Unapomwona jogoo anamfukuzia mtetea!

KUNA siku nilimwona jogoo anapita mbele yangu akimfukizia kuku mtetea. Nikarusha kipande cha mkate katikati ya jogoo na mtetea.

Jogoo yule akaacha kumfukizia mtetea. Akasimama na kwa mdomo wake akakiweka mdomoni kipande kile cha mkate. Jogoo hakuendelea tena kumfukizia mtetea.

Tendo lile la jogoo lilinishangaza na kuniacha nikitafakari. Nilidhani jogoo angekiacha kipande kile cha mkate na kuendelea kumfukuzia mtetea.

Masikini, mtetea hakuwa muhimu tena kwa jogoo mbele ya kipande cha mkate.

Tofauti na jogoo yule, wanadamu tunapaswa kuwa na malengo juu ya yale tunayoazimia kuyatenda. Hata kama si kufukuzia tuwapendao, kimapenzi!

Ndugu yangu Profesa Joseph Mbele anachangia kisa hiki cha jogoo na mtetea kwa kuniambia; “Enzi za Mwalimu Nyerere, tangu tulipopata Uhuru, tulikuwa tukifukuzia ukombozi, kujenga jamii yenye usawa, inayojitegemea, inayojiheshimu, yenye msimamo wa kulinda maslahi na heshima yake mbele ya mataifa.

Hayo yote yaliwezekana sababu ya uongozi bora. Timu nzima ya uongozi ilikuwa imara.

Mwalimu Nyerere alipong’atuka tu, ghafla bin vuu mabeberu wakarusha kipande cha mkate, na hao waliopaswa kuwa viongozi wakaanza kufukuza mkate. Ndio ufisadi unaotumaliza leo,” anasema Profesa Joseph Mbele.

Kuna wakati Wole Soyinka, mwandishi mahiri wa Bara la Afrika alipata kutamka; “A moral decay is a corruption” – kwamba uoza wa kimaadili ni rushwa pia.

Leo katika nchi hii hatushangai wala hatuhoji  tunaposoma  magazetini kuwa mbunge au waziri fulani anatoa mchango  wa shilingi milioni mia tano jimboni kwake, tena kutoka mfukoni mwake.

Hatujiulizi; amezipata wapi fedha zote hizi? Hatujiulizi, hivi waziri ni wa jimbo au wa taifa? Je, milioni zikimwagwa jimboni haiwezi kuwa na maana ya ‘kulinunua’ jimbo na kulifanya kuwa himaya yake?

Nisingependa kuamini kuwa tumefika mahali pa kukata tamaa kabisa, lakini nahofia, kuwa ukweli tunakwenda huko. Mambo yasiyofikirika katika akili ya kawaida yanafanyika mchana wa jua kali.

Kuna wanaotutaka tuone kuwa ni ya kawaida tu. Hii ni hatari kwa taifa letu. Umma wa Watanzania ukatae kugeuzwa kondoo. Ukatae kuswagwa kama kondoo. Tupelekwe kule baadhi wanapotaka wao twende.

Umma wa Watanzania haukuundwa na watu wajinga-wajinga tu. Kuna Watanzania wengi wanaoona, wanafikiri. Watanzania wamekaa kimya, lakini iko siku watasema; “Sasa  basi, inatosha”

Umma wa Watanzania unaelewa, kuwa wanachoonyeshwa sio hali halisi. Akili ya kawaida inatuambia kuna matumizi  makubwa ya fedha  za Serikali kwenye mambo yasiyo ya faida kubwa kwa watu. Baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi wameacha  kufukuzuia maendeleo ya wananchi. Wanafukuzia mikate yao, ulaji wao.

Fedha zinazotumika  kufanya sherehe na mambo ya anasa, ikiwamo safari zisizo na tija. Fedha zinatumika katika kugawana posho. Hazi ni fedha za wananchi.  Ufujaji na ubadhirifu wa mali ya umma imekuwa ni jambo la kawaida.

Tunalazimika kukemea  matendo haya maovu.  Kwamba viongozi wanatumia fedha kuwahonga wananchi kwa kisingizio cha kuwapa misaada.

Na kuna kauli za baadhi ya viongozi waandamizi zinazotolewa kutetea ‘uoza’ huu wa kimaadili. Busara ni kuacha kuendelea kutoa kauli hizi. Zinawakera Watanzania, zinatia kichefuchefu. Kiongozi makini ajipambanue na kutokubali kuwa miongoni mwa wenye kutenda maovu. Haitoshi kwa kiongozi kujipambanua kwa matendo yake. Kiongozi ajipambanue kwa kauli zake pia. Aonyeshe msimamo wa kauli hadharani. Umma utamheshimu, kinyume chake umma utapunguza imani kwake.

Kutetea ‘uoza’ huu hadharani ni kuwachanganya wananchi. Wananchi wanakosa imani hata kwa baadhi ya viongozi ambao walianza kuwaamini. Wanashindwa kuona tofauti. Wanaowaona ni ‘miongoni’ mwa hao wanaotetewa kwa maovu  waliyoyafanya.

Na hapa kuna suala la msingi lenye kuhusu imani. Kiongozi makini atapigania kubakiza imani ya  umma kwake. Kwa kiongozi muhimu ni kuwa na umma nyuma yake.  Kushiriki kutetea na kulinda maovu yanayofanywa na kundi dogo la viongozi kunahatarisha kupoteza imani kwa anaowaongoza.

Kinachoonekana sasa ni kwa baadhi ya viongozi kuwa mbali na umma. Viongozi kuwa mbali na hali halisi.  Baadhi ya kauli wanazotoa zinadhihirisha umbali huo kati yao na wanaowaongoza.

Kiongozi anayefahamu jinsi watu mitaani na vijijini wanavyoathirika na vitendo vya ufisadi hatopata kigugumizi kukemea na kulaani ufisadi kila anapopata fursa ya kufanya hivyo.

Kamwe, hawezi kutetea vitendo vya kifisadi ikiwamo matumizi ya mamilioni ya shilingi kwenye kufanya sherehe, semina na makongamano yasiyo na tija kwa mwananchi.

Hali ni ngumu kwa wananchi wengi. Ufisadi kwa maana ya rushwa kubwa ni chanzo kikuu cha hali hiyo. Rasilimali za wananchi zinatumika ovyo na kifisadi huku wananchi wakitaabika. Mikataba isiyo na maslahi kwa umma inatiwa saini kwa vile tu ina 10% ndani yake.

Tuna baadhi ya viongozi wenye utajiri wa ajabu kushinda hata hao wafadhili wanaotupa misaada. Yote hii inatokana na ubinafsi na uchoyo wa viongozi hawa. Wako tayari nchi inunue vifaa vibovu vya mamilioni ya dola za Marekani ili mradi wao wamehakikishiwa 10% yao.

Ni viongozi hao hao, ambao miaka kumi iliyopita walikuwa ni watu wa kawaida, leo ni mabilionea kwa njia haramu. Na hata wanapotuhumiwa, basi, wanatumia fedha kuficha madhambi yao. Wanachofanya ni  hadaa kwa umma. Ionekane kuwa wanakubalika.

Katiba mpya tunayokwenda kuiandaa iwe nyenzo na silaha pia ya kupambana na ufisadi na maovu mengine yanayofanyika katika nchi hii. Mathalan, Katiba iweke wazi, kuwa mbunge hawezi kuwa waziri au mkuu wa mkoa kwa wakati mmoja.

Katiba iweke wazi, kuwa kutakuwapo na ukomo wa kiwango cha fedha ambacho kiongozi wa kuchaguliwa au mtumishi wa umma anaweza kutoa kama zawadi kwa jamii.  Kinyume chake iwe ni kosa la jinai.

Naam, Katiba mpya itusaidie kuwafanya viongozi wetu wafukuzie zaidi maendeleo ya wananchi kuliko mikate yao. Inawezekana.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.