Viva Fidel!

HATIMAYE, pazia la maisha ya aliyekuwa kiongozi wa Cuba, Fidel Castro Ruz, limefungwa rasmi. Kama ilivyo kwetu sote, naye amerejea kwa Muumba wake.

Usiku wa kuamkia Novemba 26 mwaka huu; majira ya saa 4:29, moyo wa mwanamapinduzi huyu uliacha kupiga na dunia ikawa imempoteza mmoja wa viongozi muhimu wa karne iliyopita.

Hatusemi kwamba Castro alikuwa malaika. Kama mwanadamu mwingine, alikuwa na mapungufu yake. Kwa bahati mbaya, wapo watu ambao waliuishi upande mbaya wake.

Lakini Watanzania, Waafrika na wanyonge wengine duniani kote, hawana sababu ya kumchukia Castro. Na ndiyo sababu msiba wake umekuwa kama msiba wa dunia nzima.

Huyu alikuwa kiongozi wa kisiwa kidogo chenye watu milioni 11 tu. Lakini ni kisiwa kilichoweza kufanya makubwa na kushindana na mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi na kijeshi.

Waafrika watamchukiaje Castro baada ya kuwa ametuma wanajeshi wake kwenye ukombozi wan chi za Kusini mwa Afrika?

Watamchukiaje Castro wakati alikuza heshima ya watu weusi wa Cuba na kuwapa haki ambazo hawakuwa nazo kwa miaka mingi huko kwao?

Waafrika watamchukiaje Castro baada ya pambano lile kali la Cuito Cuanavale nchini Angola lililofungua mlango kwa Uhuru wa Namibia na anguko la utawala dhalimu wa makaburu wa Afrika ya Kusini?

Nelson Mandela, alipata kutamka kwamba kama isingekuwa kipigo kile cha mbwa mwizi ambacho Jeshi la Makaburu wa Afrika Kusini ilikipata pale Cuanavale, pengine historia ya ukombozi Kusini mwa Afrika ingekuwa tofauti leo.

Huyu ni Castro aliyesaidia madaktari, walimu na dawa kwa nchi masikini. Huyu ni kiongozi ambaye alikuwa chachu ya uzalendo na fahari kwa watu wote duniani waliokuwa wamefungwa na kongwa na ukoloni na ubeberu.

Kwa sababu ya umahiri na ushujaa huu wa Castro, wengine walijiamini na kusema tutaweza kupambana na ubeberu.

Kama Cuba, taifa lisilokuwa na rasilimali zozote za maana kuondoa fukwe zake na watu ilionao, imeweza kupambana na mabeberu na kudumu, vije kwa wengine wenye rasilimali za kutosha, ardhi na watu wenye bongo na afya?

Fidel amemaliza maisha yake ya hapa duniani ingawa tunafahamu kwamba ataendelea kuishi kwenye mioyo ya watu kwa miaka mingi ijayo.

Sifa kwa Castro zitabaki kuwa hazina maana endapo nchi zetu zitaendelea kuwa sehemu za kufanyia majaribio kwa sera za kiuchumi mabeberu.

Haitakuwa na maana kumsifu na kumuenzi Fidel wakati nchi zetu zitaendelea kutembeza bakuli la kuomba kwa nchi tajiri wakati hatuna sababu ya kufanya hivyo.

Ni aibu kwamba nchi kama Tanzania inakwenda kuomba msaada kwa nchi isiyo na utajiri wa rasilimali, fukwe, ardhi nzuri wala idadi ya watu kama ya kwetu.

Funzo kubwa kutoka katika maisha ya Fidel Castro ni kwamba Watanzania tukiamua tunaweza kuishi pasipo kutembeza bakuli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *