Makala
Ubunge wa EAC na mgawo wa rushwa
Ncheme Nchicheme?
Toleo la 234
11 Apr 2012

HAKIKA, katika miaka ya hivi karibuni juhudi kubwa zimefanyika miongoni mwa viongozi kuhakikisha nyadhifa walizonazo zinageuka au kugeuzwa kuwa ‘vitega uchumi’ binafsi.

Wenyewe ndiyo wamejitengenezea utaratibu wa kujimegea fungu kubwa la fedha kwa njia mbalimbali zikiwamo za posho. Utaratibu ambao wameuhalalisha kwa kutumia lugha inayozima mawazo kinzani ya wananchi wengi kuhoji zaidi,  lugha ya “kwa mujibu wa sheria.”

Ndiyo, tumesikia mara kadhaa kwa mfano, kiongozi fulani wa Bunge anatetea maslahi akisema ni kwa mujibu wa sheria. Yaani, ni kwa mujibu wa sheria na mjadala unafungwa.

Wanafunga mjadala bila kusikiliza wananchi wasioridhika na hali hii ya majibu yote kuwa ya kwa mujibu wa sheria. Watu mtaani wanataka isiwe kwa mujibu wa sheria bali iwe kwa mujibu wa hali halisi ya uchumi.

Aah! lakini wao ndiyo wenye kushikilia mpini  na akina – yakhe wameshikilia makali ya upanga, pengine kuna siku hata kama hawapendi watalazimika kuzingatia maslahi yao kwa mujibu wa nguvu ya uchumi na si kwa mujibu wa sheria.

Lugha ya “kwa mujibu wa sheria ni nzuri” lakini tatizo la sasa ni wao (viongozi) kutumia lugha hiyo pale tu inapohifadhi maslahi yao.

Yaani, hii “kwa mujibu wa sheria” inatamkika vinywani mwao pindi wanapopigania kwa mfano, nyongeza ya maslahi yao. Mbona miongoni mwao wanapeana rushwa lakini mara kadhaa hawapelekani kortini kwa mujibu wa sheria?

Inapojitokeza lugha ya “kwa mujibu wa sheria” inawabana kwa namna nyingine yoyote ile ili wasiendelee kufaidika na nyadhifa zao (ambazo wamezigeuza kuwa vitega uchumi), hapo watakaa kimya. Ni kimya tupu, kama si wao wale waliokuwa wakitetea lugha ya “kwa mujibu wa sheria.”

Naam! kama si wote, basi wengi wetu tunajua kuhusu mchakato unaoendelea wa kuchagua wabunge wa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki.

Kimsingi, uwakilishi wa namna yoyote kuhusu nchi katika nchi nyingine au jumuiya za kimataifa, si jambo la mchezo. Ni jambo linalopaswa kufanywa kwa kuzingatia nguvu za kisheria ndani ya wigo wa umakini wa hali ya juu.

Kiutaratibu, kupata wagombea wa ubunge wa Afrika Mashariki, kunaanzia katika vyama. Tumesikia kwenye CCM kazi imefanyika, lakini dosari zikidaiwa kujitokeza.

Ndani ya CCM tumesikia kuwapo kwa ushirikiano mkubwa kati ya baadhi ya viongozi na baadhi ya wagombea katika kutenda kosa la “kutoa na kupokea rushwa.”

Wapo viongozi wa CCM, miongoni mwao ni wajumbe wa Kamati Kuu wanaodaiwa kuhongwa na baadhi ya wagombea, ambao baada ya kuhonga, baadhi wameshinda na wengine kushindwa.

Lakini pia wapo watu safi, wagombea wasio na doa, wameomba ridhaa na wakapewa na Kamati Kuu ya CCM bila kutumia rushwa. Bila shaka, hawa ndiyo wale wanaoijua CCM.

Kwa bahati mbaya, kasi ya kuhonga imeendelea miongoni mwa wabunge ambao ndiyo wapiga kura kupata wabunge wa Afrika Mashariki.

Tumesikia kwa mfano, madai kwamba kiwango cha juu cha kuhonga kimefikia Sh. milioni moja (kwa mpiga kura) na kiwango cha chini ni laki tano.

Tunarudi kule kule kwamba, viongozi wetu wanapenda kupigania au kusimamia sheria pale inapotetea maslahi yao wakitumia lugha ya “kwa mujibu wa sheria.”  Lakini wenzetu hao hawatetei sheria inapopinga rushwa kwa sababu sheria hiyo inapambana na dhamira yao ya kugeuza vyeo kuwa vitega uchumi binafsi.

Tahadhari ni kwamba, kama baadhi ya wabunge watachagua wagombea waliotoa rushwa ili kushinda, basi wagombea hao watakwenda kutafuta namna ya kurejesha fedha walizowahonga wabunge, ili kufidia pengo la kipato lililojitokeza wakati wakinunua huo ubunge.

Namna mojawapo ya kuziba pengo la fedha za rushwa alizotoa mgombea ni pamoja na kutotetea maslahi ya nchi hasa anapojitokeza mtu wa kuwahonga ndani ya vikao vya Bunge la Afrika Mashariki.

Endapo kwa mfano, Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda watachagua wabunge wao bila rushwa kutumika, maana yake ni Tanzania pekee ndiyo itakayokuwa imepeleka (baadhi) watoa rushwa kwenda kuiwakilisha. Bila shaka, hao hawataweza kutetea nchi bali watakuwa tayari kutetea akaunti zao za benki zijae fedha kwa njia yoyote ile.

Kwa sababu madai ya baadhi ya wabunge kuhongwa na baadhi ya wagombea kuhonga wabunge bado yapo, basi, tunashauri wabunge kuwakataa waliowahonga au wanaohonga rushwa hata kama wamepewa mgawo.

Kura ni siri, tusichague waliotuhonga na hiyo maana yake ni kwamba, ukifanya hivyo utakuwa umekataa kuendeleza mfumo wa rushwa kununua uongozi.

Ikumbukwe kuwa, kupokea rushwa na kutekeleza kama anavyotaka aliyekuhonga, maana yake ipo siku nawe utalazimika kuhonga ili ushinde kwa sababu utakuwa umehusika kuridhia mfumo wa rushwa katika uongozi.

Ewe mbunge, kataa mfumo huo ambao unaangamiza nchi.  Rushwa ni adui wa haki, rushwa inakatazwa kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa imechelewa kuwadhibiti wagombea watoa rushwa, basi, Bunge lisimamie sheria kwa vitendo kwa kuwakataa watoa rushwa. Wakati ni huu, wabunge waonyeshe mfano wa kusimamia sheria wanazotunga.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako