Michezo
Ubunifu mavazi unapozidi kiwango cha kawaida…
Chesi Mpilipili
Toleo la 054
5 Nov 2008

NIMEPATA bahati ya kuhudhuria maonyesho mbali mbali ya wabunifu wetu wa mavazi nchini na nakiri kwamba mara kadhaa nimetoka ndani ya maonyesho hayo nikiwa sina uhakika wa nini hasa kilichokusudiwa na wabunifu na waandaji wa onyesho husika.

Imekuwa ni kawaida kwa wabunifu wetu wa mavazi nchini ambao ni wengi tu wa kutosha, kuandaa maonyesho ya mavazi, kila mmoja kwa wakati wake, kutuonyesha kipya walichobuni katika masuala ya mavazi.

Ubunifu wao huu hujumlisha mitindo mipya ya mavazi kutokana na nyakati maalumu kama vile mavazi kwa ajili ya majira ya baridi, ya joto, ya ofisini na ya kutokea jioni na pia kwa kutumia aina mbali mbali za vitambaa ikiwemo khanga, vitenge na batiki.

Tumewahi hata kuonyeshwa mitindo mipya ya mavazi iliyoshonwa kwa kutumia magome ya miti na majani kama walivyovaa mababu na mabibi zetu zamani . Ni ubunifu pia; kwani nani kasema ubunifu ni kuangalia mbele tu bila kujikumbusha ya nyuma?

Kwa hakika, wabunifu wetu wa mitindo ya mavazi wanajitahidi kadri ya uwezo wao kubuni mitindo ambayo inatufanya twende sambamba na wenzetu wengine duniani linapokuja suala la mavazi.

Ni bahati mbaya tu kwamba mpaka sasa wabunifu wetu wa mavazi nchini hawajaweza kubuni vazi ambalo tunaweza, wote kwa ujumla, tukakubaliana bila chembe ya mashaka kulitambua kama vazi la taifa.

Huwa sina neno na mingi ya mitindo mipya ya mavazi inayobuniwa na kuonyeshwa na wabunifu wetu kwa vile mara nyingi inaendana na mavazi ya kawaida tuliyozoea na kinachofanyika ni kupunguza ama kuongeza tu baadhi ya sehemu za vazi  lililozoeleka ili kulipa 'uhai' mpya.

Hata hivyo, kama nilivyosema mwanzo, mara kadhaa wabunifu wetu hubuni na kutuonyesha mitindo ya mavazi ambayo si tu watazamaji wanaishia kujiuliza mbunifu wa vazi hilo alikuwa anataka kutueleza nini kupitia ubunifu wake; bali pia ubunifu huo unakuwa kwenye hatari ya kuonekana kama kituko na mzaha zaidi kuliko kuwa ubunifu!

Tumepata kuonyeshwa vazi la ubunifu ambalo mwisho wake tumeishia kujiuliza kama ni vazi kweli ama ni matambara tambara tu yaliyofungwa fungwa pamoja, na hivyo kuwa ushahidi kamili wa jinsi baadhi ya wabunifu wetu walivyotoa uhuru kamili kwa ubongo wao wa 'kujiachia' utakavyo katika kugundua vivazi vipya!

Ni uhuru huu wa kujiachia unaofanya wabunifu wetu kubuni mavazi ambayo wale waumini wa dhana ya kuwepo kwa viumbe katika sayari nyingine hawapaswi kulaumiwa kwa kudhani kuwa ni mavazi watakayokuwa wamevaa viumbe hao pale watakapoonekana!

Ni kweli kwamba ubunifu haupaswi kuwa na mipaka, lakini kwa hakika kuna ubunifu mwingine ambao unamfanya mpenzi wa fani hiyo kudhani kuwa mbunifu alizidisha ubunifu na hivyo kusababisha ubunifu wake kuonekana kituko zaidi kuliko ubunifu.

Kwa kawaida, tunategemea kuwa baada ya wabunifu wetu kutuonyesha ubunifu wao kwenye maonyesho wanayoandaa, baada ya miezi miwili mitatu mavazi yenye ubunifu huo yanakuwa tayari yapo kwenye maduka ya mavazi nchini kwa ajili ya yeyote aliyependezwa nayo kuyanunua, na kwa maana hiyo kumpatia fedha mbunifu wake.

Hata hivyo, unapoangalia baadhi ya mavazi ya ubunifu tunayoonyeshwa unajikuta ukijiuliza kama mbunifu wake alikuwa kweli na maana ya kuliingiza sokoni vazi alilobuni na kutuonyesha.

Unajitahidi kujenga kichwani picha ya mama wa kawaida wa kitanzania akivaa vazi lile na kukatisha nalo mitaani, picha inakataa kabisa! Ataonekana kituko. Ndio picha halisi ya mavazi ya ubunifu ya wabunifu wetu yalivyo. Kumgeuza kituko mvaaji.

Mara nyingi tumepata kuonyeshwa vazi la ubunifu ambalo mwanamke wa kawaida wa kitanzania akilivaa hawezi kupanda nalo kwenye daladala maana akifanya hivyo atatoboa macho abiria wenzake kutokana na vazi hilo kuwa na 'ubunifu' wa kushonewa ncha kali kama miba ya Nungunungu!

Nakumbuka miaka kama mitatu hivi iliyopita, kwenye onyesho moja la mavazi, tulipata kuonyeshwa vazi la ubunifu lililokuwa na kitambaa kilichoshonwa kwa ufundi mkubwa na kufanana na shingo ndefu ya twiga kisha kushonwa upande wa mgongoni wa vazi hilo na kumfanya mvaaji aonekane kama ana vichwa viwili, cha binadamu na cha twiga!

Ulikuwa ni ubunifu wa kusisimua, lakini nimehudhuria sherehe kadhaa na kupita mabarabarani nikiangaza macho lakini sijafanikiwa kuuona tena ubunifu ule ukiwa umevaliwa na mwanamama wa kitanzania akikatisha mitaa na vichwa viwili, cha twiga na cha kwake!

Napata picha kwamba ubunifu ule wa kusisimua uliishia pale pale na usiku ule ule, na kwa maana hiyo kazi ile ambayo pengine ilimchukua mbunifu wake siku na hata miezi kadhaa kuiandaa, kupotea bure labda tu kama inavaliwa huko nchi za nje ambako wenzetu wako mbele kwa vivazi vya kiajabu ajabu!

Ni wazi kuwa mbunifu wa vazi lile alikuwa ameandaa vazi lake kwa ajili ya usiku ule tu na sio kwa ajili ya kulitangaza na kisha 'kulizalisha' kwa wingi zaidi ili Watanzania wenzake walinunue na kulivaa na yeye ajipatie kipato kutokana na jasho lake.

Na ndio maana ukiingia kwenye maduka mengi ya mavazi nchini utakuta yamejaa nguo kutoka China, Singapore, Uingereza na kwingineko na ni mara chache kabisa kukuta mavazi ya kitanzania tunayoonyeshwa kwenye maonyesho ya mavazi ukiachilia mbali wabunifu wetu wa mavazi wenye maduka ya kuuza nguo zao wenyewe kama Khadija Mwanamboka, Clemence Merinyo na wengineo.

Tunawapongeza wabunifu wetu kwa kazi zao mbali mbali wanazofanya na ambazo nyingine zimeanza kufahamika kimataifa. Hata hivyo, tunadhani kwamba wabunifu wetu wana changamoto kubwa ya kihakikisha kuwa ubunifu wao unawasaidia Watanzania kuwa na aina ya mavazi yanayoweza kuvaliwa wakati wote na sio mavazi ambayo faida yake ni kuonekana kwenye 'fashion shows' tu halafu basi!

Tuwaombe pia wanapobuni mitindo mipya ya mavazi wafanye hivyo wakiwa na mahitaji ya Mtanzania wa kawaida kichwani na sio kubuni tu mradi kubuni vazi ambalo pamoja kwamba litasisimua kwenye onyesho la mavazi, litakapovaliwa na mwananchi wetu wa kawaida litasababisha watoto kumfuata nyuma wakizomea kwa kutoelewa kilichovaliwa na mwananchi huyo!

Pamoja na hili, bado wabunifu wetu wa mavazi wanalazimika kuumiza vichwa vyao ili hatimaye kutupatia kile tunachoweza kukubaliana wote kuwa ni 'Vazi la Taifa'.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako