Vijana CCM Babati wakiri kucheza rafu

BABATI, MANYARA

WANACHAMA wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Babati  ‘wameungama’ kwa viongozi wa wilaya hiyo wakisema walitumika kwa kulipwa fedha ili kuchochea mgogoro wa muda mrefu ndani ya chama hicho baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana.

Viongozi wa chama hicho wilayani Babati wako katika mgogoro wa muda mrefu baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambayo yalikipa ushindi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kushinda nafasi ya ubunge na udiwani katika kata tano kati ya nane.

Aidha viongozi na wafuasi wao wamegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza mwenyekiti wa chama wa wilaya hiyo, Ally Msuya na mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Ally Sumaye, wanapingana na kundi linaloongozwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Kisyeri Chambiri. 

Mwenyekiti na mjumbe wake wa NEC pia wamezuiwa kuingia kwenye vikao vya kamati ya siasa ya wilaya na hawakuwahi kuhudhuria vikao hivyo kwa zaidi ya miezi minane.

Hata hivyo mgogoro huo umeendelea kuwa mwiba kwa chama hicho kutokana na mamlaka za juu za chama kushindwa kuutatua na wiki iliyopita kundi la vijana wa UVCCM walikiri kuwa walipotoshwa na kununuliwa ili kuwapinga viongozi juu wa chama.

Pamoja na kukiri, vijana hao pia wamendika barua kuomba radhi kwa mwenyekiti Msuya na mjumbe wa NEC Ally Sumaye na kueleza kuwa  walikuwa wanatumiwa ili kuwachafua na  walichukua uamuzi huo Oktoba 9 mwaka huu mjini Babati.

 Katika barua hiyo ambayo imetiwa saini na wanachama 13 wa UVCCM, vijana hao wamefafanua kuwa sababu kubwa ya kufichua siri yao hiyo ni kudanganywa na kundi la viongozi wanaomuunga mkono Chambiri.

 “Baada ya jimbo kupotea uongozi wa wilaya uliamua kuungana na ili wapate kisingizio na walitukusanya na kutushawishi tufanye maandamano kuwa waliosababisha jimbo kupotea na kuchukuliwa na upinzani ni mwenyekiti Msuya, mjumbe wa NEC Sumaye, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Cosmas Masauda na mjumbe wa kamati ya siasa, Zulekha Mohamed,”

“Katika maandamano tuliandika mabango ya kuwatuhumu mwenyekiti na mjumbe wa NEC kwa maelekezo kutoka viongozi wa wilaya na kwa vijana waliogoma kuandamana waliitwa wapinzani (Chadema) na kutishiwa kufukuzwa katika chama”

“Tunawaomba viongozi wetu msamaha kwani tunajuta sana kufanya maandamano bila kufanya uchunguzi na pia tunawaomba mrudi na kuanza kukijenga chama chetu,” inahitimisha barua hiyo.

 Vijana hao pia wamewalalamikia watendaji wa hasa aliyekuwa kaimu katibu wa wilaya, Bernard Ghatti, kwa kushindwa kuwalipa posho zao wakati wakiwa kwenye kambi ya vijana.

 Wanadai kuwa walilipwa posho ya shilingi 20,000 kwa siku badala ya 48,000 na kuna wakati walisusia kambi hiyo kutokana na ulaghai waliokuwa wakifanyiwa na viongozi wao.

 Akizungumza mwishoni mwa wiki Ally Sumaye alisema wamekubali kwa moyo mweupe vijana hao kuomba msamaha.

 “Hawa ni sawa na watoto wetu, hivyo mwanao anapokiri kosa na kuomba msamaha utamkubalia tu na pia kibinadamu kuomba msamaha pale tunapokeseana ni hatua ya ustaarabu,” alisema.

Kwa mujibu wa Sumaye, lawama waliozokuwa wanatupiwa kutokana na jimbo la Babati Mjini kwenda upinzani hazikuwa na maana.

 “Sababu za CCM kushindwa ziko wazi kabisa.  Hapakuwa na mikakati yoyote ya dhati kupata ushindi, walidanganya na kutengeneza makundi ndani ya chama ili kufanikisha wizi wa fedha za uchaguzi zilizoletwa kutoka makao makuu,” alisema.

Alisema fedha hizo hadi leo hazijawafikia walengwa ambao ni  mabalozi, viongozi wa matawi, wenyeviti, makatibu uchumi, makatibu uenezi, mawakala na vijana wa CCM waliopelekwa kambini ili kukisaidia chama wakati wa uchaguzi.

Kwa upande wake Msuya alisema utaratibu mbaya uliobuniwa na aliyekuwa kaimu katibu wa wilaya, Bernard Gatti, kuhusu malipo ya posho ulisababisha viongozi wote ngazi ya chini kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Akizungumzia suala hilo katibu wa CCM Wilaya ya Babati, Kajoro Vyohoroka, alisema; “Mimi nawatambua kama viongozi halali wa chama sina barua yoyote inayoeleza kuwa wamesimamishwa uongozi na kuhusu masuala ya matumizi fedha ziwezi kuzungumzia kwa sababu nimehamia hapa mwezi Septemba tu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *