Utajiri wa Gachuma, Airo watumika kushawishi wapiga kura Kirumba

VYAMA vya CCM na CHADEMA vimeendelea kukabana koo katika dakika za “lala salama” za kampeni ya kuwania kiti cha udiwani wa Kata ya Kirumba, ahadi, vijembe na hata vitisho vikiendelea kutawala kampeni hizo.

Katika kushawishi wapiga kura kwa mgombea wake, CCM mwishoni mwa wiki kiliwapandisha jukwaani wanasiasa na wafanyabiashara marufu Jiji Mwanza, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC-Taifa) kutokea mkoani Mara, Christopher Gachuma na Mbunge wa Rorya, Lameck Airo, ambao kwa pamoja waliahidi kujenga barabara ya Kabuhoro kama mgombea wa chama chao atachaguliwa.

Akizungumza katika kampeni hizo, Airo alisema yeye ni mwana Kirumba kwa kuwa amewekeza katika kata hiyo na kwa hiyo, yuko pamoja na watu wa kata hiyo katika kila hali. Airo ni mmiliki wa Hoteli ya La Kairo.

Aliwaeleza kuwa ahadi zake ni za kweli na ushahidi ni jimboni kwake Rorya ambako aliahidi na kufikia Aprili, mwakani atakuwa amekamilisha ahadi zake.

“Nina madawati kama 200 yako stoo tu, isingekuwa sheria za uchaguzi inakataza kutoa ningeyaleta hata leo, lakini hata hivyo baada ya tarehe 1, Aprili mkimchagua mgombea wetu, nitaita Mwalimu Mkuu mmoja baada ya mwingine kuwapatia,” alisema.

Akizumgumzia ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita tano inayopita katika Kilima cha Kabuhuro, alisema atasaidiana na Gachuma ili kujenga barabara hiyo kwa kuwa ana mitambo ya kujengea barabara.

Akimnadi mgombea huyo, Gachuma aliungana na Airo akisema mgombea wao, Jackson Robert, ni kijana hodari na akipewa udiwani ataumudu kwa kuwa watamsaidia.

“Nina magreda yamekaa ningeyatoa hata leo kama kufanya hivyo isingekuwa kinyume cha taratibu za uchaguzi, lakini niwahakikishie barabara hii ni kilomita tano tu wengi mnanifahamu ninawahakikishia yote yako ndani ya uwezo wetu, tutaimudu,” aliahidi.

Wakati makada hao wa CCM wakijinadi hivyo, CHADEMA wamebeza ahadi hizo kwa kusema CCM kimeishiwa sera na badala yake kinaleta porojo mpaka kwenye masuala ya msingi ya maisha ya watu.

“Wenzetu hawa wamegeuza siasa kuwa sehemu ya ghiliba, hivi wamejua leo kwamba Kirumba kuna barabara mbaya? Hawa si wako hapa kila siku walikuwa wapi siku zote, hatuna nafasi tena ya kurudi nyuma, 2010 tuliamua kuanza safari ya ukombozi kwa kuwapiga chini CCM, hatuwezi kurudi nyuma, kura zote kwa Dani Kahungu,” alisema Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza, Wilson Mshumbushi.

Alisema kuwa makada hao kama wangekuwa na dhamira ya dhati kwa wana Kirumba wasingesubiri wakati huu kwa kuwa chama chao kimeongoza kata hiyo kwa miaka 49 hiyo barabara na tatizo la madawati yalikuwepo na uwezo huo walikuwa nao, wangeweza kulifanya tatizo hilo historia lakini wanachofanya sasa ni ghiliba tu.

“Miaka hamsini ya ‘uhuni’ wa utawala wa CCM bado wana ujasiri wa kuzungumzia barabara na maji, marehemu diwani wetu Manoko ameongoza kata hii kwa miezi minane tu lakini amefanya mambo ambayo CCM haikuyafanya kwa miaka 48, msiwasikilize hawa,” alisema.

Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, aliwatahadharisha wakazi wa kata hiyo kuwa wasihadaike na CCM kwa kuwa chama hicho sasa kimekosa mwelekeo na kinahaha kujinusuru wakati tayari kimeshakata roho.

Alisema mfumko wa bei chini ya Serikali ya CCM unakuwa kwa kasi kila siku kama mtoto anavyokuwa na kuongeza; “Inafika mahali mpaka mtu anaogopa kukua kwa kuhofia mfumko wa bei, hivi mnataka iweje ndiyo mjue CCM imechoka?”

Henry Joseph, Jerry Tegete na Mrisho Ngassa watumika kushawishi kura

Katika hatua nyingine, Diwani wa CCM Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula, amewataka wana Kirumba kumchagua mgombea wa chama chake kwa kuwa atarejesha heshima na hadhi ya michezo kama ilivyokuwa awali kwa kuboresha viwanja ambavyo vitatengeneza vipaji.

 “Jack Atahakikisha viwanja vya michezo vya Magomeni na Kabuhoro vinatengenezwa ili kukuza vipaji, akina Henry Joseph, Jerry Tegete, Mrisho Ngasa wametoka hapa, lakini tangu ndugu zetu washike kata hii hatujazalisha vipaji tena, mchagueni Jack atarejesha heshima ya Kirumba” alisema.

Bidhaa za Coca zatishiwa

Mwenyekiti wa mtaa wa Kigoto, Kipara Bulemela kwa tiketi ya Chama cha Wanachi (CUF) akimnadi mgombea wa CHADEMA alisema wananchi wanachotaka si msaada wa wenye pesa, bali ni usimamizi mzuri wa mapato yao.

“Halafu huyu Gachuma anakuja hapa kututishia pesa za soda, hizo Coca Cola si tunazinunua sisi, zinatokana na pesa zetu sisi walalahoi, sasa asipoangalia tutasusia hata soda zake tunywe pepsi peke yake,” alisema.

Kauli za wagombea

Mgombea wa CHADEMA, Dani Kahungu ameahidi kuendesha harambee kubwa siku ya kuhitimisha kampeni, kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa elimu wa kata ili kuwasadia watoto wa wazazi masikini wasiojiweza katika kata hiyo.

 Amesema atasimamia upimaji maeneo ya milimani katika kata hiyo ili wananchi wamiliki halali wa maeneo yao na yawawezeshe hata kukopa kwa kuwa na dhamana ya ardhi.

 Kwa upande wake mgombea wa CCM, Jackson Robert, amewatahadharisha wafuasi wa CHADEMA kupuuza wito wa viongozi wao kukaa mita 100 kutoka kituo cha kupiga kura, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuzua vurugu zisizokuwa na sababu.

Amesema endapo tafrani yoyote itaibuka katika uchaguzi huo wataokaoumia ni wazazi, mama na baba wa vijana wa Kirumba au hata ndugu na rafiki zao na hivyo akawasihi wasiwasikilize kwa kuwa wanaohamasisha hivyo familia zao ziko mbali.

 

2 thoughts on “Utajiri wa Gachuma, Airo watumika kushawishi wapiga kura Kirumba”

  1. Robert Ndiila says:

    Ni kosa gani watu kukaa sehemu kusubiria matokeo?Hizi ahadi za akina Gachuma na La Kairo,zinaweza kutolewa karne hii?

  2. George says:

    Yap Iam suprised,what a wonderful promises!,Eti chagueni then tujenge barabara,wat if hawatamchagua ?

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *