Vyombo huru vya habari vijipange upya kujihakikishia uhuru wake

DEMOKRASIA haiwezi kustawi bila kuwapo vyombo huru vya habari. Vyombo huru vya habari, hata hivyo, haviwezi kutokea na kukua kwa hisani ya watawala au wale walio madarakani.

Nchi yoyote ambayo haina vyombo huru vya habari kimsingi iko katika utawala wa kibabe (tyrannical regime) au utawala wa kiimla (dictatorial regime). Tawala zote zenye kuhodhi madaraka bila kuhojiwa zina vyombo vya habari lakini si vyombo huru.

Vyombo Huru vya Habari ni nini hasa?

Tunapozungumzia vyombo huru vya habari hatuzungumzii tu kuwa si vya serikali. Wapo wanaoamini kuwa vyombo ambavyo havimilikiwi na serikali ndiyo vyombo huru. Kusema kweli tunapozungumzia vyombo ‘huru’ vya habari hatuzungumzii suala la umiliki tu; ni zaidi ya umiliki.

Tunapozungumzia ‘uhuru’ tunazungumzia ile hali ambayo chombo cha habari kinakuwa huru kutoka kwa ushawishi (influence) wa serikali, maafisa wa serikali, watu maarufu, wamiliki au taasisi na makampuni makubwa.

Ili vyombo vya habari viwe huru kweli vinapaswa kuwa na uwezo wa kutafuta habari, kuzihariri na kuzichapisha bila kulazimishwa au kushawishia kuhusiana na yaliyomo katika habari hizo au namna ya kuzichapa.

Wakati wowote vyombo vya habari vinapojikuta vinalazimika au kulazimishwa kuandika au kutoandika habari fulani bila kuwa na sababu ya kimsingi basi vyombo hivyo vinakuwa vimepoteza uhuru wake na habari zake zinapaswa kuangaliwa na wateja (wasomaji, wasikilizaji na watazamaji) kwa shuku.

Mambo yanayochangia vyombo vyetu vya habari kupoteza uhuru wake

Kuna mambo mengi ambayo yanachangia vyombo vyetu vya habari kuhatarisha au kupoteza kabisa uhuru wake. Kati ya hayo mengi, nitaje machache tu, ambayo naamini wahariri na wakuu wa vyombo ‘huru’ vya habari nchini wanahitaji kuyaangalia kwani yanatishia uhuru wao na kwa hakika wanatishia kushamiri kwa demokrasia nchini.

Kulipwa posho na wahusika wa habari

Kati ya vitu ambavyo vinatishia uhuru wa vyombo vya habari ni waandishi wa habari (miongoni mwao wahariri) wanapokubali kupokea posho kutoka kwa wale ambao wameenda kuwasikiliza au kuandika habari zao.

Kumekuwa na tabia ambayo imekubaliwa na vyombo vya habari (media houses) ambapo waandishi wanaitwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari au wanatumwa kufuatilia habari fulani na wakifika huko pamoja na kukusanya habari hupokea ‘bahasha za khaki’ ambazo ndani yake kunakuwa na posho ya “vikao”.

Waandishi wanaopokea posho hizo kutoka kwa wahusika wanajiweka katika nafasi ya kuwa ‘compromised’ kwa maana ya kwamba wanapoteza uhuru wao wa kuripoti mambo, kuhoji au kuchambua kwa kuhofia kuwa siku nyingine wanaweza wasipewe nafasi ya kualikwa kwenye mikutano hiyo.

Sasa, waandishi wanaopokea posho hizo hawako huru kukosoa au kuandika taarifa zinazoweza kukosoa wale waliowapatia posho. Nimewahi kusikia baadhi ya marafiki zangu wakitupiana kazi ili wao wasiandike taarifa mbaya za walioawapa posho na hivyo baadhi ya habari zinatokea kwenye vyombo vingine vya habari. Hili ni tatizo la kwanza.

Hili nimewahi kusikia limewahi kutokea hata kwenye ofisi kubwa za umma ikiwemo Ikulu na wizara mbalimbali.

Kugharimiwa safari na wanaohusika na habari

Jambo jingine linalovuruga uhuru wa habari ni hili la waandishi pamoja na wahariri wao kukubali kugharimiwa safari na wale ambao wanaenda kuandika habari zao. Hii inatokea kwa taasisi za serikali zinapoandaa semina zinaamua kuwaalika waandishi wa habari. Sasa haiishii katika kuwaalika tu bali wanaamua kuwalipia posho za safari na hata gharama ya warsha hizo.

Mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na taasisi hizo na hata makampuni na mashirika binafsi ni kuandaa warsha maalumu  kwa ajili ya vyombo vya habari. Mialiko inatolewa ya semina au warsha kwa ajili ya vyombo vya habari na vyombo vya habari vinavyotakiwa kufanya ni kupeleka wawakilishi wake. Wawakilishi wale huenda na kushiriki warsha hizo na mwisho wa warsha au semina watu wanatarajia kuwa watapa posho fulani hivi na baadhi ya waandishi wamekuwa wakilalamika endapo taasisi haina mpango wa kutoa posho (hili nimeliona katika baadhi ya taasisi za kimataifa).

Ukaribu usio na mipaka baina ya waandishi na wahusishwa wa habari

Lakini binafsi naamini jambo kubwa zaidi linalotishia uhuru wa habari nchini na hasa kutishia ukuaji wa demokrasia ni ukaribu wa waandishi na wahusika wa habari mbalimbali. Kutozingatiwa kwa miiko inayokatakaza ukaribu usio na mipaka ambapo waandishi wanapokea zawadi au malipo fulani fulani wakati wa kutekeleza majukumu yao ni hatari sana kwa tasnia ya habari nchini.

Baraza la Habari la Tanzania (MCT) limeweka katika mojawapo ya miiko yake kwa waandishi wa habari ni kutopokea ‘zawadi’ na malipo mbalimbali ya kiana. Hata hivyo miiko hii haina ukali unaostahili hasa ikiachilia waandishi kuwa huru “kupima” kama zawadi na ‘ofa’ mbalimbali haziwaweki katika mazingira mabaya ya kufanya kazi, yaani kuwa compromised.

Kila chombo cha habari kinatakiwa kiwe na miiko yake ya ndani kuhusiana na masuala haya lakini zaidi kiwe na adhabu au matokeo kwa yule anayevunja. Mwiko ambao ukivujwa hauna matokeo siyo mwiko tena.

Je, mwandishi anapopokea posho au malipo kutoka kwa watu nje ya waajiri wake kama asante ya kuhudhuria au ‘takrima’, anaweza vipi kujiita huru? Je, ili malipo hayo yaonekane yasiwe halali ni lazima mwandishi aambiwe kitu cha kufanya au kutokufanya na yule aliyempa posho au yule aliyempa malipo anatarajia mwandishi kujua ‘wajibu’ wake?

Je, malipo haya ambayo wanapewa waandishi wa habari wakati wa kutekeleza kazi zao nje ya malipo kutoka kwa waajiri wao na wanaamua kuandika habari kwa namna fulani ya kupendelea waliowalipa tuchukulie ni sehemu ya rushwa?

Je, waandishi ambao wako huru (freelance) ambao wanalipwa kutokana na kazi zao wapokee malipo haya kama sehemu ya mapato yao halali au wategemee malipo kwa kuuza kazi zao?

Baadhi ya maswali hayo na mengine mengi yanahitaji majibu. Nini kifanyike kutoka hapa nalo ni jukumu la waandishi na vyombo vya habari kufikiria.

Hata hivyo, kanuni ya msingi ambayo inahitaji kuzingatiwa ni kujua kuwa bila vyombo huru vya habari hatuwezi kuwa na demokrasia kwani vyombo vya habari vinaporuhusu kushawishiwa kwa fedha au zawadi, vinageuka na kuwa maadui wa demokrasia (enemies of democracy).

Vyombo vya habari vijichunguze na kuchunguza sera zake za ndani na kuona kama ziko huru kweli au zinajiita huru ili kuuza kazi zake tu. Na hapo hatujazungumzia nafasi ya matangazo ya  biashara kama silaha ya kutishia vyombo vya habari!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *