Uchumi wa dunia unalazimisha muungano wa Afrika

MIONGONI mwa mambo yanayolikwamisha Bara la Afrika kufikia maendeleo stahiki ni kukosekana kwa umoja.

Wiki iliyopita nilizungumzia dhana hii ndani ya nchi moja ya Kenya leo nataka niende mbele zaidi kati ya nchi na nchi.

Ninarejea kuchota uzoefu wa China ili kuiwasilisha mada hii kwa ukamilifu zaidi. Miongoni mwa mambo muhimu yaliyosaidia China kufikia hapo ilipo kwa sasa ni uwekezaji wenye malengo ya muda mrefu.

Kabla sijaendelea na hayo masuala mtambuka nianze kwanza na hili la umoja kwa sababu ndilo haswa kikwazo cha maendeleo mengine. Kuhusu umoja mazingira ya China yalikuwa tofauti kidogo tokea awali.

Ni kwamba taifa hilo lilikuwa katika mfumo wa ukabaila kikamilifu. Tawala za kifalme za Ming na Qing zilisambaa kwenye majimbo yote yanayounda leo taifa moja linaloitwa China.

Hata Wazungu walipofika China wakakuta utawala wa Qing ndiyo wenye nguvu basi wakaliita taifa zima China kwa sababu ‘Qi’ inatamkwa kama ‘chi’ kwa Wazungu ikawa ni rahisi kufupisha neno hilo kuwa ni China.

Uvamizi wa Japan mnamo mwaka 1931  ilikuwa ni kichocheo kingine cha kuunganisha nguvu za majimbo yote ambayo hadi wakati huo hayakuwa na umoja kamili kama ilivyo sasa.

Lakini uvamizi huo haukuwa mpya kwani awali kabla ya hapo taifa la Mongolia liliwahi kuvamia pia na lilikuwa tishio la kudumu hadi kujengwa kwa ule ukuta maarufu ambao leo ni kivutio kikubwa cha utalii yaani Ukuta Mkuu wa China.

Hata hivyo umoja halisi wa kitaifa unaanzia pale majeshi yaliyopambana na wavamizi kutoka Japan yalipogawanyika katika kambi mbili, kati ya yale yanayooongozwa na Mao Tse-tung na yale yanayoongozwa na serikali chini ya Chiang Kai-shek.

Tayari vita ya wenyewe kwa wenyewe ilikuwa imeanza kati ya makundi haya mawili tajwa isipokuwa uvamizi wa Japan ulisaidia tu katika kuonyesha nani ni zaidi katika mbinu za vita.

Kundi la Mao Tse-tung lilikuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba vijana wengi walikimbia majumbani mwao na kwenda kujiunga na kundi hilo katika vita. Baada ya kuyashinda majesi ya Japan tayari kiongozi mpya wa China akawa amefahamika naye ni Mao Tse-tung.

Baada ya vita hiyo jeshi lake lilifanya kazi ndogo sana ya kuyafyeka majeshi pingamizi, viongozi wengi wa majimbo huru wakaomba kujiunga na taifa hilo linaloitwa sasa Jamhuri ya Watu wa China na hatimaye Chiang Kai-shek na wafuasi wake wakakimbilia katika Jimbo la Taiwan na kulifanya kuwa nchi kamili hadi leo.

Baada ya hapo pingamzi lilitoka katika jimbo moja tu la Tibet ambalo kwa miaka kadhaa lilijiendesha kwa utaratibu tofauti na majimbo mengine. Wakati kwingineko tawala zenye mamlaka kamili zilikuwa ni falme, katika jimbo hili viongozi walikuwa wa Kibudha chini ya himaya ya Dalai Lama.

Kutokana na pingamizi hilo mwaka 1959 majeshi ya serikali ya China yalivamia katika jimbo hilo yakiwa na vifaru, malori  na zana nyinginezo za kijeshi na huo ndiyo ukawa ndiyo mwisho wa utawala wa Dalai Lama ambapo Dalai Lama wa 14 aliyepo hai hadi leo alikimbilia nchini India alikoweka makazi yake ya kudumu.

Mazingira ya Afrika ni tofauti kidogo lakini hayahalalishi kuukataa muungano ili kuunda serikali moja ya bara zima. Kimsingi wakati wa kuingia kwa ukoloni mataifa ya Afrika yalikutwa katika hatua tofauti tofauti, baadhi yakiwa yamefikia hatua inayoweza kuitwa ni ukabaila na mengine ujima.

Ukoloni ulikuja na mgawanyiko wake pia kuanzia mfumo wa elimu, lugha na utamaduni na pia hata mfumo wa utawala. Yote haya yana athari kubwa katika Afrika ya leo iliyogawanyika vipande vipande.

Wakoloni walitugawanya katika makundi makundi katika kile kilichoitwa taifa au nchi, lakini mgawanyiko huo haukuzingatia mambo mengi ambayo yamezingatiwa huko kwao Ulaya. Kwa mfano, mipaka imayakata katikati baadhi ya makundi ya kijamii, koo au makabila na yameangukia pande mbili za mipaka ya nchi.

Kwa Tanzania kuna Wamakonde, Wanyanja, Wamasai, Wajaluo n.k. Hata hivyo, upo mgawanyiko mwingine ambao ni wa rangi. Kuna Waafrika ambao ni Waarabu, na kuna wengine ambao ni machotara na wengine ni Wazungu kwa muonekano wao. Sasa ukizungumzia umoja wa Afrika hayo ni makandokando ambayo huwezi ya kuyadharau.

Bado kuna mgawanyiko wa Waafrika wanaozungumza Kingereza, Kifaransa na Kireno hizo nazo ni tofauti za kuzingatiwa. Tofauti zote hizi zimo kwenye kichwa cha Mwafrika wa leo.

Je, ufumbuzi wa kadhia hii ni upi? Hilo ndilo jambo la msingi kwa sasa. Kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wa bara hili wanapaza sauti zao bila kuchoka katika kudai umoja wa bara lao.

Hii ni kwa sababu imekwishakuthibitika kwamba viongozi wa Afrika kamwe hawawezi kuleta umoja huo. Kila mmoja anataka kuvaa viatu vya wakoloni, hakuna rais wa Afrika aliyetayari kugeuzwa na kuwa sawa na mkuu wa mkoa.

Kwa kiburi hicho cha viongozi wetu kukataa kuunda serikali moja ya bara zima ni vyema kuangalia gharama kubwa zinazotumika kuwatunza viongozi hao na kisha tunaweza kupiga mahesabu na kuona ni kwa kiwango gani gharama hizo zingepungua iwapo tungekuwa na rais mmoja.

Kwa mfano Wachina kwa ujumla wao wapo watu zaidi ya bilioni moja (1.382) na wana rais mmoja tu. Waafrika katika ujumla wetu tupo pia zaidi ya bilioni moja (1.216)  na tuna marais 54. Gharama hizo zinaenda mbele zaidi kwamba ukiweka na gharama za mabalozi wetu ndani na nje ya bara hili.

Na kwa mantiki hiyo hiyo tuna gharama kubwa sana za kuwatunza marais wastaafu na hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya marasi wa Afrika hupenda kuishi kama miungu watu toka wakiwa madarakani na hata pale wanapokuwa wamestaafu.

Iwapo tunataka kujikwamua ni muda muafaka sasa wananchi wa bara hili wakapaza sauti ili viongozi wetu wamuachie mmoja wao awe rais wa bara zima na kisha wengine wabakie na nyadhifa za ukuu wa mikoa au ukuu wa jimbo.

Kwa maana hiyo Tanzania itakuwa ni jimbo au mkoa mmoja ndani ya Serikali ya Afrika. Na kwa mantiki hiyo kutakuwa na balozi mmoja moja katika kila nchi nje ya bara hili ili wengine warejee nyumbani na kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.

Bila ukiritimba na uduni huo wa kifikra basi Afrika mpya na yenye nguvu itaibuka na itakuwa ni tishio kwa mataifa mengine duniani. Tayari Wachina wamekuwa wakisema kwamba Afrika katika ujumla wake ni bara tajiri kuliko taifa lao. Ama kweli usimwamshe aliyelala, kwani ukimuamsha utalala wewe!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *