Habari
Ugonjwa wa macho watesa Mkoa wa Mbeya
Felix Mwakyembe
Mbeya
Toleo la 234
11 Apr 2012

MATUMIZI ya miwani, hususani kwa vijana mkoani Mbeya, yamekuwa yakiongezeka huku wengi wakiamini kuwa ni urembo au mikogo tu ya vijana, lakini kwa wataalamu wa afya, hilo ni tatizo la uoni hafifu linalokua kwa kasi hivi sasa nchini.

Katika moja ya shule za sekondari jijini Mbeya, Raia Mwema ilielezwa kuwa wanafunzi 20 kati ya 200 waliojiunga kidato cha kwanza mwaka huu, wanatumia miwani kutokana na tatizo la uoni hafifu.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Luis Chomboko, analibainisha tatizo hilo akisema Mkoa huo kwa sasa unakabiliwa  ongezeko la tatizo hilo miongoni mwa wakazi wake, lakini wakati huo huo akionyesha hofu yake katika kukabiliana nalo kutokana na kudorora kwa huduma ya afya ya macho mkoani humo kunakosababishwa na uhaba mkubwa wa wataalamu.

Miongoni mwa matatizo yanayoikabili huduma hiyo ni pamoja na upungufu mkubwa wa wataalamu, upungufu wa vifaa, mwamko na uelewa mdogo wa jamii kuhusu matatizo ya macho na tiba zilizopo.

Dk. Chomboko anasema moja ya mikakati ya kukabiliana na tatizo la macho ni wananchi wenyewe kuwahi kupata matibabu ili kuzuia upofu tangu utotoni hadi uzeeni.

“Tatizo la ugonjwa wa macho linanzia kwa mgonjwa mwenyewe, mtu haumwi, mgonjwa hajisikii kuumwa hivyo hukaa tu nyumbani, tunalazimika kuwafuata wananchi kuwaelimisha ili wapimwe,” anasema Dk Chomboko.

Ukiweka kando tatizo hilo la wananchi kutohiari kwenda kupima afya zao za macho, kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu huyo, Mkoa wa Mbeya unakabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa wataalamu wa macho.

Hospitali ya Mkoa, mathalani, haina daktari bingwa, wasaidizi na wauguzi hata mmoja, huduma zake zinamtegemea zaidi mtaalamu wa kuangalia afya ya jicho na kutoa miwani.

Katibu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dories Nzigirwa anabainisha hali hiyo akisema:

“Hospitali imeomba msaada kupeleka watumishi kusoma, kitengo hakina daktari na wauguzi wa macho, tulionao hapa ni wataalamu wa kuangalia afya ya jicho na kutoa miwani tu.”

Kuongezeka kwa tatizo la afya ya macho mkoani Mbeya kumeibuliwa kupitia utafiti uliofanyika hivi karibuni katika Wilaya ya Kyela mkoani hapa, ilipobainika kwamba asilimia sita ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wana matatizo ya kutokuona na kati ya hao, asilimia 70 inachangiwa na mtoto wa jicho, asilimia nyingine 77 za wenye uoni hafifu walio  nje ya umri huo inachangiwa pia na mtoto wa jicho. 

Hali kitaifa ikoje

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania ina takribani watu 450,000 wasioona na wengine 1,350,000 wenye uoni hafifu. 

Takwimu hizo za WHO zinaonyesha zaidi kwamba tatizo la macho ni la dunia ambapo takribani watu milioni 30 wana matatizo ya kutokuona na wengine milioni 90 wakiwa na uoni hafifu.

Taarifa hiyo inabainisha visababishi vya hali hiyo kuwa ni pamoja na mtoto wa jicho (cataract) inayoelezwa kuchukua sehemu kubwa takwimu zikionyesha inachangia kwa asilimia 50.

Visababishi vingine, kwa mujibu wa takwimu hizo za WHO, ni pamoja na kove kwenye kioo cha jicho (corneal scar) inayoelezwa kusababishwa na trakoma, upungufu wa vitamin A na surua kwa asilimia 20, na shinikizo au presha ya jicho (glaucoma) inayochangia kwa asilimia 10.

Asilimia 20 iliyobaki ya tatizo la macho inaelezwa kusababishwa na magonjwa ya retina kama vile kisukari (diabetic retinopathy), umri mkubwa na upeo mdogo wa kuona.

Uchambuzi zaidi wa tatizo la macho unaonyesha kuwa kwa watoto, matatizo makuu yanayowasababishia kutokuona ni pamoja na makengeza, upeo mdogo wa kuona, mtoto wa jicho, maambukizi yatokanayo na magonjwa ya ngono toka kwa mama na matatizo ya macho ya kuzaliwa.

Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Dk. Bernadetha Shilio anabainisha matatizo yanayoikabili huduma ya afya ya macho mkoani Mbeya kuwa ni ya kitaifa na wala si ya Mkoa huo pekee.

Anayataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa watalaamu ambao wa kwa upande wa madaktari bingwa ni asilimia 80, madaktari wasaidizi wa fani ya macho asilimia 77.

Dk. Bernadetha anayataja matatizo mengine kuwa ni upungufu wa vifaa vya tiba na madawa wa asilimia 75 na mwamko na uelewa mdogo wa jamii kuhusu matatizo ya  macho na tiba zilizopo.

Serikali inavyokabiliana na tatizo la afya ya macho;

Katika kukabiliana na tatizo la afya ya macho nchini, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeridhia dira ya 2020 ya kutokomeza upofu unaoweza kuzilika ulimwenguni ifikapo mwaka 2020 (Vision 2020: The Right to Sight), ambapo katika kutekeleza malengo ya dira hiyo wizara iliandaa na kuzindua rasmi Mpango Mkakati wa Pili wa Taifa wa Huduma za Macho (2011-2016).

Kupitia mpango mkakati huo Serikali imelenga kutatua tatizo la upatikanaji wa dawa za macho na mahitaji mengine kwa ajili ya huduma za kliniki na upasuaji, kuimarisha miundombinu ikiwa ni pamoja na nafasi ya utoaji huduma na vifaa na upatikanaji watalaamu kwa ngazi zote.

Dk Bernadetha anataja malengo mengine katika mpango mkakati huo kuwa ni pamoja na kuboresha utendaji kazi wa watoa huduma, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu magonjwa ya macho na jinsi ya kuyadhibiti na kuimarisha uratibu wa huduma za macho nchini.

Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati huo, hivi karibuni kilizinduliwa kituo cha macho (Vision Center) katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, kinachotarajiwa kutoa huduma bora kwa wananchi wa mkoa huo.

Pamoja na uzinduzi wa kituo, hospitali hiyo ilipatiwa vifaa vya kisasa vya tiba ya macho, vilivyotolewa na Kituo cha Kimataifa cha Elimu ya Huduma ya Macho (International Centre for Eyecare Education).  

Ni wazi kwamba katika matatizo hayo sugu yanayoikabili huduma ya afya ya macho, la majengo na vifaa laweza patiwa ufumbuzi wa haraka, tofauti na la uhaba wa wataalamu, hili linaelezwa kuendelea kulisumbua Taifa kutokana na ukweli kwamba linahitaji uwekezaji wa muda mrefu kwenye rasilimali watu.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako