Ujerumani katika mtanziko wa kijeshi

WAKATI Vladmir Putin akizichafua nchi za Ulaya Mashariki, Mashariki ya Kati na mgogoro wa Asia ambao umezua wimbi jipya la wahamiaji kuelekea barani Ulaya, na Rais Donald Trump akihoji ushiriki wa Marekani katika umoja wa NATO, Ujerumani ina sababu hasa ya kujisikia si salama.

Kansela wa Ujerumani, Angeka Merkel, aliwaambia Wajerumani mwezi Mei mwaka huu kwamba “ni lazima tupambane kwa ajili ya mustakabali wetu kama wazungu.” Majeshi ya Ujerumani yamekuwa yakipelekwa katika maeneo mbalimbali duniani, kuanzia Lithuania hadi Afghanistan na Mali. Na Merkel ameahidi kuongeza matumizi ya kijeshi ya nchi yake.

Lakini Ujerumani na Kansela wake wanakabiliwa na tatizo moja kubwa –kwamba Wajerumani wengi hawapo tayari kwenda katika mkondo huo.

Wanalitazama jeshi lao wenyewe kwa wasiwasi – mtazamo ambao umetiwa nguvu na kashfa ya hivi karibuni inalolihusu jeshi hilo maarufu kama Bundeswehr. Kupeleka askari wa nchi hiyo kwenda nchi za kigeni kunazuiwa sana na sheria za nchi hiyo pamoja na Bunge. Na kikubwa zaidi, mitazamo imejengwa na kivuli cha historia.

Mataifa ya nje yamefanikiwa katika kuhakikisha kwamba Ujerumani haipati nguvu kubwa za kijeshi – kama ilivyo kwa Wajerumani ambao wanaguswa sana na historia yao ya vita – ambayo leo taifa hilo lenye nguvu zaidi barani Ulaya linatarajiwa kuendelea kukimbia uwanja wa mapambano ya kivita.

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kumekuwa na mabishano iwapo Ujerumani inapaswa kuwa na jeshi. Mwisho ulipaswa kufikiwa, walidai, katika mzunguko ambao ulianza na ubabe wa kijeshi wa Prussia na kuishia kwa makossa ya kivita ya Nazi.

Wakati Ujerumani Mashariki ambayo ilikuwa inatawaliwa na Wakomunisti iliunda Jeshi la Watu kufuata tamaduni za kijeshi za Ujerumani, katika Ujerumani Magharibi ya kidemokrasia – ambayo ilikaliwa na Uingereza, Ufaransa na Marekani – mfumo tofauti kabisa wa jeshi ulijitokeza.

Jeshi la Bundeswehr, lilizaliwa katikati ya miaka ya 1950, lilikuwa ni jeshi dogo, ambalo lilikuwa na lengo la kulinda ardhi ya Ujerumani Magharibi, na si kupigana nchi za kigeni. Vijana waliokuwa wanajiunga na jeshi hilo walikuwa wanafundishwa kujifikiri wao wenyewe kama “raia ndani ya gwanda za jeshi.”

'Kutoaminiana kusikokwisha'

Kwa kweli, magwanda yenyewe, anasema mtaalamu wa mambo ya historia, James Sheehan, “kweli inafanana na ile anayovaa dereva wa basi kuliko wanajeshi halisi.”

Ujerumani ya leo, anasema Sheehan, “inafikiri juu ya jeshi lake kama vile ambavyo mataifa mengi yamekuwa yanafikiri juu ya majeshi yake ya polisi.”

Kile anachokiita “kuendelea kutoamini taasisi zote za kijeshi,” anaongeza, “kunaendelea kuwa na nguvu, na katika njia fulani kumezidi kupata nguvu zaidi.”

Kilicho chini ya haya yote ni kumbukumbu ya maovu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia – sio tu aibu ya maovu ya Nazi lakini pia uharibifu ambao uliwafika raia.

Werner Kraetschell, kasisi wa Kiprotestanti kutoka familia ya zamani ya Prussia ambaye alikuja kuwa kamanda wa kijeshi, anazungumza juu ya maelfu ya Wajerumani ambao walikuwa wanakua baada ya vita “bila baba.” Hilo bado linazua kile anachokiita “mshtuko wa ndani” wa Wajerumani linapokuja suala la kijeshi.

Kwa muda mrefu, anasema mtaalamu wa masuala ya kijeshi Sophia Besch kutoka Centre for European Reform, “Iwapo ungekuwa ni askari nchini Ujerumani usingeweza kusafiri ndani ya treni ukiwa umevaa magwanda yako. Ungefuatwa na abiria ambao wanakuita ‘muuaji.’”

Changamoto za kiusalama

Wakati Vita Baridi vilipomalizila na Ujerumani kuunganishwa tena, watu wake waliamini kwamba amani sasa ni ya kudumu. Lakini mwanasiasa wa chama cha Christian Democratic na waziri wa zamani wa ulinzi Franz Josef Jung anasema “ukweli umetuumbua.”

Lakini pia anakubali kwamba “raia wetu wamekuwa na mtazamo ambao kwa sehemu kubwa umejengwa na hasira.”

“Inabidi tuweke wazi,” anadai, mahitaji ya kuwa na sera mpya ili “kukabiliana na changamoto za kiusalama za nje na ndani.”

Tangu muungano Ujerumani imeanza kupeleka wanajeshi wake katika nchi za kigeni kwa mara ya kwanza.

Mwaka 2009 kulikuwa na shutuma za kujaribu kuficha kashfa iliyohusu shambulizi la kijeshi nchini Afghanistan lililohusisha majeshi ya Ujerumani ambalo lilisababisha vifo vya raia. Dkt Jung alilazimika kujiuzulu kutoka serikalini.

Usimamizi wa kibunge wa kupeleka majeshi nje ya nchi hiyo ni mkali – huku chama cha Kijani kikiwa miongoni mwa vyama vinavyokosoa zaidi. Doris Wagner, mbunge wa chama hicho na mtaalamu wa masuala ya ulinzi, anasema anataka kuendelea na mtazamo wa Wajerumani kuwa “inayojizuia zaidi katika masuala ya kivita.”

'Uhusiano unaoumiza'

Wakati huo wazo la zamani la jeshi la raia limekuwa na wakati mgumu kuweza kudumu hadi leo. Ujerumani imepiga marufuku kwa raia wa nchi hiyo kujiunga na jeshi kwa lazima na sasa limeelekeza nguvu zaidi, kama yalivyo majeshi ya kisasa, katika jeshi dogo la wataalamu.

Hali ya wasiwasi wa muda mrefu juu ya jeshi iliibuka upya mwezi uliopita wakati kashfa ambayo inahusu mahafidhina ambao waliingia katika Jeshi la Bendewehr – ikiwemo njama za kuwaua watu wanaotafuta hifadhi nchini humo na kusheherekea tamaduni za enzi za Manazi.

Baadhi walisema kwamba tatizo lilikuzwa kutokana na hasira. Lakini inaonyesha, anasema Sophia Besch, “kwamba bado kuna uhusiano mgumu baina ya jeshi na watu wa Ujerumani.”

Madai ya Donald Trump kwamba NATO ni ‘bure’ na kuhoji kwake juu ya sera ya ulinzi wa pamoja imekuwa ni mshangao mkubwa kwa Wajerumani anasema Bethold Kohler, mhariri wa gazeri la Frankfurter Allgemeine Zeitung. “Hakuna mtu ambaye aliweza kudhani kama Rais wa Marekani anaweza kusema maneno ya aina hiyo.”

Kwa sasa Ujerumani inatumia kiasi cha asilimia 1.2 ya pato lake la taifa kwenye ulinzi.

Werner Kraetschell, ambaye anamfahamu vizuri Angela Merkel, anasema anahitaji “jeshi lenye nguvu la Ujerumani ambalo lina uwezo wa kuchukua majukumu ya kimataifa.” Lakini kikwazo chake ni “watu wa Ujerumani ambao wanapinga jeshi.”

Historia bado inawasumbua. Chochote ambacho kitatokea, hakutakuwa na haraka ya kwenda vitani ugenini. Badala yake, jeshi la Ujerumani litapiga hatua kwa tahadhari kuelekea katika siku za usoni zisizotabirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *