SAYANSI bila dini ni ulemavu. Dini bila sayansi ni upofu
Ubabe uliozoeleka kutumika tena? VI
KATIKA sehemu ya tano ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Katiba ya Muungano ya muda ya 1965 ilivyotungwa bila kushirikisha wananchi na kuzaa udikteta kiutawala; na jinsi ilivyoingiza baadaye imla ya utawala wa chama kimoja kinyume cha matakwa ya Mkataba wa Muungano.
Ubatili na udikteta wa Katiba hii ulirithiwa mzima mzima na Katiba ya kudumu ya 1977, ambayo kwa kuzingatia mchakato wa sasa wa Katiba mpya, kunatarajiwa kumea na kukua kwa Katiba mpya juu ya majivu yake. Je, ni sahihi kwa Katiba yenye uhalali unaohojika kuwa msingi wa Katiba mpya? Tuone majibu katika sehemu hii ya sita na ya mwisho.
Uhalali wa Katiba ya 1977 unahojika
Katiba makini ni ile inayotokana na ushiriki wa wananchi katika kutungwa kwake; kinyume chake ni Katiba ya kibabe ambayo uhalali wake unahojika. Katiba zetu zote tangu uhuru hadi hii ya sasa, zimo katika kundi hili.
Katiba ya 1977 ilitungwa na kusimikwa juu ya mafiga matatu ya kurithi kutoka Katiba ya 1965 ambayo ni: kwanza, ni Rais beberu, asiyeambilika (imperial presidency); pili, ni Muungano wenye Serikali mbili; na tatu, ni Serikali ya chama kimoja. Kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992 na marekebisho yaliyofuata, hakujaondoa harufu ya mafiga hayo, licha ya kupakwa manukato lukuki.
Kuhojika kwa uhalali wa Katiba hii unatokana na namna ya kutungwa kwake, kulikotanguliwa na Kamati ya watu 20 wa vyama vya TANU na ASP, iliyoteuliwa kuandaa mapendekezo ya kuunganishwa kwa vyama hivyo.
Baada ya kukamilisha kazi hiyo na vyama hivyo kuungana na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM), tume hiyo iligeuzwa (kwa utashi wa chama) kuwa tume ya kupendekeza Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano, ilimradi ionekane kwamba ni tume inayotajwa kwenye ibara ya 7 (a) ya Mkataba wa Muungano, wakati ilikuwa ni kinyume chake.
Nimeeleza huko nyuma kwamba, vyama vya siasa havikuwa moja ya mambo 11 ya Muungano; kwa hiyo mwenyekiti wa chama, wala NEC ya CCM, hawakuwa na mamlaka ya kuteua tume (ya chama) ya kupendekeza Katiba ya Muungano kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Muungano. Hapo ndipo ubatili unapoanzia.
Tume hiyo ya chama ilipeleka mapendekezo yake kwenye Halmashauri Kuu (NEC) ya chama ambayo iliyaridhia kwenye Kikao cha siri (in camera). Ikumbukwe kwamba, siku tume ya Katiba ilipoteuliwa, ndiyo siku hiyo hiyo Bunge la Katiba (Constituent Assembly) lilipoteuliwa, ambalo wanachama wake walikuwa ni wabunge wote wa Bunge la Muungano. Tofauti na inavyokusudiwa katika mchakato wa sasa, ambapo wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kutoka Zanzibar watashiriki, wajumbe wa Baraza la Mapinduzi (wakati huo) hawakushiriki.
Ni kusema kwamba, safari hii, Zanzibar italeta washiriki wa aina tatu: kwanza, ni wale wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Zanzibar; pili, ni wajumbe wote wa Baraza (Bunge) la Wawakilishi; na tatu, wengineo wanaoweza kuteuliwa na Rais kuwa wajumbe.
Iliichukua NEC ya CCM saa tatu tu kuridhia mapendekezo ya tume, na muda huo ulitumika kwa sehemu kubwa kusifia mapendekezo hayo. Mapendekezo ya tume/NEC yaliwasilishwa na kujadiliwa kwa saa mbili tu na Bunge la Katiba, Aprili 25, 1977 na kupitishwa siku hiyo hiyo kuwa sheria, na kufumba na kufumbua, mapendekezo hayo yakawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano sawia.
Mpaka hapo ni dhahiri, kwamba licha ya kukiukwa kwa matakwa ya Mkataba wa Muungano katika kutunga Katiba, Katiba ya 1977 haikuwa matokeo ya mjadala wala ushiriki wa wananchi, mambo ambayo ni muhimu kuweza kuhalalisha Katiba ya kidemokrasia.
Mihemko mipya ya Kikatiba
Kama ilivyotarajiwa, Katiba ya 1977 ambayo haikutokana na ridhaa ya wananchi, kwa kipindi chote kati ya miaka ya 1970 na 1980, ilizua mitafaruku, vilio na madai kutaka mabadiliko ya haraka. Madai ya wananchi yalikuwa ni pamoja na kutoa demokrasia zaidi kwenye mfumo wa Serikali; kuheshimiwa kwa utawala wa sheria na haki za binadamu pamoja na uhuru wa kujieleza.
Katika mjadala wa kitaifa wa Kikatiba mwaka 1983 dhidi ya Katiba ya 1977, yaliyojitokeza kwa upana zaidi ni pamoja na wito wa kurejeshwa kwa ukuu na mamlaka ya Bunge kama taasisi kuu inayodhibiti sera za taifa na Serikali; kuwa na wabunge wengi wa kuchaguliwa badala ya wabunge wa kuteuliwa; kuingizwa katika Katiba kipengele cha Haki za Binadamu (Bill of Rights) ili kulinda haki za wananchi za kushiriki kwa uhuru katika mambo ya nchi na uhuru wa kushirikiana na wengine bila kuingiliwa na Serikali.
Kilio kingine muhimu kilikuwa dhidi ya ukiritimba wa chama. Wananchi walitaka kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kutokana na ukuu wa chama (Party Supremacy) kubaka mamlaka ya wananchi ya kusimamia na kudhibiti masuala ya Kitaifa, katika nchi yenye watu milioni 18 wakati huo, dhidi ya wanachama milioni tatu tu wa CCM.
Kero za Muungano nazo zilikuwa hoja kubwa, ambapo wengi, hasa Wazanzibari, walitaka muundo sahihi wa Muungano uliokusudiwa ufahamike, pamoja na hofu ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika.
Hoja hii ya mwisho, kama nilivyokwishaeleza mwanzo, ilimgharimu Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, nafasi zote za kichama na kiserikali baada ya kutuhumiwa kuandaa madai kuiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri na ufafanuzi sahihi. Jumbe alihoji pia ukuu wa chama juu ya Muungano, ambapo chama kilikuwa si jambo la Muungano.
NEC ilipoketi Juni 1984, ilishughulikia machache tu kati ya mengi ya malalamiko ya umma. Ilikubali kupunguzwa kwa nusu ya wabunge wasiochaguliwa; ilikubali kuingizwa kwa haki za binadamu katika Katiba. Mengine yote yalitupiliwa mbali.
Kuingizwa kwa haki za binadamu kwenye Katiba kulifanyika shingo upande, maana haki hizo zilitolewa kwa mkono wa kulia na kunyakuliwa kwa mkono wa kushoto kwa njia inayojulikana kisheria kama “saving clauses/provisions”, ambapo vifungu vyote vilianza na maneno “Bila kuathiri……..”, kwa maana kwamba, kile kilichotajwa “bila kuathiriwa” (Sheria, matakwa ya ibara kadhaa kandamizi za Katiba) na ibara hizo za Katiba, zilikuwa juu ya haki za mwananchi.
Hiyo ndiyo Katiba yetu ya Kudumu ya 1977, iliyopendekezwa na kamati ya wanachama 20 wa CCM. Mapendekezo yakajadiliwa kwa siri na kuridhiwa na NEC ya CCM katika muda usiozidi saa tatu, yakawasilishwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria ndani ya saa mbili tu siku hiyo hiyo yaliyowasilishwa.
