Michezo
Vijana Jazz isiachiwe ife
Ibrahim Mkamba
Toleo la 015
6 Feb 2008

VIJANA Jazz au Vijana Orchestre, vyovyote utakavyoiita, iko taaban na imelazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi ingawa ukiiangalia inaonekana kuwa na afya njema.

Ndiyo, inaonekana ina afya njema kutokana na mseto wa wanamuziki mahiri ilio nao wanaojumuisha watu wazima wenye uwezo mkubwa wa aina ya muziki wa kiutu uzima na vijana walio mahiri katika midundo ya ujana ujana.

Penye mseto kama huo ni lazima patoke vitu vikali vya kuwafurahisha watu wazima na vijana lakini mbona mambo hayaendi?

Bendi hii haipaswi kufa kwani ni mali ya vijana na ni alama ya harakati za vijana wa Tanzania za kujenga nchi yao. Ilianzishwa mwaka 1974 katikati ya vuguvugu la kuwahamasisha vijana wajibu wao wa kujenga nchi na kujiandaa kupokea uongozi wa nchi kutoka kwa wazee.

Kiongozi wa kwanza wa bendi hii kwa muda mfupi alikuwa John Ondolo, mwanamuziki Mtanzania aliyeishi Kenya kwa miaka mingi na kujipatia umaarufu mkubwa katika fani ya muziki nchini humo bila wengi kujua kuwa alikuwa Mtanzania, wakiamini alikuwa Mkenya hadi aliporudi nyumbani mwaka 1971.

Muda mfupi baadaye, marehemu Hemed Maneti Ulaya alipokea mikoba ya uongozi wa bendi hiyo kutoka kwa John Ondolo. Maneti alikuwa ametokea Morogoro kwenye bendi ya TK Lumpopo ya Marehemu Juma Kilaza.

Kimuziki, marehemu Maneti aliibuliwa, kuinuliwa na kulelewa na marehemu Kilaza. Sauti yake inasikika sana kwenye nyimbo za "Maisha Ya Sasa", "Esther Chaguo Langu"," Inanyonya Subusubi" na nyingine za TK Lumpopo.

Marehemu Maneti alipochukua uongozi wa bendi ya Vijana Jazz alianza nao na mtindo wa Kokakoka. Vibao maarufu vya mwanzo mwanzo vya bendi hiyo vilikuwa "Nimeruka Ukuta" uliofahamika na wengi, "Sabina" na Magdalena". Kwenye wimbo wa Sabina alimuomba mpenzi wake Sabina arudi kwani siku nyingi zilikuwa zimepita tangu aondoke na kwenye wimbo "Magdalena" alikuwa analalamika kuzuiwa na wazazi wake kumuoa Magdalena kwa sababu alikuwa na ulemavu wa jicho wakati yeye alikuwa akimpenda sana.

Pamoja na nyimbo hizo, nyimbo nyingine za mwanzo mwanzo za bendi hiyo zilikuwa, "Zuhura Naondoka", "Kamata Sukuma" waliotumia kujitaja majina, "Salima", "Nimeruka Ukuta Namba Mbili" na "Magdalena Namba Mbili" ambamo Maneti alifurahi baada ya wazazi wake kukubali amuoe Magdalena.

Kama ilivyoelezwa awali, bendi hii ilikuwa na majukumu rasmi katika kuwapo kwake. Hii inathibitishwa na aina ya nyimbo ilizowahi kutunga. Hebu angalia mifano hii: Kwanza bendi hii ni bendi pekee nchini kuwahi kutunga wimbo usio na lugha ya mafumbo wala utata wa kukemea rushwa, Huu ni ule wimbo uliorekodiwa RTD mwaka 1976 ambapo mpwa ameenda kumuomba mjomba wake nauli ya kurudi kijijini akawe mjamaa kamili baada ya kukosa ajira mjini kutokana na kuombwa rushwa ndipo aajiriwe.

Katika wimbo huo, kuna mahali marehemu Maneti aliimba,"nitapata wapi pesa ya kumpa ikiwa na mimi natafuta kazi, tabia kama hii lazima ikomeshwe"

Pili,ni bendi hii pekee ndiyo iliyojitokeza na kuunga mkono wito wa chama tawala (Chama cha TANU wakati huo wa mfumo wa chama kimoja) uliotolewa mwanzoni mwa mwaka 1976 wa kuanzishwa kwa maduka ya ushirika.

Waliimba hivyo katika wimbo wa "Operesheni Maduka" waliourekodi pamoja na huo wa Rushwa. Nyimbo nyingine katika toleo hilo zilikuwa "Masido", "Uhuru wa Mapenzi" na nyingine.

Tatu, ni Vijana Jazz pekee ndiyo iliyotunga nyimbo kadhaa za kuwahimiza vijana nchini kujua wajibu wao wa kulinda na kujenga nchi. Walifanya hivyo katika utunzi wao wa mwaka 1978 na mwingine wa mwaka 1983. Nyimbo hizo zote mbili zilikuwa zinaihusu CCM kwa sababu kwa wakati huo ndiyo kilikuwa chama pekee cha siasa nchini mwetu wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Vilevile, ni bendi hii pekee ndiyo iliyotunga wimbo wa kuwalaani "Magaidi" wa Msumbiji mwaka 1987.

Inasikitisha kwa bendi hii leo kuchoka namna hii bila wadau wa muziki nchini kujali. Huwezi kuamini leo kama bendi hii kwa nyakati tofauti imewahi kuwa na wanamuziki maarufu kama Hemed Maneti, Hamza Kalala, mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba,  Hassan Dalali ambaye ni mpiga solo mahiri aliyestaafu muziki na kujihusisha na soka.

Pia Athumani Momba "Sauti ya Chuma", Max Bushoke, Jerry Nashon "Dudumizi", George Mpupua, Cosmas Chidumule, John Kitime, Aggrey Crispo Ndumbalo na Benno Villa Anthony.

Wengine ni Suleiman Mbwembwe, Shaaban Yohana "Wanted", Hassan Shaw, Eddy Sheggy, Adam Bakari"Sauti ya Zege", Mohammed Gotagota, Mohammed Shaweji, Rashid Pembe, Kida Waziri na maarufu wengi sana ambao kwa bahati mbaya sana wamesahaulika katika orodha hii. Miongoni mwa wanamuziki hao wamo waliotangulia mbele ya haki.

Kwa upande mwingine, kufikia kilele chake cha mafanikio, bendi hii, pamoja na nyimbo zilizokwishatajwa, imetoa nyimbo maarufu kwa mitindo ya Kokakoka, Heka heka, Takatuka, Pambamoto na Air Pambamoto kama "Hekaheka Anapata", "Ngoma", "Jirekebishe Bibi"," Chiku (saizi yangu)", "Matata"," Jiko limenuna", "Maisha ya Amba" "Zenaba", "Ibrahim Nashangaa", "Zena", "Penzi Halina Umaarufu", "Mzee Tupatupa (anayependa uvulana na kukataa shikamoo kwa ajili ya kufukuzia wasichana Wadogo) "Tambiko la Pambamoto", "Mary Maria", "Ilikuwa Lifti Tu"," Shemeji wa Darisalama", na "Mundinde".

Nyingine maarufu ni"Ogopa Tapeli", "Wivu", "Penzi Haligawanyiki" namba moja na namba mbili yake ya shingo feni na macho balbu, "Mama wa Kambo Ni Mama", "Azza","Mwisho wa Mwezi", "Wifi Zangu Mnaninyanyasa", "Heshima ya Mtu", " The Top Queen Of Morocco Road", "Mama Chichi", "Shoga","Mfitini", "VIP" na nyingi nyinginezo zilizoifanya bendi hii iwe kubwa na maarufu mno.

Ni ukubwa wa muziki wake ndiyo uliifanya bendi hii ikawa na wapenzi wengi ndani na nje ya nchi. Aidha, ni changamoto ya muziki wake wa Kitanzania ndiyo iliyozilazimisha bendi za kikongo za wakati wake kama Marquiz Original, OSS, Orchestre Makassy na Kyauri Voice kupiga miondoko ya Kitanzania ili zinyang'anyane mashabiki na bendi hiyo na DDC Mlimani Park, Wana Msondo Ngoma, UDA Jazz na nyinginezo.

Endapo bendi za kikongo zingepiga miondoko ya kikongo wakati huo, zisingepata mashabiki wa kutosha kwani mashabiki wa Tanzania wa wakati huo walikuwa wamechizika na miondoko ya hapa hapa kutokana na umaarufu wa wakati huo wa bendi za hapa.

Mada hii ya wanamuziki wa Kikongo wa wakati huo kupiga miondoko ya kibongo na wa sasa kupiga ya kikongo itajadiliwa kikamilifu siku zijazo kwenye safu hii tukijaaliwa uhai.

Naamini kifo cha Vijana Jazz kimeandaliwa kutokana na mtazamo wa kinyakati (timing) ya hali hiyo. Bendi hii ilianza kudorora baada ya Umoja wa Vijana wa CCM, mmiliki wa bendi hiyo, kukumbwa na dhoruba kali kufuatia mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kutoka CCM kwa uchaguzi wa mwaka 1995.

Umoja huo ulijihusisha sana na mchakato huo kwa kujibainisha wazi wazi kuwa kwenye ushabiki wa baadhi ya wagombea. Kwa bahati mbaya kwao, aliyeshinda hakuwa mmojawapo wa wagombea wa chaguo lao! Baada ya uchaguzi tu wa mwaka huo, umoja huo ukawa katika mtikisiko mkubwa ulioikumba pia bendi yake!

Wakati bendi hiyo ikianza kuchechemea, ilitunga wimbo mzuri sana wa "Kisa cha Simu ya Mkononi" ambao, akiwa Rais, Benjamin Mkapa aliueleza kwenye Mkutano wa hadhara katika sherehe moja ya siku ya wanawake duniani kwamba alikuwa haupendi kwani unawadhalilisha wanawake.

Kilichofuata ni kwa uongozi wa bendi hiyo kueleza kuwa wasingeacha kuutumia wimbo huo hadi wapate amri rasmi ya kuuzuia. Kauli hiyo ilionekana kama kumdharau Rais! Baada ya hapo ndipo bendi hii ilipoanza kuwa hoi bin taaban ikitoa nyimbo chache chache nzuri kama "Mabaamedi."

Ni busara bendi hii isiuawe kwa sababu yoyote ile.Wadau ndani na nje ya Umoja wa Vijana wa CCM wajipange kuiinua tena bendi hii. Kama wanamuziki wake waliikosea CCM au serikali, waonywe na wasamehewe.

Tena, kutokana na tabia ya wanamuziki wetu kuhamahama bendi, inawezekana walioikosea CCM na serikali,kama kweli lipo kosa lililotendwa na wanamuziki wa bendi hiyo, leo hawapo katika bendi hiyo.

Katika kuiinua tena bendi hiyo, wadau wanaweza kuandaa mikakati mingi lakini naomba nishauri mkakati mmoja. Mkakati huo ni kurudisha mipigo asilia ya Pambamoto.

Hilo litafanikiwa kwa kuwarudisha kundini magwiji wa zamani wa bendi hiyo kama Komandoo Hamza Kalala, Benno Villa na wengine walio bado katika shughuli ya muziki. Vyovyote iwavyo, Vijana Jazz isife.Ikifa nani atanufaika?

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako