Ripoti Maalum
Ukaburu wilayani Mbarali III
Felix Mwakyembe
Toleo la 230
14 Mar 2012
  • Watafiti wahadharisha kuhusu mikataba ya ardhi kama Kapunga

KAMA ilivyokuwa katika toleo lililopita la gazeti hili, leo, Mwandishi Wetu, FELIX MWAKYEMBE wa Nyanda za Juu Kusini, anaendelea kueleza alichobaini kutokana na uchunguzi wake kuhusu mgogoro kati ya mwekezaji na wanakijiji wa Kijiji cha Kapunga. Mgogoro kati ya pande hizo mbili unahusu shamba la mpunga lililopo katika Kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Leo anajikita katika athari za kiuchumi kwa wananchi wa kata za Chimala, Ihai na Itamboleo, ambao ni wadau wa ardhi hiyo.


WAKATI shamba la Kapunga wilayani Mbarali linabinafsishwa, wananchi waliokuwa wakilima katika shamba hilo waliweza kuzalisha hadi tani sita za mpunga kwa hekta moja, lakini leo hii uzalishaji shambani humo umeshuka hadi tani zisizozidi nne kwa hekta.

Kushuka kwa tija katika uzalishaji mpunga kwa wananchi wanaolizunguka shamba hilo kunahusishwa moja kwa moja na kukosa maeneo yenye miundombinu ya umwagiliaji, huku hata maeneo ya pembezoni walikokimbilia pia hunyanyaswa na mwekezaji kwa madai kuwa yote ni ardhi yake.

Ushahidi juu ya kuporomoka kwa tija katika uzalishaji wa zao hilo kwa wananchi wanaolizunguka shamba la Kapunga uko wazi. Ghala la mazao la Chimala ambalo hivi sasa hukosa mpunga wa kuhifadhi tofauti na miaka sita iliyopita, ni uthibitisho.

Kabla ya kuuzwa shamba hilo ghala la Chimala lilikuwa likijaa mpunga, kiasi cha kulazimu waendeshaji wa mradi wa stakabadhi ghalani kujenga mahema kuhifadhia mpunga nje ya ghala hilo. Hali hiyo ni tofauti kabisa leo hii.

Katika kipindi hicho cha ‘neema’, Chimala SACCOS, kupitia mpango huo wa stakabadhi ghalani, ilikuwa na uwezo wa kununua tani 3,368 za mpunga kutoka kwa wakulima wadogo, wakati leo hii wananunua kati ya tani 1,200 hadi 1,500 tu.

“SACCOS yetu inaendelea, ila mpango wa stakabadhi ghalani umeathirika kwa kiwango kikubwa kwa sababu hakuna mpunga wa kununua, kama sio kuuzwa kwa shamba lile leo hii tayari tungekuwa na benki yetu ya wananchi hapa Chimala,” anasema mkulima aliyefahamika kwa jina la Mwashikumbulu, kisha anatoa sababu za kushuka kwa kiwango cha mpunga unaonunuliwa kupitia mpango huo akisema; “kukosekana kwa miundombinu ya umwagiliaji kumeathiri sana uzalishaji mpunga, kabla ya shamba la Kapunga kuuzwa wananchi walilima katika shamba hilo na wale wa pembezoni walipata huduma ya maji bila tatizo.”

Wananchi walioathirika na uamuzi wa Serikali kulikabidhi shamba hilo kwa mwekezaji si wanakijiji wa Kapunga pekee, bali pamoja na wananchi kutoka kata tatu zinazozunguka shamba hilo ambazo ni kata mama ya Chimala, Ihai na Itambilo.

Ukubwa wa tatizo unajibainisha kwa njia nyingi ikiwamo ya idadi ya kaya, sambamba na idadi ya watu kwa Kijiji cha Kapunga. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2006 na 2007, kijiji hicho kina kaya 1,000 zenye watu 3,000.

Kwa ujumla, kata hizo tatu zinakadiriwa kuwa na wakazi takribani 20,000 na endapo idadi ya wananchi kutoka nje ya kata hizo waliokuwa wakilima kwenye shamba hilo kabla ya kubinafsishwa ikijumuishwa, basi waathirika wa uamuzi huo wa Serikali wanakadiriwa kuzidi 20,000.

Shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi hawa ni kilimo cha mpunga kinachotajwa kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa miji ya Chimala, Igurusi na mingine midogo iliyopo kati ya Igawa na Jiji la Mbeya, pembeni  mwa barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya.

Hatua ya Serikali kuliuza shamba hilo pamoja na lile la Mbarali ilitosha kuporomosha uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo na ni hatua iliyopingwa kwa nguvu zote na wataalamu wa masuala ya uchumi wa kilimo pamoja na wanahabari, hususan kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Wadau wote hawa waliamini kuwa ni hatua ya kuwanyang’anya wenyeji (wananchi masikini), nguzo yao pekee ya kiuchumi na kumkabidhi tajiri mmoja mgeni.

“lilikuwa kosa kubwa sana kuuza shamba lile, kwa mfano iwapo lilikuwa likiingiza shilingi bilioni 10, fedha hiyo ilisambaa kwa watu zaidi ya 20,000, kwa kumkabidhi mtu mmoja hata kama atazalisha, ina maana ile shilingi bilioni 10 inaondolewa kwa wananchi wale masikini zaidi ya 20,000 na kumkabidhi mtu mmoja tena mgeni, ni Tanzania tu unakoweza kukutana na vihoja vya namna hiyo,” anasema mchumi mmoja wa masuala ya kilimo.

Taarifa kutoka idara ya ardhi wilayani humo zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya eneo la Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya liko ndani ya hifadhi ya taifa, kwa  mantiki hiyo, wananchi hawaruhusiwi kuendesha shughuli zao zozote ndani ya eneo hilo.

Mgawanyo halisi wa ardhi wilayani humo ni kwamba kati ya hekta milioni 1.6 za wilaya hiyo, hifadhi pekee inahodhi hekta 960,000 ikiwemo ardhi oevu ya Ihefu, wakati ardhi inayofaa kwa kilimo ni hekta 321,500 huku eneo linalolimwa likiwa ni hekta 160,00.

Kutokana na ardhi kubwa ya wilaya hiyo kuingia kwenye hifadhi ya taifa, wananchi wamejikuta katika wakati mgumu wa kupata maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi, hususan kilimo cha mpunga ambao ni zao kuu la biashara.

Wadau mbalimbali wa kilimo walipendekeza mashamba hayo kuendelea kuwa chini ya usimamizi wa Serikali lakini yakilimwa na wananchi, na ni kwa kufanya hivyo ndipo ingetekeleza kwa vitendo kaulimbiu yake iliyoiingiza madarakani mwaka 2005 ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania.”

“Watanzania sio masikini, ni matajiri, kinachotakiwa ni kupewa fursa, utajiri upo katika kilimo, tunaomba huyu mwekezaji atoke,”anasema Elibauli Mwinuka ambaye ni mkulima katika Kijiji cha Kapunga.

Wananchi hao wamebaki wakiishangaa Serikali kwa kaulimbiu na sera ambazo kwa vitendo inashiriki kuzibomoa, kama anavyoshangaa mkulima mwingine wa kijiji hicho, Sekela Sandube.

Sandube anapohoji;  “Malengo hayajafikiwa zaidi ni maumivu tu, malengo ya maisha bora kwa kila Mtanzania ni maisha feki kwa kila Mtanzania, wana Kapunga tulikuwa na uwezo wa kulima ekari nne hadi kumi, lakini leo hata ile moja ni shida, tulikuwa na uwezo wa kusomesha watoto, leo hii hatuwezi tena, biashara hakuna,” kisha anaishangaa kauli ya kilimo kwanza akisema; “Kilimo kwanza unalima wapi ardhi amepewa huyo mgeni wanayemwita mwekezaji, halimi anakodisha, ploti nyingi ni nyasi.”

Wakulima hao si kwamba wanashindwa kusomesha watoto tu, hata ujenzi wa nyumba bora umesimama baada ya uchumi wa wao kuporomoka kutokana na kuuzwa kwa shamba hilo huku eneo kubwa la ardhi likichukuliwa na Serikali kwa kuliweka katika hifadhi ya taifa.

Wananchi wilayani ni wakulima wasiosubiri kuchapwa viboko ndipo waende shambani, kilimo ni ajira yao na wamethibitisha kuwa uwezo huo wanao kwani ndio wanaongoza kwa uzalishaji wa mpunga nchini. Wao wanaamini kuwa kuwanyang’anya ardhi yao na kumkabidhi mgeni kwa mgongo wa uwekezaji usiokuwepo ni kutia ufukara, ni uonevu uliofanywa na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

“Kama Serikali haina pesa ya kumrudishia huyo mwekezaji wao, wananchi wa Kapunga tupo tayari kumrudishia, tunao uwezo, shamba lirudishwe mikononi mwa wananchi,” anasema mkulima Ismail Mbwile.

Migogoro ya ardhi imejitokeza kuwa moja ya matatizo makubwa nchini hivi sasa, na hakuna dalili kwamba Serikali inashitushwa na hali hiyo pamoja na hadhari zinazotolewa kupitia mashirika mbalimbali ya kimataifa, hususan yanayojishughulisha na tafiti za ardhi duniani.

Taarifa ya Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) iliyotolewa Februari, mwaka jana iliweka wazi jinsi mataifa ya Afrika,Tanzania ikiwemo, yanavyojiweka katika hatari kwa kuwapatia wawekezaji maeneo makubwa ya ardhi kupitia mikataba yenye usiri, kama huo wa shamba la Kapunga wilayani Mbarali.

Taasisi hiyo ilibainisha kuwa mbali ya usiri, mikataba hiyo ya ardhi haijathibitisha kuwa ya manufaa kwa nchi za Afrika.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa miongoni mwa mikaba mingi iliyopitiwa wananchi wamekuwa hawashirikishwi katika ngazi za uamuzi na kwamba ni Serikali ambayo huamua, huku ikionyesha ahadi tu za mwekezaji, kama vile kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wanaozunguka eneo la uwekezaji, ahadi ambazo hata hivyo hazitekelezwi.

Inaelezwa na watafiti hao kuwa, wananchi ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji na wawindaji wangeweza kuitumia ardhi hiyo kwa vizazi vyao vyote hivyo kuiona kuwa ni mali yao.

Hali ya uuzaji wa shamba la Kapunga haiko mbali na ukweli uliobainishwa na watafiti hao, wananchi walifichwa katika mchakato wa uuzaji wa ardhi yao, wakalazimishwa kumkubali mnunuzi aliyeitwa mwekezaji, ambaye mpaka sasa hajathibitisha uwezo wake katika kilimo hicho cha mpunga na ni wazi amechangia katika upungufu wa chakula, hususan mchele nchini.

Inaendelea...

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako