MWAKA jana nilipoandika makala kwenye gazeti moja la kila wiki kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania, nilisema moja ya mambo muhimu ili kupata Katiba bora ni usawa wa washiriki.
Washiriki wanapaswa kuwa sawa na huru kusema ndiyo au hapana kwa jambo lolote litakaloletwa mbele yao. Aidha, kwa kuwa Katiba mpya inaandikwa, washiriki wana fursa na uhuru wa kujadili na kulitolea mapendekezo jambo lolote linalohusu Tanzania.
Na kwa kuwa mwisho wa zoezi hili Watanzania watatakiwa kutoa kauli ya mwisho kwa njia ya kura ya maoni, basi Watanzania hao wawe na haki na uhuru wa ama kukubali mapendekezo yote, kukubali baadhi tu ya mapendekezo na kuyakataa mengine, au kuyakataa mapendekezo yote kama yanaonekana kwenda kinyume cha matarajio au matakwa yao.
Usawa kwenye Tume ya Katiba
Katika suala hili la Katiba usawa upo katika ngazi mbili. Kwanza kwa kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili, usawa wa kwanza ni kati ya nchi zinazounda Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar. Pili ni usawa wa wajumbe wa Tume iliyochaguliwa au kuteuliwa. Kipengele hiki ni muhimu kusije kutokea mjumbe au kikundi cha wajumbe ndani ya Tume chenye kauli zaidi ya wengine.
Katika hatua ya kwanza kipengele cha usawa kati ya Zanzibar na Tanganyika kimezingatiwa kwa maana ya kuwa na idadi sawa ya wajumbe katika Tume. Katika hatua ya pili suala la usawa limepelekwa mbele zaidi kwa kuwaangalia marais wa Zanzibar na wa Tanzania kuwa ngazi moja wanaposhughulikia suala la Katiba.
Usawa huu wa marais una makandokando yake kwa sababu haiwezekani ukajitokeza na kuishia kwenye suala la Katiba tu. Kuna uwezakano mkubwa usawa huu ukadaiwa ujitokeze na katika maeneo mengine yanayohusu sehemu hizi mbili za Muungano.
Katika hatua ya tatu na ya mwisho usawa umejitokeza kwa wajumbe kupewa hadhi, nyenzo na vitendea kazi sawa. Jambo lililobaki ni kwa wajumbe wa Bunge la Katiba kutanguliza mbele uzalendo na maslahi ya taifa wakati wa kujadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa kwao na Tume.
Huo ni wakati wa kuweka kando ushabiki wa vyama vya siasa na kuangalia Tanzania itakavyosonga mbele kuelekea miaka 100 au hata miaka 150 ijayo. Ukweli ni kwamba kura ya maoni itakayopigwa na raia ni kuhalalisha tu yaliyopitishwa na Bunge la Katiba. Wajumbe wa Bunge hilo wajue kwamba wana wajibu mkubwa siyo kwa vyama vyao bali kwa taifa la Tanzania.
Masuala haya ni muhimu kuyatafakari kwa sababu kuna mamlaka ambazo tayari zimeweka mipaka ya mambo ya kujadili na yasiyo ya kujadili, namna ya kujadili na mambo yasiyotakiwa kuingizwa au kutoondolewa kwenye Katiba ya sasa.
Hadhari ni kwamba je, haya mamlaka yenye uwezo wa kuweka mipaka ya mijadala hayatakuwa na uwezo wa kuelekeza hatima ya zoezi la kuandika Katiba? Ingawa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba amesema wajumbe waachwe huru kufanya kazi waliyotumwa, uwepo wa mamlaka inayoweka mipaka ya nini cha kujadili na namna gani, kunazusha maswali na wasiwasi kuhusu uhuru wa Tume na wa Watanzania kwa ujumla.
Kati ya mambo ambayo uwepo wake katika Katiba unatakiwa usihojiwe kwa mujibu wa sheria ya Bunge ni pamoja na Muungano, Urais, Baraza la Mapinduzi, Bunge, Serikali mbili katika Tanzania, Baraza la Wawakilishi na mengine mengi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya 1977 ibara 8(1) (a) madaraka yote ya nchi hii yako mikononi mwa wananchi na viongozi wote hupata madaraka kutoka kwa wananchi. Kimsingi na ndivyo tunavyoelezwa na wataalamu wa masuala ya Katiba kwamba, katiba ya nchi huandikwa na wananchi kwa ajili yao na nchi yao, wakiainisha jinsi wanavyotaka kujitawala.
Katika kuainisha namna ya kujitawala jambo la kwanza kabisa ni kukubaliana muundo wa nchi na mfumo wa serikali. Muundo wa nchi unaweza ukachukua sura ya shirikisho, muungano au nchi moja tu. Shirikisho linapatikana pale nchi kadhaa zinapoamua kuunda taifa moja kama vile Marekani na Ujerumani, au nchi kuamua kujigawa katika majimbo yanayojitawala kama vile Nigeria.
Muungano hupatikana pale nchi huru mbili au zaidi zinapoamua kuungana na kuunda taifa moja ambalo hupewa madaraka makubwa kuongoza na kuendesha serikali ya taifa jipya. Muundo wa tatu ni wa nchi moja na utawala wa moja kwa moja.
Nchi zenye muundo huu hasa katika Afrika ni nyingi. Mifumo ya serikali mikubwa ni miwili ambayo ni mfumo wa kifalme ambapo kiongozi na mkuu wa nchi huwa ni mfalme au malkia. Mfumo wa pili ni wa kijamhuri ambapo kiongozi na mkuu wa nchi huwa ni rais ambaye ama huwa ni mtendaji au asiye mtendaji kama vile India, Italia na Israel.
Wadau wa Katiba wakishakubaliana na hayo yote ndipo hatua ya kuunda taasisi za kusimamia na kuendesha serikali huchukuliwa na kuamua mgawanyo wa madaraka kati ya serikali kuu, nchi shiriki au majimbo na mihimili mikuu ya dola katika ngazi mbalimbali. Ninafikiri na ninaamini Watanzania wa leo wamekomaa kifikra, kisiasa na kidemokrasia kuweza kupitia katika mchakato kama huu na kufikia uamuzi sahihi bila ya mamlaka yoyote kuwaamrisha la kufanya.
Ni kutokana na niliyoyaeleza hapo juu nafikiri si sahihi kusema wananchi wanaweza kujadili maboresho ya Muungano kwa uzuri bila ya kuujadili Muungano wenyewe. Mfumo wa serikali na mgawanyo wa madaraka vinategemea muundo wa Muungano.
Lengo Katiba mpya au marekebisho?
Kama Tanzania inafanya marekebisho tu ya Katiba baadhi ya maeneo katika Katiba ya sasa hayatajadiliwa, lakini kama inaandika Katiba mpya basi Watanzania wanayo haki ya kujadili kila kipengele kitakachoingizwa kwenye Katiba na kukiweka kwa namna wanavyotaka.
Ni dhahiri kutakuwa na vipengele ambavyo havitakubaliwa na watu wote lakini la msingi ni kuungwa mkono na walio wengi. Ni vizuri kuondoa shaka. Hivi leo Watanzania walio wengi hawatakubali kuingiza udini katika serikali, kuwepo kwa utawala wa kifalme au kutokuwa na rais, Bunge au Mahakama. Mihimili hiyo itarudishwa kwenye Katiba mpya lakini yaweza kufanyiwa marekebisho makubwa kwa lengo la kuboresha utendaji na kuleta ufanisi.
Katika kuainisha namna ya kujitawala wananchi wanaweza na wana haki ya kuamua kuwa na waziri mkuu mtendaji na rais asiye mtendaji. Kujadili Muungano, Urais, Bunge, Mahakama na Baraza la Mapinduzi Zanzibar na kufikia uamuzi ni kipimo cha ukomavu wa kisiasa wa wananchi na nchi yenyewe. Hapa ni kuondoa hofu.
Wakati wa kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa wananchi wengi walikuwa hawataki kwa hofu kwamba huenda upinzani ukashika dola na nchi ikaingia kwenye misukosuko. Leo ni miaka 20 tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe hapa Tanzania, hakuna chama cha upinzani kilichoshinda na kushika dola wala kudhibiti Bunge.
Kuna wakati nchini Canada viongozi wa Jimbo la Quebec walikuja na sera ya kujitenga na Shirikisho la Canada. Serikali kuu iliruhusu waende kwa wananchi na kura ya maoni ikapigwa. Sera ya kulitenga Jimbo la Quebec ilishindwa na Canada inaendelea kuwa nchi moja hadi sasa. Wananchi si dhaifu kiasi hicho kimawazo kwamba mtu yeyote au kikundi cha watu kinaweza kuja na sera potofu kikaungwa mkono.
Kuujadili Muungano ni muhimu kwa sababu mbili. Kwanza kuna manung’uniko makubwa hasa kutoka Zanzibar. Manung’uniko ya watu wa Tanzania Bara mengi yana sura ya kujibu mapigo ya Zanzibar. Miongoni mwa malalamiko ya Zanzibar ni kupotea kwa utaifa wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar kutotambuliwa kimataifa, kutokuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe, kutokuwa na uhuru wa kukopa na kujiunga na mashirika ya kimataifa na kwamba Muungano ndiyo sababu ya kudumaa kwa uchumi na maendeleo ya Zanzibar.
Tafakari ya mtu mwenye akili
Ukizitafakari sababu zote hizi utagundua kuwa zinatokana ama na kutoelewa maana ya Muungano au zinalenga kutaka kuuvunja. Haiwezekani kwa mtu mwenye akili ya kawaida akaingia kwenye Muungano na bado akataka abaki na yote hayo wanayodai.
Mambo ambayo Zanzibar wanadai imeyapoteza hata Tanganyika iliyapoteza. Hayo yote yalihamia katika nchi inayoitwa Tanzania ambamo Watanzania wote bara na visiwani wanayo fursa na haki sawa. Hapa panahitaji uelewa. Kuwa na fursa au haki ni jambo jingine na kushiriki ili kufaidi fursa au haki zinazotolewa na Tanzania, ni suala jingine kabisa.
Wazanzibari wanaelekea kutozitumia fursa nyingi zinazotokana na uwepo wao ndani ya Muungano kwa sababu tu wanataka waonekane ni nchi tofauti. Ninaamini kuna fursa nyingi za kiuchumi, kibiashara, kimaendeleo na hata kimichezo ambazo Zanzibar yaweza kunufaika nazo kwa Wazanzibari kukubali kushiriki mambo kama Watanzania.
Maswali yasiyojibiwa, ipo siku yatajibiwa
Sababu ya pili ya kujadili Muungano ni ofisi ya rais. Inawezekana jambo hili nimeliona peke yangu. Hapo awali nilisema katika mchakato wa kuunda Tume usawa umezingatiwa kati ya Zanzibar na Tanganyika.
Idadi ya wajumbe sawa, nyenzo na huduma kwa wajumbe sawa na nikaongeza kwamba na ofisi ya rais wa Tanzania na rais wa Zanzibar zimepewa hadhi sawa.
Niwakumbushe tu kwamba usawa huu ulifikiwa baada ya Wazanzibari kuudai kwa nguvu kiasi cha kuchana hadharani nakala ya muswada wa sheria ulioandaliwa ili kuupa uhalali wa kisheria mchakato wa kutunga Katiba mpya. Hapa kuna maswali yanayohitaji majibu na yasipojibiwa sasa, yatajibiwa tu siku moja.
Je, usawa wa marais hawa wawili utaishia kwenye mchakato wa Katiba tu au utaendelea katika nyanja nyingine za Muungano? Je, kwa kitendo hicho ambacho leo kinaweza kuonekana kama ni kidogo, hatujafungua pandora’s box kiasi kwamba madai ya baadaye itashindikana kuyakidhi kama tunataka Muungano ubaki na maana?
Ikumbukwe kwamba mwaka 1964 tulianza na taifa moja Tanzania lenye bendera moja, wimbo wa taifa moja na rais mmoja mwenye makamu wa rais wawili, mmoja mkazi wa Zanzibar na mwingine mkazi wa Tanganyika.
Leo miaka 48 baadaye (2012) tuna mataifa mawili, nyimbo za taifa mbili, bendera mbili na marais wawili ambao, kwa kuzingatia mchakato wa Katiba, wana hadhi sawa. Kama hilo halitoshi, kuna madai kutoka Zanzibar ya kutaka rais wao awe na kiti Umoja wa Mataifa na juzi juzi tu hapa wamepinga vikali Tanzania kuomba kuongezewa ukanda wa bahari. Kati ya wananchi waliotoa madai hayo wengine ni mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi na wapo madarakani hadi sasa.
Kitendo cha Wazanzibari kupinga Tanzania kuomba kuongezewa ukanda wa bahari kinatoa taswira kwamba Zanzibar si sehemu ya Tanzania na kwamba kilichofanywa na Tanzania ni kuingilia uhuru wa Zanzibar.
Ukiacha hilo kuna taarifa kwamba Wazanzibari hivi sasa wanakusanya saini zifike 450,000 ili kuilazimisha serikali yao iitishe kura ya maoni kuamua kama wanautaka Muungano au hapana. Aidha kuna mihadhara inayohimiza Wazanzibari kuukataa Muungano.
Sasa katikati ya haya yote Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuja na mapendekezo yanayotaka, pamoja na mambo mengine, Muungano ubaki kama ulivyo, yaani hakuna cha kujadili. Mapendekezo ya CCM ambacho Mwenyekiti wake ndiye Rais wa Tanzania na ndiye aliyeteua Tume, yana uzito wa kipekee. Ni rahisi kuhitimisha kuwa Tume haitafanya kinyume chake.
Hapa ninapata maswali. Hivi baada ya madai mazito na matukio niliyoyataja hapa na ambayo sikuyataja yanayotokea Zanzibar, ni kweli hakuna jambo la kujadili kuhusu Muungano tunapoandika Katiba mpya? Tukiyafumbia macho na kunyamaza, tunataka kufanikisha nini? Nilidhani wakati huu wa kuandika Katiba matatizo ya Muungano yangeshughulikiwa ili mwisho wa zoezi Tanzania iibuke imara zaidi kuliko ilivyo sasa.
Kwa kawaida katika Katiba yanayoingia ni mambo yaliyokubaliwa na pande husika. Inanipa taabu, tutaingiza nini katika Katiba kuhusu Muungano kama hatujakubaliana? Hili si jambo la kupuuza kwa sababu wanaotoa malalamiko ni Wazanzibari wa kada na rika zote kuanzia viongozi hadi raia wa kawaida.
Tusubiri wakati wa kutoa maoni labda ndipo tutapata dira ya wapi tunaelekea. Zoezi hili linahitaji kushughulikiwa kwa uangalifu na umakini mkubwa vinginevyo linaweza kuja na matokeo yasiyotarajiwa. Kwa jinsi zoezi zima lilivyoandaliwa karata dume. wamelamba wazanzibari na wao wanajua hivyo.
Nani anatunga Katiba?
Mwisho nizungumzie suala la nani anatunga Katiba. Wataalamu na wanasiasa mashuhuri wamekaririwa wakisema wananchi waachwe watoe maoni yao kuhusu Katiba wanayoitaka.
Kuna wakati kulikuwa na kauli kwamba vyama vya kisiasa na kiraia visiwaingilie wananchi bali viwaache waseme Katiba wanayoitaka. Nakubaliana na msimamo huu kwamba Katiba ya nchi hutungwa na wananchi wenyewe.
Kinadharia ndivyo ilivyo lakini kihalisia sivyo. Katiba hutungwa na wawakilishi, wataalamu na wanasiasa na wananchi baada ya kuelezwa kilichomo ndani ya Katiba huombwa waipitishe kuwa sheria kuu kwa kupiga kura kuikubali.
Wawakilishi kwa kufanya kazi bega kwa bega na wataalamu na wanasiasa ndio wenye uelewa mpana kati ya Katiba nzuri na isiyo nzuri. Wanaelewa nini kiingizwe kwenye Katiba na kina manufaa gani kwa nchi na wananchi.
Suala la kuandika Katiba linafanana na suala la ulinzi wa nchi. Tunasema ulinzi wa nchi ni wa wananchi wote. Lakini mapambano yanapotokea wanajeshi ambao ndio waliofunzwa mbinu za kivita huchukua nafasi ya mbele. Raia hushiriki kwa maelekezo ya wanajeshi. Ukiacha tu kila raia aende mstari wa mbele kama anavyojisikia, kupata mafanikio yaweza kuwa vigumu.
Suala la Katiba kadhalika lina askari wake wa mstari wa mbele. Hawa ni pamoja na wanasiasa, wasomi na wanaharakati katika vyama vya kiraia. Makundi haya yanaijua Katiba ya sasa ya Tanzania, wanazijua Katiba za nchi mbalimbali na wanaweza kufanya ulinganifu na wanayajua mahitaji ya nchi yetu na wataendelea kujua zaidi wanapokutana na wananchi katika mikutano ya kutoa elimu.
Lengo la kusema hivi ni kwamba makundi haya yapewe nafasi ya kutosha yaweze kutoa mchango mkubwa katika Katiba itakayoandikwa. Lugha kwamba wanasiasa na wanaharakati watawapotosha wananchi isiwepo kwa sababu hakuna mteule wa kuwaambia Watanzania ukweli na kweli tupu.
Tunashuhudia nchini mwetu jinsi ambavyo baadhi ya viongozi na hata watendaji walivyokuwa mstari wa mbele kuibia umma na kuhujumu maendeleo ya wananchi. Hivyo basi, kama CCM kilivyoonyesha njia na vyama vingine vya siasa na vya kiraia vianze kutoa elimu kwa wananchi na mapendekezo yao kwa Tume ili hatimaye Tanzania ipate Katiba nzuri kwa wananchi wote.
Toa maoni yako