KATIKA sehemu ya tatu ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi Tanganyika huru ilivyopania kubadili Katiba kwa kasi ya kutisha ili kuingia kwenye utawala wa ki-imla, kwa madai ya kusukuma mbele kwa kasi kubwa gurudumu la maendeleo.
Mchakato kuelekea njia hiyo ulianza na mabadiliko ya Katiba ya Uhuru ya 1961, kwenda Katiba ya Jamhuri (1962) ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikiri ilimpa madaraka makubwa mno kufanya awe dikteta kwa vigezo vyote.
Hatua ya pili ilikuwa ni mchakato wa kubadili Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962, kuiingiza nchi kwenye udikteta wa chama kimoja na ukuu wa chama (Party Supremacy), mchakato ambao uamuzi ulikwishatolewa mapema na Halmashauri Kuu ya TANU.
Wakati Serikali ikikamilisha hatua ya kuigeuza Tanganyika kuwa nchi ya chama kimoja, tukio moja kubwa na muhimu ambalo halikutarajiwa kutokea lilitokea. Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuunda Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964.
Si Rais wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere, au Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, wala Watanganyika na Wazanzibari, waliotarajia nchi hizo zingeungana kwa sababu kabla ya tukio hilo hapakuwa na wazo hilo.
Nyerere hakukusudia Muungano wa Tanzania
Kuonesha kwamba Nyerere alitaka kuona Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) likiundwa na si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliwahi kunukuliwa akisema, alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika hadi hapo Kenya na Uganda zitakapopata uhuru kisha waungane kuunda EAF. Na katika mkutano wa nchi huru za Afrika uliofanyika mjini Addis Ababa mwaka 1960, alisisitiza nia hiyo akisema:
“Litakuwa ni jambo zuri kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki…..mipaka inayozigawa nchi zetu iliwekwa na mabeberu…..tusiruhusu itumiwe dhidi ya umoja wetu; tusiisakame ofisi ya makoloni kwa kudai uhuru wa Tanganyika pekee, kisha uhuru wa Kenya na Uganda na baadaye Zanzibar; bali tudai uhuru wa Afrika Mashariki kama shirikisho moja la kisiasa”.
Nyerere, Kenyatta na Obote hawakukusudia kuona Muungano mdogo, tena dhaifu, kama ule kati ya Tanganyika na Zanzibar, mbali na Shirikisho la Afrika Mashariki. Katika Azimio lao la kuunda shirikisho, kumbukumbu namba 13/931/63 PDT/1, la Juni 5, 1963, viongozi hao walisema:-
“Sisi Viongozi wa watu na Serikali za Afrika Mashariki, tunaahidi kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo ni kielelezo cha shauku yetu ya (kuunda) Umoja wa Afrika, na sio ubinafsi na matakwa ya umoja wa kikanda. Hii ni siku yetu ya kitendo katika kulinda na kusimamia maadili na imani yetu ya umoja na uhuru ambao tumeusumbukia kwa kujitoa mhanga”.
Kwa kuzingatia pia kwamba Zanzibar ilikuwa kwenye mchakato kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi unaofuata, Julai 1963, Azimio hilo (uk. 4) lilisema:
“Ingawa Zanzibar haikuwakilishwa kwenye Kikao hiki, tunataka ieleweke kuwa, nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuunda Shirikisho hili, punde itakapomaliza Uchaguzi Mkuu mwezi ujao”.
Wazo kuu la wakati huo, na ambalo Nyerere alikuwa mratibu wake mkuu, lilikuwa ni kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) ambapo Zanzibar ingekaribishwa kushiriki baada ya uhuru uliotarajiwa Desemba 9, 1963. Hata wakati Mapinduzi ya Zanzibar yakifanyika Januari 12, 1964, Mwalimu Nyerere alikuwa mjini Nairobi na viongozi wenzake, wakijadili mchakato wa shirikisho hilo la nchi nne za Kenya, Uganda, Tanzania na Zanzibar.
Na pale Kenya na Uganda zilipoitambua Serikali mpya ya Mapinduzi Zanzibar siku mbili baadaye, Nyerere alikataa kufanya hivyo, pengine kwa sababu kuu mbili; kwanza (alitamka) kwamba hakuwa na hakika kama kweli Karume alikuwa ameshika madaraka; pili, tukio la Mapinduzi lilitibua akili na mipango yake kuelekea Shirikisho la Afrika Mashariki, bila kujali ni Serikali ipi ingeshika madaraka Zanzibar baada ya uchaguzi.
Wakati Sultani wa Zanzibar, Jamsheed Bin Khalfa, alipofukuzwa Zanzibar kutokana na Mapinduzi, alikimbilia Kenya na kujaribu kutia nanga Mombasa kutafuta hifadhi, lakini Serikali ya Kenya ilikataa kumpokea. Ndipo akageuza safari kwenda Dar es Salaam na kupokewa na Nyerere, akapewa hifadhi hadi alipokamilisha mipango yake ya kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza.
Ni pale tu Kenyatta na Obote walipoghairi mpango mzima wa Shirikisho, ndipo Nyerere alipogeukia ghafla Muungano wa nchi mbili; Tanganyika na Zanzibar, tena kwa mazingira ya dharura na kwa kasi ya kutisha.
Kujitoa kwa Kenyatta na Obote kwenye mchakato wa Shirikisho ilikuwa baada ya kubaini kuwa, Shirikisho la Afrika Mashariki lililokusudiwa, ulikuwa ni mkakati madhubuti wa Waingereza kuziweka nchi hizo kwenye kapu moja kuweza kuzidhibiti kirahisi kwa njia ya ukoloni mamboleo, kuliko kufanya hivyo kwa nchi moja moja.
Wakati huo huo, Uingereza na Marekani zilitaka Zanzibar iingizwe na kumezwa kwenye tumbo kubwa la EAF ili kuzuia isiingie kwenye kambi ya Ukomunisti enzi hizo za vita baridi, kati ya mataifa makubwa – Urusi na Marekani.
Miezi minne baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, Kenyatta alinukuliwa na gazeti la “The London Times, la Agosti 3, 1964, akisema; hakuwa tayari kupiga magoti kwa Nyerere na Tanganyika. Kwa nini?
Na kuhusu aina ya Muungano uliokusudiwa, Nyerere aliweka wazi jambo hili baadaye katika makala yake kwenye jarida la Africa Forum (Vol. I No. 1, 1965, uk. 46) kwa kusema:
“Si lazima liwe taifa lenye Serikali moja yenye nguvu. Lazima iwe Serikali moja ya Muungano yenye mamlaka kamili kwa mambo kadhaa ya kimuungano kwenye maeneo fulani fulani tu, ambapo Serikali za nchi husika (hazitakufa) zitaendelea kuwa na mamlaka kwa mambo mengine yote yasiyo ya Muungano. Hii ni kusema kwamba Muungano huu wa Afrika mpya na wa aina ya Shirikisho”.
Kwa mtazamo huo wa Nyerere wa mapema kabisa, wengi wanaamini kwamba hata ule Muungano uliokusudiwa baadaye kati ya Tanganyika na Zanzibar, ulikuwa wa aina ya Shirikisho, ila ulichakachuliwa mwaka mmoja baadaye na kuzua kero za Muungano zinazoendelea hivi leo.
Huko Nyasaland (Malawi) Rhodesia Kaskazini (Zambia) na Rhodesia Kusini (Zimbabwe) nako, nchi hizo nazo zilikatisha mchakato wa kuunda Shirikisho la nchi tatu kwa sababu hizo hizo.
Katiba ya Muungano ya Muda
Ilikuwa asubuhi, Aprili 22, 1964, wakati Mwalimu Nyerere alipowasili Ikulu ya Zanzibar, akiwa na rasimu ya Mkataba wa Muungano mkononi, na kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, ili hao wawili watie sahihi kuunganisha nchi zao.
Katika ziara hiyo fupi, Nyerere alifuatana na mashahidi muhimu watatu, Bhoke Munanka, Job Lusinde na Oscar Kambona. Kwa upande wake, Karume alikuwa na mashahidi watatu pia, ambao ni Abdallah Kassim Hanga, Abdul-Aziz Twala na Ali Mwinyigogo.
Mkataba huo, ulioandaliwa kwa njia ya dharura na kwa lugha ya Kiingereza na Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika wa wakati huo, Roland Brown, ulitiwa sahihi na viongozi hao wawili. Mkataba huo wa kimataifa unajulikana kama Hati ya Muungano, au kwa lugha nyingine “The Articles of Union, of 1964”.
Kama ilivyo ada kisheria, Mkataba wa Kimataifa kama huo hauwezi kuwa na nguvu ya kisheria kwa utekelezaji mpaka upate ridhaa ya Bunge, ndivyo ilivyokuwa, kwa Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar, yaliporidhia Mkataba huo, Aprili 25, 1964 na kuwa Sheria ya Muungano namba 22, ya 1964. Aprili 26, 1964 Muungano ukatangazwa rasmi, ukijulikana kama “Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar”.
Muungano bila Katiba?
Kwa namna ambayo Muungano huo ulifikiwa kwa njia ya dharura, tena bila ya kutarajiwa, hapakuwa na muda wa kuandaa Katiba ya Muungano. Ili kuziba ombwe hilo, iliwekwa wazi ndani ya Mkataba huo (ibara ya 3) kwamba, katika kipindi cha mpito cha miezi 12 hadi Muungano utakapopata Katiba yake, “Katiba ya Muungano itakuwa (ile) Katiba ya Tanganyika kama itakavyorekebishwa” kuingiza mambo yote 11 ya Muungano. Hii ndiyo iliyofahamika kama “Katiba ya Muungano ya Muda” ya 1964.
Mambo hayo 11 ya Muungano yalikuwa ni: Katiba ya Muungano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya Nje; Ulinzi (sasa Ulinzi na Usalama tangu 1984); Polisi; Mamlaka kuhusu mambo ya hali ya hatari; Uraia na Uhamiaji.
Mengine ni biashara ya nje na mikopo; utumishi wa umma katika Jamhuri ya Muungano; kodi ya mapato na ushuru wa forodha; bandari, usafiri wa anga, posta na simu za maandishi (telegraphs). Mambo hayo sasa yamefikia 23; Serikali hizi mbili hazijawahi kukutana kukubali kuyaongeza.
Mambo mengine yasiyo ya Muungano yaliachwa kusimamiwa na Serikali za Tanganyika na Zanzibar, kila moja kwa upande wake kwa kutumia sheria zilizokuwepo (angalia ibara ya 5 ya Mkataba).
Na kwa mujibu wa ibara ya 5 ya Mkataba huo, ukiondoa mambo ya Muungano, “Sheria za nchi ya Tanganyika na zile za Zanzibar zitabakia kuwa na nguvu katika nchi hizo”: yaani, “the existing laws of Tanganyika and Zanzibar shall remain in force in their respective territories”.
Na kwa mujibu wa kifungu namba mbili cha Sheria ya Muungano, neno “sheria zilizopo” (existing laws) kama zilivyokuwa kabla ya siku ya Muungano, limetafsiriwa kumaanisha sheria zote zilizoandikwa na zisizoandikwa, lakini si pamoja na Katiba ya Tanganyika kwa mambo ya Tanganyika.
Vivyo hivyo, chini ya Mkataba na kwa mujibu wa Sheria ya Muungano, “hadi hapo Bunge la Katiba litakapopitisha Katiba ya Muungano, Bunge na utawala (the executive) wa Jamhuri ya Muungano, vitasimamia pia Serikali ya Tanganyika”.
Hii ni kwa sababu Zanzibar na Tanganyika zilibakia na Serikali zake zenye mamlaka kwa mambo yote yasiyo ya Muungano kwa kuongozwa na “sheria zake zilizopo kabla ya Muungano”, muhimu kati ya hizo kwa Tanganyika, ni Katiba ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano.
Ni kusema kwamba, Rais wa kwanza wa Muungano, Mwalimu Nyerere, alikuwa pia Rais wa Tanganyika kwa pamoja na kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, si Tume ya Katiba wala Bunge la Katiba lililoweza kuteuliwa au kuitishwa, kwani, Machi 18, 1965 (siku saba tu kabla ya kutimia miezi 12 ya nchi kupata Katiba yake), Bunge lilipitisha sheria namba 18 ya 1965 kuongeza (kuahirisha) muda wa kuteua tume na wa kuitisha Bunge la Katiba hadi kipindi kingine “mwafaka”.
Moja ya sababu za kuahirishwa kwa tume na kwa Bunge la Katiba, ni kutokana na waasisi wa Muungano huo kuanza kuwa na mitizamo tofauti hasi juu ya muundo na uendeshaji wa Muungano. Vitisho vya kuvunja Muungano vilianza kusikika, kama ambavyo wakati mmoja Karume alinukuliwa akisema: “Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua”.
Naye Mwalimu Nyerere, katika hali ya kuanza kukata tamaa, alinukuliwa na Gazeti la “The London Observer” la Aprili 20, 1968, akisema: “Kama umma wa watu wa Zanzibar, bila ya kulaghaiwa kutoka nje, na kwa sababu zao wenyewe, wataona kuwa Muungano huu hauwafai, na kwamba una athari kwa uhai wao, sitawashurutisha waendelee nao…Muungano utakoma pale nchi (mbili) wanachama zitakapojitoa”.
Bunge la Katiba laota mbawa
Lilikuwa ni sharti kuu la Mkataba wa Muungano kwamba, Katiba ya Muungano ipatikane ndani ya miezi 12 tangu siku ya Muungano. Utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa ibara ya 7 ya Mkataba, ni kwa Rais wa Muungano, kwa kukubaliana (sio kushauriana) na Makamu wa Rais, ambaye alikuwa pia Rais wa Zanzibar; (a) Kuteua tume ya kupendekeza Katiba, na (b) Kuitisha Bunge la Katiba lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar kwa idadi watakayokubaliana ili kupitia mapendekezo ya tume na kupitisha Katiba ya Muungano.
Huu ndio utaratibu usioepukika tunapotaka kupata Katiba halali ya Jamhuri ya Muungano; na ndio utaratibu sahihi uliowekwa kwenye sheria ya sasa ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011; nje ya hapo ni ubatili mtupu, kwa sababu Mkataba wa Muungano ni msingi mkuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kinachogomba hapa ni sheria hiyo ya Bunge kutaja idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba, mamlaka ambayo ni ya Rais pekee kwa njia ya Amri ya Rais (Presidential Decree) kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Muungano ya 1964.
Wadadisi wa mambo ya kisiasa wanaona kwamba, kama Karume angeendelea kutawala kwa miaka mingine mitano baada ya 1972, huenda Muungano huo ungefikia kikomo kwa namna ya kusikitisha.
Ni kwa sababu hii kwamba, kwa miaka 13 tangu mwaka 1964, Muungano uliendeshwa kwa Katiba ya Muda “mkweche” ya “funga kamba twende” hadi ilipopatikana Katiba ya Kudumu mwaka 1977, ambayo nayo hata hivyo, kwa namna ilivyopatikana, uhalali wake unahojika.
Inaendelea...
Toa maoni yako