Michezo
Twiga Stars haoooo
Mwandishi Wetu
Toleo la 224
1 Feb 2012
Twiga stars

TWIGA Stars imethubutu, inaweza na yaendelea kupasua anga. Sasa itapaa hadi Ethiopia kuwavaa wahabeshi katika mfululizo wa michezo ya kutafuta kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake.

Sasa Twiga itakabiliana na Ethiopia baada ya kuiondoa kwenye michuano hiyo timu ya Namibia. Iliifunga kwao kwa mabao 2-0 na hapa nyumbani mwishoni mwa wiki iliyopita ikaichabanga kwa mabao 5-2 hivyo kuendelea na michuano kwa kuifunga timu hiyo jumla ya mabao 7-2.

Kwa mara nyingine, Twiga imewapa faraja wapenzi wa soka wa Tanzania. Imewafanya warudi nyumbani kuizungumzia au kuifurahia timu inayowahusu. Siyo siri kwamba hivi sasa mashabiki wengi wa soka wana mapenzi na soka la nje ya Tanzania na hasa Ligi ya England.

Zinavyoshabikiwa timu za klabu za Barcelona ya Hispania, Chelsea au Liverpool za England utadhani timu hizo ziko Tanzania au zina matawi yake yanayofahamika na klabu hizo ndani ya Tanzania. Kumbe ushabiki huo pamoja na ukweli kwamba zinacheza vizuri, unatokana pia na kufanya vibaya kwa timu zetu za hapa nyumbani.

Twiga Stars imeiondosha Namibia wakati mashabiki wengi wa soka nchini macho yao yakiwa Malabo, Guinea ya Ikweta ambako Fainali za Soka za Bara la Afrika kwa upande wa wanaume zinaendelea. Tanzania ilishiriki fainali hizo kwa mara ya mwisho mwaka 1980, enzi za akina Jella Mtagwa na Rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).          

Ni jambo la kufurahisha kwamba Twiga Stars, pamoja na dalili za kufanya vizuri kwa upamde wake kuanza zamani, sasa imekuwa na mvuto zaidi. Wadau mbali mbali wameanza kujitokeza. Ushindi wake wa mabao 5-2 uliopatikana kwenye Uwanja wa Taifa na mchezo huo kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni umewafurahisha wengi na kuwaibua hata wabunge.

Wabunge kadhaa akiwamo, waziri mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa walijitokeza kuipongeza  timu hiyo mara baada ya ushindi wake mkubwa mwishoni mwa wiki. Waliitakia heri na safari safari yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za ubingwa wa wanawake barani Afrika zitakazofanyika Mei mwaka huu.

Mpinzani ajaye wa Twiga Stars ni Ethiopia ambayo imeonyesha ya kuwa si timu ya kuidharau pamoja na ukweli kwamba huko nyuma Twiga iliwahi  kuiondoa katika mashindano muhimu kama haya. Kwamba timu hiyo imeiondosha Misri kupata nafasi ya kucheza na Twiga ni jambo la kulitilia maanani kwamba si timu ya kuibeza.

Licha ya ukweli kwamba Ethiopia imewahi kutolewa na Twiga huko nyuma, ushindi wake mkubwa wa mwishoni mwa wiki utaifanya Ethiopia kujandaa kikamilifu.  Ni dhahiri kwamba itacheza na Twiga ikijua kwamba ni kiboko yake na ni timu inayokuja juu kwa kasi kuwa moja ya vigogo wa Afrika katika soka la wanawake. 

TFF imetangaza kwamba inafanya mpamgo wa kuitafutia Twiga michezo ya kirafiki dhidi ya timu za Kenya na Uganda katika kujiandaa na mchezo wake na Ethiopia. Hilo ni jambo jema. Hivyo basi, na maandalizi yake pia yakianza mapema kama TFF ilivyotangaza, uwezekano wa Ethiopia kuwa asusa nyingine ya Twiga ni mkubwa mno.

Ni vyema basi misaada ikazidi kumiminika ili  maandalizi ya timu hiyo katika kuikabili Ethiopia isiandamwe na tatizo lolote kuanzia sasa wakati ari za wachezaji wake zikiwa bado ziko juu.

TFF nayo isiwwe kikwazo kingine, itimize vyema wajibu wake kwa kuwalipa wachezaji wa timu hiyo posho zao wanazostahili kuondokana na aibu ambayo ilipata timu hiyo iliporejea tu kutoka Namibia iliposhinda kwenye ofisi zake karibu siku nzima wachezaji wakidai posho.

Penye nia pana njia. Twiga kweli inaweza kuwa moja ya vigogo vya Afrika katika soka la wanawake. Hao wanaoweza wana nini? Inawezwekana mradi kila mtu atimize wajibu wake. Kila la heri Twiga Stars.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.