- Mila na desturi vyatumiwa kuuhalalisha
- Ni ripoti ya serikali iliyowasilishwa mkutanoni
MWAKA huu, Tanzania imekuwa moja ya nchi 16 duniani zilizopata nafasi ya kuwasilisha taarifa ya hali ya haki za binadamu katika nchi zao kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN). Uwasilishaji huo, kama ilivyo utaratibu, umefanyika katika Kikao cha mapito ya taaarifa hizo (Universal Periodic Review) cha Baraza la Haki za Binadamu.
Mchakato wa uwasilishaji wa taarifa kama hii huwa ni mrefu; unaohusisha wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi ili kufikia hatua ya mwisho ya uwasilishaji na kuomba taarifa husika iweze kuridhiwa na Baraza la Haki za Binadamu.
Uandaaji na uwasilishaji wa taarifa hii ni kwa mujibu wa makubaliano yaliyoridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Machi mwaka 2006; na kwa mujibu wa kanuni za kawaida (general guidelines) zilizoridhiwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Juni mwaka 2007.
Kikao cha mapitio ya taarifa ya nchi husika kinachofanywa na Baraza la Haki za Binadamu huzingatia taarifa ya serikali ya nchi hiyo kuhusu haki za binadamu, taarifa mbalimbali zinazokusanywa na Umoja wa Mataifa kuhusu nchi yenyewe na muhtasari wa taarifa za wadau mbalimbali wa haki za binadamu kama vile taasisi zisizo za kiserikali (NGO’s) na tume mbalimbali.
Katika kundi hili la tatu, kwa Tanzania, pamoja na NGO’s mbalimbali, ipo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoanzishwa mwaka 2000 kwa mujibu wa kifungu cha 129 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ikaanza kufanya kazi rasmi Julai mwaka 2001. Tume hii, kisheria inafanya kazi zake kama chombo huru.
Hata hivyo, katika uwasilishaji wa taarifa, ni ujumbe wa serikali tu ndio wenye jukumu la kuiwasilisha, kujibu hoja, maswali na mapendekezo ya nchi mbalimbali duniani kuhusu taarifa hiyo. Wengineo, kama NGO’s na tume ya haki za binadamu kama ipo, wanabaki kuwa watazamaji tu.
Hapa kwenye kujibu hoja na mapendekezo ya wadau na nchi mbalimbali duniani kuhusu taarifa yake ya haki za binadamu mwaka huu, Serikali ya Tanzania na ujumbe wake ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora, Mathias Chikawe, wameibua suala ambalo haliwezi kupita hivi hivi bila kujadiliwa.
Katika majibu ya masuala mengi yaliyoonekana ni tata na yanahitaji ufafanuzi wa kina, masuala yaliyohusu hali halisi ya haki za binadamu nchini Tanzania, vigezo vitatu: mazoea, mila na desturi au utamaduni, vilionekana kutumiwa zaidi na serikali kama utetezi wa mambo mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu nchini Tanzania.
Yapo masuala kadhaa ambayo yameibuliwa na wadau katika taarifa yake kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu nchini. Ni masuala haya ambayo yaliibua maswali mengi kwa Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani wakati wa mjadala wa taarifa hii ya haki za binadamu.
Makubwa kati ya hayo ilikuwa ni kuendelea kuwepo kwa matumizi makubwa ya nguvu ya jeshi la Polisi dhidi ya wananchi, hasa wahalifu na wakati wa maandamano; hususani ya kisiasa.
Pia swali kuhusu kwanini Tanzania inaendelea kukumbatia adhabu ya kifo liliulizwa na wawakilishi wa nchi nyingi; huku wakishangaa kwa nini Tanzania imekuwa ‘mzito’ sana kukomesha adhabu hii.
Aidha, kwa kuzingatia taarifa ya wadau wa haki za binadamu iliyowasilishwa kama muhtasari katika kikao cha mapitio ya hali ya haki za binadamu nchini Tanzania, nchi nyingi zimepaza sauti zao kusikitishwa na jinsi uonevu, manyanyaso na ukatili dhidi ya wanawake na watoto unavyoendelea kutawala nchini. Hii ni katika ngazi za familia, kwenye kazi na hata katika upataji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Taarifa hiyo ya pamoja ya wadau au asasi zisizo za kiserikali imeeleza kuwa mauaji ya vikongwe kwa imani potofu za kishirikina bado yanaendelea katika mikoa ya kanda ya ziwa; na kwamba pamoja nakuwepo kwa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2001-2015), juhudi za serikali kushughulikia matatizo kama hayo zimeendelea kuwa hafifu na zisizoridhisha.
Kwa mfano, kuhusu vitendo vya ukatili kwa watoto, taarifa ya wadau wa haki za binadamu nchini Tanzania, imeonessha pamoja na kuendelea kwa tatizo la ukeketaji kwa watoto wa kike katika baadhi ya jamii, kumekuwa pia na vitendo vya udhalilishaji wa watoto wa kike na kiume vya ubakaji na kulawiti katika sehemu za Tanzania visiwani, mijini na vijijini.
“Watoto waathirika wa vitendo hivi wamekuwa wakinyanyapaliwa na wazazi au wakubwa wao wamekuwa wakipendelea zaidi kuyatatua matatizo haya kwa njia zisizo rasmi badala ya kuyawasilisha kwa vyombo husika. Taarifa ya pamoja ya wadau imeeleza jinsi pia kesi kadhaa za aina hii zilivyotupwa na kutoshughulikiwa na jeshi la Polisi”, umeeleza muhtasari wa taarifa iliyowasilishwa na wadau kama ilivyoandaliwa na Umoja wa Mataifa.
Katika sekta ya elimu, pamoja na Tanzania kusifiwa kwa kupata tuzo ya Umoja wa Mataifa kwa kufikia malengo ya Milenia ya elimu ya msingi kwa wote miaka mitano mapema kabla ya mwaka wa tathmini (2015), wadau na nchi mbalimbali wameeleza kutoridhishwa na ubora wa elimu inayotolewa.
Matatizo yaliyotajwa kuwa chanzo cha kiwango cha elimu kilicho duni nchini ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kusomea kama vile vitabu na vifaa vingine, idadi kubwa ya wanafunzi madarasani na hivyo kuwepo kwa uwiano mbovu wa walimu na vyumba vya madarasana pia kuwepo kwa ukatili dhidi ya wanafunzi unaofanywa na baadhi ya walimu. Suala la masilahi duni kwa walimu pia limetajwa kuwa limekuwa tatizo la kudumu nchini.
Yapo pia malalamiko kwa serikali juu ya wawekezaji hasa wa kutoka nje kukiukahaki za binadamu kwa namna moja au nyingine. Malalamiko hayo yaliyotolewa na wadau katika taarifa yao, pamoja na nchi mbalimbali duniani yanahusu madai ya serikali kuwakumbatia zaidi wawekezaji hawa badala ya kujali zaidi masilahi ya wananchi.
Hii ni pamoja na malalamiko ya kuwepo kwa mikataba tata ya kuchimba madini; na kuwa pamoja na kuwepo kwa Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2010, bado tatizo la rasilimali hizo kutonufaisha wananchi linaendelea kuwepo.
“Taarifa ya pamoja ya asasi zisizo za kiserikali imependekeza kuwa serikali ya Tanzania inapaswa kuongeza zaidi uwazi katika mikataba inayofanya na wawekezaji; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepedekeza kuwa Tanzania inapaswa kuzingatia haki za binadamu katika sekata hii ya uchumi na biashara, huku ikianisha vizuri majukumu hasa ya makampuni, mawakala wa serikali na wadua wengine”, ilisema taarifa ya Umoja wa Mataifa yenye muhtasari wa maoni ya wadau wa haki za binadamu nchini Tanzania.
Huku masuala haya yote yakiwa ni baadhi tu yaliyohitaji majibu muafaka ya serikali, juu ya hatua gani inachukua katika kuhakikisha uboreshaji wa hali za binadamu katika nyanja hizo zote, serikali ilionekana ikijisetiri zaidi katika mwamvuli wa ‘mazoea, mila na desturi’ katika majibu yake.
Mathalani, kiongozi wa ujumbe wa serikali, Waziri Chikawe, wakati akianza kujibu kwa ujumla hoja za wadau na nchi mbalimbali zilizoibuliwa kuhusu matatizo ya haki za binandamu nchini, alisema kuwa “kati ya mambo mengi yanayoturudisha nyuma katika kuzingatia haki za binadamu ni mila na tamaduni zetu, na pia sababu nyingine ni taratibu za dini mbalimbali tulizonazo”.
Kwa upande mmoja, utetezi wa Chikawe waweza kukubaliwa katika nyanja kadhaa kama vile mauaji ya vikongwe kwa imani potofu za kishirikina. Hata hivyo, kinacholeta ugumu zaidi katika kukubaliana na Chikawe ni pale alipotumia sababu hii kama vile ndiyo iliyo kuu inayosababisha matatizo ya haki za binadamu kwa asilimia kubwa. Pia kingine kinacholeta tatizo ni jinsi alivyotumia silaha hii kupata ‘huruma’ kwa Watanzania, wadau na nchi mbalimbali wanaohitaji maelezo na mkakati madhubuti wa kuboresha hali ya haki za binadamu nchini kwetu.
Kwa mfano, akitoa majibu kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi-Albino na mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina, Chikawe amethubutu kuuambia ulimwengu kuwa haya yanaendelea kuwepo kwasababu ya “ukosefu wa elimu na dini katika eneo yanapotokea”. Huku akiweka mkazo kuwa maeneo hayo dini zilichelewa kufika!
Inafahamika na wengi kuwa, mauaji kama hayo yamekuwa yakifanywa si tu kwasababu za kitamaduni au mila, lakini imekuwa ni suala linalofanywa na watu wenye masilahi yao kama ya kibiashara. Hawa wana elimu zao na pia wengine wana dini zao.
Majibu kama haya ni kama jinsi mtu anavyohalalisha kitendo cha rushwa kinafanyika kwasababu ya kuwepo kwa mishahara isiyotosha.
Mazoea pia yalitumika kukwepa kutoa majibu madhubuti kwa maswali magumu kuhusu haki za msingi. Mathalani kuhusu haki ya uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya habari , Chikawe amediriki kusema kuwa kwa kuwepo kwa vyombo vingi vya habari nchini, serikali imeruhusu uhuru wa maoni bila mipaka; huku akiongeza kuwa: “Hakuna yoyote anayevidhibiti vyombo hivi vya habari.”
Hili ni jibu linalotazama masuala kwa mazoea, halichambui uhalisia. Yapo masuala kadhaa ambayo ni tata kuhusu uhuru wa maoni na vyombo vya habari.
Kwa mfano, kama taasisi ya kutetea masuala ya uhuru wa vyombo vya habari duniani inayojulikana kama Article 19 ilivyoainisha katika muhtasari wa taarifa za wadau wa haki za binadamu kuhusu Tanzania, uliotolewa na Umoja wa Mataifa, baadhi ya sheria zimeendelea kuwa mwiba mkali kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Sheria hizi ni pamoja na ile ya Magazeti (Newspaper Act) ya mwaka 1976; Hii ni sheria ambayo, pamoja na kuhusika na usajili wa magazeti na mambo mengine, imempatia Waziri wa habari mamlaka makubwa mno juu yakuyafungia au kuyachukulia hatua magazeti.
Nyingine ni Sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970, ambayo imeipa serikali mamlaka makubwa ya kuamua na kutafsiri kipi ni taarifa inayofaa na isiyofaa kwenda au kutolewa kwa umma.
Kwa sababu ya kuendelea kuwepo kwa sheria hizi, katika mjadala wa mapitio ya taarifa ya hali ya haki za binadamu nchini, kwenye baraza la Umoja wa Mataifa, nchi kadhaa zilihoji ni lini Tanzania itaondokana na sheria hizi ili kuweka sheria zinazoendana na viwango vya haki za binadamu duniani.
Mwakilishi wa Canada aliuliza moja kwa moja kuwa “Ni lini hasa ule msuada mpya wa Sheria ya Vyombo vya Habari na ule wa Uhuru wa Habari itapelekwa kujadiliwa bungeni ili kuwa sheria”?
Kama wanavyoeleza Article 19, matatizo ya uhuru wa habari pia yapo kwenye vyombo vya habari vya vinavyosemwa kuwa ni vya umma-yaani kama vile TBC na TVZ, kuwa vyombo hivi vinatambulika tu kuwa vya umma, lakini ukweli ni kuwa haviwajibiki kwa umma kama inavyotakiwa bali vinawajibika kwa serikali.
Aidha, Article 19 wameeleza kuwa hakuna sheria nchini inayolinda uhuru wa waandishi (editorial independence) hasa wa vyombo vya habari ‘vya umma’, na pia hakuna kifungu chochote katika Katiba-ya Jamhuri wa Muungano na ile ya Zanzibar wala sheria inayowapa haki vyombo vya habari wanahabari kuhifadhi au kutotaja vyanzo vyao vya habari.
Masuala haya na mengine mengi juu ya haki za binadamu, katika ulimwengu wa leo yanahitaji kujadiliwa na kuzingatiwa kwa kutumia hoja mahususi na uhalisia tulionao.
Yawezekana kuwa ni kweli mazoea, mila na tamaduni zetu zimekuwa kwa namna moja au nyingine vyanzo vya ukikwaji wa haki za binadamu, lakini hivi haviwezi kuchukuliwa tu kama ndio uhalalisho wa ukiukwaji huo, na hivyo yafaa tutumie uhalisia na mikakati zaidi kuondoa uvunjifu wa haki za binadamu.
Toa maoni yako