFF kuliko inavyopata vilabu vyetu.

Inashangaza kwa mfano klabu zote za Ligi kuu zinapokuwa na aina moja ya jezi na tofauti inakuwa kwenye rangi tu! Mdhamini huyu anashindwaje kutoa nafasi kwa klabu za Ligi kuu kuchagua aina ya jezi wanazotaka kuliko hii ya klabu zote za Ligi kuu kuvaa jezi yenye mchirizi kifuani? Kuna tatizo gani kwa kila klabu kubuni ama kuchagua aina ya jezi wanayotaka kuchezea na mdhamini akatoa pochi tu?

Hilo ni moja. Lingine ni hili la kwamba katika masuala ya biashara, nembo ama logo ya kampuni ni kitu muhimu sana kiasi kwamba hata kubadilisha rangi yake tu ni mlolongo mrefu unaofuata kanuni na sheria zake. Huamki tu asubuhi na kubadilisha rangi ya logo yako kama unavyobadilisha mboga yako ya siku!

Inapotokea Vodacom (T) wakakubali kubadili rangi ya nembo yao ili tu kukidhi matakwa ya timu moja ya Afrika isiyoshiriki hata Ligi ya Mabingwa ya bara hilo tunajiuliza kama uamuzi huu umeanzia makao makuu ya kampuni hiyo huko London Uingereza ama hapo Afrika Kusini.

Je kila timu ama ligi inayodhaminiwa na kampuni hiyo itakapotaka logo ya kampuni hiyo kubadilishwa rangi ama herufi ili kukidhi matakwa ya timu, rangi rasmi ya logo ya kampuni hiyo itajulikana tena?

Ndio maana tunahoji uharaka huu wa Vodacom (T) kukubaliana na Yanga kubadilisha rangi ya Logo yao ili kukidhi matakwa ya Yanga. Wenyewe huko London wana habari?

Je, Yanga haiwezi kuingia matatizoni kwa kuvaa logo ya kampuni yenye rangi isiyo rasmi ya kampuni ya Vodacom Itakapotokea kuwa uamuzi wa kubadilisha rangi ya logo hiyo umetoka hapa hapa Dar tu na haukuhusisha wenye Logo na kampuni yao huko Uingereza?

Ni kwa kuwa na mikataba yenye Uwazi tu ndio tatizo kama hili la Logo na mengineyo yanayochangia katika kupunguza utamu wa Ligi kuu yetu yatakapotoweka. Hatuhitaji mikataba ya ki-Mangungu katika karne hii ya 21.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako