Makala
Uchaguzi wa Arumeru umetufundisha mengi
Ayub Rioba
Toleo la 233
4 Apr 2012

UCHAGUZI wa Arumeru Mashariki umemalizika salama na mshindi amepatikana. Wananchi wa jimbo lile wamesikiliza hotuba, ahadi, maneno matupu na hata kejeli na matusi na mwisho wamefanya uamuzi wao. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yenye viongozi wapya imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuwadhihirishia Watanzania kwamba ingependa waiamini.

Upo umuhimu wa kutoa pongezi. Kwanza kwa wananchi wa Arumeru kushiriki katika kuiimarisha demokrasia na kutumia haki yao ya kikatiba kumchagua mwakilishi wao waliyemuona anawafaa. Pili pongezi kwa Tume yenyewe kwa kutangaza matokeo bila kujenga mazingira kwamba kuna njama za kuchakachua matokeo.

Tatu ni pongezi kwa vyama vilivyoshindwa, kikiwamo chama tawala, kwa kushiriki na hata kukubali matokeo. Nne ni kwa waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje kwa kufuatilia mwenendo wa uchaguzi hadi mwisho. Tano ni kwa wana usalama waliofanya kazi kubwa kuhakikisha hali inakuwa ya usalama muda wote wa kampeni hadi siku ya uchaguzi. Na mwisho, lakini pia muhimu, ni kwa waandishi wa habari waliofanya kazi yao kitaaluma katika kufuatilia, kuchunguza na kuwahabarisha Watanzania kuhusu yaliyokuwa yakitokea katika kampeni na hata siku ya uchaguzi.

Ni dhahiri kwamba uchaguzi huu umetoa mafunzo kadhaa ambayo hatuna budi kujifunza. Na jambo la kwanza ni kwamba wananchi wameanza kuelewa, tofauti na propaganda za huko nyuma, kwamba kuchagua mtu wa chama cha upinzani si uhaini. Lakini pili ni dhahiri kwamba ile hofu ya kuamini kuwa kila uchaguzi ni lazima uchakachuliwe haina usahihi wa muda wote.

Tatu, imedhihirika kuwa wananchi wameanza kupima zile ahadi na kufuatilia utekelezaji wake na baadaye kutumia matokeo ya ahadi zile kufanya uamuzi. Kuna kila sababu ya kuamini kwamba wananchi wa Arumeru Mashariki hawakuridhika na jinsi CCM walivyotumia dhamana waliyopewa kuwawakilisha wananchi wale.

Nne, kama nilivyosema awali, katika makala yangu ya nyuma, iko haja ya kuangalia kama ni sahihi kwa chama kilicho madarakani kuendelea kumtumia rais mstaafu katika kampeni, na hasa ikizingatiwa kwamba kampeni zetu zinazidi kujaa hila, kejeli, matusi na hata kukashifiana na kuchafuana bila kujali staha inayoendana na utamaduni wa Kiafrika.

Lakini tano, wale wote waliokwenda katika kampeni kushindana katika kuzua, kukashifu, kutukana na kuchafua watu wengine, tena wasiogombea, wajiulize wamejifunza nini Arumeru Mashariki? Na endapo nitaazima msemo wa Jenerali Ulimwengu, ninaamini kwa vile wengine katika kampeni zile ilikuwa ni kama walivua akili zao na kuziacha pahala na kwenda katika kampeni wakiwa watupu basi huenda sasa watakumbuka walikoziacha ili wazipitie ziwasaidie katika kufikiri na mambo mengine ya kila siku.

Leo ningependa kudadisi jambo moja lenye somo muhimu katika chaguzi zetu na hasa nyakati za kampeni. Tumeshuhudia kwamba katika miaka ya hivi karibuni ushindani umekuwa ukiongezeka baina ya chama tawala na vyama mbadala. Na kadiri ushindani unavyozidi kuwa mkali ndivyo tunavyoona wanasiasa wakienenda kama vile siasa ni uadui. Na katika kudhihirisha kwamba wanasiasa wanaweza kuvuruga demokrasia yametokea matukio ya kusikitisha huko Mwanza kwa wabunge kushambuliwa.

Je wananchi wetu, wawe wa mijini au vijijini, wanayo matarajio gani kutoka kwa mwakilishi wao? Je ni kweli kwamba huwa wananchi wale wanakaa kusubiri ahadi walizotoa wanasiasa kuhusu maji, visima, zahanati, bei nzuri za bidhaa, barabara au daraja? Je, ni kweli kwamba wananchi wale huwa wanasahau kila baada ya miaka mitano kiasi kwamba wakidanganywa tena wao huamini uongo mpya?

Je, ni kweli kwamba yote yanayoahidiwa na wanasiasa yanakuwa yameshindikana kwa wananchi wenyewe na kwamba huwa hawawezi kabisa kutumia akili zao, nguvu zao na mikakati yao na kutatua baadhi ya matatizo yao huko huko waliko? Je, ni kweli kwamba wananchi wakichagua mbunge wa chama tawala wanakuwa katika nafasi nzuri kupelekewa maendeleo kuliko kama wakichagua mbunge wa vyama mbadala?

Inakuwaje basi kwamba baadhi ya sera zinazowaumiza wananchi leo hii zinakuwa zimepitishwa kutokana na wingi wa wabunge walio katika chama tawala? Kwa mara kadhaa kumekuwa na matukio ya wananchi kugombana na wawekezaji ambao ama wamechukua ardhi yao yenye rutuba bila kutoa fidia ya haki; au matukio yasiyoisha ya wananchi kuuawa migodini kutokana na wao kutafuta haki?

Je, licha ya uchache wao bungeni ni nani ambaye hajaona kazi kubwa iliyofanywa na baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani kwa maslahi ya taifa na wananchi wake?

Ipo haja ya kuanza kujadili namna bora ya kufanya kampeni za uchaguzi kwa kuheshimu misingi ya ushindani ya kutofautiana bila kukashifiana; ya kupingana kwa kuheshimiana; ya kukuza na kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana.

Lakini pili, ipo haja ya kubadili namna ya kutafuta ushindi katika uchaguzi kwa kuendekeza utamaduni wa kuwafanya wananchi kwamba wao hawana uwezo wowote na wanapaswa kukaa na kusubiri kupelekewa maendeleo na mbunge wao. Hii ni dhana potofu na hatari sana. Matokeo ya kujengeka kwa dhana hii ni tabia ya wabunge wengi tu tunayoiona ya kudai posho zaidi kwa maelezo kwamba wanakwenda kutatua matatizo ya wananchi wao.

Inawezekanaje mbunge badala ya kutumia mshahara au kipato chake kumwezesha kufanya utafiti, kununua vitabu vya kujisomea, mawasiliano, mikutano, na mambo kama hayo, akazitumie kutatua matatizo binafsi ya mwananchi mmoja mmoja? Kwani maana hasa ya uwakilishi kule bungeni ni ipi? Je, hivyo ndivyo tunavyoamini maendeleo ya wananchi wetu yatapatikana?

Matokeo ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki, na zinginezo wiki iliyopita,  yatoe funzo muhimu si tu kwa vyama vilivyoshiriki bali kwa Watanzania wote wanaoamini katika demokrasia ya maendeleo.  Kwamba inawezekana vipo vyama vinavyoamini kwamba kwa vile wananchi wengi huwa wana njaa basi vinaweza kutumia njaa ile katika kuhonga, kununua shahada au kutumia hila ili kushinda.

Tanzania tunayoishi leo imebadilika sana. Mawasiliano ya simu, kwa mfano, yameongeza kasi na wigo wa wananchi wengi, wakiwamo wa vijijini,  kujua ni nini kinachoendelea mijini ikiwamo makao makuu ya serikali. Wanafuatilia kwa karibu, wanajadili, wanapima na wanabadilika. Pili wapiga kura wengi leo na kesho ni vijana ambao hawana ukaribu mkubwa na historia ya nchi. Hawana emotional attachment na TANU wala uhuru.

Vijana wa sasa hivi wanatafuta namna ya kuboresha maisha yao na wanaamini nchi yao inazo rasilimali za kutosha. Wanaona zinavyotapanywa bila sababu huku wao wakiambiwa maisha bora hayatawafuata vijiweni – kitu ambacho ni kweli. Lakini kuwaambia vijana kwamba maisha bora hayatawafuata vijiweni kwa vile tu uchaguzi umepita ni kuwatukana matusi ya nguoni. Endapo kweli tungependa kujenga siasa zinazozingatia pia ukweli basi vijana wale wangelielezwa kule kule katika kampeni kwamba wasikae vijiweni kupiga soga bali watafute shughuli ya kufanya kwa sababu maisha bora huja kwa mtu kujituma na kujishughulisha.

Ya Arumeru Mashariki ni hatua nyingine katika ujenzi wa demokrasia na Watanzania wote bila kujali itikadi wanapaswa kutafakari na kujifunza kutokana na matokeo yale.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Dkt.
Ayub Rioba
ayubrioba@hotmail.com
+255-713250594

 

Dkt. Ayub Rioba ni mwanasafu wa muda mrefu wa Raia Mwema na ni mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Toa maoni yako