Makala
Mchakato wa Katiba mpya
Ubabe uliozoeleka kutumika tena? V
Joseph Mihangwa
Toleo la 222
18 Jan 2012

KATIKA sehemu ya nne ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Serikali, chini ya Katiba ya Jamhuri ya 1962, ilivyokabiliwa na ukinzani kila mara kutokana na misuguano ya ndani (contradictions), na kuamua kubadili Katiba ili kuzima kwa nguvu ya kidikteta, uhuru na demokrasia nchini. Tuliona pia juu ya uamuzi wa NEC ya TANU usiohojika, wa kuanzisha mfumo wa chama kimoja mwaka 1963, na jinsi utekelezaji ulivyoahirishwa kwa muda kupisha mchakato wa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, na hivyo kuzaliwa kwa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika ya 1964.

Muungano huo ulifikiwa kwa kutiwa sahihi Mkataba (Treaty) uitwao “Hati ya Muungano” (Articles of Union), na kuridhiwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar, kuwa Sheria (Namba 22) ya 1964, ijulikanayo kama “Sheria ya Muungano”. Ifahamike kwamba, Sheria na Mkataba wa Muungano ni mihimili ya kikatiba inayodhibiti na kuongoza Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, kiasi kwamba Katiba yoyote haipati uhai bila pumzi ya Mkataba wa Muungano.

Katiba ya Muda ya Muungano ya 1965

Katiba ya 1965 ni ya nne tangu Uhuru. Tume ya kupendekeza Katiba, iliyoteuliwa na Rais mwaka 1963, ilikamilisha taarifa yake na kuwasilisha kwenye kikao cha pamoja cha NEC za TANU na ASP, Mei 3, 1965. Uamuzi wa NEC hizi mbili ndio uliozaa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano (Sheria Namba 43 ya 1965), iliyogeuza nchi kuwa ya chama kimoja cha siasa; TANU (Tanganyika) na ASP (Zanzibar) vilitanganzwa kuwa vyama pekee kwa nchi hizo.

Katiba hiyo (ibara 3 (3)) iliagiza kuwa shughuli zote za kisiasa (na za Serikali) nchini zitafanyika chini ya mamlaka ya chama pekee cha TANU.

Kuonesha kuanza kwa madaraka makubwa na ukuu wa chama dhidi ya Bunge na Serikali, Oktoba 30, 1965, Bunge lilijinyonga lenyewe kwa kupitisha sheria iliyojulikana kama “The National Executive Committee (Powers and Privileges Act,” Namba 49 ya 1965, ambapo chini ya sheria hiyo, NEC ilipewa uwezo wa kuhoji na kuita mashahidi, kuchukua ushahidi na kutolewa kwa nyaraka dhidi ya mtu yeyote aliyetuhumiwa kuingilia au kudhalilisha shughuli zozote za nchi, na uongozi wa Chama na Serikali.

Sheria hiyo iliweka adhabu kali kwa kutotii agizo au wito wa NEC, au kwa kukataa kuchunguzwa, au kukataa kujibu maswali na kwa kutoa taarifa au hati za uongo kwa lengo la kudanganya. Aidha, iliagizwa pia kuwa, wajumbe wa NEC wasio wabunge walipwe mishahara na marupurupu sawa na wabunge.

Haya yote hata hivyo, hayakuweza kumaliza ukinzani na misuguano ya kitabaka ndani ya Chama na Serikali. Kwa sababu hiyo, ili kukomesha “choko choko” dhidi ya watawala, NEC ya TANU, iliketi mjini Shinyanga, kuanzia 10 – 12 Machi 1975, na kuagiza chama kishike hatamu zote za uongozi wa nchi na Serikali (Party Supremacy). Kwa hiyo, Juni 3, 1975, Bunge lilipitisha sheria ya mabadiliko ya Katiba kukitangaza chama (TANU) kuwa juu ya vitu na mambo yote nchini, kisheria na kiutendaji.

Tafsiri ya mabadiliko hayo ni kwamba, Bunge halikupashwa kwenda kinyume na chama, na lilifanywa kuwa kamati ya chama. Kufutwa uanachama wa mbunge kulimaanisha kupoteza ubunge pia.

Kwa mfano, mwaka 1968, Mbunge wa Iringa Kusini, M. Choga, aliongoza kikundi cha wabunge bungeni, kutaka Serikali ieleze uhalali wa TANU kuwa juu ya Bunge; akawasilisha hoja ya kutaka kurekebishwa kwa ibara ya 6 (2) ya Katiba ili kulipa Bunge ukuu juu ya chama. Alishambulia pia sharti la wabunge kuwa wanachama wa TANU kwa kuwa hawachaguliwi wala kuongoza wana-TANU pekee. (Hansard Julai 22, 1968).

Mbunge wa Taifa, Wilfred Mwakitwange, yeye aliitaka Serikali ifafanue, kama ni TANU iliyoongoza Serikali au Serikali ndiyo iliyoongoza TANU. Alishambulia pia kuwepo kwa nafasi ya wabunge wa kuteuliwa: “Siamini lugha na dhana hii ya kuteuliwa, kwani huyo anayeteuliwa lazima afuate ya anayemteua. Kama walivyosema wahenga, amlipaye mpiga zumari ndiye huchagua wimbo, hivyo ndivyo ilivyo kwa wateuzi na wateuliwa”. (Hansard, Julai 12, 1968).

Jambo hili halikuvumiliwa na NEC ya TANU. Katika kikao chake mjini Tanga, Oktoba 15, 1968, NEC iliwafukuza uanachama Chogga na wabunge wenzake sita kwa “kukiuka maadili ya chama, kwa mtazamo, kwa vitendo na kwa kuonyesha upinzani dhahiri kwa chama, siasa na sera zake” (Msekwa: Towards Party Supremacy, uk 48).

Waliofukuzwa uanachama na kupoteza ubunge walikuwa ni G. Kaneno (Karagwe), T. Bakampenja (Ihangiro); J. Kasella – Bantu (Nzega Mashariki); W. Mwakitwange (Taifa) na S. Kibuga (Mufindi).

Wengine walikuwa ni Oscar Kambona (Morogoro Mashariki na alikuwa Waziri pia) na Elly Anangisye (Rungwe Kaskazini na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa TANU wa zamani – TYL). Hawa walifukuzwa kwa “kutokuwa waumini wa TANU na itikadi yake ya Ujamaa”.

Mchakato wa Katiba ulikiuka taratibu

Nimeeleza mwanzo, kwamba kwa mujibu wa ibara ya saba ya Mkataba wa Muungano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilipashwa kupatikana ndani ya miezi 12 kwa Rais kuitisha Bunge la Katiba. Kinyume chake, Serikali ilipeleka muswada bungeni na Bunge likapitisha sheria namba 18 ya 1965, ya kuongeza muda wa kuitisha Bunge hilo bila ridhaa wala makubaliano na Serikali ya Zanzibar.

Kupitishwa kwa sheria hiyo haikuwa tu ni kurekebisha Mkataba (Hati) wa Muungano kwa nguvu ya upande mmoja, bali pia Jamhuri ya Muungano haikuwa na uhalali, wala uwezo kisheria na kikatiba kubadili mkataba ulioizaa.

Tena, bila makubaliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha ibara ya 3 ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano, kuitangaza Jamhuri ya Muungano kuwa ya chama kimoja na kuingiza TANU (Chama pekee Tanganyika) ndani ya Katiba wakati ikifahamika wazi kuwa, vyama vya siasa havikuwa moja ya mambo 11 ya Muungano.

Kwa kufanya hivyo, Bunge la Jamhuri lilikuwa limeshinikiza na kupandikizwa kwa nguvu, utawala wa TANU juu ya Zanzibar, bila kujali kwamba nchi hiyo ilikuwa na chama chake cha ASP, licha pia ya kwamba, wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana, hazikukubaliana vyama vyao viwe na mamlaka kwa Jamhuri ya Muungano; bali zilikubaliana kutohusisha mambo ya vyama na Muungano.

Vivyo hivyo, suala la TANU kushika hatamu za uongozi wa nchi nzima kikatiba mwaka 1975, halikuwa na uhalali kisheria na kikatiba; huo ulikuwa ni ukiukaji na uvunjaji mkubwa wa Mkataba na wa Sheria ya Muungano ya 1964.

Kwa kifupi, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilivuka uwezo wake wa kisheria, na kikatiba, licha ya kwamba halikuwa na uhalali wa kutunga sheria kufanya TANU kuwa na mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano; au kutunga sheria juu ya TANU. Kwa mantiki hii, sheria hizo, Katiba na mabadiliko hayo vilikuwa batili na haramu.

Ni mambo haya, pamoja na mengine, yaliyomsukuma Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Mapinduzi Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, kuandaa Hati mwaka 1984, kwa lengo la kuwasilisha Mahakama Kuu, kutaka ufafanuzi juu ya muundo sahihi wa Muungano, na kwa mambo yaliyojiri na yaliyoonekana kukiuka Mkataba (Articles) na Sheria ya Muungano.

Rais Jumbe alitumia haki yake hiyo ya kikatiba kwa kuongozwa na ibara ya 125 ya Katiba ya Muungano, inayoelezea kazi pekee ya Mahakama Maalumu ya Katiba, kwamba; “….ni kusikiliza shauri lililotolewa mbele yake, kutoa uamuzi wa usuluhishi, juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”.

Hati hiyo ilipotea katika mazingira ya kutatanisha na kuibukia mikononi mwa Rais na Mwenyekiti wa chama (CCM), Mwalimu Julius Nyerere. Haraka haraka, NEC ikaitishwa, na hali ya “kuchafuka kwa hewa ya kisiasa Zanzibar” (na kwa CCM), ikatangazwa kwa sababu tu ya Jumbe kuthubutu kutua mahali (patakatifu) ambapo “malaika” hawathubutu kutua.

Jumbe aliwekwa kiti-moto mjini Dodoma kwa “kuhoji mamlaka ya chama” na kwa “kudhalilisha Muungano”. Mwishowe alivuliwa uanachama na kupoteza nafasi zote za kiserikali na za chama, kwa maana ya urais wa Zanzibar, umakamu wa Rais wa Muungano na umakamu mwenyekiti wa CCM taifa. Kwa kipindi fulani, Jumbe alikuwa chini ya ulinzi nyumbani kwake Mji Mwema, Jijini Dar es Salaam.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar aliyeandaa Hati ya mashitaka hayo, Al Haj Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana aliyeitwa na Jumbe kuja kushika wadhifa huo baada ya kumrejesha Bara aliyekuwa Mwanasheria Mkuu visiwani humo, Jaji Damian Lubuva (Sasa Mwenyekiti, Tume ya Uchaguzi), alifukuzwa na kurejeshwa kwao Ghana.

Nilishiriki kwa njia moja au nyingine, mimi na wenzangu kutoka Bara, kwenye zoezi la kusafisha hali ya hewa ya kisiasa iliyochafuka visiwani. Moja ya maswali magumu yaliyotupa wakati mugumu tulipotembelea taasisi muhimu visiwani kuelezea yaliyotokea na ilivyotokea (na Muhammed Seif Khatibu ni shahidi), ni hili: “Je, Chama cha Mapinduzi, ambacho si moja ya mambo ya Muungano, kina uwezo na mamlaka gani kumteka nyara nchini Tanganyika, Rais wa (nchi ya) Zanzibar, ambaye amechaguliwa na kuongoza nchi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar?”

Kwa kuzingatia ukweli kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, huwezi kujibu kwa usahihi kwa ilivyotokea.

Uhalali wa Katiba ya 1965

Uhalali wa Katiba ya Muungano ya 1965 unahojika. Tunafahamu, kama tulivyoona mwanzo, kwamba Katiba ya nchi hutungwa na Bunge maalumu la Katiba ambalo baada ya kukamilisha kazi yake, hufa.

Katiba ya 1965 haikutungwa na Bunge kama hilo, wala haikutungwa chini ya utaratibu batili uliozoeleka, wa Bunge la kawaida kujigeuza kuwa Bunge la Katiba. Kinyume cha yote haya, safari hii Katiba (ya 1965) ilitungwa na Bunge la kawaida, kama sheria ya kawaida ya Bunge, ambalo mamlaka yake yanaishia kufanyia Katiba hai marekebisho madogo madogo tu, kama nilivyoeleza mwanzo.

Ni kusema kwamba, sheria hii ya Bunge iliyoitwa “Katiba ya 1965”, yalikuwa ni marekebisho tu ya Katiba, yaliyofuta Katiba na kuweka Katiba mpya mahali pake.

Katiba ya 1965, ilisimama juu ya mafiga matatu: Kwanza, ni Rais beberu asiyeambilika (imperial Presidency); pili, Muungano wenye Serikali mbili; na mwisho, nchi ya chama kimoja.

Pamoja na kwamba wananchi hawakushirikishwa katika kutunga Katiba hii, ubabe uliohifadhi Katiba hiyo uliua nguvu ya Bunge na kutia hofu demokrasia, kwa maana ya demokrasia ya uwakilishi; na kufanya wabunge waonekane mazezeta.

Kwa mfano, mwaka 1966 badala ya kuwasemea wananchi kwa ushapavu na kujiamini, mbunge mmoja alipoteza muda wa Bunge akitaka maelezo kwa nini askari hawawapigii saluti wabunge!

Mwingine, mwaka 1968 alitumia dakika 20 akijenga hoja kwamba wabunge waheshimiwe kwa njia ya mitaa mipya kupewa majina yao! (The African Review, Vol. 2, No 3, 1972 uk 365).

Mafiga haya matatu ya Katiba ya 1965, yaliimarishwa zaidi katika Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977; hasa kufuatia kuungana kwa TANU na ASP, kuunda CCM.

Hata hivyo, utata unajitokeza juu ya uhalali wa Katiba hiyo ya kudumu, kuhusiana na jinsi na namna ilivyotungwa. Je, ilizingatia matakwa ya Mkataba na ya Sheria ya Muungano? Je, rasimu ya Katiba hiyo ilijadiliwa na wananchi?

Je, ni sahihi kwa Katiba (mpya) inayotarajiwa, kumea na kukua juu ya majivu ya Katiba ya 1977 inayohojika?

Inaendelea...

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Joseph Mihangwa
jmihangwa@yahoo.com
+255-713526972

Toa maoni yako