Katiba ya nchi ni ya wananchi wote na kwa ajili ya wananchi wote, wawe wanachama au si wanachama wa chama tawala au chama kingine chochote. Usiri na udharura uliotumika katika kutungwa kwa Katiba hiyo (kama ule usiri na udharura uliotumika kufikiwa kwa Muungano wa Tanzania), uliwanyima wananchi haki yao ya kiraia ya kujadili na kutoa maoni juu ya Katiba wanayoitaka. Huu ulikuwa ni ubabe wa aina fulani.
Kwa sababu hii pia, Katiba hiyo, badala ya kuleta amani ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini ilizua mitafaruku (na kuzidisha kero za Muungano) ambayo haikutarajiwa. Kwa kifupi, upungufu mwingi wa Katiba hii umesababisha madhara makubwa kisaikolojia kwa jamii ya Kitanzania kuliko Katiba nyingine yoyote tangu uhuru.
Ni kwa sababu hii pia, umma wa Kitanzania uliwashangaa na kuwaona kama wasaliti na adui wa umma Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, walipodai kwa pamoja mwaka jana kwamba hapakuwa na haja ya kuwa na Katiba mpya, bali iliyopo ifanyiwe marekebisho tu. Hata hivyo, wengi tulijua kwamba kilichowasumbua ni hofu juu ya usalama wa kitumbua chao, lakini tukasema walikuwa wanajaribu kuzuia mafuriko (ghadhabu ya umma) kwa viganja vya mikono. Kwa hilo, “wakati” umekuwa shahidi mzuri kwao na kwetu, kwani “wakati ukuta”.
Kombani na Werema washaurike kwamba misimamo yao hasi kwa maslahi ya wananchi na taifa ya kutaka kufurahisha tabaka fulani katika jamii inawapunguzia heshima kitaaluma na kijamii na kusema kweli, ipo siku moja wataitwa “maadui wa umma na wa haki za raia” hadharani. Hapo ndipo watajaribu bila mafanikio kutafuta shimo la kujificha kwa aibu ya kuwa “vikaragosi”, wasilipate.
Katiba makini inapatikanaje?
kama nilivyoeleza tangu mwanzo wa makala hii, Katiba ni mali ya wananchi na inapatikana kwa ushiriki wao kuanzia na aina na muundo wa Katiba wanayoitaka. Katiba si tunda la chama cha siasa, kikundi cha viongozi au cha watu wanaojiona wana akili zaidi kuliko wengine kuweza kuwa-amria wananchi Katiba wanayoitaka wao. Bila ushiriki wa wananchi, Katiba haiwezi kuitwa ya kidemokrasia na hivyo itakosa uhalali wa kijamii na kisiasa (Socio-political legitimacy).
Kwa maoni yangu, kuna njia mbili za kuweza kupata Katiba makini. Moja ni hii inayopigiwa chepuo na watawala kila mara, inayoanza na Kamati ya kupendekeza Katiba na kumalizika na Bunge maalumu la Katiba. Huu ni utaratibu unaotajwa kwenye Mkataba wa Muungano wa kupata Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Lakini kama tulivyoona mwanzo, utaratibu huo umekosa uwazi, ukweli na uadilifu; umetumika vibaya na kupatikana kila mara Katiba za kitabaka, zenye kulinda maslahi ya kichama au kundi lenye nguvu katika jamii, badala ya kulinda matakwa na maslahi ya wananchi wote.
Ni kwa sababu hii, Katiba zilizopatikana kwa njia hii zilizua mitafaruku mikubwa zaidi kuliko mwanzo na kulazimika, ama kufanyiwa marekebisho haraka au kuandikwa Katiba nyingine, lakini kwa lengo, si la kukidhi matakwa ya kikatiba ya wananchi, bali kudhibiti hali kwa (kubana demokrasia na kujilinda) manufaa ya tabaka la watawala madarakani. Madhumuni ya Sheria ya Katiba ya 2011 na mchakato mzima wa kupata Katiba mpya wa sasa, umeingia katika mtego huu.
Utaratibu wa pili na ambao mimi naona ni bora zaidi, ni ule wa ngazi nne, kwa kuanza na mkutano wa kitaifa wa Katiba (National Convention) na kufuatiwa na Kamati ya Katiba (Constitutional Commission), Bunge la Katiba (Constutional Assembly) na kumalizika kwa kura ya maoni (Referendum).
Mkutano wa kitaifa wa Katiba, ni jumuiko la wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii katika nchi, ambalo kazi yake pekee ni kujadili na kuweka misingi ya jumla itakayoongoza na kuunda misingi ya kisiasa na kikatiba kwa mazingira yaliyopo.
Jumuiko hili linaweza kujumuisha wajumbe kama vile kutoka vyama vya siasa, taasisi na vikundi vya hiari, wanafunzi, vijana, vikundi vya kina mama, wanataaluma, wakulima na wafanyakazi, wafanyabiashara, viongozi wa dini na hata watu binafsi mashuhuri.
Lengo ni kupata sampuli mbalimbali za mawazo, maoni na matakwa tofauti katika jamii ili hatimaye yaweze kutumika katika kujenga msingi wa kuandikwa kwa Katiba mpya. Ifahamike hapa kwamba, kazi ya mkutano huu si kuandika rasimu (draft) wala kupokea na kuridhia Katiba mpya.
Mara misingi itakapofahamika vyema, inakuwa ndio mwongozo kwa Kamati ya Wataalamu au Kamati ya Katiba kuandaa rasimu ya Katiba inayotarajiwa. Wakati mwingine, mkutano huu wa kitaifa unaweza kuchagua pia wajumbe wa Kamati ya Katiba.
Rasimu ya Katiba ikikamilika, itasambazwa kwa wananchi ili iweze kujadiliwa kwenye vituo, mikutano, makongamano na majukwaa mbalimbali na kwa mawazo chanya kuzingatiwa.
Hatua ya nne ni uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba. Hapa, patahitajika kutungwa sheria itakayoongoza uchaguzi huo na kuonyesha pia mamlaka ya Bunge hilo. Uchaguzi usiwe kwa misingi ya vyama vya siasa, bali kwa msingi wa “universal suffrage” kutoka sehemu zote mbili za Muungano. Ni dhambi kuu kuwafanya wabunge wote wa sehemu hizi za Muungano kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba kwa kuwa “uchama” utajitokeza na kutawala mchakato mzima dhahiri. (Angalia athari zake, sehemu ya kwanza ya makala haya).
Bunge la Katiba litajadili na kupitisha rasimu hiyo ya Katiba, lakini halitakuwa na uwezo au mamlaka ya kutunga Katiba. Rasimu iliyopitishwa na Bunge hilo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni kwa mtindo wa “NDIYO” au “HAPANA”.
“NDIYO” zitakapokuwa nyingi, itamaanisha imekubaliwa na wananchi, na kwa njia hiyo itahesabika Katiba imetungwa na kupewa nguvu ya kisheria.
Kwa njia hii, Katiba mpya itaweza kutafsiriwa kumaanisha kupata nguvu ya kisheria kutoka kwa wananchi; itakuwa na uhai wa kisheria na uhalali wa kisiasa (political legitimacy) unaotokana na watu. Kwa jinsi hii, kwa historia ya Katiba ya nchi yetu, tutakuwa tumefanya mapinduzi makubwa kwa kupiga teke ukale wa kikoloni, na ubabe uliozoeleka katika kupata Katiba zilizoshindwa kukidhi matakwa ya wananchi katika jamii inayobadilika haraka.
Waziri Celina Kombani amesema, tena kwa kauli za manyanyaso dhidi ya wale wote waliohoji mambo kadhaa juu ya Muswada wa Katiba mpya. Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema naye amenena, tena kwa maneno makali na vitisho vya faini kubwa na kifungo kwa wale wote watakaojaribu kuhoji mantiki ya Sheria ya Katiba ya 2011; kana kwamba yeye pekee ndiye mwenye hatimilki ya mawazo ya kidemokrasia ya nchi hii. Ndiyo, wao wamekwishasema; sasa ni zamu ya wananchi wenye nchi kusema, licha ya vitisho vya faini kubwa na kifungo.
Add new comment