Makala
Tafakuri Jadidi
UVCCM imegeuka ‘klabu maalumu’ ya watoto wa vigogo?
Johnson Mbwambo
Toleo la 263
17 Oct 2012

WIKI iliyopita kulikuwa na orodha iliyokuwa ikisambazwa kwa kasi kwenye mitandao na pia kupitia ujumbe wa sms ikiambatanishwa na maelezo kuwa ni baadhi ya watoto wa vigogo waliojitokeza kuwania uongozi wa ngazi ya taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Zaidi ya wasomaji wangu 10 wa safu hii walinitumia pia orodha hiyo kwa sms na e-mails wakiitumia kuniunga mkono katika kile nilichopata kuandika huko nyuma kwamba CCM ya sasa na jumuiya zake sio tena chama kinachowakilisha maslahi ya wakulima na wafanyakazi wa nchi hii; bali matajiri na familia za wakubwa.

Baadhi ya wasomaji walionitumia orodha hiyo waliniomba niitumie kuwaambia Watanzania kwamba sasa ni dhahiri watoto wa masikini katika chama hicho na jumuiya zake hawana tena chao!

Sitaki kuijadili orodha hiyo jina kwa jina kwa sababu yawezekana kati yao wapo wachapakazi kweli kweli ambao wala hawakubebwa na wazazi wao kufikia hapo walipofikia kisiasa, na hivyo sitakuwa nimewatendea haki. Kwa sababu hiyo, nitajadili kijumla tu madhara ya CCM na jumuiya zake kuongozwa kifamilia, na si kujadili jina moja moja katika orodha hiyo.

Lakini pia nashindwa kujizuia kujiuliza; wasomaji wangu wanataka niandike nini zaidi ya niliyoyaandika katika toleo Na. 259 wakati ule mke wa Mwenyekiti wa CCM (Rais Kikwete), Salma Kikwete na mwanae, Ridhiwan Kikwete, walipopita bila kupingwa katika patashika za wilayani za kugombea ujumbe wa NEC wa chama hicho? Wawili hao pia ni wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa CCM.

Ndugu zangu, inapotokea Rais na Mwenyekiti mwenyewe wa CCM (Kikwete) anaonyesha mfano kwa kuwabeba kisiasa wanafamilia yake, tutawalalamikiaje vigogo wengine nchini wakifanya hivyo hivyo? Si hawa wanaifuata tu njia iliyoonyeshwa na mkubwa?

Ni nani asiyejua kwamba ndani ya kipindi cha miaka saba tu ya urais wa Kikwete, mkewe Salma na mwanaye Ridhiwan ambao hawakuwa lolote ndani ya medani za uongozi wa kisiasa nchini, sasa tayari ni wajumbe wa NEC na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM? Mtoto mwingine wa Rais Kikwete, Halfan Kikwete (11) naye ni kiongozi wa kitaifa wa chipukizi wa CCM, tena naambiwa wakati alipochaguliwa Desemba 29, 2009, mjini Morogoro, mwenyewe hakuwepo hata ukumbini!

Sasa, kama uongozi ni kuonyesha njia, ni dhahiri basi kwamba ‘njia’ ambayo Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, anawaonyesha vigogo wenzake ndani ya chama hicho na ndani ya jumuiya zake, na hata ndani ya serikali, ni kuwasukuma watoto wao katika nafasi za uongozi.

Na katika mazingira hayo, kwa nini tusiamini kwamba linapokuja suala la uongozi watoto wa masikini, hususan watoto wa wakulima, hawana tena chao ndani ya CCM ya sasa na jumuiya zake?

Kwa nini tusiziamini zile kejeli zinazotolewa mitaani dhidi ya CCM kwamba chama hicho sasa kinaongozwa kwa mtindo wa BMWs; yaani kwa staili ya Baba, Mama na Watoto kubebana kiuongozi? Tutasita vipi kuamini hilo; ilhali ushahidi u-wazi kabisa kwa mwenye macho kuona?

Pengine isingesikitisha sana kama kubebana huko ki-ndugu au kifamilia (nepotism) kungeishia tu kwenye medani za siasa; lakini hata katika ajira nzuri na zinazolipa vizuri, hali ni hiyo hiyo!

Tembelea makampuni ya simu, mabenki au asasi zozote za hapa Dar es Salaam zinazolipa mishahara mikubwa na marupurupu manono uone kama utakuta idadi ya kutosha ya watoto wa wakulima! Huko wamejazana watoto wa wakubwa; tena baadhi yao wakiwa na bongo zisizohalalisha wao kushika nafasi hizo.

Ndiyo maana baadhi yetu tutaendelea kumsifu na kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hadi tuvutapo pumzi zetu za mwisho hapa duniani; maana kama si uongozi wake wa haki na usio wa upendeleo, mimi mtoto wa mkulima masikini ningefikaje hapa nilipofika maishani?

Ninachojaribu kueleza hapa, ndugu zangu, ni kwamba kidogo kidogo tunazidi kuligawa taifa katika matabaka mawili ya wazi – tabaka la matajiri na viongozi na tabaka la wafanyakazi na wakulima masikini. Kwa maneno mengine, tabaka la walicho nacho na tabaka la wasicho nacho. Walicho nacho wanazidi kuongezewa; ilhali wasicho nacho hata kile kidogo wanapokonywa! Huo ndio ukweli mchungu wa hali ilivyo hivi sasa hapa Tanzania.

Huko mbele tuendako, itakuwa maajabu kama migongano ya matabaka haya mawili haitasababisha umwagaji damu; hasa tofauti kati ya matabaka hayo mawili itakapozidi kuongezeka, kuongezeka na kuongezeka zaidi!

Tukirejea kwenye umoja huo wa vijana wa CCM, itashangaza kuuona umoja ambao ngazi yake ya juu imejaa watoto wa vigogo na wa matajiri, ukiwatetea masikini wa nchi hii; hususan vijana wenzao ambao baba zao ni wafanyakazi au wakulima masikini.

Watakachofanya hao watoto wa vigogo na matajiri ni kuigeuza tu UVCCM kuwa “klabu yao maalumu” watakayoitumia kupanga mikakati ya ki-makundi ya namna wanavyoweza kukwea zaidi ngazi za uongozi wa kitaifa au namna wanavyoweza kuwasaidia wazazi wao kukwea zaidi ngazi za kisiasa.

Kwa mfano, kama watoto wa vigogo kadhaa wanaopanga kuwania urais mwaka 2015 watakuwa ndani ya uongozi wa kitaifa wa UVCCM, itashangaza kama hawatautumia umoja huo kuwapigia chapuo wazazi wao kama wataamua kuigombea tiketi ya CCM ya uchaguzi huo wa urais.

Ni maoni yangu kwamba Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) si umoja tena unaotoa fursa sawa kwa wote ki-uongozi. Ni umoja uliotekwa na watoto wa wakubwa na matajiri kwa minajili ya kuutumia wao wenyewe kupanda ngazi za kisiasa, lakini pia ikibidi kuutumia kuwapigia kampeni wazazi wao wanaowania nafasi za juu za uongozi wa nchi.

Baadhi yao si vijana wanaosononeshwa na umasikini au ukosefu wa ajira wa vijana wenzao wa familia za kimasikini. Baadhi yao wanatambiana wenyewe kwa wenyewe, si tu kwa ukubwa na vyeo vya kimamlaka vya wazazi wao, lakini pia kwa utajiri. Dunia ya umasikini wanayoishi vijana wenzao wa familia za kimasikini iko mbali sana nao!

Miaka michache iliyopita mimi na rafiki yangu mmoja tulipenda kwenda kunywa bia kwenye hoteli moja ya hapa mjini Dar es Salaam, mbele kidogo ya daraja la Salander (nashawishika kutoitaja jina), ambako watoto hao wa wakubwa hupendelea kukutana usiku kunywa pombe.

Siku moja tulikaa karibu na meza yao, na ilikuwa rahisi kwangu kuyasikia maudhui ya mazungumzo yao ya kila usiku wanapokutana hapo kunywa pombe.

Naweza kusema kwamba sehemu kubwa ya mazungumzo yao ilikuwa ni kusifiana tu kuhusu maisha yao na ya familia zao. Huyu akitamba kuwa wiki iliyopita alikuwa Brussels, mwingine atatamba alikuwa New York!

Mmoja akisema anafanyiwa mipango kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza, mwingine atadakia kuwa mipango yake ya kwenda Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani imefikia pazuri! Vivyo hivyo watashindana kujisifia magari ya kifahari wanayoendesha, vifaa vya kisasa vya teknolojia wanavyomiliki kama vile simu za mkononi, laptops nk!

Sikupata kamwe kuwasikia wakijadiliana kuhusu mustakabali wa nchi yao Tanzania au hali za maisha za jamii inayowazunguka au hata umasikini wa taifa letu licha ya utajiri mkubwa wa maliasili iliyonayo.

Na ndiyo maana sikushangaa sana kuwaona baadhi yao wakijitosa katika siasa na kufanikiwa kuwa viongozi. Kwa mtazamo wangu, kuna sababu mbili tu zinazoweza kuwa ndizo zimewasukuma kuwania nafasi hizo za uongozi.

Moja inawezekana kwamba wameshawishiwa na wazazi wao ambao tayari ni viongozi na wanazeeka. Kwa sababhu wazazi hawa wanazeeka na muda si mrefu watalazimika kuondoka uongozini, wanataka kuutumia muda wao uliosalia kuwasukuma mbele vijana wao ili wawaache pazuri wakati hatimaye watakapolazimika kuondoka uongozini.

Kwa maneno mengine, wanataka watoto wao nao wawe viongozi kwa sababu, katika Tanzania ya leo, kuwa kiongozi ni kujihakikishia utajiri na maisha mazuri.

Japo baadhi ya vijana hawa tayari ni matajiri (baadhi tayari wamejengewa majumba ya ghorofa na baba zao), ulafi tu wa pesa ndio unaowasukuma kuwania uongozi ili wawe matajiri zaidi.

Lakini sababu ya pili inaweza kuwa ni ubinafsi wao tu unaoendana na kujiona. Baadhi ya watoto hao wa vigogo wakiwaona watoto wengine wa vigogo ni mawaziri au wabunge au wajumbe wa NEC, nao huzitamani nafasi hizo ili kulinda hadhi zao – ili nao wawe na cha kujivunia wanapokutana usiku kwenye klabu zao za pombe!

Hawa ndo wale wanaowasumbua wazazi wao ili wawapigie chapuo nao wawe wakubwa: “Baba, mbona mtoto wa fulani yeye ni waziri, na mimi nautaka uwaziri. Baba, mbona mtoto wa mkubwa mwenzio ni mjumbe wa NEC? Na mimi nautaka ujumbe wa NEC”. Baba, mbona mtoto wa yule mkubwa mwenzio ni mbunge? Na mimi nautaka u-bunge”!

Na kwa kuwa wazazi wao hawana moyo wa Nyerere, na wala hawana chembe za uadilifu aliokuwa nao Baba wa Taifa, wananywea kirahisi kwa shinikizo hilo la watoto wao ambao baadhi unaweza kabisa kuwaita spoiled brats (watoto waliodekezwa), na hivyo kuwajibu; “basi kachukue fomu ugombee, nami nitaangalia ninachoweza kufanya kukusaidia ushinde.”

Ni kwa njia hiyo uongozi ndani ya CCM na jumuiya zake na ndani ya serikali sasa umejaa wanafamilia. Na ndiyo sababu CCM sasa inakejeliwa mitaani kuwa ni ya BMWs ki-uongozi; yaani baba, mke na watoto.

Na kama nilivyoeleza mwanzo, kama kiongozi mkuu wa nchi mwenyewe ameibeba ki-uongozi familia yake, kwa nini vigogo wengine walio chini yake wasifuate nyayo zake? Je, mkuu wa nchi anaweza kuikemea hali hiyo vikaoni; ilhali mfano kauonyesha yeye mwenyewe?

Hitimisho langu kwa wale wasomaji wangu walionitumia orodha hiyo ya watoto wa vigogo wanaowania uongozi wa UVCCM taifa, ni kwamba njia pekee niionayo ya kuzuia nepotism hiyo isiote mizizi katika Tanzania, ni kuiondoa madarakani CCM.

Nina hakika CCM kikishakoma kuwa chama tawala na chama dola, watoto hao wa vigogo watajiondoa, kama watakavyofanya pia baba zao na matajiri wengine; maana hawatakuwa na cha kufaidi tena ndani ya chama hicho.

Hiyo itatoa fursa kwa wale wenye mapenzi ya dhati na CCM, na ambao wanavutwa kwenye chama hicho kutokana na siasa yake na visheni yake ya kutetea maslahi ya wanyonge, kukijenga upya chama chao ili kiweze tena kukamata dola; na haijalishi ni miaka mingapi baadaye!

Kwa hiyo, kwa masikini wote katika Tanzania ambao wanajiona hawana chao katika CCM ya sasa ambayo imegeuka kuwa ya vigogo na watoto wao, lojiki kwao ni kukiasi chama hicho kwa kuhamia CHADEMA ili kwa pamoja waking’oe madarakani CCM katika uchaguzi mkuu wa 2015, na hivyo kuikata kabisa mizizi ya nepotism isizidi kukita katika ardhi ya nchi yetu.

Tusipofanya hivyo, kuna siku baadhi ya spoiled brats hawa wa vigogo watakamata uongozi wa juu wa nchi yetu, na hebu fikiria itakuwa nchi ya namna gani hiyo; maana na wao wataanza kuwaandaa watoto wao ili wawarithi nafasi hizo za uongozi watakapokuwa nao wamezeeka!

Tafakari.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Johnson Mbwambo
mbwambojohnson@yahoo.com

Toa maoni yako