NINAIPENDA sana nchi ya Japan, kwanza kutokana na utengenezaji wake wa bidhaa imara mbalimbali zinazowafanya watengenezaji bidhaa wengine kuzipa majina bidhaa zao yanayofanana fanana na majina ya bidhaa za Japan ili kuzipa soko.
Ndio maana sisi tunaonunua bidhaa macho juu juu tunajikuta tukinunua redio na televisheni za Sonq tukidhani tumenunua Sony na Panasoanic tukidhani tumepata Panasonic. Ndio biashara huria hiyo!
Lakini zaidi ninaipenda mno Japan kutokana na utaratibu ambao raia wa nchi hiyo na vyama vyao vya siasa wamejiwekea katika masuala ya uongozi ambao hautoi nafasi kwa kiongozi anayeboronga kuendelea na kuboronga kwake.
Ni utaratibu ambao hufanya kiongozi aliyeko madarakani anapoboronga utashi wake mwenyewe humfanya ajiuzulu; hata kabla taratibu za chama chake kumuondoa hazijaanza.
Kwa utaratibu huu, katika kipindi cha miaka minne tu iliyopita Japan imejikuta ikiongozwa na mawaziri wakuu wanne akiwemo wa hivi karibuni Yukio Hatoyama ambaye ameongoza kwa miezi tisa tu na kulazimika kujiuzulu kwa vile tu alishindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni zake ya kuondoa kambi ya jeshi la Marekani iliyopo kisiwa cha Okinawa.
Hilo tu likatosha kumuondoa Mheshimiwa Hatoyama madarakani.
Hii ni tofauti sana na nchi zetu za Kiafrika ambapo wakati wa kampeni kiongozi anaweza akaahidi mamilioni lakini akatekeleza makumi kwa ‘kwa utaratibu tuliojiwekea’, na bado akapewa nafasi ya kinachoelezwa kuwa ni “kumalizia kutekeleza majukumu aliyojiwekea”!
Wakati utaratibu waliojiwekea raia wa visiwa vya Japan umevifanya visiwa hivyo kuwa vyenye nguvu kubwa za kiuchumi na teknolojia, utaratibu waliojiwekea raia na viongozi wa nchi zetu za Kiafrika unazidi kudidimiza nchi hizo kimaendeleo na kiuchumi.
Hivi karibuni, mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete alichukua na kurejesha fomu ya kugombea uraisi baada ya kukamilisha taratibu za udhamini. Anataka kugombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.
Kutokana na “utaratibu” ambao Chama cha Mapinduzi kimejiwekea wa kumuachia rais aliye madarakani kumalizia ngwe ya pili ya urais wake, Kikwete hategemewi kupata mpinzani kutoka ndani ya Chama kwa nafasi hiyo.
Hiyo ndiyo aina ya demokrasia ambayo chama tawala cha CCM kimejiwekea kwa kile kinachoelezwa kwamba ni kumpa nafasi rais aliyeko madarakani kumalizia kazi aliyoianza kwenye awamu ya kwanza ya uongozi wake.
Huko kwenye vyama vya upinzani hakuna afadhali katika hili. Tumeshashuhudia mara kadhaa mitafaruku inayotokea pale mwanachama anapojitokea na kutangaza nia ya kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama.
Kwa hakika, inashangaza kuviona vyama vya upinzani vikibeza Chama Cha Mapinduzi kuhusu utaratibu kilichojiwekea wakati huko kwenye vyao (kwa mfano CUF) kuna watu wamekuwa wagombea pekee wa nafasi ya urais kwa awamu ya tatu sasa ambayo ni jumla ya miaka kumi na tano!
Kuna maswali kadhaa tunayopaswa kujiuliza kuhusu utaratibu huu ambao, kwa kanuni ya maisha ya ‘kawaida ni kama Sheria’, sasa umekuwa kama sheria ama kifungu cha ziada cha katiba za vyama vyetu vya siasa.
Kwa vyovyote vile, waliojiwekea utaratibu huu wa ‘kumuachia raisi aliye madarakani kumalizia muhula wake wa pili’ watakataa, lakini ni lazima tukubali ukweli kwamba utaratibu huu ni sawa na kuisigina demokrasia na kuwageuza wananchi wetu kuwa ni misukule isiyokuwa na utashi.
Inapotokea Rais Jakaya Kikwete kuwa mgombea urais pekee kutoka chama tawala, je tuamini kwamba wanachama karibuni milioni nne wa chama hicho wote wanakubaliana na yale yote aliyoyafanya katika miaka yake mitano ya kwanza, na hivyo kuwa radhi awe mgombea pekee?
Tunapaswa kujiuliza; Ni kweli kwamba wanachama wapatao milioni nne wa chama kimoja wanaweza wote kwa pamoja na kwa wakati mmoja kuwa na mawazo ya aina mmoja kiasi cha kutokuwa na sababu ya kumbadilisha kiongozi aliyeko madarakani baada ya awamu yake ya kwanza ya uongozi?
Je, wanachama karibuni milioni nne wa Chama Cha Mapinduzi wote kwa pamoja wanakubaliana na kauli ya mwenyekiti wao kuwa hajui umasikini wa Watanzania unatokana na nini kama alivyopata kunukuliwa akisema akiwa katika moja ya safari zake nyingi nje ya nchi?
Ni kweli kwamba wanakubaliana na msimamo wa mwenyekiti wao wa chama ambaye ndiye raisi wa nchi kwamba serikali anayoiongoza inayoundwa na chama hicho haina uwezo wa kuongeza mishahara ya wafanyakazi, wakiwa ni pamoja na wanachama wa chama hicho, kwa miaka minane ijayo kama alivyopata kunukuliwa akiwaambia wazee wa CCM wa Dar es Salaam?
Je, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wanaamini kwa dhati kabisa kutoka mioyoni mwao kwamba serikali ya chama chao haina uwezo wa kuongeza mishahara ya wafanyakazi wake, wakiwemo wao wenyewe, kwa miaka nane ijayo lakini pamoja na hayo hawaoni sababu ya kumpa nafasi mwanachama mwingine anayeweza kuwa na mikakati mbadala ya kukabiliana na hali hiyo?
Lakini pia tunapaswa wote kwa umoja wetu kujiuliza bila ya unafiki wowote. Kama tokea Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alipong’atuka tumempa kila rais aliyefuata ngwe ya pili ya uongozi ‘ili kumalizia kazi aliyoanza awamu ya kwanza’, mbona basi maisha yetu yako pale pale kama sio yanazidi kudidimia?
Hizi kazi ‘wanazomalizia’ ni zipi zisizojionyesha katika hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida?
Kwa nini hatufiki mahali pa kuona kuwa ‘utaratibu wa kumuachia nafasi rais aliye madarakani kumalizia kazi alizoanza kwenye awamu ya kwanza’ hakujatusaidia kuondokana na matatizo yetu na wakati sasa umefika wa kuweka utaratibu mwingine wa ‘kuweza kumpigia kura ya kumuondoa madarakani wakati wowote kiongozi tunayeona ameshindwa kutekeleza malengo na sera za chama alizoombea kura?
Tumeshuhudia kwamba kile kinachoitwa ni “kuwapa viongozi nafasi ya kumalizia kazi waliyoianza awamu ya kwanza” kimeishia kuwa ni kile ambacho vijana wetu husema ni ‘kufungulia mbwa’; pale viongozi hao wanaposhika kasi kufungua makampuni ya biashara na kununua hisa katika kile kinachoonekana ni kujiweka sawa kwa ajili ya maisha ya ustaafu; mambo ambayo kiongozi mcha Mungu hapaswi kuyafanya kwa sababu tayari taifa limeshamhakikishia kumtunza kwa gharama kubwa hadi mwisho wa uhai wake!
Watanzania tuamke. Ni wazi kuwa huu utaratibu wa “kumuachia rais aliye madarakani ngwe ya pili kumalizia kazi aliyoanza ngwe ya kwanza” uliowekwa na watu wasiozidi milioni nne miongoni mwetu, haupo kwa maslahi ya Watanzania milioni 40.
Na hata katika hao milioni nne, ni wachache sana wanaofaidika nao. Wengine ni ‘bendera fuata upepo’ tu kama sisi wengine milioni 35 tunaondelea kupigika kila uchao licha ya maraisi wetu kupewa nafasi “kumalizia yale waliyoanza ngwe ya kwanza ya utawala wao”!
Itatuchukua muda mrefu kuifikia Japan kiuchumi na kiteknolojia, lakini tunaweza angalau tukajaribu kujenga aina ya utaratibu waliojiwekea wa viongozi wanaoboronga kujiondoa wenyewe madarakani; hata kabla raia hawajafanya hivyo. Hili halina gharama yoyote zaidi ya utashi tu.
Toa maoni yako