Vazi la taifa kwa nchi ya wavaa mitumba?

TANGU nijihusishe na harakati za utunzaji wa mazingira nikiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), nimepata fursa ya kutembelea vijiji vya mikoa kadhaa ya Tanzania.

Kila mara niwapo katika vijiji hivyo hupendelea kutembelea magulio ya wanavijiji; hasa yale yanayofanyika siku za Jumapili.

Hatua hii hunipa fursa ya kujua mambo mengi kuhusu wanavijiji wetu; kama vile uwezo wao wa manunuzi, aina za bidhaa wanazopeleka gulioni, bei zake.

Ukiwa katika eneo la magulio hayo, hutachelewa kugundua ni bidhaa gani zenye makundi makubwa ya wanunuzi. Miongoni mwa bidhaa hizo ni mitumba!

Mara nyingi utakuta wauza mitumba wametengewa sehemu zao maalumu ndani ya magulio hayo, na ndiko ambako utayakuta makundi makubwa ya wanavijiji wakichakura marundo kwa marundo ya nguo za mitumba wakitafuta zinazowafaa ili wazinunue.

Mara kadhaa nimepata kuyakaribia makundi hayo na kuangalia wanavijiji wanavyoshindana kuchakura marundo hayo wakitafuta nguo nzuri ambazo hazijachakaa sana.

Inasikitisha kwamba baadhi ya nguo wanazozinunua kutoka katika marundo hayo ya mitumba ni zile ambazo hazilindi heshima ya mtu na utu wake. Nazungumzia nguo za ndani kama vile sidiria, bukta na hata chupi!

Nina hakika wale wanaonunua nguo hizo za ndani za mitumba (au Kafa-Ulaya kama tulivyokuwa tukiziita zamani), hawafanyi hivyo kwa kupenda; bali kwa kulazimishwa na mazingira yao ya umasikini.

Kwa hakika, hakuna Mtanzania hata mmoja ambaye stahili yake ni kuvaa mitumba. Ni umasikini tu ndio unaotufanya tutegemee mitumba.

Yaani wanavijiji wanalazimika kuvaa sidiria na chupi za Kafa-Ulaya, kwa sababu hawana uwezo wa kifedha wa kumudu kununua mpya kabisa; hata kama zingekuwa zinapatikana vijijini mwao.

Ndugu zangu, ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba karibu asilimia 75 ya wanavijiji katika Tanzania hutegemea mitumba. Na ndio maana ni nadra katika vijiji vya Tanzania, miaka hii, kukuta maduka yanayouza nguo mpya kabisa au vitambaa vipya kabisa vya kushona.

Kwa hakika, hata mafundi cherehani wanatoweka kwa kasi vijijini siku hizi; maana hakuna wanaowapelekea vitambaa vipya ili wawashonee nguo, kwa sababu kinachotamba huko vijijini ni mitumba, mitumba na mitumba zaidi!

Lakini hata ukiiweka kando hiyo asilimia 75 ya wananchi wetu vijijini, hali si tofauti sana hata katika miji yetu; maana nako huko wengi wetu pia tunaokolewa na mitumba.

Kwa mfano, si wengi wetu hapa Dar es Salaam wana uwezo wa kwenda kununua nguo mpya katika maduka maarufu ya katikati ya jiji ambako shati moja la aina ya Van Hausen linaweza hata kufikia bei ya Sh. 250,000!

Kwa macho yangu mwenyewe nimepata kushuhudia, mara kadhaa, kwenye mabaa, watu wakinunua mashati na suruali za mitumba zinazotembezwa na Machinga. Kwa hiyo, si wanavijiji tu wanaotegemea mitumba; bali hata sisi wa mijini.

Labda swali la kujiuliza ni hili: Kwa nini tumeruhusu asilimia 80 ya Watanzania waishio vijijini na asilimia ndogo ya waishio mijini, wategemee kujivisha mitumba (Kafa-Ulaya)?

Hili ni swali linaloweza kuibua majibu mengi; lakini la msingi ni kwamba hatuna viwanda vyetu wenyewe vya nguo ambavyo vingetengeneza nguo hizo na zikauzwa hapa hapa nchini kwa bei nafuu ambazo wananchi wangezimudu.

