Uchumi wa viwanda unapokuwa uchumi wa vimada laghai (2)

“KILA mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe” (Mithali 14:1).

Siku moja hivi karibuni, nikiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) nikisubiri kusafiri kutoka uwanja huo, nilipata nafasi ya kujadili na mmoja wa viongozi vijana “machachari” wateule wa Rais John Pombe Joseph Magufuli (JPM), kuhusu hali na mwelekeo wa siasa, uchumi na maendeleo nchini na kimataifa, na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuweka mzani sawa katika yote hayo.

Mara, kwa kujiamini kupita kiasi, kiongozi huyo kijana akageuka kunipa somo akisema: “Angalia kada (wa chama?) mwenzangu; ninyi wazee wasomi na viongozi wa zamani mnaojinasibu kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndiyo mliobomoa nchi kwa mikono yenu kufikia mahali tulipo”.

Tulikatisha mjadala baada ya kunena hayo kuitika tangazo la kututaka abiria tuanze kuelekea kwenye ndege na sijakutana naye tena kuendeleza mjadala huo.

Kauli ya kiongozi huyu iliniacha na maswali mengi kutaka kujua alimaanisha ni “wazee wasomi na viongozi wa zamani” wapi waliobomoa nchi na kwa vipi.  Nikajihoji, je, pengine hii ndiyo siri ya JPM kuteua vijana wengi kushika madaraka na kuwatupa kwenye jumba la makumbusho “wazoefu” wote?.

Kwa kutaja “JKT” nadhani alikuwa akimaanisha wazee waliohitimu elimu ya juu kati ya mwaka 1966 ilipofanywa kuwa lazima kwa kila msomi kupitia kwanza JKT kabla ya ajira, na utaratibu huo kuendelea hadi miaka ya mwisho ya 1980, pale sharti hilo lilipolegezwa.

Kama ni JKT, basi, awamu hiyo ya viongozi inajumuisha pia wale wa kabla ya 1966 kwa sababu amri ya 1966 iliwataka pia wasomi wote waliokuwa madarakani wakati huo, akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwenda JKT kupata “kipaimara” cha kutumikia taifa kwa uzalendo. Je, nao hao wamo katika orodha ya waliobomoa nchi?.  Haiwezekani, kwa sababu hao walijaa uzalendo usiohojika.

Nchi yetu na Afrika huru kwa ujumla, imeshuhudia vizazi vitatu vya viongozi kwa shinikizo la mazingira na la nyakati. Cha kwanza ni kile cha harakati za uhuru kuanzia miaka ya 1950 hadi miaka ya mwanzo ya 1960. Kizazi hiki kilijikita zaidi katika kudai/kupigania uhuru kwa kuongozwa na ule msemo mashuhuri wa Rais wa kwanza wa Ghana -nchi ya kwanza kupata uhuru barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Dk. Kwame Nkrumah, kwamba, “Utafuteni kwanza ufalme wa Kisiasa na mengine yote mtazidishiwa”; kwa maana kwamba bila uhuru hakuna maendeleo wala kitakachofanyika cha kuendeleza nchi.

Kizazi cha pili ni kile kufuatia uhuru (1960-1980) ambacho kilijikita zaidi (kilipaswa?) katika kuunganisha, kuimarisha na kulinda matunda ya uhuru kwa kuweka mipango na sera madhubuti za maendeleo kuhakikisha kwamba uhuru na maendeleo ya nchi havitekwi nyara na ubeberu wa kimataifa kwa njia ya ukoloni mamboleo, huku Nkrumah akitahadharisha kwa kurudia msemo wa V.I. Lenin kwamba “Ubeberu, ni hatua ya juu kabisa ya ubepari”.

Kizazi cha tatu cha viongozi ni cha “maendeleo”, Uhusiano wa Kimataifa, Sayansi na Teknolojia.  Kwa kizazi hiki, maendeleo maana yake ni “maendeleo ya vitu” badala ya “maendeleo ya watu” kwa kudhani kwamba vizazi viwili vya kwanza vilikwishatekeleza wajibu wake kwa mafanikio kufikia kuitwa “affluent society”, yaani jamii inayojitosheleza kwa mahitaji muhimu kwa binadamu wakati ni kinyume chake.

Na kwa umbumbumbu wake kuhusu harakati za ukombozi na uchungu wa kutawaliwa, kilishindwa kutambua maadui wa nchi  wa ndani nan je na mbinu zao.

Ni kizazi kilicho na mzio (allergy) kwa umasikini na masikini wa nchi kwa sababu kwa lugha yake ya utanashati wa kimataifa, umasikini ni matokeo ya kujitakia unaoweza kupigwa vita na kumalizwa kwa misaada kutoka nje, hasa  kutoka mataifa ya ukoloni mamboleo kwa masharti maalum (ya WB na IMF), yenye kukinzana na mahitaji halisi ya wananchi.

Hapa, watu wanachukuliwa kuwa mawakala na marubani wa mabadiliko badala ya kazi hiyo kufanywa na serikali. Kizazi hiki mateka kinataka serikali kujiondoa katika kupanga na kusimamia uchumi wa nchi, na kuchukulia sekta binafsi kama ndiyo treni ya maendeleo badala ya sekta ya umma.

Ni kizazi ambacho kwake, kinyume cha lahaja cha “Masikini” sio “tajiri” bali “Wafadhili”;  udadisi wake sio juu ya “namna masikini walivyofukarishwa na wanavyoendelea kufukarishwa”, bali ni kuhusu wananchi “wangapi ni masikini, masikini wa kati, masikini sana, na itachukua muda gani kuondoa umasikini kwa njia ya wafadhili?”.

Kama kiongozi kijana yule angekuwepo bado karibu nami, ningemuuliza: “kati ya vizazi vitatu hivi, ni kipi kilichobomoa nchi kwa mikono yake mithili ya mwanamke mpumbavu?”.

Na hili la JPM, la kuteua viongozi vijana ni jambo la kawaida kihistoria katika kuleta mageuzi, mradi tu vijana hao wawe na maono juu ya hatima ya nchi na minyororo ya “utumwa” inayoepukika. Hoja ni kwa kiasi gani wanazielewa mbinu za mkoloni mpya alizobuni kama chambo kwa jina la “usasa”, uhusiano wa kimataifa, sayansi na teknolojia kwa Injili ya Utandawazi, Soko Huria na minyororo mingine iliyoandaliwa na Mashirika ya Bretton Woods (WB, IMF, WTO)  tangu mwaka 1945 kwa nchi masikini kumeza ndoano na chambo?.

Tuna mifano mingi juu ya matumizi bora ya vijana katika uongozi:  Rais wa Marekani, John Fitzigerald Kennedy, baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo mwaka 1961, alizungumzia namna ya kuwaunganisha Wamarekani kwa kuwasikiliza vijana ili Marekani “isikilizwe” kote. Alitaka kuifanya Marekani isiwe ya kibaguzi na kuupa mchakato huo jina la “New Frontier” – Mpaka Mpya. 

Alitengeneza “Peace Corps”, taasisi iliyosimamiwa na kitengo cha “New Frontier” ambapo Wamarekani vijana walijitolea kufanya kazi ndani na nje kwenye nchi za dunia ya tatu katika nyanja za Udaktari, Ualimu, Ufundi, Miundombinu na Kilimo ambako walitumika pia kama majasusi wa Marekani.

Alikusanya vijana wenye akili na ujuzi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini humo kuwa washauri wake katika sera.  Wengi hawakuwahi kufanya kazi serikalini na alipenda wazo hilo akijua wana mawazo mapya kuweza kutatua matatizo ya zamani. 

Mmoja wa vijana hao waliopewa jina “Whiz-kids” au “Brain Trust”, alikuwa Robert MacNamara ambaye alifanywa Waziri wa Ulinzi katika kipindi hicho cha vita baridi duniani, na baadae akawa Rais wa Benki ya Dunia. Kennedy alipenda kuwaambia Wamarekani, “Usiulize nchi yako itakufanyia nini; uliza utafanya nini kuisaidia nchi yako”, kuthibitisha uzalendo kwa nchi.

Tofauti na Marekani ya 1961 iliyotaka utatuzi wa matatizo ya zamani kwa njia ya vijana, Afrika inataka utatuzi wa matatizo ya sasa (ukoloni mambo leo, utandawazi) ili kurejesha uhuru wa zamani unaoyoyoma ili mengine yote mema tuweze kuzidishiwa. 

Ni kwa kiasi gani “Whiz – kids” wetu wako tayari kupambana na mifumo angamizi ya uchumi chini ya ukoloni mpya na utandawazi kwa mbinu za ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo kwa pamoja wakati kwa mtizamo wao ni “mambo poa na shwari”, wakati ukweli “hamkani, si shwari tena?”.

Kuna mantiki katika usemi kwamba, “You have to look back in order to go forward”; kwamba ukitaka kusonga mbele kwa uhakika, lazima utizame nyuma kwanza. Kwa hili, “Whiz – kids” wetu bado watahitaji pia “busara ya kale” kwa sababu vita tuliyomo sasa ni ya historia kujirudia, tofauti na vita yoyote mpya. Yataka zaidi “kipaimara” cha JKT badala ya “kipaimara” cha soko huria na utandawazi unaoua.

Sasa tuangalie ilivyotokea, ilivyo na kama kizazi cha uongozi cha sasa kina maono, mapafu na utashi wa kusimika sera za uchumi na sekta madhubuti ya viwanda tuliyoibomoa kwa mikono yetu wenyewe.

Mwaka 1978, Rais, Mwalimu Nyerere alitembelewa na ujumbe kutoka IMF kumshawishi akubali nchi iridhie masharti ya IMF kama sehemu ya mkakati wa kufufua uchumi.  Masharti hayo ni pamoja na kupunguza thamani ya fedha na athari yake kwa uchumi wa nchi na jamii ni kuongezeka bei kwa bidhaa na huduma kwa mlaji na kwa vipuri kutoka nje na hivyo kuathiri sekta ya viwanda.

Pili, kupunguza matumizi ya serikali kwa kutoza malipo kwenye huduma za jamii kwa wote, kama vile tiba na elimu.  Athari yake ni pamoja na kupunguza watumishi (retrenchment) na kwa masikini kukosa huduma hizo muhimu.

Tatu, kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi kwao na kuruhusu kuhamishia nje faida na mitaji (capital flight) wanavyotaka bila kuingiliwa.

Nne, serikali kujiondoa katika kupanga, kushiriki au kusimamia uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuuza kwa sekta binafsi (kubinafsisha) mashirika yote ya umma, vikiwamo viwanda na mabenki kwa bei ya kutupa na kutokana na kupungua thamani kwa fedha ya nchi kwa shinikizo.

Tena, IMF ilikuwa inataka kuondolewa kwa ruzuku kwa bidhaa muhimu kwa mlaji (sembe, sukari, pembejeo) na kupandisha riba ya ukopaji kwenye mabenki yawe kwa wachache wenye ukwasi pekee; na masharti mengine.

Mwalimu aliwauliza IMF, nani kawatuma.  Wakasema, walikwishafanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Edwin Mtei ambaye aliona muhimu kwa nchi kukubali masharti hayo.  Kwa ghadhabu ya mlipuko, haraka Mwalimu aliwaonesha mlango wa kutokea nje bila kutazama nyuma akisema, hakuwa tayari kuona wananchi wake wakiumizwa kijinga, uchumi na uhuru wa nchi kuparanganyika kwa sera mumiani za IMF na WB. Siku hiyo, Mtei akapoteza nafasi yake ya uwaziri.

Kutetereka kwa uchumi kipindi hicho halikuwa tatizo la Tanzania pekee bali kwa nchi zote za dunia ya tatu kutokana na kwanza, nchi hizo kurubuniwa kukubali uchumi wake kuwa sehemu ya uchumi wa dunia; pili, uhusiano wa biashara usio wa haki kati ya nchi hizo na nchi za viwanda; tatu, mgogoro katika mfumo wa kibenki wa dunia; na mwisho, nchi za Magharibi kutokuwa tayari kuwekeza mitaji yake kwa maendeleo ya nchi changa ila tu inapokuwa kwa ajili ya kupora rasilimali za nchi hizo kuzifukarisha ziwe tegemezi.  Na hayo ndiyo madhumuni yaliyofichika ya IMF na WB.

Kuanzia mwaka 1980 – 85, Serikali ya awamu ya kwanza ilianzisha Programu kabambe ya Kitaifa ya Kunusuru Uchumi (National Economic Survival Programme) – NESP kwa kuongeza mauzo ya mazao ya kilimo nchi za nje, kujitosheleza kwa chakula, kuongeza uzalishaji wa Viwanda vyake.

Lakini Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilipoingia madarakani mwaka 1985, ilifutilia mbali NESP na kuanzisha mazungumzo na IMF, na mwaka 1986 ikatia saini mkataba kuipa IMF “ruksa” ya kuogelea na kuvuruga mipango ya uchumi ilivyotaka.

Ni Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Chimwaga, Dodoma mwaka 1992, uliopigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la sera za umma na sekta ya viwanda nchini, pale uliporidhia Sera mpya za Kijamii na Kiuchumi zenye kushabihiana na IMF kwa kuachana na Azimio la Arusha.

Mkutano ulipitisha Programu mpya ya kiuchumi dhidi ya NESP ambayo, kwa mujibu wa msomaji maazimio ya kikao hicho, ambaye pia alikuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, uliitaka serikali kujitoa, kutoingilia wala kuwa mshiriki katika uchumi wa nchi na badala yake iwe mwezeshaji, mwendelezaji na mratibu tu wa maendeleo ya uchumi.

Pili, kwamba serikali iingilie kati tu katika uchumi inapohusu umiliki na udhibiti wa mikakati ya shughuli za kiuchumi; na Tatu, kwamba, Ujamaa wa Kitanzania ujengwe kwa umiliki uchumi kupitia sekta binafsi na vyama vya ushirika bila kuingiliwa na serikali, tamko ambalo linakinzana na Azimio la pili hapo juu.

Kingunge Mwiru, gwiji la Usoshalisti nchini aliyebakizwa kama Waziri asiye na Wizara maalum kwa awamu tatu mfululizo baada ya Mwalimu ili kusimamia Ujamaa, alisema “Mageuzi” hayo yalihitaji CCM yenye uongozi wenye maono na uelewa wa mambo; na kwamba kulitakiwa uamuzi wa kijasiri kuzipitia upya Kanuni za Azimio la Arusha na aina ya Ujamaa ambao Chama na Serikali vilitakiwa kufuata.  Cha kushangaza ni kwamba, maazimio yote hayakuwa na Programu ya maendeleo ya Viwanda ila ubinafsishaji usiojali pekee.

Je, Kingunge Ngombale Mwiru hakujua kwamba alichotangaza kilikuwa kitanzi kwa uchumi wa viwanda na uhuru wa nchi?.  Ni msaliti gani huyo, “Yuda Iskariote”, kama si kimada laghai, “Delillah”, aliyeshirikishwa kuandaa kitanzi hicho kutumaliza?.

….Itaendelea..


jmihangwa@yahoo.com/0713-526972

One thought on “Uchumi wa viwanda unapokuwa uchumi wa vimada laghai (2)”

  1. idrissa says:

    Mihangwa, sjui miaka ya 1980 ulikuwa wapi. Kwa MTU aliyekuwa Dar anaelewa hali halisi ys ya wakati ule. Umesahau kwamba wiki takriban Tatu baada ya hutuba ya kigoma na kuondolewa mtei tulishusha thamani ya shilingi Mara mbili. Umesahau kwambs baada ya viys vys kagera viwsnda vilianza kufa kimoja baada ya kingine. Kufa huko kukazaa likizo bila malipo kwa wafanya kszi, halafu mgao wa bidha muhimu na maduka ya kaya-au tukuonyeshe kadi za za mgao. Hakukuwa na chochote madukani. Miundo mbinu iliporomoka Barbara zikabaki mashimo matupu. Naomba msiwadanganye vijana waambie ukweli. Ruksa ilianza na Mwalimu mwenyewe, baada ya hutuba ya kigoma na kumuondondoa mtei, tabriban miezi miwili baadaye tulishusha thamani ya shilingi zaidi Mara mbili. Mitumba ambayo inatajwa kama mojs ys sababu kufa kwa viwsnda iliruhusiwa tangu mwska 1984, kabla ya Mwl kung'atuka na Dr. Salim akiwa waziri Mkuu alipotembelea mtwara kina mama kuja kwenye mkutano wakiwa wamevaa Viroba. Unachosifia kama mpaka kujitosheleza kwa chakula ulifeli walsti uleule wa awamu ya kwanza.  Sisi wengine sio wachumi lakini kuna tofauti kati ya Ubora wa maisha(standard of living) na cost of living(gharama za maisha). Kuisha Dar ni  rahisi zaidi kuliko kuishi Newyork, na ubora wa wa maisha ya New York kuliko Dar. Hebu tuiweke hivi, wakati wa awamu ya kwanza. kulikuws hakins simu za mkpnoni, umeme ulikuwa maeneo machache hats mijini, ulikuwa hutaji television, radio kubwa zaidi 277. Lakini pia safari nyingi fupi tulikuwa tunazifanya kwa miguu. Nilikuwa nstoka magomeni mwembechai kwa niguu mpska kariakoo au posta. Leo ni  wangapi wanafanya hivyo? Mtoto asipochaguliwa kwenda sekondari(nasisitiza asipochaguliwa maana walikuwa wakifaulu wengi) ilikuwa ndio mwisho wa masomo, isipokuwa wazazi wachache wsliokuwa na uwezo private. Nilimaliza shule ya msingi Darsjsni- Dar mwaja 1983 walifaulu wanafunzi wawili tu kati Zaidi ya 150. Hivi kweli hii iliondoa tulichofundishwa kuhusu ubaya wa elimu ya kikoloni kuwa ilikuwa na umbile la  pyramid.. Mwisho jiulize hivi marehemu Sokoine mpaka anafariki mwska 1984 . alikuwa anapambana mini? Ufisadi, uhujumu uchumi, uhaba wa bidhaa na kutokuwajibika. Naomba usome kitabu cha kumbukumbu ya miaka 40 ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, angalia hutuba ya Marehemu Prof Sethy Chachage"miaka 40 ya Uhuru kwanini Tanzania bado masikini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *