“Urais utamshinda Magufuli”

KAZI ya Urais itamshinda Rais Dk. John Magufuli kwa sababu yeye mwenyewe ameonyesha kutoipenda na hakuandaliwa wala kujiandaa kwa majukumu hayo, Raia Mwema limeambiwa.

Hayo ni sehemu ya maoni ya watu kadhaa waliozungumza na Raia Mwema wiki hii wakirejea kauli ya mwishoni mwa wiki iliyopita ya Rais Magufuli aliyewaambia Watanzania katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kwamba yeye “alijaribu tu kuomba nafasi hiyo lakini akajikuta amesukumwa kwenye nafasi hiyo”.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dk. Helen Kijo-Bisimba.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kutoa kauli ya namna hiyo; lakini mara hii viongozi wastaafu, wanasiasa na wanasheria wanaoheshimika nchini, wamejitokeza hadharani kuonyesha wasiwasi wao kuhusu kauli hiyo ya Rais.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, akizungumza na gazeti hili kutoka nje ya nchi, alisema kauli hiyo ya Rais inamaanisha kitu kimoja tu, kwamba hataweza kutekeleza majukumua yake hayo ipasavyo.

Sumaye amesema ya kuwa kwake ulikuwa ni mshituko mkubwa kwamba Rais, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alitoa kauli hiyo katika sherehe ambayo kimsingi ni ya kijeshi na wapiganaji wakiwa mbele yake.

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye

“Rais Magufuli alipokuwa Arusha juzi wakati wa sherehe za kuwatunuku nishani wanajeshi alisema, urais ni kazi ngumu sana na ‘anajuta kuwa rais’ na kwamba yeye alikuwa ‘anajaribu tu akasukumiziwa huko’. Haya ni maneno ya hatari sana kwa nchi hasa yanaposemwa na Amiri Jeshi Mkuu mbele ya wanajeshi.

“Kabla ya hayo maneno, Rais wetu amewahi kusema yeye si mwanasiasa na hawapendi wanasiasa. Rais pia amewahi kusema serikali haitatoa chakula kwa wananchi wenye njaa kwa sababu serikali haina shamba.

“Amewahi kusema wanaoishi kama malaika atahakikisha wanaishi kama shetani, suruali za zamani msizitupe mtazihitaji baadaye, watakaobakia Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli, na kadhalika.

“Katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Magufuli sote tumeshuhudia jinsi demokrasia inavyokandamizwa, Katiba na sheria za nchi kuvunjwa, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa vyombo vya habari kupokonywa, viongozi na wanachama wa vyombo vya upinzani kukamatwa au kupata mateso mbalimbali na mambo mengine ambayo hayakuwa utamaduni wetu.

“Kwa matendo hayo na misemo hiyo ya huko nyuma na mingine mingi, wengine tulikuwa tunashangaa kwanini Rais hana huruma na anatoa mwelekeo wa mateso kwa Watanzania anaowaongoza badala ya kuwa mfariji wao mkuu?

“Kwa maneno haya ya Arusha sasa tatizo tumelijua. Rais Magufuli tunakushukuru kwa kuwa muwazi. Tatizo ni CCM kutuwekea kwa nguvu mtu ambaye kazi hiyo ya urais haitaki, na kama kazi huitaki hutaiweza.

“Watanzania tunashangaa nini maisha yanapokuwa magumu hivi? Tunashangaa nini tunapoona biashara nyingi zinafungwa na wawekezaji wapya kutukimbia? Tunashangaa nini watoto wanapomaliza vyuo vikuu wakakosa ajira?

“Hivi nani alaumiwe kwa haya yote yanayotokea? Magufuli alikuwa anajaribu tu akasukumiziwa na chama chake. CCM tuambieni mnawezaje ‘kuisukumiza’ nchi kwa mtu asiyeutaka urais na hata sasa anajuta kuwa Rais?

“Tunataka CCM iwaeleze Watanzania kwanini imewawekea Rais wa majaribio na wakamsukumizia nchi? CCM imefanya hayo kwa kiburi cha kujiona kuwa chama pekee Tanzania. Kama CCM haitatujibu swali hilo tukaridhika, basi umma utaijibu CCM mwaka 2020”, alisema Sumaye.

Sumaye ni waziri mkuu mstaafu ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – chama alichohamia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 akitokea CCM ambako nafasi yake ya mwisho madarakani ilikuwa ni uwaziri mkuu katika serikali ya Benjamin Mkapa kwa kipindi cha miaka 10. Kabla ya kuhamia Chadema alijaribu bila mafanikio kupitishwa kuwania urais kupitia CCM.

Akizungumzi kauli hiyo ya Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alisema hata yeye hakuwa ameandaliwa kuwa Rais na chama chake mwaka 2010 lakini alilazimika kukubaliana na matakwa ya wenzake waliomwona anafaa.

Alisema kinachomtokea Rais Magufuli sasa kinafanana na hali yake ya wakati huo na akasema si vema kuichukulia kauli hiyo kwa uzito mkubwa kama wanavyofanya baadhi ya watu.

“Nadhani pale Rais Magufuli alikuwa anazungumza na wananchi wake. Pengine alikuwa anataniana nao tu lakini si maneno ya kuyachukulia kwa uzito. Mimi sikujiandaa kuwania urais mwaka 2010 lakini nilisukumwa na wenzangu ndani ya Chadema na nikawa mgombea. Haya ni mambo ya kawaida kwenye siasa,” alisema Dk. Slaa aliyezungumza na Raia Mwema kutoka nchini Canada anakoishi sasa.

Kwa upande wake, akizungumzana Raia Mwema  wiki hii, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema anaogopeshwa na kauli za mara kwa mara za Rais Magufuli kudai kwamba wakati anaomba urais kupitia CCM, alikuwa anajaribu tu.

Alisema Dk. Bisimba: “Inaogopesha. Mimi kwa kweli imeniogopesha kwa sababu si mara ya kwanza kusema maneno ya namna hiyo.

Tulitarajia kwamba angejidhatiti kwa kuchukua mifano ya kiuongozi kwa marais wastaafu waliomtangulia angalau marais wa vipindi vya hivi karibuni.”

Bisimba alioanisha kauli za sasa za Rais Magufuli na staili Rais magufuli ya kujitokeza kuwania urais kupitia CCM akisema pia ya kuwa  hakujipambanua kama mtu aliyefanya maandalizi ya kutosha.

“Na hata suala la kuchukua fomu alikuwa wa mwishomwisho. Na kama unakumbuka niliwahi kuhojiwa na kituo kimoja cha redio kama namuonaje mgombea aliyependekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais, nikamwambia mtangazaji kwamba namuona Magufuli kama mtendaji kuliko kiongozi.

“Mtendaji anaangalia katika eneo lake analolifanyia kazi, lakini kiongozi anaangalia maeneo mengi zaidi. Nikashauri wakati huo kwamba huyu (Rais Magufuli) alitakiwa apatiwe elimu ya diplomasia ambayo itamsaidia katika mawasiliano na watu wengi kama ambavyo watangulizi wake wa karibuni; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walipitia.

“Unapokuwa kiongozi mkuu wa nchi unatakiwa uwasiliane na vyama vya upinzani, mashirika mbalimbali pamoja na taasisi za kijamii katika kuhakikisha changamoto zinazokabili nchi zinapatiwa ufumbuzi. Na pia vilevile kwenye mambo ya kidiplomasia unatakiwa uwasiliane na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi wakiwamo mabalozi wanaowakisha nchi zao hapa Tanzania,” alisema.

Akitoa ushauri wake kwa chama kilichomuwezesha Rais Magufuli kuwa madarakani, alisema: “Nakishauri chama chake(CCM) wasijaribu tena kumpendekeza na akiona mambo magumu sana (Magufuli), Katiba ya nchi inamruhusu kuachia nafasi hiyo.”

Juhudi za kumpata Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, ili aseme chochote kuhusu kauli ya Rais na maoni dhidi ya kauli hiyo hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni ingawa zilifanyika juhudi za kumpigia simu na kumtumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi (CCM).

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa juu wa CCM aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yake alisema hashangazwi na maneno hayo ya Sumaye na mama Bisimba kwa sababu aliyatarajia.

“Unatarajia Sumaye atakuwa fair kwa Magufuli? Ni lini Bisimba aliitendea haki Serikali ya CCM? Ulisikia akipiga kelele wakati Watanzania wakiuawa Kibiti?

“ Sidhani kama kuna sababu ya kupoteza nguvu na muda kuwajibu akina Sumaye. Wao wasubiri mwaka 2020 waone kama wananchi hawatampa Magufuli ushindi wa kishindo kuliko ilivyokuwa mwaka 2015,” alisema kigogo huyo.

Na katika hatua nyingine,  mmoja wa waliokuwa wagombea kwenye nafasi ya urais kutoka CCM mwaka 2015 ambaye ametaka hifadhi ya jina gazetini ameshauri kwamba Magufuli aulizwe kwamba wakati anawania nafasi hiyo ya juu kabisa ya nchi matarajio yake yalikuwa nini?

“Muulizeni ni nani aliyemsukuma, na matarajio yake yalikuwa nini?”

Akizungumza na Raia Mwema, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu alisema: “Mimi nadhani ni bahati mbaya, ingawa wote tunafahamu kwamba Magufuli hakuwahi kujiandaa kuwa Rais na kwamba mtu ambaye alikuwa amejiandaa ni Edward Lowassa .

“Kwa hiyo yuko right (sahihi) kuwa hakujiandaa kuwa Rais. Moja ya kazi ya vyama vya siasa ni kuwaandaa viongozi na hili limempa matatizo kwa kuwa amesema ni mzigo mkubwa lakini ni mzigo kwa kuwa ameamua kuubeba peke yake,” alisema Profesa Baregu.

Kwa mujibu wa Profesa Baregu, suala analopambana nalo Rais Magufuli ni ufisadi ingawa ajenda ya ufisadi tangu mwanzo ilikuwa ikizungumzwa na kusimamiwa na vyama vya upinzani na si chama chake.

“Sasa hao wote waliyoiandaa ajenda hiyo unawanyamazisha. Ajenda hiyo wakati inajadiliwa Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri. Anauona mzigo mkubwa kwa kuwa hakuwa amejiandaa.

“Sasa sijui kwa kuwa aliamua kuubeba peke yake ili aonekane anapambana peke yake. Na mzigo huu unaweza kubebwa kidemokrasia tu kwa kuzungumza, kuelimishana hiyo kazi ilikuwa imeshaanza kufanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikisimamiwa na Mwenyekiti wa  Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, Katiba yenye kuonesha misingi ya Tanzania,” alisema Baregu ambaye ni mmoja wa wasomi wanaoheshimika nchini.

Akirejea kauli za Magufuli alizozitoa kwenye baadhi ya mikutano yake, Profesa Baregu alisema jambo la Rais Magufuli la kujaribu na kusukumwa kuwa Rais amekuwa akilirejea zaidi ya mara mbili sasa.

Alisema: “Hili jambo analirudia mara mbili au tatu. Si jambo zuri kuwakumbusha Watanzania kwamba ana maadui wakubwa (Rais). Akumbushwe kwamba suala la kudai Katiba mpya si ajenda yake bali ni ajenda ya Watanzania ambayo wamekuwa wakiitetea.

“Kama ni kupunguza mzigo kwenye kushughulikia ufisadi na rushwa, ni vyema kurudisha mjadala wa Katiba Mpya ambapo mambo hayo yatatatuliwa kuliko ilivyo hivi sasa tumbua tumbua ambayo haitatufikisha popote zaidi ya watumbuliwa kushinda kesi na baadaye kurudishwa kazini,”alisema Baregu.

Akiwa kwenye sherehe ya kuwatunuku kamisheni baadhi ya maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine Rais Magufuli alisema kwamba, ameamua kuwa sadaka ya Watanzania.

“Nimeamua kuwa sadaka ya Watanzania kwa ajili ya kuwanyoosha mafisadi. Hamjui mateso ninayopitia, ni shida kuwa Rais, nimeyaona mateso kuwa Ikulu, niliomba kwa kujaribu nikasukumwa huko.

“Sababu niliingia bila kutoa rushwa lazima nifanye kazi kwa ajili ya Watanzania, hakuna fisadi aliyenichangia hela hivyo sitaogopa kumtumbua yeyote na nitawatumbua kwelikweli, ” alisema.

7 thoughts on ““Urais utamshinda Magufuli””

 1. Massanda O'Mtima Massanda says:

  Kwani, maneno haya yanaoneshaje kwamba hakujiaandaa na kwamba uraisi hauwezi?:
  “Nimeamua kuwa sadaka ya Watanzania kwa ajili ya kuwanyoosha mafisadi. Hamjui mateso ninayopitia, ni shida kuwa Rais, nimeyaona mateso kuwa Ikulu, niliomba kwa kujaribu nikasukumwa huko.

  “Sababu niliingia bila kutoa rushwa lazima nifanye kazi kwa ajili ya Watanzania, hakuna fisadi aliyenichangia hela hivyo sitaogopa kumtumbua yeyote na nitawatumbua kwelikweli, ” alisema.

 2. asaka says:

  Nakubaliana na Dr. Slaa (nasikiliza bendi ya kampeini 2010 inayoelezea ”Dr. Slaa anaweza sana). Nyerere pia alishasema huko nyuma, kazi yake aipendaye ni Ualimu, na Urais/uongozi ilibidi aifanye kwa kuhitajika, pia alisema Ikulu si pa kukimbilia, ni mzigo mzito sana. Sasa kwa manaeno hayo utamuelewe Magufuli, na anafanya kazi kweli kweli kuwatumikia wananchi na Tanzania kama Nyerere, Sokoine, Kawawa, Salim Salim etc.. Kuna watu wapendao vyeo na kazi kubwa zenye hadhi kwa maslahi binafsi, ufahari, maisha ghali sana, sifa za kijinga na hawana haja ya kuwatumikia watu, bali wao watumikiwe. Nimekutana na watu wengi sana wenye sifa hii mbaya sana. Mtu kama magafuli anaweza kutembea na miguu barabarani ili aone wananchi wa kawaida wanaishije na matatizo yao na pia vipi maofisa wa chini yake na ”civil servants’ wanawatumikiaje wananchi. Wapendao vyeo na ufahari hutawakuta kwa hayo, zaidi ya kuwa kwenye magari ghali sana ya kifahari na kwenye tafrija zisizo na tija yoyote zaidi ya kunywa mvinyo ghali na pilau ya biriani. na wanapenda kisifiwa na wapambe, wanafiki watakao maslahi tu

 3. Sallu Bucheyeki says:

  Wasukuma wamegawanyika mara nne.Kuna wasukuma wa Mashariki; Kaskazini, Kusini na Magharibi.

  JPM, ni msukuma wa Magahribi ambao wanasifika kwa semi za ki lugha za utani na mafumbo. Ukikaa na wasukuma wa Magharibi sharti kichwa chako kiwe na weledi mkubwa wa kufumbua mafumbo yao. Vinginevyo, utaishia mtu wa kukariri na kuelewa jambo ambalo wenzio hawana maana ile!

  Kauli za mheshimiwa, mara ingine hubeza ujumbe wenye utani na mafumbo! Kwa mfano, mwenzio anaweza amefurahi kuwa kiongozi wa ngazi ya juu wa taifa lakini katika kujieleza akajifanya hajapenda kupata mamlaka yale katika kuondoa kile watu wangedhania ‘anajivuna’ kupitia kauli!

  Nadhani, hili ndilo linalofanyika. Hakika kuelewa maana halisi ya kauli za wasukuma wa Magharibi ambao huitwa ‘Banang’weli’ sharti uwe na kichwa chenye upeo wa kujua utani na kupambanua mafumbo.

 4. Abdulla Traore says:

  Hii ndiyo makala iliyofanya gazeti kufungwa? Mbona iko balanced. In fact, katika mataifa yaliyostaarabika (civilized nations) , makala hii ingekuwa kichocheo tu cha maoni ya aina tofauti katika mitandao.
  Zamani nilikuwa napinga istilahi hiyo ya (civilized nations), lakini sasa naanza kuamini kweli kuna ‘mataifa yaliyostaarabika’ na ‘mataifa mashenzi’

 5. scholatitus says:

  Ana maana Wakati anachukuwa fomu ya kugombea hakujuwa Tanzania kulikuwa na uwozo kama huo. Nchi ni rahisi kuiongoza kama uongozi uliopita ulikuwa mazuri. Mimi nafikiri Pamoja na upungufu Rais Magufuli amefanya kazi ngumu sana. Sio rahisi kuongoza watu waliozowea kuishi kwa dili, sio rahisi kuongoza wavivu, sio rahisi kuongoza watu wasioelewa, sio rahisi kuongoza watu waliozowea kuiba pesa za umma bila ya kukemewa, na sio rahis kuongoza watu wenye upungufu wa Elimu ni kazi kubwa kuwaelewesha. So far Hakuna mwingine, wengi ni kusema tu na kupinga. Demokrasia sio tu Freedom of speech. Demokrasia ni zaidi ya hayo. Wale wanaosema Wakati wa Kikwete kulikuwa na Demokrasia hawasemi ukweli. Watu walikuwa wakinyang’anywa mashamba yao, hata wakilalamika Pamoja na magazeti walikuwa hawasikilizwi. Mwenye pesa ndiye alikuwa Mwenye sheria. Wenye pesa walikuwa hawalipi kodi, masikini wakilipa kodi. Macontainer yakipita bandalini bila ya kodi. Ni mengi uwozo wa kutosha. Tumuachie Rais Magufuli afanye kazi yake pale wengi walishindwa na kuwaunga mkono mafisadi.

 6. Remarua Mondosha says:

  Mnajidanganya wote.Juhudi na mafanikio watanzania wanayopata pamoja na ninyi hamyaoni.Huu ni unafiki uliopitiliza.Kuweni wa kweli jamani.Naamini hamjisemei ninyi kwa uhakika kuna watu mnaowasemea.

 7. Remarua Mondosha says:

  Mnajidanganya wote.Juhudi na mafanikio watanzania wanayopata pamoja na ninyi hamyaoni.Huu ni unafiki uliopitiliza.Kuweni wa kweli jamani.Naamini hamjisemei ninyi kwa uhakika kuna watu mnaowasemea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *