
- Mhasibu adaiwa kughushi na kuchota mamilioni NMB
MATUKIO ya ufisadi yamezidi kuitikisa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha baada ya watumishi wake wawili wa ngazi juu kutiwa nguvuni na polisi kwa tuhuma za kugushi malipo hewa ya fedha, shilingi milioni 4.2 na kuhamisha fedha hizo kutoka akanti ya halmshauri hiyo kwenda katika akaunti ya kampuni moja ya mjini Arusha.
Taarifa zilizofikia Raia Mwema kutoka vyanzo mbalimbali na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi zinawataja watuhumiwa hao kuwa ni Mweka Hazina, Julius Maheri na Ofisa Usafirishaji, Bakari Jabu. Kwa pamoja wanatuhumiwa kugushi hundi hiyo wiki iliyopita.
Habari zaidi zinaeleza kuwa watumishi hao walishirikiana na kugushi malipo kwa kutumia mfumo wa uhamishaji fedha (TT) katika Benki ya NMB tawi la Monduli, kwenda Benki ya Exim ilipo akaunti ya kampuni hiyo inayojihusisha na uuzaji mafuta ya petroli na dizeli mkoani Arusha (jina linahifadhiwa), bila idhini ya uongozi wa halmashauri hiyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Akili Mpwapwa, alithibitisha kukamatwa kwa mweka hazina huyo na mwenzake ambao pia wamekwishahojiwa kuhusu kuhamishwa kwa fedha hizo mwishoni mwa mwezi uliopita.
“Ni kweli tukio hilo lipo na watuhumiwa wameshahojiwa na askari wa upelelezi wa kitengo cha “fraud” na wameachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi unaendelea dhidi yao na tunatarajia kuwafikisha mahakamani mara uchunguzi huo utakapo kamilika” anasema Kamanda Mpwapwa.
Taarifa zaidi kutoka Monduli zinaeleza kuwa wizi wa fedha hizo ambazo zilikuwa katika akaunti ya utawala (General Account) uligundulika mwishoni mwa Novemba, mwaka huu, wakati watumishi wa idara ya fedha wakiandaa utaratibu wa kulipa mishahara ya watumishi.
“Wahasibu walipokwenda kuangalia salio la fedha katika akaunti hiyo waligundua kuwa kuna upungufu wa fedha na baada ya kufanya mawasiliano ya ndani ya uongozi wa Benki ya NMB ndipo walipoelezwa kuwa fedha hizo zilichukuliwa na wahusika wakitumia mfumo wa TT,” anaeleza moja wa watumishi wa halmashauri hiyo jina linahifadhiwa.
“Uongozi wa benki uliwaeleza wahasibu kuwa uhamishaji wa fedha hizo ulisimamiwa na wahusika hao wawili na pia baada ya kukagua saini zao ilibainika kuwa sahihi zilizokuwa katika nyaraka za uhamishaji fedha hizo zilikuwa zimegushiwa na wahusika,” anaeleza mtoa taarifa huyo.
Mtumishi huyo alieleza kuwa hatua hiyo iliwashangaza wahasibu hao kwani kampuni iliyohamishiwa fedha hizo kumbukumbu zilionyesha kuwa haikuwahi kuleta hati yoyote ya madai (invoce) kwa halmashauri na wala haikufanya biashara yoyote yenye kustahili kulipwa kiasi hicho cha fedha.
Aliongeza kuwa, kutokana na utata huo waliripoti suala hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Samwel Mlay, ambaye naye aliripoti kwa vyombo vya dola, ikiwa ni pamoja na polisi na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mgessa Mulongo.
“Baada ya mawasiliano yaliyochukua siku mbili ndipo polisi walipomtia mbaroni mweka hazina na mwenzake na kuhojiwa kwa siku mbili mwishoni mwa wiki iliyopita, aina hiyo ya wizi imetikisa halmashauri nzima kwa sasa,” aliongeza.
Habari zaidi zilizolifikia gazeti hili kutoka Monduli zinadai kuwa fedha zilizoibwa zilipangwa kutumika kuwapa rushwa madiwani wawili (majina yanahifadhiwa) ambao wanadaiwa kuwa mwiba ndani ya vikao vya kamati ya fedha kwa kuwabana watumishi hao dhidi ya matukio ya ufisadi unaodaiwa kushamiri kwenye halmashauri hiyo.
Madai hayo yalitolewa na mmoja wa madiwani wa halmashauri hiyo ambaye alidai kuwa fedha hizo ziliibwa kwa lengo la kuwaziba mdomo madiwani wawili vijana ambao ni wajumbe wa kamati ya fedha na muda wote wamekuwa wakimshikia ‘bango’ mweka hazina na mwenzake wakiwatuhumu kuhujumu halmashauri hiyo kwa kufuja fedha za miradi.
“Huyo bwana naona baada ya kushambuliwa sana aliamua kuwapoza madiwani hao kwa fedha za halmshauri ambazo wao walikuwa wanapigia kelele kuwa zinafujwa, ni sawa na mtu aliyeamua ‘kuwakaanga’ madiwani kwa kutumia ‘mafuta’ yao wenyewe,”anasema kwa dhihaka dhihaka.
Hata hivyo, bado haikufahamika iwapo madiwani hao walichukua fedha hizo kwani bado haijathibitishwa iwapo fedha hizo zilipoingizwa katika akaunti ya kampuni hiyo ya mafuta zilitolewa na kukabidhiwa kwa wahusika.
Diwani huyo alidai kuwa kabla ya tukio hilo, mweka hazina huyo alikuwa asimamishwe kazi kwa madai ya kuhusishwa na upotevu wa shilingi milioni 40 za halmshauri ambazo, upotevu wake uligunduliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alioufanya katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/2010.
“CAG aligundua madudu katika ukaguzi wake na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema ilishauri kuwa watumishi wote waliohusika na ufisadi katika halmshauri hiyo wafukuzwe kazi mara moja na kufikishwa mahakamani lakini sehemu kubwa ya ushauri huo bado haijatekelezwa na serikali” aliongeza.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika kile kinachoonekana kuwa kukithiri kwa vitendo vya matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za halmashauri hiyo, ofisa usafirishaji Bakari Jabu kati ya Julai na Agosti, mwaka huu, alikodisha mashine ya kutengenezea barabara (loader) mali ya halmashauri kwa kampuni binafsi ya ujenzi huku akisingizia kuwa mashine hiyo ilikuwa mbovu na imepelekwa karakana kwa matengenezo.
Baada ya uongozi wa halmashauri kumbana na kufuatilia ilibainika kuwa mashine hiyo ilikuwa imekodishwa na kwa kampuni binafsi ya ujenzi (jina linahifadhiwa) iliyokuwa imepewa kandarasi ya kutengeneza barabara katika moya ya wilaya mkoani Arusha na haikuwa imeharibika kama ilivyoelezwa awali na ofisa huyo.
Uongozi pia ulibaini kuwa mtumishi huyo alikuwa ameikodisha mashine kwa malipo makubwa ambayo alikuwa anatoza kwa siku na fedha hizo zinadaiwa kuingia mfukoni mwake bila halmashauri kupata chochote.
“Kwa kweli hali ya ufisadi inatisha katika halmshauri hii karibu idara zote muhimu watendaji wake wamejitumbukiza katika vitendo vibaya vya kuhujumu mali, mapato na fedha za halmashauri na wakati hayo yanatendeka ufanisi katika kuhudumia wananchi ni mdogo sana,” anaeleza mmoja wa watumishi wa ngazi ya chini katika halmashauri hiyo.
Akizungumzia matukio hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Samwel Mlay, alithibitishia Raia Mwema kuwa ni kweli mweka hazina huyo anahojiwa polisi kwa tuhuma za kughushi malipo hewa na kuhamisha fedha hizo kwenda katika akaunti ya kampuni hiyo inayojihusisha na biashara ya mafuta.
“Suala hilo lipo ila kwa sasa siwezi kulizungumzia hadi katika kikao cha Baraza la Madiwani litakalofanyika Desemba 16, mwaka huu na pia vyombo vingine vya dola vinalifanyia kazi na muda muafaka ukifika tutawaeleza hatua zilizofikiwa,” alisema Mlay.
Aliongeza kuwa sasa wanafanya ukaguzi wa hesabu ya ndani ili kufahamu iwapo kuna matukio mengine ya aina hiyo na baada ya ukaguzi huo, watajua vizuri zaidi wahusika wa uhujumu huo ni watumishi gani.
“Lakini si kwamba halmashauri yetu inaongoza kwa ufisadi, kwa ufahamu wangu katika maeneo yote ambayo kuna mzunguko wa fedha lazima kuwa na matukio ya udokozi kutoka kwa watumishi wasiowaaminifu, hata katika kampuni binafsi na mashirika ya umma bado kuna watumishi wengi ambao si waaminifu na cha msingi ni kuwabana na pale wanapobainika kuwachukulia hatua kali za kisheria,” anasema mkurugenzi huyo.
Hii si mara ya kwanza kwa halmashauri hiyo kukumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za umma. Mapema Juni, mwaka huu, halmashauri hiyo ilikumbwa ya kashfa iliyosababisha miradi kadhaa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa ofisi za Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa, kusimama kwa muda baada ya fedha zilizotengwa kufujwa na watumishi.
Kutokana na tuhuma hizo, baraza la madiwani liliagiza Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango, kuwasimamisha kazi mara moja watumishi wawili wa halmashauri hiyo na pia kuwashusha cheo wengine wawili kutokana na kuhusika kwao katika tuhuma kadhaa za ufisadi.
Waliopendekezwa kusimamishwa kazi wakati huo walikuwa ni pamoja na Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Sylivester Chinengo na Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Monduli, Kanaeli Pallangyo.
Waliooshushwa vyeo vyao ni wa watumishi wa kawaida ni ofisa Ardhi Kitunda Mkumbo pamoja na Ofisa Ugavi wa Halmashauri hiyo, Mangwala Kilanga ambao tayari wameanza kutumikia adhabu dhidi yao.
Ufisadi katika halmashauri nyingi nchini umekithiri , ukitajwa kuwa kikwazo kikuu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi huku juhudi zinazofanywa na mamlaka za kiserikali kudhibiti hali hiyo zikiwa zinagonga mwamba mara nyingi kwa wahusika na sababu kubwa ikielezwa kuwa ni kujengeka kwa tabia ya kulindana miongoni mwa watumishi wa serikali wa ngazi zote.
Toa maoni yako