Na kwa sababu hatuna viwanda vyetu wenyewe (naambiwa hata Kiwanda cha Nguo cha Urafiki sasa kimekuwa show-room ya magari), tunalazimika kununua nguo zilizotengenezwa Ulaya au Mashariki ya Mbali ambazo ni ghali mno.

Wengi wetu tusio na uwezo wa kununua nguo hizo ndio hao tunaokimbilia kwenye mitumba; hata kwa mahitaji ya nguo za ndani kama chupi na sidiria – nguo ambazo hazilindi heshima na utu wa mtu kama zinanunuliwa kwenye mitumba!

Lakini labda niwakumbushe vijana wetu wa sasa kwamba hali haikuwa hivi miaka ya nyuma. Huko nyuma tulishaanza kuwa na viwanda vyetu wenyewe vya kututengenezea nguo – tena nguo za viwango vya juu.

Nakumbuka miaka ile ya sabini nilipokuwa nasoma mjini Tanga kulikuwa na kiwanda cha nguo pale Kwaminchi kilichokuwa kikitengeneza mashati ya lebo maarufu duniani kama vile Gossage, Robin Hood, Arrow, Shikibo na nyinginezo.

Kiwanda kile cha Tanga sasa kimetoweka kwa namna ile ile vilivyotoweka viwanda vingine nchini mwetu, na sasa tunalazimika kutegemea kununua mashati ya Van Hausen ya mitumba kutoka Ulaya!

Ninapoutafakari ukweli huu mchungu wa kwamba asilimia 80 ya wanavijiji wetu wanategemea nguo za mitumba, nashindwa kuelewa kilichomsukuma  Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,  Emmanuel  Nchimbi, kuanzisha mchakato wa kutafuta eti vazi la taifa?

Kuna lojiki gani kutafuta vazi la taifa kwa nchi ambayo asilimia 75 ya wananchi wake wanategemea nguo za mitumba kutoka Ulaya? Kuna lojiki gani kutafuta vazi la taifa kwa nchi ambayo imeua karibu viwanda vyake vyote vya nguo na inasuasua hata kwenye kilimo cha pamba?

Mimi nadhani kina Nchimbi na wenzake serikalini wangetumia muda wao kazini kushughulikia masuala au matatizo mazito yanayoisumbua nchi yetu na watu wetu badala ya kupoteza muda kutafuta eti vazi la taifa!

Hivi sasa kuna tangazo linalorudiwa mara kwa mara redioni (ikiwemo Radio One) ambalo wizara hiyo inawahamasisha Watanzania wajitokeze kushiriki mchakato huo wa kutafuta vazi la taifa!

Kwa mtazamo wangu, tangazo hilo ni mfano mmoja wa jinsi ambavyo  Serikali imeacha kutumia redio kuhamasisha wananchi kwa masuala mazito ya maendeleo na yenye sura ya kitaifa kweli kweli, na badala yake inazitumia kuhamasisha wananchi kwa mambo mepesi mepesi na yasiyo na sura yoyote ya kitaifa; kwa maana ya kugusa Watanzania wote – wa mijini na vijijini.

Zimetowekea wapi zile zama ambapo RTD ilitumika kuhamasisha Watanzania; hususan wanavijiji wetu mambo mazito na muhimu kwao kimaisha kama vile kampeni za Mtu ni Afya, Mvua za Kwanza ni za Kupandia au Kata Mti Panda Mti?

Tangazo lile la wizara ya Nchimbi kwenye redio linajaribu kuwaaminisha Watanzania kwamba suala hilo la vazi la taifa ni muhimu mno katika maisha yao kwa sasa? Je, ni kweli? Jibu langu ni hapana.

Nina hakika wasomaji wangu watakubaliana nami kwamba kati ya matatizo mengi na nyeti yanayoisumbua nchi yetu, hili la vazi la taifa si mojawapo.

 Hebu jiulize: Vazi la taifa kwa ajili ya nani? Kwa ajili ya wakulima wetu vijijini wanaotegemea mitumba au kwa ajili ya mawaziri wetu wakienda Ulaya kuhudhuria mikutano ya kimataifa?

Kama ni kwa ajili ya wakubwa wakienda Ulaya na Marekani kuhudhuria mikutano ya kimataifa, mbona tunajua kwamba wanapenda mno kuvaa suti za kileo za ki-Magharibi, na wengine hata wakitamani kuvaa zile maalumu (designer suits) za kina Gucci?

Sasa kwa nini tupoteze muda wetu kutafuta hicho kinachoitwa vazi la taifa wakati tuna hakika wakubwa wetu wala hawatalivaa vazi hilo?

Ujumbe wangu kwa Bw. Nchimbi ni kwamba asipoteze muda kushughulikia vitu vyepesi vyepesi kama hicho; bali ajikite kwenye mambo ya msingi na nyeti yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.

Kwa mfano, badala ya kurukia kwenye suala la vazi la taifa angejikita kwanza katika kutafuta njia za kudhibiti uvamizi wa tamaduni mbaya za ki-Magharibi katika nchi yetu.

Si siri kwamba hivi sasa tumeathiriwa mno na uvamizi wa utamaduni wa Ulaya Magharibi (cultural imperialism) kwa sababu ya maendeleo haya ya sasa ya teknolojia ya mawasiliano. Vitu vinavyopapatikiwa hivi sasa na vijana wetu kama vile matamasha haya wanayoyaita summer jam, fiesta au vitu kama vile big brother, ushoga, au hata kule tu kutangaziwa moja kwa moja kwenye redio zetu (kupitia airwaves zetu) mechi za ligi ya soka ya England badala ya ligi yetu wenyewe, ni mifano inayonijia haraka haraka kichwani mwangu ya kutekwa kwetu kitamaduni kidogo kidogo na Wazungu!

Hivi sasa Watanzania, wakiwemo wa vijijini, wanamjua vizuri mno Wayne Rooney wa Manchester United kuliko wanavyomjua Juma Kaseja wa timu yetu ya Simba! Nimeshuhudia vijijini vijana wanavaa fulana zenye picha za Wayne Rooney!

Kwa mtazamo wangu, hili la kudhibiti mambo ya ovyo ya utamaduni wa ki-Magharibi yasisambae na kukubalika nchini (mazuri yapokelewe, mabaya yasipokelewe), ni la maana zaidi kwa sasa kuliko kukimbilia kutafuta eti vazi la taifa ambalo nina hakika katika mazingira ya sasa halitakubalika; kwa maana kwamba si wengi watakaolivaa.

Huko nyuma wapo wakubwa serikalini waliojaribu kuanzisha mchakato wa kutafuta vazi hilo, lakini hawakufika mbali; kwani mchakato ulikufa kifo cha asili.

Nina hakika hata huu wa kina Nchimbi, Merinyo na wenzake nao utakufa kifo cha asili, kwa sababu, kama nilivyosema mwanzo, kati ya matatizo mengi ya sasa yanayoisumbua nchi yetu, vazi la taifa si mojawapo. Watu wanataka mkate mezani, watu wanataka madawati kwa watoto wao shuleni na  si vazi la taifa!

Na isitoshe, heshima ya taifa na utambulisho wa taifa upo katika uchapakazi wa wananchi wake na viongozi wao, upo katika uungwana na uadilifu wa wananchi wake na viongozi wao, na si katika vazi la taifa.

Sisi wananchi pamoja na viongozi wetu tunaweza kuvaa vazi la taifa kwa saa 24, lakini hatuwezi kuheshimika popote  pale duniani kama tu vinara wa ufisadi, ubaradhuli, ubazazi na uvivu.

Hebu jenga picha hii kichwani mwako: Waziri  wetu amevaa vazi la taifa na yupo ofisini akisaini na Mzungu mkataba wa kifisadi baada ya kukatiwa ten percent yake!

Nadhani Mzungu huyo atalitazama vazi la taifa alilovaa waziri wetu na kuuangalia mkataba wa kifisadi aliosaini, na kisha atacheka kimoyomoyo!

Tafakari.

 

Comments

Hatutachelewa kuambia gharama kubwa zimutumika katika mchako wa kutafuta vazi la taifa.Kuanzia waziri mwenyewe nchimbi,pamoja na viongozi wote hawajui utaifa ni nini nashangaa hilo vazi watalipata wapi.Unaweza kupata vazi la taifa kama unatengeneza nguo zako mwenyewe nchini.Huwezi kuwa na vazi la taifa ambalo nguo au uzalishaji wa vyanzo vya hilo vazi lenyewe ni China,India au Thailand!!!

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.