Makala
Ukaburu waibuka Dawasco
Mwandishi Wetu
Toleo la 024
9 Apr 2008

MAMBO si shwari ndani ya Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco)ambako baadhi ya wafanyakazi wanawachochea  wenzao kuikataa menejimenti, imefahamika.

Habari ambazo Raia Mwema imepata zinasema wasiotakiwa na baadhi ya wafanyakazi hao ni Ofisa Mtendaji Mkuu, Injinia Alex Kaaya, Ofisa Mkuu wa Biashara, Raymond Mdolwa, Ofisa Mkuu wa Utawala, Joy Chidosa na Meneja Uhusiano Badra Masoud.

Wengine wanaotajwa katika mpango huo wa wafanyakazi ni mameneja wa mitambo ya maji ya Ruvu Chini Joseph Bamwenzaki, Ibrahim Marwa (Ruvu Juu) na Masoud Omari (Mtoni).

Kati ya madai ya wafanyakazi dhidi ya timu hiyo ya manejimenti ni kwamba inawajali zaidi wasomi na wafanyakazi wapya walioajiriwa karibuni na kampuni.

Injinia Kaaya ameiambia Raia Mwema wiki hii kwamba chokochoko hizo ni za muda sasa na zilijitokeza zaidi katika mkutano wa wafanyakazi uliofanyika kiasi cha wiki mbili zilizopita.

“Mambo haya yalianza muda kidogo uliopita. Lakini unajua unapotaka kumgeuza mnyama aliyezoea kulalia mgongo pana shughuli. Kila mara atataka kujigeuza. Na hicho ndicho kinachotokea hapa. Lakini mimi nimedhamiria.

“Hata siku ile ya kikao niliambiwa kwamba kutakuwa na mambo ya kutaka mimi niondoke. Kwamba walikuwa wamepanga mapema na kuna kakikundi kanapita kakihamasisha kwa ajili hiyo. Wakasema ile risala kwa Katibu Mkuu wa TUICO iungwe mkono nia ni wapate mabadiliko ya uongozi.

“Nikashauriwa nisiende, lakini mimi si mtu mwoga. Sitaki kusemwa wakati sipo. Nataka kusikia kila hoja, na kweli hadi mwisho sikuona hoja pale.

“Eti wanasema afadhali warudi Dawasa. Na hoja hii ya Dawasa inashangaza sana, ni hoja iliyopandikizwa. Ni kama kuna mtu anafurahia kushindwa kwangu au anataka kuchukua nafasi yangu ama yote mawili.

“Lakini nasema mimi nina taaluma. Nikitoka tu pale nje nitapata kazi nyingine. Katika muda huu niliokuwa hapa tumefanya mambo mengi mazuri ya kuikwamua kampuni. Na kwa kweli nimekuwa mkali. Na mimefukuza wengi hapa.

“Mwanzoni niliitisha mkutano hapa nikawasema wote waliokuwa wakituhumiwa na nikawapa muda wa kujirekebisha, walioshindwa tumewaachisha kwa mujibu wa sheria.

“Kwa hiyo sasa tunasuburi TUICO wanasema nini katika yale yaliyozungumzwa kwenye risala ya wafanyakazi kwa maana kwamba kuna mambo ambayo TUICO walisema kwamba yatahitaji tukae nao, mengine ni utekelezaji na mengine ya kimahakama,” alisema Kaaya.

Alisema kwamba anatarajia katika wiki hii masuala yote yatakuwa yamejadiliwa na yatakayoshindikana yatapelekwa kwa Waziri.

Mtuhumiwa mwingine, Meneja Uhusiano Badra Masoud alipoulizwa kuhusu mpango huo wa wafanyakazi wiki hii aliiambia Raia Mwema kwamba alikuwa amesikia tetesi za mpango huo lakini hakujua undani wake hasa.

“Haya ni mambo ambayo nimesikia yakisemwasemwa, lakini sina hakika nayo. Mimi sina shaka, hapa tunajaribu kubadili mfumo wa utendaji ili kampuni ifanye kile hasa inachotakiwa kufanya.

“Wakazi wa Dar es Salaam wanahitaji maji, si malumbano yetu ya ndani ya kampuni. Timu hii inataka watu wapate maji. Ikibidi kutoka hapa nitatoka kama nilivyoingia. Nyinyi mnajua kwamba mimi nilikuwa huko, si ajabu nikarudi kwenye uandishi wa habari,” alisema Badra.

Habari zaidi zinasema kwamba badhi ya wafanyakazi wa Dawasco hawafurahishwi na jinsi ambavyo timu mpya ya Kaaya na wenzake inavyofanya kazi kutokana na kwamba inaonekana kuziba mianya ya ulaji ambayo kwa miaka mingi imezoeleka katika kampuni ya mashirika ya umma.

Kiasi cha wiki mbili zilizopita, wafanyakazi wa Dawasco wakishriki mkutanoni, walimzomea Kaaya katika kile ambacho baadhi ya watu walisema kuwa ishara ya kwamba mambo si shwari ndani ya kampuni.

Dawasco imechukua nafasi ya City Water kampuni ya kigeni iliyokuwa imepewa jukumu la kusambaza maji lakini ambayo dhahiri ilishindwa kufanya hivyo na mwisho kufukuzwa.

Pamoja na Dawasco kuna pia Dawasa ambayo ina jukumu la kusimamia miundombinu ya maji na ambayo imekuwa ikichota mapato ya kiasi cha asilimia 21 kutoka Dawasco.

Kiasi cha wiki mbili zilizopita baadhi ya wafanyakazi wa Dawasco walitishia kumwaga sumu katika vyanzo vya maji suala ambalo linaendelea kuchunguzwa huku baadhi ya vyanzo hivyo vikilindwa na Dola.

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako