Waandishi Arusha wamgomea Waziri Lukuvi

22/12/2016 – 

WAANDISHI wa habari Mkoa wa Arusha leo wamegoma kuripoti ziara ya  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya kukamatwa kwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha ITV, Halfan Lihundi.


Lihundi ambaye huripoti ITV kutokea Arusha, alikamatwa jana na polisi kupitia amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, kwa kile kilichoitwa kosa lakuandika habari za uchochezi.

Awali, kabla ya hatua hiyo ya waandishi kugoma walimwomba Waziri Lukuvi kuingilia kati suala hilo la kushikiliwa mwandishi huyo kwa kuwa habari anazotuhumiwa kuandika zinatokana na migogoro ya ardhi. Hata hivyo, Lukuvi aliwaeleza kuwa hawezi kuingilia suala hilo kwa kuwa liko nje ya mamlaka yake.

Kutokana na kauli hiyo, waandishi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu,   waliweka msimamo wa kususuia ziara ya Waziri Lukuvi.

"Mnapohitaji waandishi habari mnatuita lakini waandishi wa habari wanapokuwa na matatizo hamtaki kuwasikiliza na kuingilia kati kutatua matatizo hayo," 'alisema Gwandu.

Baada ya msimamo huo wa waandishi hao kupitia kwa mwenyekiti wao, Waziri Lukuvi aliondoka na msafara wake kuelekea Arumeru akiongozana na waandishi wa Shirikika la Habari la Utangazaji la Tanzania (TBC).

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *