Habari
Vumbi kiwanda cha saruji kikwazo Songwe Airport
Felix Mwakyembe
Mbeya
Toleo la 256
29 Aug 2012

HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kutumia Uwanja wa Ndege wa Songwe, mkoani hapa, unaoendelea kujengwa imehitimisha muongo wa siasa chafu dhidi ya mradi huo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Matumaini ya wananchi mkoani Mbeya kuhusu kukamilika kwa uwanja huo yalipata nguvu zaidi pale mradi huo ulipotengewa shilingi bilioni 17, katika bajeti ya mwaka huu.

Hata hivyo, wakati matumaini ya kukamilika kwa uwanja huo yakiwa makubwa kiasi hicho miongoni mwa wananchi, baadhi ya watalaamu wa masuala ya anga wamebainisha kuwa, bado kuna tatizo la vumbi kutoka Kiwanda cha Saruji Songwe, ambacho kipo jirani na uwanja huo.

“Lile vumbi linalotoka pale kwenye Kiwanda cha Saruji Songwe si zuri kwa usalama wa ndege, ni hatari kwa injini za ndege,” anasema mtaalamu wa masuala ya anga jijini Mbeya, ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa maelezo kuwa si Msemaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania.

Mtaalamu huyo, hata hivyo anatoa ufumbuzi wa tatizo hilo kuwa ni kulielekeza vumbi hilo chini (ardhini) badala ya kuliacha lisambae hewani.

“Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ndiyo waliofanya utafiti na kuamua uwanja ujengwe hapo. Kwa hiyo, wanalifahamu suala hilo, kiwanda kinaweza kuelekeza lile vumbi chini badala ya kuliacha lisambae angani,” anasema mtaalamu huyo.

Mbali ya tatizo la vumbi, taarifa za ndani za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania pamoja na wizarani zinabainisha kusita kwa serikali kutangaza rasmi tarehe ya kukamilika kwa mradi huo, kutokana na kutokuwapo kwa uhakika wa kukamilika kwa vifaa vyote vinavyohitajika katika uendeshaji wa viwanja vya ndege.

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe anachukua tahadhari kila anapohojiwa kuhusu kukamilika kwa uwanja huo, tahadhari ambayo wadau wa usafiri wa anga wanaielezea kuwa inatokana na waziri huyo kutokuwa na uhakika kuhusu kuwapo kwa vifaa wakati ujenzi utapokuwa umekamilika. 

Kwa mujibu wa mratibu wa kampuni inayojenga uwanja huo, Omindo Paul, tayari asilimia 85 ya kazi imekamilika hivyo iliyobaki ni asilimia 15 tu, ambayo anasema wanahitaji shilingi bilioni tano tu kuikamilisha.

Anazitaja kazi zilizokamilika kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (run-way), barabara ya kiungio (taxiway), eneo la kuegesha magari, wakati eneo la maegesho ya ndege (apron) limebaki tabaka la mwisho la zege.

Kiwanja cha Ndege cha Songwe kinajengwa kwenye Bonde la Ufa la Magharibi katika Wilaya ya Mbeya Vijijini, takribani kilometa 20 kutoka katikati ya Jiji la Mbeya.

Mradi wa ujenzi wa uwanja huo ulichukua sura ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, baadhi ya wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi waliokuwa na nia ya kuwania urais kupitia chama hicho tawala waliupiga vita wakiamini ulikuwa unamjenga zaidi kisiasa, Profesa Mark Mwandosya.

Prof. Mwandosya alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliokuwa wakiwania kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na kutokana na nafasi yake serikalini, akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi (wakati huo) alihusika moja kwa moja katika usimamizi wa ujenzi wa uwanja huo.

Siasa chafu kuelekea uchaguzi huo zinatajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa kusuasua kwa ujenzi wa uwanja huo kwa kutotengwa fedha za kutosha hivyo kusababisha kutumia zaidi ya miaka 10 uwanja huo ukiendelea kujengwa.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Suleiman S. Suleiman, inaeleza kuwa mkataba kwa ajili ya awamu ya tatu ya mradi huo uliwekwa sahihi na pande zote husika na ulisainiwa Septemba 12, mwaka 2008 ukiwa umetarajiwa kuchukua miezi 18 hadi kukamilika kwake.

Kaimu Mkurugenzi huyo anazitaja sababu zilizochangia ucheleweshaji wa mradi huo kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa malipo ya awali kutoka serikalini, ongezeko kubwa la kazi ya kukata na kusoma udongo kutoka mita za ujazo 90,000 hadi 800,000.

Sababu nyingine ni mabadiliko ya usanifu wa tabaka la msingi (base course) kutoka kutumia kokoto hadi kutumika saruji, kuharibika kwa mtambo wa kupikia lami na mkandarasi kusitisha shughuli za ujenzi kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Taarifa za ndani kutoka mamlaka hiyo zinaitupia lawama Hazina (Wizara ya Fedha) kuwa kiini cha tatizo la ucheleweshaji, ikiwa imebainika kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, kwa mfano, mkandarasi aliwasilisha hati za madai za kazi zilizokamilika shilingi bilioni 5.1 mapema, huku Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nayo ikiwahisha kupeleka hazina, lakini malipo yalicheleweshwa hadi Julai19, 2012.

Uchelewesha huo unatajwa kuathiri kwa kiwango kikubwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa uwanja huo.

Mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe ulianza Januari 2001, huku miundombinu yake ikiwa ni yenye kuwezesha ndege aina ya FK50 kutua na kuruka, lakini kabla ya kuanza utekelezaji awamu ya pili, serikali iliamua kupanuliwa kwa miundombinu ya kiwanja hicho ili kiweze kuhudumia denge za ukubwa wa Boeing 737.

Uamuzi huo wa serikali ulisababisha kubadilika kwa miundombinu ya uwanja na hivyo kulazimisha kuongezwa muda wa kukamilika awamu ya pili ya ujenzi ambapo sasa ilianza mwaka 2004 na kukamilika 2008.

Katika awamu hiyo ya pili kandarasi ya ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, zimamoto, matanki ya kuhifadhia maji safi, ununuzi na ufungaji wa pampu zake ulifanywa na Kampuni ya Tanzania Building Works Ltd, huku kazi ya ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara ya kiungo na ile ya kuingilia kiwanjani inafanywa na kampuni kutoka Kenya, Kundan Singh Construction Ltd.

Baada ya kukamilika kiwanja hicho kitakuwa na barabara ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa kilomita 3.34 na upana wa mita 60, barabara ya kuingia moja na eneo la maegesho lenye uwezo wa kuegesha ndege nne aina ya Boeing 737 kwa pamoja.

Kiwanja cha Songwe kitakuwa na majengo yote muhimu likiwamo jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 300 kwa saa, jengo la kuongozea ndege, zimamoto na jengo la utabiri wa hali ya hewa.

Baadhi ya marubani wenye kufika mkoani Mbeya, wameonesha shauku ya kukitumia kiwanja hicho kwa sasa pamoja na kutokukamilika kwake, ikiwa ni pamoja na kutokuwapo kwa vifaa muhimu kwa usafiri wa anga.

Kapteni Dominic Bomani aliyerusha ndege iliyomleta Rais Jakaya Kikwete mkoani Mbeya hivi karibuni anathibitisha kuwa kwa sasa, uwanja huo unaweza kutumika kwa ndege za abiria.

“Uwanja ni mzuri sana, hauna bumps, uko smooth, mrefu, runway yake pana, upo eneo zuri, upo clear sana,” anasema Kapt. Bomani katika mazungumzo yake na mwandishi wa makala hii, mara baada ya kutua uwanjani hapo na ndege aina ya F28.

Uwanja huo wa Songwe licha ya ukubwa wake lakini bado unayo nafasi kubwa ya upanuzi hapo baadaye. Ni uwanja uliopo katika eneo lisilo na miti wala miinuko mbali ya safu za Mlima Loleza na Mlima Mbeya, inayoonekana kwa  mbali.

Iwapo Rais kautumia uwanja huo pamoja na kutokukamilika, nani tena wa kukwamisha ukamilishaji wa ujenzi wa uwanja huo? hili ni swali linalosanifu vichwa vya watu mbalimbali hapa mkoani Mbeya, kwani wananchi wanaamini kuwa hatua ile ya Rais Kikwete kutumia uwanja huo ni amri kwa wasaidizi wake kuhakikisha mradi unakamilika mapema, kabla mwisho wa mwaka huu.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako