Makala
Ushindi wa CHADEMA, jimbo mashakani?
Mwandishi Wetu
Mwanza
Toleo la 299
19 Jun 2013

USHINDI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kata ya Nyampulukano jimbo la Sengerema, ni salaamu tosha kwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, William Ngeleja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao, imeelezwa.

Katika uchaguzi mdogo wa uchaguzi wa udiwani uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, mgombea wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Emmanuel Mnwanis, aliibuka kidedea kwa kupata kura 1,486 dhidi ya mgombea wa CCM, Charles Rugabandana aliyepata kura 1,073, huku mgombea wa NCCR-Mageuzi akiambulia kura 45 na CUF kura 37.

Aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM kabla ya kukiacha chama hicho na kujiunga na CHADEMA mwaka jana, Khamisi Tabasamu, ameliambia Raia Mwema kwamba kata ya Nyampulukano ni kipimo cha hali ya siasa katika jimbo hilo, na kwamba mbunge wa sasa katika jimbo hilo, Ngeleja, anapaswa kujiandaa kufungasha virago kwa kuwa mwaka 2015 jimbo hilo litakuwa mikononi mwa CHADEMA.

"Kata ya Nyampulukano imebeba siasa za jimbo la Sengerema. Kata hii ni kitovu cha mabadiliko, na katika uchaguzi huu wa udiwani, tulikuwa tunapambana na mbunge wa Sengerema (Ngeleja), hatukuwa tunapambana na diwani na salaamu zetu amezipata, huu ndiyo mwanzo wa mabadiliko ya siasa za Sengerema," alisema Tabasamu.

Tabasamu anasema atakuwa miongoni mwa wanachama wa CHADEMA ambao wataomba kuteuliwa kuwania ubunge mwaka 2015 ili aweze kuwatumikia Wanasengerema kwa namna inavyostahili kama chama chale hicho kitampa ridhaa hiyo.

Mtazamo wa kata hiyo kuwa kitovu cha siasa katika jimbo hilo unaweza ukathibitishwa pia na nguvu ambazo CCM ilitumika katika kampeni zake, ambazo zilizinduliwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Katika uzinduzi huo, Nape aliwaita wapinzani kuwa ni wasindikizaji, akiwalinganisha na mpambe wa bwana harusi ambaye kazi yake ni kumfuta jasho bwana harusi, hali ambayo imekwenda kinyume.

"Mnajua kazi ya wasindikizaji, ni kufuta jasho na kurekebisha tai ya bwana harusi, hata kama msindikizaji ana suti nzuri kuliko ya bwana harusi, lakini anabaki kuwa msindikizaji tu, ikifika saa sita usiku, wanaishia mlangoni, na wakitaka kuingia chumbani wataharibu harusi, hata hawa jamaa zangu ni wapambe tu," alinukuliwa Nape wakati akimnadi mgombea wa CCM, Rugabandana.

Mmoja wa makada wa CCM wilayani Sengerema, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, amefichua kwamba kushindwa kwa CCM katika kata hiyo, ni pigo kubwa kwao na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, na Uchaguzi Mkuu wa 2015.

"Kata hii kwa kweli ndiyo ilikuwa kipimo cha hali ya siasa katika jimbo la Sengerema. Kuipoteza, si dalili nzuri kwa Chama, ni lazima tujiweke sawa kwa mikakati mipya, vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika chaguzi zijazo," alisema kada huyo.

Hata hivyo, anasema dalili za kushindwa katika kata hiyo zilianza kuwa dhahiri tangu siku ya kwanza ya kampeni za chama chao, akitaja baadhi ya mambo ambayo viongozi wa CCM walijichanganya na hivyo wananchi kuashiria kuwaunga mkono wapinzani.

Anasema kauli ya Mwenyekiti CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma, katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa kampeni hizo, iliashiria jinsi ambavyo hawakuwa wamejipanga kukabiliana na changamoto za wakati huu kwenye kata hiyo.

"Siku ile ya uzinduzi, Msukuma alisema Serikali haieleweki na akaongeza kwamba angegombea Khamis (Tabasamu Khamisi ) asingekwenda kwenye kampeni hizo, ni wazi aliwapa wapinzani hoja ya kutumaliza…lakini hiyo ndiyo siasa, tumeshidwa tutajipanga upya," alisema kada huyo.

Kwa upande wa kata ya Lugata, iliyoko jimbo la Buchosa, mgombea wa CCM, John Kando, ameibuka kidedea kwa kumshinda mgombea wa CHADEMA, Adrian Tizeba, ambaye hata hivyo amesema pamoja na kushindwa, chama chake kimepiga hatua kubwa jimboni humo hali anayoieleza kuwa ni mwelekeo mzuri kwa CHADEMA.

Tizeba alisema katika uchaguzi wa mwaka 2010, akiwa mgombea wa CCM, alipita bila kupingwa kwa sababu wapinzani hawakuwa na mgombea, na zaidi kwamba upinzani haukuwa na nguvu wakati huo. Hata hivyo, anasema hali hiyo imebadilika sasa kwa CHADEMA kuwa na wanachama na wafuasi wengi.

"Matumaini yetu ni makubwa. CHADEMA kina nguvu sana wakati huu jimboni humu pamoja na nguvu kubwa ya mawaziri na rushwa iliyotumika, lakini bado tumeonyesha uhai. Kwa sasa jimboni humu tunao wanachama zaidi ya 3,000 ikilinganishwa na mwaka 2010. Ninaweza kusema kwa uhakika kwamba CHADEMA kimefanya vizuri sana," alitamba Tizeba, ambaye alisema mwaka 2015 atakiomba chama chake kipya hicho kimteuea kugombea ubunge wa jimbo la Buchosa.

Akielezea uvumi kwamba wakati wa kampeni hizo alimpiga mama yake, Tizeba alisema kuwa taarifa hizo ni za uongo zilizosambazwa na mahasimu wake kwa lengo la kumchafua kisiasa.

"Mimi sijawahi kumpiga mama yangu na wala siwezi kufanya hivyo. Lakini kumekuwa na uzushi ambao unaenezwa na mdogo wangu (Naibu Waziri wa Mawasiliano na mbunge wa jimbo la Bushosa, Dk Charles Tizeba) kwa sababu ya tofauti zetu za kisiasa. Yeye yuko CCM na mimi niko CHADEMA," alisema Tizeba ambaye ametishia kumpelekea mahakamani mdogo wake huyo kwa madai hayo ya kuchafuliwa jina lake.

Juhudi za kumpata Naibu Waziri, Dk Tizeba kuzungumzia uzushi huo na tishio hilo dhidi yake la kupelekwa mahakamani na kaka yake, hazikufanikiwa. Alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi na kujitambulisha, aliomba apigiwe baadaye, lakini alipopigiwa baadaye hakupokea simu, na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako