Vilio na vicheko sekta ya benki

SEKTA ya benki nchini huenda ilikabiliwa na hali ngumu ya kibiashara kwenye robo ya mwisho ya mwaka jana, baada ya ripoti za benki mbalimbali kwenye kipindi hicho kuonyesha kupungua kwa amana za wateja, faida na mikopo kwenye sekta mbalimbali za uchumi.

Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa viashiria hivyo, bado baadhi ya benki, zikiwemo kubwa zimefanya vizuri kwenye upande wa kukusanya akiba za wateja, ambacho ni kiungo kikuu cha biashara ya benki.

Kwa ujumla, benki kubwa na zile za kati zikiwemo Stanbic, Citibank, NBC, Standard Chartered Bank na KCB zilifanya vizuri japokuwa kulikuwepo na upunguaji wa amana za wateja pamoja na mikopo.

Kwa mujibu wa ripoti za benki mbalimbali  ambazo Raia Mwema imezifanyia uchambuzi, faida kwa asilimia kubwa ya benki ilipungua kwenye robo ya nne ya mwaka ikilinganishwa na kipindi hicho hicho cha mwaka 2015.

Benki ya FNB ndiyo ilionekana kuwa katika wakati mgumu baada ya ripoti zake kuonyesha kwamba hasara yake imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 5.1 robo ya nne ya mwaka jana kutoka hasara ya shilingi bilioni 5 kwenye kipindi kama hicho cha mwaka juzi.

Ripoti za benki hiyo pia zimeonyesha kwamba amana za wateja nazo zilipungua kutoka shilingi bilioni 171 za robo ya nne ya mwaka juzi hadi shilingi bilioni 142 kwenye robo ya nne ya mwaka jana.

Hata hivyo, pamoja na kushuka kwa amana za wateja na kuongezeka kwa hasara, benki hiyo iliongeza kiwango cha ukopeshaji hadi shilingi bilioni 134 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka bilioni 129  za robo kama hiyo ya mwaka juzi.

Benki ya biashara ya DCB nayo ilichechemea baada ya kupata hasara ya shilingi milioni 541 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka faida ya milioni 271 za kipindi kama hicho cha mwaka juzi.

Mbali na kukuongezeka kwa hasara, ripoti za benki hiyo ambazo hazijakaguliwa zimeonyesha kwamba amana za wateja nazo zilishuka hadi shilingi bilioni 84 robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi bilioni 85 ya robo ya nne ya mwaka juzi.

Hata hivyo,DCB iliongeza kiwango cha mikopo kwa wateja hadi kufikia bilioni 93 kwa robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi bilioni 91 zilizokopeshwa kwenye robo ya nne ya mwaka juzi.

Benki ya UBA nayo ilishuhudia kuongezeka kwa hasara kutoka shilingi milioni 890 za robo ya nne ya mwaka jana kutoka hasara ya milioni 819 za robo ya nne ya mwaka juzi huku mikopo ikipungua kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka bilioni 91 za robo ya nne ya mwaka juzi hadi bilioni 41 za robo ya nne mwaka jana.

Ripoti za benki hiyo zimeonyesha kwamba amana za wateja nazo zilishuka hadi kufikia shilingi bilioni 35.9 kutoka shilingi bilioni 38.4 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Benki ya Ecobank, ambayo kwenye robo ya nne ya mwaka juzi ilipata hasara ya shilingi bilioni 13.7 imeendelea kufanya vizuri baada ya kupunguza hasara hiyo mpaka shilingi bilioni 8.l kwenye robo ya nne ya mwaka jana.

Amana za wateja wa benki hiyo ziliongezeka hadi kufikia shilingi  bilioni 123 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi bilioni 113 za robo ya nne ya mwaka juzi huku mikopo ikipungua hadi shilingi bilioni 147 kutoka bilioni 181 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Faida kwa upande wa benki ya NMB, ambayo ni moja ya benki kubwa nchini ilishuka hadi kufikia bilioni 38 hadi bilioni 31 kwenye kipindi hicho huku  mikopo yayo ikipungua kutoka shilingi trilioni 2.80 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi trilioni 2.85 kwenye robo ya nne ya mwaka juzi.

Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa faida na kiwango cha mikopo, benki hiyo iliongeza kiwango cha amana za wateja hadi kufikia shilingi trilioni 3.65 za robo ya nne mwaka jana kutoka shilingi trilioni 3.43 kwa robo ya nne ya mwaka 2015.

Kwa upande wa benki ya Stanbic, faida iliongezeka mara tatu hadi shilingi bilioni 13.4 za robo ya nne ya mwaka jana kutoka bilioni 4.4 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Benki ya NIC nayo ilifanya vizuri kwenye faida baaya ya kuongezeka kwa takribani mara mbili hadi shilingi milioni 818 kutoka shilingi milioni 441 huku mikopo ikipanda hadi shilingi bilioni 97 kutoka shilingi bilioni 90.

Standard Chartered Bank nayo ilifanya vizuri kwa upande wa faida kwani imepanda kutoka hasara ya shilingi bilioni tatu kwenye robo ya nne ya mwaka juzi hadi faida ya bilioni 8.8 za robo ya nne ya mwaka jana.

Amana za wateja wa benki hiyo zilishuka hadi kufikia shilingi bilioni 908 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi trilioni 1.01 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Kwa upande wa mikopo, benki hiyo ilikopesha kiasi cha shilingi bilioni 687 kwenye robo ya nne ya mwaka jana kutoka mikopo ya shilingi bilioni 732 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Citibank nayo ilikubwa na kushuka kwa viashiria hivyo kwani mikopo na faida vilipungua katika kipindi hicho lakini amana za wateja ziliongezeka kwa kiwango kidogo.

Benki ya NBC ilifanya vizuri katika kipindi hicho baada ya faida yake kuongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 7.8 robo ya nne ya mwaka jana kutoka faida ya shilingi bilioni 5.5 za robo ya nne ya mwaka 2015.

Hata hivyo, pamoja na kuongezeka kwa faida, upande wa mikopo ulipungua hadi kufikia shilingi trilioni 1.23 za robo ya nne ya mwaka jana kutoka shilingi trilioni 1.26 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Benki ya KCB, ambayo pia imeorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam nayo ilifanya vizuri kwenye upande wa faida baada ya kuongezeka hadi shilingi bilioni 2.7 kutoka shilingi bilioni 1.9 za robo ya nne ya mwaka 2015.

Ripoti za benki hiyo zimeonyesha kwamba, amana za wateja na mikopo viliongezeka kwenye kipindi hicho, japokuwa ongezeko hilo halikuwa kubwa sana.

ACB Bank nayo ilifanya vizuri kwenye kipindi hicho japokuwa faida yake ilipungua hadi shilingi bilioni 2.4 kutoka shilingi bilioni 2.6. Vilevile, mikopo na amana za wateja wa benki hiyo viliongezeka kwenye kipindi hicho.

Benki nyingine ambazo faida zake zilishuka katika kipindi hicho kwa mujibu wa ripoti za hesabu ni Habib kutoka bilioni 1.2 hadi bilioni 1.1, BancABC kutoka shilingi bilioni 3.3 had milioni 239 na Uchumi Commercial Bank kutoka shilingi milioni 37 had milioni 9.

Access bank imeweza kufuta hasara yao ya shilingi milioni 187 ya robo ya nne ya mwaka juzi kwa kupata faida ya shilingi milioni 928 huku Benki ya Biashara ya China nayo ikishusha hasara yake hadi kufikia shilingi milioni 685 robo ya nne mwaka jana kutoka hasara ya shilingi bilioni 1.1 za robo ya nne ya mwaka juzi.

Benki ya Equity ilifanya vizuri baada ya viashiria vyake vyote vitatu kuwa chanya kwenye kipindi hicho vikiwemo faida, amana za wateja na mikopo.

Ripoti ya Equity Bank ya robo ya nne ya mwaka jana imeonyesha kwamba faid imeongezeka hadi shilingi bilioni 1.7 kutoka shilingi bilioni 1.6 wakati mikopo ikiongezeka hadi shilingi milioni 344 kutoka shilingi 326 huku mikopo ikiongezeka hadi shilingi bilioni 319 kutoka shilingi bilioni 309 za robo ya nne mwaka 2015.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *