Tuzijali afya zetu kama tunavyojali mali zetu

WIKI iliyopita, taifa letu limekumbwa na misiba ya viongozi takribani watano waliopoteza maisha katika kipindi cha wiki moja tu. Kwa namna ya kipekee, Raia Mwema linapenda kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wote walioguswa na misiba hiyo.

Wote waliofariki walipoteza maisha kwa maradhi tofauti. Hakukuwa na kiongozi aliyepoteza maisha kwa ajali au kwa kuvamiwa na majambazi. Wote walipoteza maisha kwa sababu ya maradhi.

Vifo hivyo vya viongozi vinatakiwa kuwa kielelezo cha namna Watanzania wanavyopoteza maisha kwa magonjwa mbalimbali. Kama takwimu sahihi za watu wanaofia hospitalini na majumbani zingekuwa zinapatikana, pengine wengi wetu tungetishika na hali ilivyo.

Lakini ukweli usiopingika unabaki kuwa mmoja; kwamba Watanzania tunakufa kwa kiwango kikubwa. Hali iko hivi mijini na vijijini; na wanaokufa ni watu wa marika yote, jinsia zote na hali zote.

Jambo la kusikitisha ni kwamba kuna watu wengine wangeweza kuishi maisha marefu zaidi kama wangekuwa na utaratibu wa kutazama afya zao. Watu wana bima za afya lakini wanaenda hospitali wakiwa wagonjwa tu.

Watu hawahawa wanaoshindwa kutazama afya zao, ndiyo haohao ambao kila mwisho wa mwezi huyapeleka magari yao kwa mafundi kwa ajili ya ukaguzi. Ni watu hawahawa ambao mali zao wameziwekea bima.

Tunadhani kwamba taifa letu linahitaji kiwango kikubwa sana cha utolewaji wa elimu kuhusu umuhimu wa watu kutunza na kulinda afya zao. Tatizo hili ni kubwa pengine kuliko hata ukosefu wa dawa.

Tunashauri kwamba fedha ambazo serikali imeokoa kwa kununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani badala ya kupitia madalali, zingetumika kwa ajili ya kutoa elimu ya umma kuhusu watu kujilinda.

Elimu kuhusu usafi wa mazingira. Kwamba malaria na kipindupindu vinaweza kuepukwa bila dawa bali kwa kuhakikisha watu wanaishi katika mazingira safi na salama.

Kwamba magonjwa haya yanayoibuka siku hizi kama kisukari na shinikizo la damu yanaweza kupunguzwa kwa watu kufanya mazoezi na kutokula vyakula hatari.

Dawa pekee hazitatosha kuokoa maisha ya Watanzania hawa. Kimsingi, kwa umasikini wetu, serikali haiwezi kununua dawa za kutosheleza mahitaji. Lakini, inaweza kuamua kuelimisha watu wake ili kupunguza vyanzo vya magonjwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *