Kiasi cha wiki mbili zilizopita Rais Jakaya Kikwete alimteua Profesa Benno Ndulu kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Mwandishi wetu LIVINGSTONE RUHERE amehojiana na Profesa Ndulu pamoja na mambo mengine, juu ya changamoto zilizo mbele yake. Haya ndiyo yaliyojitokeza katika mahojiano hayo.
Swali: Wasifu wako unaonyesha kuwa ulipata kuwa mchezaji soka mzuri. Na ulipokuwa Sekondari ya Azania ulikuwa kati ya wachezaji mahiri wa wakati huo. Leo ungekuwa bado unacheza soka ungekuwa wapi?
Profesa Ndulu: Naipenda sana soka, na ningetamani niwe juu katika soka. Lakini pia ningetaka nifanye kazi ya uchumi, ninayoifanya sasa hivi.
Swali: Benno Ndulu huyu ametokea wapi hasa?
Profesa Ndulu: Mimi ni mzaliwa wa Ifakara, Morogoro. Palepale Ifakara mjini. Baba yangu ni Joseph Ndulu na mama Regina Mpangile.
Katika familia yetu tuko watano. Wavulana wawili na wasichana watatu. Nilisoma Shule ya Msingi Ifakara na kumaliza mwaka 1961. Nikahamia Mahenge kwenye Seminari ya Kasita mpaka mwaka 1966.
Nilipotoka Kasita nilikwenda Semonari ya Itaga, Tabora kati ya mwaka 1967 na 1968. Kutoka Itaga nilikuja Azania Sekondari mwaka 1969/1970, na baada ya hapo nikaenda Jeshi na Kujenga Taifa Oljoro.
Swali: Hizi seminari ulikopota zinadhirisha kuwa ulipitia katika makuzi ya kipadre. Ilikuwaje hukuendelea na uchungaji?
Profesa Ndulu: Ni kweli nimekulia katika seminari. Lakini wakati huo mimi nilikuwa mdogo. Hiyo ni kuanzia darasa la tano mpaka la 12. Na unajua mambo hayo ya upadre yanakwenda na wito.
Kufika seminari ndivyo Mungu alivyoniongoza na kwenda Azania ni mwongozo wa Mungu vilevile.
Swali: Baada ya Azania na JKT ulikwenda wapi?
Profesa Ndulu: Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikosoma uchumi. Nimefanya shahada tatu, ya kwanza (BA), ya pili ya uzamili (MA) na ya tatu ya uzamivu (PHD) niliyofanya Marekani.
Kwanza niliajiriwa kama mhadhiri mwanafunzi mwaka 1974 baada ya kumaliza shahada ya kwanza. Baadaye Niliporudi nikawa napanda, nikawa mhadhiri; kisha nikawa mhadhiri mwandamizi; baadaye nikawa profesa mshiriki na kisha nikawa profesa.
Nilikwenda mbiombio kidogo, kufika mwaka 1988 nilikwisha kumaliza ngazi hizo zote kuanzia mwaka 1979.
Baada ya hapo nilikwenda African Research Consortium mwaka 1989 kama mwanzilishi pamoja na mwenzangu mmoja. Mimi nikiwa Mkurugenzi wa Utafiti kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.
Nilikaa pale kwa miaka karibu 10, lakini kabla na baada ya kujiunga hapo, nilikuwa mkurugunzi kwenye Bodi ya Benki Kuu (BoT) kwa miaka sita wakati wa ugavana wa Gilman Rutihinda na wakati wa gavana Dk. Idris Rashidi.
Na kipindi hichohicho pia Rais aliniomba niwe Mwenyekiti mwanzilishi wa Tanzania Revenue Authority (TRA). Tulifanya kazi hiyo kwa karibu kabisa. Kingine ambacho huwa napenda kukizungumzia ni kwamba kati ya mwaka 1991 na 1994, kwa wakati wangu mwenyewe, nilikuwa nikienda Afrika Kusini kuwasaidia kwa maandalizi ya mabadiliko ya uongozi. Nilifanya kazi na karibu viongozi wote pale ambao sasa wako madarakani.
Swali: Hizo safari za Afrika Kusini zilikuwa za mambo ya uchumi?
Profesa Ndulu: Nilikuwa nashughulikia kuwaandaa kutoka katika kipindi cha ubaguzi kwenda katika kipindi cha demokrasia katika uchumi. Kwamba mabadiliko hayo waende nayo namna gani katika masuala ya uchumi. Nilikuwa kama mshauri.
Swali: Turejee TRA. Ukiitazama TRA leo, inakidhi matarajio mliyokuwa nayo wakati mkiianzisha?
Profesa Ndulu: Kwa kweli sisi tulisisitiza vitu vikubwa vitatu. Cha kwanza ni kuhakikisha kwamba TRA inapata wafanyakazi waadilifu na wenye uwezo. Tulipoianzisha hatukuwa na mtumishi aliyeinga moja kwa moja kutoka Idara ya Kodi. Wote walipita mchujo. Waliopita walipita na walioshindwa walishindwa. Na baadhi ya viongozi pia hawakupita.
Pili, tulitilia mkazo kuhakikisha kuwa zile njia za kuvujisha mapato tunaziziba na namna ya kuziziba ni moja: kuweka kabisa mpango ambao una uwazi na pili kuweka udhibiti vizuri na tatu kuhakikisha kuwa tunatoa vivutio kwa wafanyakazi. Na kwa kipindi tulichokuwa pale tuliweza kuongeza mapato karibu mara tatu.
Nadhani tuliweka msingi, na sehemu kubwa ya msingi upo, na viongozi wengi waliopo pale ndio wale walioingia kipindi kile.
Kwa hiyo mimi kwa jumla nafurahi, japo kazi bado ipo, na ipo kubwa tu ya kuendelea kuongeza mapato na kuziba mianya, lakini kwa ujumla shirika lile limekwenda vizuri.
Swali: Kuna watu wanasema bado TRA inaweza kukusanya mapato zaidi ya milioni 400. Unadhani kiasi hicho kinaweza kupatikana?
Profesa Ndulu: Uwezo wa kuongeza mapato upo. Uwezo huo utategemea ukuaji wa uchumi na shughuli zilizopo. Kuonekana wazi kwa vyanzo vya mapato. Maana sehemu kubwa ya mapato ya nchi hii hayako kwenye wigo wa kodi. Na hilo ni jambo ambalo kwa maoni yangu itabidi waendelee kulishughulikia.
Swali: Mwaka jana uliteuliwa kuwa Naibu Gavana kabla ya mwaka huu kuteuliwa kuwa Gavana. Tangu mwaka jana, umeona nini ndani ya BoT?
Profesa Ndulu: Nimeona mambo makubwa mawili. Moja ni kuwa kuna watu wenye uwezo ndani ya benki. Na kiujumla katika zile kazi zake maalumu za kibenki kuu, hiki ni chombo ambacho kimefanya kazi zake vizuri na si tu kwa wana uchumi, bali pia mashirika mengi ya ulimwengu yanatambua hivyo. Na wafanyakazi wakipata nafasi nzuri ya kuendelea na utendaji huu kazi itakuwa bora zaidi.
Pili, kuna vitu vingi tu ambavyo si sehemu muhimu ya Benki Kuu, lakini ambavyo Benki imeombwa ifanye.
Swali: Vitu kama?
Profesa Ndulu: Sisi tunalea skimu za dhamana na tunalea na pensheni. Vitu hivyo vyote ni kwa kuwa tu vyombo vinavyopaswa kuvisimamia havipo. Lakini shughuli hizo ambazo si hasa za msingi za Benki Kuu zinaleta ushindani kidogo katika utendaji wa mambo hasa ya msingi ambayo ni ya Benki Kuu.
Nadhani kutakuwa na umuhimu wa kuona huko tunakokwenda kupunguza kidogo wigo wa shughuli zetu isije kuwa kila kitu kikianza kipya kinakwenda Benki Kuu.
Swali: Katika hali hiyo unashauri nini?
Profesa Ndulu: Tunachoshauri ni kutengeneza hivi vyombo vingine ili baada ya wakati fulani viweze kuchukua shughuli hizi. Huko ndiko sehemu zao na vyombo hivi vinaweza vikawekwa huko. Kwa mfano, kuna TIB (Benki ya Rasilimali) inafanya mambo ya mikopo na maendeleo, kwa nini wasifanye skimu hizi za maendeleo?
Hii ni kama mfano, sisemi kuwa ndivyo inavyopasa, lakini ni muhimu kuangalia maeneo haya. Benki Kuu ibaki zaidi na shughuli zake ambazo ni za kibenki kuu hasa.
Swali: Raia wa kawaida wanaweza kujiuliza, hizo shughuli za Benki Kuu ni nini hasa?
Profesa Ndulu: Benki Kuu ina shughuli kubwa tatu. Moja ni utulivu wa uchumi. Watu wawe na uhakika, kwamba nikiamua hiki leo, kesho bei zitakuwa zimefanana, karibu ni zilezile. Ya pili, ni gharama za riba. Maana ya riba ni kwamba mikopo ndiyo inayosaidia kukua kwa shughuli za uchimi.
Ya tatu, ni kuhakikisha kuwa benki zetu ni salama. Watu wanawekeza fedha zao wakijua kesho watazikuta.
Swali: Umegusia juu ya mfumuko wa bei. Wewe mikakati yako ya kupambana na mfumuko wa bei ni ipi?
Profesa Ndulu: Kuna njia tatu. Ya kwanza ni kuhakikisha kuwa ujazi wa fedha unalingana na upatikanaji wa vitu. Maana yake pesa ikiwa nyingi na vitu vikawa vichache, bei itafumuka.
Tumekuwa tukifanya jitihada nzuri tu kwa upande huo na katika kota hii iliyopita tulipunguza sana ukuaji wa ujazi wa fedha uliopo.
Unajua, kwa kawaida tuna malengo ya ujazi. Ujazi huo unapimwa ki bilioni. Safari hii iliyopita mpaka tulipomaliza kota ilikuwa ni 1915 bilioni. Ambayo ni trilioni 1.9, ndiyo ilitakiwa kuwa ujazi.
Lakini, hasa tulimaliza tukiwa na kiwango cha kiasi cha 1890 hivi kwa maana ya lengo lile. Maana yake ni kuwa ujazi ulikuwa ni pungufu kwa karibu milioni 30 hivi.
Lengo ni kwamba ujazi usizidi ile trilioni 1.9. Ikizidi hapo maana yake fedha zitakuwa ni nyingi mno. Sasa inabidi tuendelee hivi. Kwa kuwa kama hatuvuki kiwango hicho maana yake mfumuko wa bei nao utakuwa umepungua.
Njia ya pili ni kuhakikisha ya kuwa riba za mikopo zinabakia chini kusudi kupunguza gharama za uzalishaji. Maana gharama hizo nazo zikiwa kubwa katika uendeshaji bei zinakuwa kubwa.
Hilo pia tumeweza kufanikiwa katika miezi mitatu iliyopita. Tumeshusha riba za dhamana za Serikali kutoka wastani wa asilimia 17 hadi wastani wa asilimia 10. Kama tutaendelea hivi, riba zikabaki huko chini, basi hata riba za mikopo zitapungua.
Tatu, ni kuhakikisha kuwa tunasaidia upatikanaji wa mikopo kwa kukuza benki na kukuza njia za benki ili uzalishaji uendelee, na vitu vinavyozidi kuwa vingi kuna uhakika kuwa bei zitaremka.
Swali: Unaweza kuiweka hiyo katika lugha rahisi? Maana watu wanaona mchele bei yake iko juu ya 1,000 huku wewe ukisema mfumuko wa bei uko chini?
Profesa Ndulu: Mfumuko wa bei maana yake ni mabadiliko kutoka mwezi hadi mwezi au mwaka hadi mwaka. Yale mabadiliko ndiyo mfumuko. Lakini kiwango ni kiwango.
Kwa mfano. Kama bei ya nyanya mwaka jana kilo moja ilikuwa shilingi 10 mwaka jana mwaka huu ikawa shilingi 11, basi mfumuko wa bei hapa ni asilimia 10, yaani ni shilingi moja katika kila shilingi 10.
Kiwango cha bei kimepanda kutoka shilingi 10 hadi shilingi 11. Kwa hiyo vile viwango vya bei vikisha kupanda vinabakia pale lakini haina maana ikisha kufika 11, kwa mfano, ikateremka kutoka 11 labda kutokana na uzalishaji nyanya umekuwa mkubwa, au kama mananasi yalivyo sasa, inapunguza bei, na hiyo ndiyo tunayoita mfumuko hasi.
Swali: Watu wanasema uchumi unakua, katika hali hiyo kinachomaanishwa ni nini?
Profesa Ndulu: Uchumi unapokua kwa kawaida tunatarajia upatikanaji wa bidhaa na kipato. Vinatakiwa viongezeke zaidi ya bei zitakavyoongezeka. Maana yake umeongeza kitu mfukoni.
Kiasi kikikua kidogo kuliko bei zilivyoongezeka basi mtu anakuwa hana kitu mfukoni. Sasa kwa nchi yetu tunaposema uchumi umepanda, vyanzo vikubwa vya kupanda ni pamoja na uchimbaji wa dhahabu, utalii, kilimo kwa kiasi fulani. Sasa namna ya kutafsiri kutoka uchumi kukua hadi kipato inategemea pale ulipo.
Uchumi unapanda zaidi kwenye dhahabu na dhahabu hiyo sasa iko mikononi mwa watu wachache ambao labda baadhi yao wako nje, kwa hiyo kishindo cha kipato mfukoni mwa Mtanzania kinakuwa si kikubwa.
Kwa hiyo inategemea ni sekta gani hasa zimekuwa kwa haraka. Kilimo ndicho kinatakiwa kikue kwa haraka kwa kuwa huko ndiko wengi wanakopatia kipato.
Toa maoni yako