Uingereza kuanza mazungumzo ya kujitoa Umoja wa Ulaya Machi 29

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May alitumaini kuliruka bunge katika mchakato wa kujitoa Ulaya.

LONDON, UINGEREZA

WAZIRI Mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kuutaarifu rasmi Umoja wa Ulaya kwamba nchi yake inajitoa katika umoja huo siku ya Jumatano ijayo.

Ofisi ya Waziri Mkuu huyu huko Downing Streed imesema kwamba ataandika barua kwenda kwa wanachama wengine 27 wa Umoja wa Ulaya, na kuongeza kwamba anategemea kwamba majadiliano juu ya kujitoa huko yataanza haraka iwezekanavyo.

Hatua hiyo inakuja miezi tisa baada ya asilimia 51.9 ya watu wa nchi hiyo kupiga kura ya kuunga mkono pendekezo la kujitoa kwa nchi hiyo kwenye Umoja wa Ulaya huku asilimia 48.1 wakipinga.

Mazungumzo juu ya masharti ya kujitoa na mahusiano ya hapo baadae baina ya pande hizo hayaruhusiwi kuanza mpaka pale Uingereza itaapouarifu rasmi Umoja wa Ulaya kwamba inajitoa.

Iwapo kila kitu kitakwenda vizuri kulingana na ratiba ya majadiliano hayo, Brexit inatarajiwa kutokea rasmi mwezi Machi 2019.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, Sir Tim Barrow, aliliarifu Baraza la Ulaya, linaloongozwa na Rais Donald Tusk, mapema leo juu ya tarehe ambayo kifungu cha 50 cha kitafunguliwa rasmi.

Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema kwamba baada ya kifungu hicho kufunguliwa, inatarajiwa kwamba wanachama wote 27 wa umoja huo watakubaliana na masharti yake na kwamba wanatarajia upokea majibu ndani ya saa 48.

Msemaji huyo alisema kwamba serikali inataka mazungumzo kuanza mapema inavyowezekana lakini akaongeza kwamba wanatambua kuwa ni haki ya wanachama hao wa Umoja wa Ulaya uwa na muda wa kutosha kukubaliana na msimamo wao.

Mwaka jana May alisema kwamba aliuwa na mpango wa kuutaarifu Umoja wa Ulaya kwamba nchi yake inampango wa kujitoa kwenye umoja huo ifikapo mwisho wa mwezi Machi mwaka huu. Hatua hiyo iliungwa mkono na Bunge la nchi hiyo wiki mbili zilizopita, hivyo kumpa mamlaka Waziri Mkuu kuanza kuchukua hatua za kujitoa.

Wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya wamesema kwamba wanataka kukamilisha majadiliano hayo ndani ya miezi 18 ili kuruhusu masharti ya kujitoa kwa Uingereza yapitishwe na mabunge ya Uongereza na Ulaya, na pia kuungwa mkono na sehemu kubwa ya wanachama wa Umoja huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *