Makala
Ukaburu wilayani Mbarali II
Felix Mwakyembe
Toleo la 229
7 Mar 2012

Katika toleo hili la leo, Mwandishi Wetu, Felix Mwakyembe wa Nyanda za Juu Kusini, anaendelea kueleza alichokibaini kutokana na uchunguzi wake kuhusu mgogoro kati ya mwekezaji wa kigeni na wanakijiji wa Kijiji cha Kapunga. Mgogoro kati ya pande hizo mbili unahusu shamba la mpunga la Kijiji cha Kapunga, wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya.

Ukaburu kijijini Kapunga

“Hadi leo kiuno hakina kazi, na kiume change (changu) ameharibu, siwezi fanya kazi, nipo tu siwezi kuhudumia wake zangu,” ni kauli inayoumiza kuisikia ya Mwigulu Ngulo (45) ambaye ni mfugaji katika Kijiji cha Kapunga, na mmoja wa wananchi wanaodaiwa kufanyiwa unyama na Kaburu wa Kapunga.

Sio rahisi kuamini lakini ni mambo yanayofanyika hivi sasa ndani ya ardhi ya Tanzania, kwamba raia wa kigeni anayo madaraka makubwa kufanya akitakacho dhidi ya wananchi.

Ngulo anasimulia mkasa wake huo akisema; “Ilikuwa tarehe kumi mwezi wa saba mwaka jana, niliamka vizuri tu, nikafungulia mifugo yangu napeleka malisho, mimi natoka kitongoji cha Mkanada, kinapakana na mwekezaji, ilipofika saa saba cha ajabu nikaona mwekezaji anashuka na gari yake, nilikuwa na mwenzagu naye anachunga mifugo, ghafla alishuka na askari wake, wakazingira mifugo yetu na sisi tukawa tunaokoa mifugo yetu wasikamate,” anaendelea kuelezea akisema; “Wazungu walikuwa wawili, Mwafrika mmoja anaitwa Chacha, wakanilengesha bunduki, akanisogelea, akafyatua risasi nikachanganyikiwa, alinirushia rungu nikakwepa, akaanza kutumia gari kunifukuza, nilimkwepa mara mbili, ya tatu akanigonga, mimi kweli niliokolewa na Mungu, niliangukia kwenye shimo na ndio ilikuwa pona yangu, alinigonga na bomba (ngao) la mbele ya gari, lilinichoma matakoni, liliweka shimo refu kama mkono, vidole vinaingia vyote.”

Ngulo alifanyiwa unyama huo kwenye ardhi ya kijiji chao, hakuwa ameingia ndani ya shamba la mwekezaji, alikuwa kwenye eneo ambalo tangu enzi za NAFCO lilifahamika kuwa nje ya shamba hilo, wananchi walilitumia kulima na kulisha mifugo.

“Mwekezaji ana haki hata kwenye mali za wananchi, ametugeuza kuwa mbwa, serikali iko kimya kama vile haipo, hata kama tungeingia eneo lake, taratibu si zipo, atoe taarifa polisi, akishaharibu anakimbilia polisi, anatengeneza mambo yake hadi hospitali,” anasema Ngulo na anaendelea kuelezea jinsi alivyohangaika na matibabu akisema;

“Nililazwa Hospitali ya Chimala tangu siku ile ile (Julai 10, 2011) nilikosa huduma, nikakimbilia Mbeya, Hospitali ya Ifisi, nimekaa pale kama miezi miwili, tangu tarehe 18 Julai hadi tarehe tisa Novemba, mwaka jana.”

Ngulo mwenye Wake wawili na watoto wanne analizungumzia tukio hilo kwa uchungu, anaumia kwamba hawezi tena kuwahudumia “kinyumba” wake zake hao kutokana na kuharibiwa nguvu zake za kiume.

Hata hivyo, anaamini wanayaelewa masaibu anayokabiliana nayo kutokana na ukweli kwamba aliwaoa akiwa mzima na alikuwa akiwahudumia kama mume wao kabla ya kukutwa na unyama aliofanyiwa na huyo kaburu.

Kama uthibitisho wa mtazamo hasi alionao dhidi ya Watanzania hao, Kaburu huyo wanayemtaja kwa jina moja la Geri hakutoa msaada wowote wa matibabu kwa kijana huyo mfugaji pamoja na unyama wote huo aliomfanyia.

Unyanyasaji unaofanywa na kaburu huyo dhidi ya wananchi wa kijiji hicho, umewafikisha mahali wanahoji umakini wa serikali kuwakaribisha na kuwakumbatia jamii hiyo iliyoasisi itikati ya ubaguzi maarufu kama “apartheid. “

“Afrika Kusini imepata uhuru 1994, sasa hawa makaburu wamesafishika kiasi gani kuweza kukubaliana na sera za ujamaa, kauziwa ardhi na watu, aliamini sisi wote tu vibarua wake, tunapokataa haelewi, huo ndio mfumo wa maisha yake,” anasema Jairo Kiule wa kijiji hicho cha Kapunga.

Msimamo wa Serikali mkoani Mbeya

Imekuwa kama ndoto ya mchana, kwamba serikali mkoani Mbeya safari hii imeguswa na masaibu yanayowasibu wananchi hao wa Kijiji cha Kapunga pamoja na vijiji vya jirani, kutokana na uwepo wa mwekezaji huyo, ni msimamo ulio tofauti sana na uliokuwepo tangu mashamba ya Kapunga na Mbarali yalipotangazwa kuuzwa hadi Desemba 2010.

Kwa mara ya kwanza serikali imemfikisha mahakamani meneja mmoja wa shamba hilo kutokana na hatua ya mwekezaji kunyunyizia dawa kwenye mashamba ya wananchi, ekari 494.5 za  mpunga na kuyaunguza.

Wananchi 154 waliathirika na kitendo hicho cha kinyama na kusababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 718.

Kufikishwa mahakamani kwa kaburu huyo kunatokana na msimamo wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro ikielezwa kuwa alitamka wazi kwa uongozi wa jeshi hilo mkoani hapa kwamba hatakubaliana nao kama “kaburu” huyo hatafikishwa mahakamani.

Mbali ya serikali ya mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali, Cosmas Kayombo naye hakubaliani na vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na viongozi wa shamba hilo, na taarifa kutoka ofisi ya mkuu huyo wa wilaya zinaonyesha kuwa alishawahi kumtahadharisha mwekezaji kuhusu msimamo wake wa kunyunyizia dawa kwenye mashamba ya wananchi.

“DC alidokezwa na mmoja wa wataalamu waliofika pale shambani kuhusu msimamo wa mwekezaji huyo kunyunyizia dawa mashamba ya wananchi akidai wanalima ndani ya shamba lake, alimuonya asinyunyizie, lakini yule kaburu jeuri, alipuuza na kuendelea na uamuzi wake huo,” kinaelezea chanzo chetu kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbarali.

Tayari kesi hiyo ipo mahakamani na kwa mara ya kwanza kaburu huyo alifikishwa mahakamani na kupewa dhamana.

Mbali ya kufunguliwa kwa kesi hiyo dhidi ya kaburu huyo, serikali ya mkoa imechukua hatua zaidi kwa kuwasiliana na watalaamu kutoka Wizara ya Kilimo na tayari Mkurugenzi Matumizi Bora ya Ardhi, Mhandisi Paul Tarimo, ameshafika shamani hapo na kituo cha utafiti wa dawa ya kilimo kilichopo Arusha walimtuma Mhandisi Julius Paul kuchunguza dawa yaliyopuliziwa kwenye mashamba ya wananchi.

Wananchi wanasemaje?

Wananchi wengi hawamhitaji tena mwekezaji huyo kuendelea kumiliki shamba hilo, wanaitaka serikali imnyang’anye na kama haina fedha wao wako tayari kumrudishia fedha zake.

“Wananchi tupo tayari kumrudishia pesa yake, hizo shilingi bilioni 2.5 tulimiliki wenyewe pamoja na serikali, hata wakati wa uuzaji tulikuwa tayari kulipa zaidi ya shilingi bilioni tatu, CRDB walikuwa tayari kutukopesha, kilichotushangaza ni serikali kumuuzia huyo mwekezaji tena kwa kiwango cha chini ya kile ambacho sisi tulikuwa tayari kulipa,” anasema mwanakijiji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwashikumbulu.

Msimamo wa wananchi hao unatokana na ukweli kwamba tangu kuwasili kwa mwekezaji huyo uhusiano wake na wananchi hauridhishi, anadaiwa kuwanyanyasa wananchi hao, lakini wakati wote huo viongozi wa serikali kuanzia wilayani hadi taifa wakiangalia bila kuchukua hatua.

Pamoja na unyanyasaji wananchi, uzalishaji katika shamba hilo la Kapunga unaelezwa kushuka mno kutokana na hatua ya mwekezaji huyo kutolima na badala yake hukodisha kwa wananchi tena kwa gharama kubwa, tofauti na miaka sita iliyopita wakati likilimwa na wananchi.

“Mgogoro wa Kapunga ni wa muda mrefu, vyombo vya habari mmeripoti, serikali imeambiwa lakini hadi leo iko kimya, kwa hiyo tutegemee umwagaji damu huko mbeleni.

Miongoni mwa viongozi wenye kulaniwa na wakulima hao ni pamoja na Joseph Mungai ambaye wakati wa uuzaji mashamba hayo alikuwa Waziri wa Kilimo na Juma Ngasongwa, aliyekuwa na dhamana ya uwekezaji. Mawaziri hao wa zamani wanadaiwa kuhusika kushinikiza shamba hilo kuuzwa kwa mwekezaji aliyepo na kuwakandamiza wananchi hao walipohitaji kulinunua.

“Mungai na Ngasongwa walikuja hapa, wakalazimisha mwekezaji kupewa shamba, wakatuambia tukae mkao wa kula lakini huu ni mkao wa kufa,” anasema mwanakijiji mmoja na kuongeza;

“Tangu aingie mwekezaji uchumi wetu umeporoka, maendeleo ya familia yaliyokuwepo mwaka 2005 na miaka mingine ya nyuma hayapo tena, analazimisha wananchi kuhama, mwaka 2006 alichoma moto nyumba 18 za wananchi, amenyang’anya baiskeli zaidi ya 70 za wananchi, hajenga shule ya msingi kama ilivyo kwenye maandiko ya mradi, ametimua walimu kwenye nyumba za shamba.”

Wananchi hao wanawaona Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Kayombo ni viongozi wanaotoa nuru mpya kutokana na jinsi wanavyolishughulikia tatizo la shamba hilo, ikiwa ni tofauti na watangulizi wao.

Msimamo wa wananchi hao ni kwamba hawako tayari kumuona mwekezaji akiendelea kumiliki shamba hilo, wanataka wakabidhiwe wao kwani serikali imekiuka makubaliano ya awali ilipoomba eneo hilo, wakati wa kuuza hawakuwashirikisha pamoja na ukweli kuwa ndio wenye hiyo ardhi na sehemu ya shamba hilo kama inavyojibainisha katika andiko la mradi.

Inaendelea...

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako