Michezo
Uzi huo huo Simba, Yanga ikaze buti
Francis Chirwa
Toleo la 017
20 Feb 2008

SIMBA ya Dar es Salaam imeanza vyema michuano ya awali ya soka ya hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa kuichabanga Awassa ya Ethiopia kwa mabao 3-0.

Ushindi  huo wa kuvutia uliopatikana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umeiweka timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kuingia katika hatua inayofuata wakati  timu hizo zitakaporudiana mjini Addis Ababa.

Lakini  mambo hayakuwa  hivyo kwa timu nyingine ya Dar es Salaam inayoshiriki michuano  ya Kombe la Shirikisho, Yanga. Timu hiyo ya Jangwani ilichapwa bao 1-0 na AS Adema ya Madagascar katika mchezo uliofanyika Antananarivo.

Kwa wanaofuatilia kwa makini ushiriki wa timu hizo katika michuano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), matokeo hayo si ya kushangaza sana. Si ya kushangaza kwa kaungalia matokeo ya mchezo wa Simba.

Simba ni timu inayotisha inapokuja michuano ya kimataifa. Licha ya kuwahi kucheza fainali ya Kombe la CAF, timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ndiyo pekee ambayo ina rekodi ya kufurukuta dhidi ya timu za Uarabuni ambazo huzinyanyasa mno timu zilizoko kusini mwa Afrika kwa kuzifunga mabao mengi.

Cha kujiuliza ni kama Simba, baada ya ukimya mwingi, ndiyo safari hii  inataka kutikisa tena soka la Afrika katika ngazi ya klabu au la.

Hakika mabao 3-0 ni mengi na huo si ushindi mdogo.  Jambo la kufurahisha ni kwamba  hata baada ya kutoka uwanjani na ushindi huo mzuri,  Simba inaonyesha ya kuwa ‘inajuta’ kwa kutoibebesha timu hiyo ya Ethiopia kapu zima la mabao ilipocheza nayo Dar es Salaam.

Si viongozi wala wachezaji, hakuna anayeonekana kuvimba kichwa kwamba watakuwa na kazi ya mteremko watakaporudiana na timu hiyo. Hiyo ina maana ya kuwa timu hiyo  itacheza mchezo huo wa marudiano bila ya kuzingatia matokeo ya mchezo uliofanyika Dar es Salaam.

Golikipa wa kutegemewa wa timu hiyo, Juma Kaseja aliwaambia waandishi wa habari kwamba aonavyo yeye, kipigo walichopata Waethiopia kitawafanya waje juu kama mbogo wakati watakaporudiana nao.

Alisema kwamba anaona kama wamechokoza nyuki kwani wachezaji wa timu hiyo si kwamba walifungwa mabao hayo kwa sababu ni ‘wachovu.’  Alisema wachezaji wa timu hiyo wanajua kumiliki mpira na wana kasi.

Kingine ambacho hakukisema Kaseja ambacho wachezaji wa Simba ni lazima wazingatie ni ukweli kwamba watakapocheza nao, watawaona wenzao hawachoki uwanjani kwani Waethioipia wana pumzi mno kutokana na nchi yao kuwa katika ukanda wa juu mno. Ndiyo maana nchi hiyo inafanya vizuri katika mchezo wa riadha duniani.

Lakini hiyo ni tofauti na wenzao timu ya Yanga. Yanga  imefungwa bao 1-0 na ukweli wa matokeo hayo ni kwamba imeanza vibaya. Lakini ajabu, timu hiyo ndiyo inayojipa moyo mno wa kusonga mbele kuliko hata Simba!

Ndiyo, ni vizuri kujipa moyo, lakini ni lazima mtu uwe mkweli katika kujipa moyo huo. Unaweza ukafanya katika namna ambayo ikakufanya ubweteke. Kuna wawasi wa Yanga  kufanya hivyo isipojiangalia.

Nasema hivyo kwa sababu baada ya timu hiyo kufungwa Madagascar katika mchezo huo wa kwanza, kianchozungumzwa na uongozi wa klabu hiyo ni “kuwapo bado nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano.”

Ni kweli kama anavyosema Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lucas Kisasa kwamba suala la kufungwa ugenini ni sehemu ya mchezo, lakini kufungwa huko isiwe sehemu ya mkakati wa timu yake ya kukazania kufungwa bao moja ugenini kwamba ndiyo ‘ushindi.’

Kisasa alinukuliwa akisema kwamba kufungwa bao moja ugenini ni sehemu ya kufanya vizuri na akisisitiza kwamba mbaya ni kama ingefungwa zaidi ya bao moja ndipo angeona kwamba Yanga ina hali ngumu. 

Kufungwa ni kufungwa  liwe bao moja, mawili au matatu. Hakuna kufungwa vizuri kwa sababu katika mpira, timu inaweza kufungwa bao moja  ikashindwa kuridisha na ikafungwa mabao matatu  ikarudisha yote kama ilivyowahi kufanya Liverpool ya England kwa AC Milan ya Italia katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kikubwa ambacho uongozi wa Yanga  unastahili kufanya ni kuhamasisha maandalizi kamambe kwa ajili  ya mchezo huo wa marudiano ili warudishe bao hilo na kuongeza jingine au mengine kuweza kusonga mbele

Ingawa Madagascar ni taifa la mchanganyiko wa Wabantu, Wafaransa na idadi kuwa ya Wahindi. Timu yao iliyopambana na Yanga si ‘nyepesi’ kama pengine mashabiki wengi wa soka nchini walivyokuwa wamefikiria, ndiyo maana Yanga  imetoka huko na kipigo.

Kwa vile walicheza kufa au kupona kwa muda wote na kufaulu kufunga bao moja, Yanga inahitaji kujiuliza kwa maana ya kujifua kwa namna ambayo itajihakikishia kwamba inarudisha bao hilo na kuongeza mengine.

Iwe na mtazamo kama wa Simba katika mechi hiyo. Kwamba ina kazi kubwa mbele yake licha ya kushinda 3-0. Yanga nayo iwe inajua kwamba ina kazi tena kubwa zaidi maana inabidi igomboe bao na kuongeza jingine au mengine ya kufanya ifaulu kusonga mbele.

Tatizo la timu zetu na hasa Yanga ni mpira wake ‘kuchezwa’ zaidi magazetini. Magazetini hizi ni timu zinazotisha kama Arsenal, Manchester, Liverpool na Real Madrid. Lakini linapokuja suala la usakataji hasa wa  soka uwanjani, utashangaa.

Pia ni timu zinazotoa picha zinazokanganya katika Ligi Kuu ya Vodacom mtu ushindwe kuelewa wakati mwingine kama zinashinda kweli kwa uwezo wa usakataji kabumbu au zinashinda kwa mizwengwe?

Lakini angalau kwenye michuano inayoandaliwa na CAF,  uwezo halisi wa kila timu huonekana wazi, hivyo,  ni juu ya  timu zetu za Simba na Yanga kuonyesha uwezo halisi na si ule wa kupambwa magazetini tu. Kila la heri, Simba na Yanga kwenye michuano hiyo.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako