PAMOJA na kwamba nguzo kuu tatu za maendeleo ya dola ni watu, ardhi na uongozi unaotekeleza siasa safi, bado katiba ya CCM (1977) katika ibara za 5(3), 5(9), 5(14), 5(15) na 5(16) inatamka, kwa usahihi, kwamba maendeleo tajwa hayawezi kuja bila watu waliotumbukia na kunasa katika pango la umaskini kukamilishwa kijamaa na majirani zao wa karibu katika dola kwa kuwaweka huru dhidi ya ufisadi, ujinga, ugonjwa na wapambe wengine wa umaskini.
Lakini, ni wazi kwamba leo hii, kizazi kimoja baadaye Watanzania wengi bado wametumbukia na kunasa katika matope yaliyo katika pango la umaskini kiasi kwamba hawawezi kamwe kuungana na Watanzania wenzao katika kusherehekea Mwaka mpya wa haki na amani.
Hivyo, katika makala hii tunajadili tangazo hili la vita dhidi ya ufisadi, ujinga, ugonjwa na wapambe wengine wa umaskini ili kubaini mantiki na sababu zake.
Ufisadi ni mpambe nambari wani wa umaskini
Na kama tunavyoelewa, ikiwa mtu aitwaye “A” anayo haki ya kudai kitu kiitwacho “B” kutoka kwa mtu aitwaye “C” kwa sababu ya maelezo ambayo hapa tuyaite “D”, basi ndugu “A” huitwa mtu anayedai haki, kitu “B” huitwa kinachodaiwa, ndugu “C” huitwa mtu aliye na wajibu wa kutimiza madai, na maelezo “D” huitwa sababu inayoeleza uhalali wa madai haya. Hizi ndizo kona nne za mraba wa haki.
Katika dola, kuanzia kwa mtu binafsi, kupitia familia, kitongoji, kijiji, wilaya, mkoa hadi Ikulu, kuna miraba ya haki na majukumu iliyoungana kama mnyororo.
Na mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika kiwiliwili cha dola, kuanzia mtu binafsi kupitia familia hadi Ikulu na kuendelea kama uti wa mgongo katika mwili wa binadamu.
Lakini, wapambe wa umasikini kama vile ufisadi, ujinga na ugonjwa hufyatua mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika kiwiliwili cha dola na hivyo kuzifanya sehemu mbalimbali za dola kupoteza mawasiliano kama ambavyo viungo vya mwili wa mgonjwa aliyeteguka mgongo visivyo na mawasiliano!
Tuone ukweli huu kwa kumchunguza mpambe nambari wani wa umaskini ambaye ni ufisadi. Sababu inayohalalisha tangazo la vita ya kudumu dhidi ya ufisadi, ni ukweli kwamba katika dola iliyotekwa na mafisadi, mnyororo wa miraba ya haki na majukumu huteguliwa na mafisadi, na hivyo kuhujumu maendeleo ya taifa kwa kusitisha mawasiliano kati ya Ikulu na familia, vijiji, wilaya na mikoa.
Kwa ujumla, ufisadi ni kitendo chochote kinachohusisha matumizi ya cheo cha kiofisi, iwe ni katika sekta binafsi, sekta ya kiraia au sekta ya umma. Hapa afisa mhusika hutumia dhamana ya madaraka aliyopewa kuziba mifereji ya haki na majukumu kinyume na matakwa ya taratibu rasmi za ofisi yake.
Na kwa kufanya hivyo, bila kustahili, afisa huyo huweza akajifaidisha yeye binafsi au akawafaidisha familia yake, ndugu zake wa damu, ndugu zake wa ukweni, kabila lake, dini yake, kanda yake kijiografia, chama chake cha siasa, wafanyibiashara wenzake na kadhalika.
Hivyo, kwa kuzitengua pingili za mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika dola, matendo ya kifisadi huziba mifereji ya haki na majukumu, na kisha kuipindisha mifereji hiyo kuelekea kusiko, haya yote yakiwa kinyume na matakwa ya taratibu rasmi za kiofisi.
Na matendo ya aina hii huweza kutegua pingili ya mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika ngazi yoyote kwenye dola. Yakitegua pingili iliyo kati ya Ikulu na jumuiya za kimataifa ufisadi wa kimataifa huwa umetendeka.
Ikiwa yametegua pingili iliyo kati ya Ikulu na Baraza la Mawaziri, au yakategua pingili iliyo kati ya Bunge na Baraza la Mawaziri, au yakategua pingili iliyo kati ya Jimbo la Uchaguzi na Bunge, basi ufisadi mkubwa wa kitaifa huwa umetendeka. Kuteguliwa kwa pingili katika ngazi za chini humaanisha ufisadi mdogo.
Kwa ujumla, mafisadi hutegua pingili zilizo katika mnyororo wa miraba ya haki na majukumu, mnyororo ambao huanzia kwenye kitongoji hadi ikulu na kuzidi.
Na kwa njia hiyo mafisadi hufanikiwa kuifanya serikali ishindwe kutimiza majukumu yake kwa umma na badala yake ikabaki kuwatumikia wao! Kwa maoni yangu, ufisadi ni uhaini.
Ujinga ni mpambe nambari mbili wa umasikini
Lakini ufisadi hauko peke yake katika kuwatumbukiza watu katika pango la umasikini. Mpambe mwingine wa umasikini ni ujinga. Kama ilivyo kwa ufisadi, sababu inayohalalisha tangazo la vita ya kudumu dhidi ya ujinga, ni ukweli kwamba ujinga pia hutegua pingili za mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika dola, na hivyo kuhujumu maendeleo ya taifa.
Jamii yenye watu wajinga ni jamii ya watu wanaotembea uchi kiakili. Jamii yenye watu wajinga ni jamii inayoweza kujikuta ikitapeliwa kwa sababu ya wepesi wake wa kusema “ndiyo” kwani haijui kwa nini iseme “hapana”. Jamii ya aina hiyo hufanyiwa ubabe kwa njia ya mzunguko (coercion by omission), kwa kupewa habari robo robo isizoweza kusuta hata kama ni potofu.
Jamii yenye watu wajinga hubaki ikihemea wataalam kutoka ng”ambo kutokana na ukweli kwamba haina ustadi wa kazi (skills) unaoweza kukidhi mahitaji yake.
Katika jamii ya aina hii stadi za ualimu, uganga, unesi, udereva, uongozi wa makampuni makubwa ya umma, uendeshaji wa miradi na stadi zingine huwa ni bidhaa adimu. Hivyo, hubaki ni jamii tegemezi.
Jambo hili ni kinyume cha hadhi ya kipawa cha utu wa binadamu (human dignity). Hivyo, panahitajika elimu kamilifu, elimu sahihi, na elimu kwa wakati sahihi kwa ajili ya kumwezesha kila binadamu kufikiri, kuamua na kutenda atakavyo katika hekaheka zake za kutimiza malengo aliyo nayo maishani.
Hiyo ndiyo sababu ya kuweka mfumo wa elimu rasmi unaoongozwa na mitaala yenye kuboreshwa mara kwa mara.
Na elimu bora ni ile ambayo huwafanya watu wawe wepesi kuongozwa lakini ikawafanya wawe wagumu kuburuzwa na ulimwengu kama kondoo asiye na hazina ya uwezo wa kufikiri, kuamua na kutenda atakavyo!
Ugonjwa ni mpambe nambari tatu wa umasikini
Mbali na ufisadi na ujinga, kuna mpambe mwingine sugu wa umasikini aitwaye ugonjwa. Kama ilivyo kwa ufisadi na ujinga, sababu inayohalalisha tangazo la vita ya kudumu dhidi ya ugonjwa, ni ukweli kwamba ugonjwa pia hutegua pingili za mnyororo wa miraba ya haki na majukumu katika dola, na hivyo kuhujumu maendeleo ya taifa.
Jamii inapokuwa na huduma hafifu za tiba, wagonjwa wengi huongezeka, kwa sababu ya wagonjwa kuongezeka, utoro kazini huongezeka, kisha uzalishaji hushuka, na hatimaye rasilimali haba huzalishwa katika taifa. Hatima ya yote haya ni kwamba jamii hubaki imenasa katika pango la umasikini.
Wapambe wengine wa umaskini
Kwa ujumla, wapambe wakuu wa adui yetu umaskini ni ufisadi, ujinga na ugonjwa. Wapambe hawa wanahusiana kama babu, baba na mwana. Ufisadi husababisha ujinga na ugonjwa, ujinga ukasabaisha ugonjwa, na kisha ugonjwa ukasababisha ujinga!
Hatimaye wapambe hawa watatu huwaalika marafiki zao, ambao ni wapambe wengine wa umasikini, wakashirikiana kulikarabati na kulipanua pango la umasikini!
Wapambe hawa wengine ni pamoja na ukosefu wa masoko ya mazao, miundombinu dhaifu katika sekta za usafiri, uchukuzi, habari na mawasiliano, nishati, elimu, tiba na utafiti; uongozi dhaifu; ukosefu wa ajira za uhakika; ukosefu wa mitaji; uharibifu wa mazingira; madawa ya kulevya; mirija inayofyonza wataalam wetu kuelekea ughaibuni (brain drain); ubaguzi wa kitabaka katika sekta mbalimbali za jamii yetu, na orodha inaendelea.
Kwa ufupi, basi, katika pango la umasikini kuna watumwa ambao miguu yao imenaswa kwa minyororo inayowatenganisha na mwanga wa jua la maendeleo; kwamba bila watu hawa kukamilishwa kijamaa na majirani zao wa karibu katika dola ni vigumu kwao kujinasua katika minyororo hii.
Na kwamba kwa watu wa aina hii, kifungua kinywa, chakula, mavazi, malazi, makazi, mafuta ya taa, chumvi, sabuni, tiba, barabara zinazopitika, masoko ya mazao, nauli ya basi, elimu bora, habari muhimu, mitaji na ajira ni bidhaa adimu sana.
Na, katika haya yote, ni rai yangu kwamba: Ikiwa tunataka kuutokomeza ufisadi, ujinga, ugonjwa, na wapambe wengine wa umaskini na hatimaye kuwawezesha binadamu wanaoishi katika pango la umaskini kuuona mwanga wa jua la maendeleo, basi tunalo jukumu la kujitegemea kijamaa katika ngazi mbalimbali za dola kama ambavyo tunalo jukumu la kukamilishana kijamaa katika ngazi mbalimbali za dola ile ile.
Katika makala ijayo tutaona utetezi wa rai kwamba: Utawala wa sheria ndiyo mbinu pekee ya kupambana na unyumbulifu wa akili ya binadamu.
Toa maoni yako