Utadhani hawa watangazaji walisomea upadre jinsi wanavyopenda kuhubiri

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,

Uzitoni Street,

Bongo.

Mpenzi wangu,

Uko salama wangu? Maana siku hizi kitu muhimu usalama au vipi? Na baada ya kuwa salama, unaendelea vizuri? Bila shaka unapanga lini utajileta katika mji huu wa matamko na vitisho. Nakubali yataka moyo mpenzi lakini njoo unifariji na mimi jamani ninavyokaa na hofu na wasiwasi.

Vinginevyo, mume wangu mtarajiwa, nina swali. Hivi nikiandamana kuja kwako utanitia ndani tehe tehe tehe? Mbona ingekuwa furaha sana kwangu hata ukinitia ndani maisha! Naanza kuona kwamba maandamano ndiyo njia pekee ya kuweza kukaa na mpenzi wangu wa moyo moja kwa moja.

Hapa, mambo yanaendelea kama kawaida. Bosi bado anadhibiti maandamano ya sisimizi na kumbikumbi kila mahali na hataki kusikia namba fulanifulani. Juzi Binti Bosi alimchokoza kwa kumpa Bosi hesabu za kichwa maana Bosi anajidai kwamba yeye ni yeye kwa hisabati. Basi BB akaanza

16 x 16

18 x 20

Bosi akafanya bila wasiwasi. Kisha BB akauliza

22 x 12

Wacha Bosi alipuke. Akamtupia kisu chake alichokuwa anakitumia na kuondoka bila hata kumaliza steki anayoipenda. Mama Bosi alishangaa na kumwuliza BB kulikoni lakini BB akajifanya hamnazo hivyo ilibidi nije jikoni na kufanya hesabu kwa kutumia kalamu. Hebu fanya na wewe! Mimi kwanza bado sikuelewa kisha mwanga ukanija. Wacha nicheke peke yangu hadi MB akaanza kulikoni ikabidi niongope umenitumia vichekesho. Yaani watu wanvyoogopa watu kuungana katika sherehe ya Muungano, sijawahi kuona.

Si ajabu tutapewa amri ya kutokutoka majumbani kwetu kabisa, au walinzi wetu watajitolea kusafisha mazingira ya jiji tena kama wakati ule. Nadhani hapo wenyeviti wa mitaa watafurahi kweli maana, angalau kwa wiki ile hakuna kufuata amri ya kibosile wetu kuhusu mahali pa kumwaga takataka tehe tehe tehe.

Lakini BB sijui yukoje. Haogopi kupotezwa ndani ya chumba chake bila kuonana na mtu yeyote hadi atubu na kusema chochote kile anachotakiwa kusema? Hajui baba yake ameshamwadhibu hivyo huko nyuma? Mpaka Shemeji Bosi akaja kuokoa jahazi? Mmmmh! Siku hizi imekuwa nchi ya amri badala ya nchi ya ahadi.

Lakini tuache hayo mpenzi maana, kwa jinsi hali ilivyo, bora kuongea na ukuta. Angalau ukuta hautakuadhibu hata kama haukusikilizi. Leo ngoja nimalize bifu yangu na vipindi vya redio.

Yaani napata shida kubadilishabadilisha kituo kila mara, unajua kwa nini. Nikiwa kazini, napenda kweli kusikiliza mjadala, lakini mjadala si mtu mmoja anatoa wazo kisha watu wote wanakubaliana naye kama vile ni mwenyekiti wa chama fulani. Mjadala ni watu kutoa mawazo yanayotofautiana. Lakini mjadala utapata wapi. Wote wako upande mmoja tu, mmoja akisema, wenzake wanamwunga mkono kama vile nabii.

Kisha utadhani hawa watangazaji walisomea upadre au uchungaji au ushehe jinsi wanavyopenda kuhubiri. Sijui ukipata kipaza sauti kinakulewesha, au vipi, maana watahubiri weeeeeeeee, na kutamba katika kutuambia sisi jinsi tulivyo mafala kwa kufanya hiki au kile.

Kwa mfano leo, wakaanza kuongea kuhusu matumizi ya mtandao. Si unanijua mimi mpenzi, hohehahe mwenye simu ya tochi tu lakini najua watu wanavyopenda kupeana stori na kuelezea maisha yao kwa marafiki zao.

Kumbe, kwa mujibu wa watangazaji, kuelezea umezuru kaburi ya babu yako, au umetoka auti mahali ni kosa. Kosa gani? Eti wanatangazia mema yao tu, kwani walitaka watangaze mabaya. Kisha wanahimiza sheria ifanye kazi.

Mimi sijakataa nisingependa kuona matusi kwenye mitandao, na si ajabu hata mimi nisingependa kuanika maisha yangu hadharani watu wote waone. Kwa mfano, nitawezaje kuandika … jamani eeee … mbona mpenzi wangu hataki tufunge ndoa … kila mwezi, kila mwaka … ahadi tu … ahadi tu … ngoja …. Subiri tehe tehe.

Siwezi kuandika hivyo lakini siwezi kumzuia mwingine ajianike hivyo. Si ni juu yake. Au sheria mwisho itatuambia tuandike nini na tusiandike nini kana kwamba mitandao nayo ni jela? Natamani kweli watangazaji waache hizo.

Kwa nini wasiulize maswali na kukaribisha wengine waseme? Kwa nini wasiwaalike watu wenye mawazo tofauti ili wabishane na sisi tujue vizuri zaidi? Lakini kuhubiri dakika kumi au kumi na tano nzima. Ndiyo maana natafuta kituo kingine.

Sasa unapokwenda kwenye hiki kituo cha pili ndiyo mbaya zaidi. Sina shida na matangazo ya biashara tena mengine nayapenda kweli hasa yale yanayochekesha.

Labda yazidi lakini kimsingi najua ni sehemu ya kipindi. Ninachoshangaa ni watangazaji wa kipindi kugeuka watangazaji wa biashara.

Kwa hiyo, leo watatangaza kwamba benki fulani ndiyo bora kabisa, hakuna mfanowe, tena wanatangaza kama vile ni wao kabisa wanaweka pesa zao pale, kesho wanatangaza benki nyingine kuwa bora zaidi kabisa, hakuna mfanowe.

Sasa hiki ni kitu gani? Wanalipwa na hizi benki? Kama ni hivyo watuambie tujue moja. Ndiyo. Kisha, yeye kama yeye, au wao kama wao wanatangaza mambo kama kubeti na kutuaminisha kwamba mwisho wa umasikini ni kubet kupitia kwa kituo chao. Huu si udanganyifu wa moja kwa moja. Jamani eee. Kama ni watangazaji wa biashara watuambie, tujue moja vinginevyo naona wanavyotushawishi ni dhambi kabisa.

Na matokeo yake, sisi tunapokwenda kupata muziki kidogo ili tufanye kazi vizuri zaidi tunabaki kubadilisha kituo tu kila dakika tatu. Jana kidogo nitupe redio kwa hasira kabisa.

Ni wapi tutapata nafasi ya kuwaambia hawa watangazaji kwamba wakijipenda na sauti zao kiasi hiki, kwa nini wasiende porini na kuwatangazia akina simba. Labda wao watapenda kubiri, na kutamba, na utangazaji wa biashara zaidi yetu.

Mwenye kujiandaa kuandamana hadi kwako

Hidaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *