Ukamilifu wa ubinadamu wetu utathibitishwaje na wageni?

UTAMADUNI wa jamii yeyote ni kama mfumo wa mishipa inayosafirisha damu kutoka sehemu mbalimbali za mwili hadi kwenye moyo. Nakumbuka shule ya msingi tuliimbishwa wimbo mmoja uliosema: “Taifa Lisilo na Utamaduni ni Sawa na Lililokufa”. Kwamba “Utamaduni ni Mhuri Unaomtambulisha Mtu na Asili Yake”. Kuacha (au kuachishwa) utamaduni wako na kudakia (au kudakishwa) wa mgeni jumla jumla ni sawa na kuondoa mishipa yako ya asili inayosafirisha damu mwilini pamoja na moyo wa asili na kuwekewa vya plastiki.

Lakini kabla sijaendelea na kusisitiza umuhimu wa utamaduni, sina budi kutoa angalizo mapema. Hakuna, kokote kule, ambako utamaduni hai unaishi kama ulivyo bila marekebisho ya hapa na pale au bila kukaribisha vionjo fulani fulani kutoka tamaduni zingine. Na wakati mwingine zipo mila fulani fulani huonekana zimepitwa na wakati au madhara yake yakawa wazi zaidi kwa jamii na hivyo zikaachwa kwa manufaa ya jamii husika na si kwa shinikizo kutoka kwa wageni. Hivyo msisitizo wangu ni kwamba utamaduni pia hukua.

Jamii zote duniani zinazoishi sasa haziwezi kuwa zinafuata mila na desturi zote za miaka 2,000 iliyopita kama zilivyofuatwa na babu na bibi zao. Lakini, kwa mfano, bado ukifuatilia ndugu zetu Wachina au Wahindi unabaini hawajaruhusu usasa kufuta mizizi ya tamaduni zao zinazowatambulisha asili yao na zinazobeba dhima ya dira ya jamii zao.

Umuhimu wa utamaduni katika maisha ya wanadamu hasa katika kuchangia maendeleo yao umeelezwa katika historia ya jamii mbalimbali duniani. Ni kweli na wazi kuwa zipo tamaduni ambazo zinaonekana kama hazichochei watu kufanya mabadiliko ya kuboresha maisha yao. Na kwamba zipo tamaduni zingine zinazochochea watu kutaka kuboresha maisha yao kila siku.

Lakini inaonekana dhahiri kwamba kwa asili, jamii ya binadamu yeyote kamili huwa na sifa kuu zifuatazo: Kwanza ni sifa muhimu ya kujinusuru. Jamii hufanya kila linalowezekana kuhakikisha hazifutwi katika uso wa dunia ama kwa majanga asilia, ikiwamo kuliwa na wanyama wakali, au kwa vita na matukio mengine kama hayo. Na sambamba na sifa hii ni sifa ya kujidumisha kwa kuhakikisha kizazi kinaendelezwa kwa njia ya kuzaliana. Pili ni sifa ya kujilisha. Jamii hufanya kila linalowezekana kuhakikisha hazifi kwa njaa au utapiamlo kwa sababu ya kukosa chakula na lishe ya kutosha.

Tatu ni sifa ya kujihifadhi. Jamii hufanya kila linalowezekana kuhakikisha zinajihifadhi salama kukidhi mahitaji ya mazingira zinamoishi ili kuhakikisha haziadhiriki wala kuathirika kutokana na kukosa makazi na malazi salama (ikiwamo sehemu ya kujihifadhi kweli). Nne ni sifa ya kujiendeleza. Jamii hufanya kila linalowezekana kuhakikisha zinajifunza kutokana na uzoefu, maono, vipaji na utafiti na kurithisha mafunzo haya kwa watoto na vijana ili kujiendeleza. Mafunzo haya huhusu namna watakavyoendesha familia, namna ya kutawala rasilimali na mazingira yanayowazunguka na jinsi ya kuchangia kuhakikisha jamii inajinusuru, inajihami na kujiendeleza.

Tano ni sifa ya kujiboresha. Jamii hutumia uzoefu, utafiti, maarifa, vipaji na uwezo mwingine zilio nao katika kijiboresha au kuboresha hali za maisha ya wanajamii. Kwa mfano; kama huko nyuma akina mama (natumia mfano halisi) walipaswa kubeba vyungu vikubwa vya maji na kutembea kilomita zaidi ya kumi kuteka maji na kurejea nyumbani; lakini baadaye mwanajamii akabuni na kutengeneza mkokoteni wa kukokotwa na ng’ombe ili ufanye kazi ile iliyokuwa ikifanywa na mama. Kwa maana hiyo, ubunifu wa usafiri wa mkokoteni unampunguzia mzigo, maumivu na adha mama yule ambaye sasa hutumia muda wake kwa shughuli nyingine inayomhitaji na isiyomuumiza.

Sita ni sifa ya kujihami. Jamii hufanya kila linalowezekana kuhakikisha zinajihami na kujilinda dhidi ya tishio lolote liwe la nguvu ya aina yoyote au maradhi. Na katika kujihami, jamii pia huhakikisha zinalinda watu wake wote na rasilimali zake zote dhidi ya uporaji wa aina yoyote ili kukidhi ‘hitaji’ (mahitaji) namba moja la kujinusuru na kujidumisha. Sambamba na dhana ya kujihami dhidi ya vitisho vya kisiasa, jamii pia hufanya kila liwezekanalo kuhakikisha zinawawezesha wanajamii kujihami kisaikolojia.

Saba ni sifa ya kujistarehesha. Jamii baada ya kujihakikishia zimejinusuru, zimejilisha, zimejihifadhi, zimejiendeleza, zimejiboresha, zimejihami, zinafikia sasa fursa ya kujistarehesha na kufurahia maisha.

Huenda kila msomaji angependa aamini kwamba kabla ya ujio wa wakoloni jamii zetu zilikuwa zikiishi kwa kufuata sifa saba za msingi nilizozitaja hapo juu. Na kwamba ujio wa wakoloni haukuleta jambo lolote jipya katika kuwafundisha babu na bibi zetu kuhusu umuhimu wa sifa hizo saba zinazomtambulisha binadamu kamili, bali walichokifanya ni kuleta mtazamo wao wa kuziangaliaa sifa hizo.

Na ilikuwa katika mtazamo wao wa jinsi binadamu kamili anavyopaswa kuishi ndipo walipofanikiwa kuwaaminisha wengi wa babu na bibi zetu kwamba maendeleo maana yake ilikuwa ni usasa. Na kwamba wao wenyeji wasingeweza kamwe kuendelea endapo wangelibakia na ukale wao, imani zao, mila zao, majina yao, tamaduni zao. Kwamba wakoloni walifanikiwa sana katika kuvuruga utamaduni wa Mwafrika wakijua fika umuhimu wa kufanya hivyo halina ubishi hata kidogo.

Wiki iliyopita nilitoa mfano rahisi tu wa majina ya watu kuonyesha jinsi wakoloni na wageni wengine kutoka nje ya bara hili walivyofanikiwa kuteka fikra za Mwafrika na kuua utamaduni wake huku wakipandikiza tamaduni zao. Na kama nilivyoeleza huko nyuma mtu anayekuja kwako na kukuambia jina lako ni la ovyo kuanzia leo itwa fulani - ukakubali; akakuambia yeye kavumbua Mlima Kilimanjaro na wakati kakukuteni mnaishi pale miaka na miaka – bado ukakubali; au akakwambia dini yako ya ovyo kuanzia leo abudu dini hii – na wewe ukaacha yako ukafuata yake (ikiambatana na utamaduni wa kabila lake);

Au akakueleza uvaaji wako ni wa ovyo, kuanzia leo vaa hivi (huko mbele nitajadili suala la vazi la taifa kwa udadisi zaidi) – na wewe ukatii. Au akakuambia mila zako za kishenzi kuanzia leo ishi hivi – nawe ukatii; au akakuambia unakula chakula kishamba kuanzia leo kula kwa utaratibu huu – ukafuata bila kuhoji; na kadhalika na kadhalika. Endapo wewe unayeambiwa hivyo utatii kila unaloambiwa na mgeni yule bila kuhoji, utakuwa unamsaidia katika kuhitimisha nadharia aliyokuwa nayo awali kwamba huenda wewe si binadamu kamili.

itaendelea

Comments

je watanzania tutatokaje huko maana kilakitu cha majuu ndio tunachoshabikia

Tukilielewa somo lako  Ndugu Lioba hatutakuwa na makafiri,walokole boko haraam,shabab nk. Kwani tutakuwa tumerudi kwenye imani zetu za asili,babu na bibi zetu wamjua mungu pia. Tunaona fahari kujitambulisha kwa imani za wazungu au waarabu.Natamani kuiona afrika inarudi kwenye asili yetu.Wachaga,wanyamwezi,wahaya,wasukuma,wanyakyusa,wahehe nk tutaniana tu katika njia zetu za kuabudu.sio chuki kama tulivyo sasa.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.