TUNAWEZA kuungana na yeyote atakayejitokeza hadharani na kudai, baadhi ya viongozi wa Serikali, hasa wanaohusika katika kuhakikisha nishati muhimu ya petroli inapatikana wakati wote nchini, ni legelege.
Ulegevu wa viongozi hao umedhihirika katika siku hizi za mwanzo mwa wiki hii (Jumatatu), baada ya Jiji la Dar es Salaam kukumbwa na uhaba mkubwa wa petroli na nishati nyingine za aina hiyo.
Yapo madai kwamba uhaba huo ni matokeo ya hujuma zinazoratibiwa bila woga, na genge la wafanyabiashara ya petroli nchini.
Kutokana na uhaba huo unaotajwa kutokuwa wa lazima, usumbufu mkubwa umejitokeza miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam kuanzia Jumatatu, wiki hii.
Kwa nini tunaamini kuna viongozi wa Serikali legelege katika usimamizi wa sekta hii ya nishati? Sababu ni moja ambayo ni ukweli kwamba, hii si mara ya kwanza kwa tatizo hili kujitokeza. Kwa nini wahusika hawakujifunza kutokana na matukio ya aina hii yaliyotangulia?
Juzi Jumatatu, wakazi wengi wa Dar es Salaam waliishi maisha kama vile hakuna Serikali, au kama vile Serikali kupitia kwa viongozi wake wa mamlaka husika, wametiwa mfukoni mwa wafanyabiashara fulani.
Ulegevu huu ulikuwa dhahiri na ulisababisha msongamano mkubwa katika vituo vya vichache vya kuuza petroli vilivyokuwa vikiendelea na shughuli zake. Barabara karibu zote zilijaa foleni za magari kuingia vituo vya petroli.
Inashangaza kuona wakati wakazi wa Dar es Salaam wakiwa katika usumbufu mkubwa, viongozi wa wahusika ambao wengi wako jijini humo, wanaendelea na shughuli zao za kawaida ofisini, kama hakuna kinachotokea.
Usingizi wa namna hii kwa viongozi husika kuelekea katika ofisi zao kila asubuhi na kudharau mamia ya wananchi waliopanga foleni katika vituo ya mafuta, si jambo zuri.
Si ishara nzuri, tungependa kuona viongozi wakiwajibika kutatua dalili za matatizo na si hali hii ya kufumbia macho matatizo ya dhahiri. Si picha nzuri ,kwa nchi ambayo majuzi ilisherehekea miaka 50 ya Uhuru kujikuta ikiwa katika matatizo ya kujitakia kama haya ya upungufu wa mafuta.
Toa maoni yako