Waandishi na Magufuli: Mbwambo amemwaga sumu

NACHANGANYIKIWA nianzie wapi kuandika hiki ninachokusudia kupitia gazeti hili, ambalo walau, kwa mtazamo wangu, lina uzito wake na heshima yake miongoni mwa magazeti yanayochapwa nchini na kusomwa na jamii ya Watanzania.

Kinachonifanya nichanganyikiwe, ni kitu kimoja. Nakusudia kujadili, kwa nia ya kukosoa makala ya Johnson Mbwambo, mmoja wa waandishi nguli nchini, lakini pia kaka na mwalimu wangu muhimu, si katika tasnia hii ya habari pekee, bali hata katika aina ya mwenendo sahihi wa maisha unaomstahili binadamu kuuishi ndani ya jamii inayotuzunguka!

Hata hivyo, kwa kuwa ni wajibu wangu kufanya hivyo, na kwa kuwa nadhani ni fahari pia kwake Mbwambo kuona anapata changamoto kutoka kwa mwanafunzi wake, basi namuomba Mwenyezi Mungu aniongoze katika hili ninalotaka kulifanya kupitia makala haya.

Nazungumzia makala ya Mbwambo katika matoleo mawili ya gazeti hili kwa wiki mbili mfululizo zilizopita, iliyokuwa imebeba kichwa cha habari kisemacho: “Waandishi kaeni chonjo na Magufuli,” huku kichwa hicho kikubwa kikipambwa na kichwa kingine kidogo kilichobeba msisitizo kwa waandishi hao wa habari wa Tanzania hii, kikisema: “Msiendekeze kumsifu, mkosoeni kwa anayokosea.”

Makala hayo yalibeba maudhui kadhaa, ambayo ni pamoja na wosia maalumu kwa waandishi  wa habari kwamba wao wana wajibu mkubwa wa kitaaluma kumsimamia na kumrekebisha Rais Dk. John Magufuli, ili awe rais mzuri, na alete mabadiliko ya kweli ya nchi yetu kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mbwambo anaonekana kuwa na hofu ya uwezekano wa Magufuli kugeuka kuwa Rais dikteta kamili tofauti na alivyokuwa akimfikiria na kumuona mwanzo kuwa anaweza akaishia kuwa dikteta poa.

Ili kuitekeleza kazi hiyo ya kumkosoa, kumdhibiti na kumfunga gavana Magufuli, Mbwambo anawahimiza zaidi waandishi wa habari waungane na Watanzania kwa ujumla wao, Bunge, vyama vya siasa, NGOs, vikundi vya kiraia, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu katika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao huo.

Kwa maoni na mtazamo wa Mbwambo vyombo vya habari vikijisahau tu, kwa kuendekeza kumsifia na kumpamba Rais Magufuli bila kumkosoa, huku tayari wananchi nao kwa upande wao wakiendelea kumtukuza na kujenga matumaini makubwa kwake, anaweza kubadilika.

Tatizo ninalolipata katika wosia huu wa Mbwambo wa kukosoa ni moja tu. Mwanzo hadi mwisho wa wosia wake huo, hakuna mahali popote alipowaasa waandishi wake hao kutekeleza wajibu wao huo, lakini kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari katika ukosoaji huo kwa Rais Magufuli, wala hakuna popote anapowakumbusha umakini katika ukosoaji huo, pamoja na wajibu wao kwa umma wa nchi hii na pia wajibu wao kwa taifa lao hili!

Jenerali Ulimwengu, katika safu yake ya Rai ya Jenerali, Gazeti la Rai, Toleo Na 580, ameandika: “Hofu yangu ipo kwa vyombo vya habari vipya katika kutumia uhuru mpya, uliopatikana wakati ule wa kufanya kazi ya Kuarifu, Kuelimishana na Kuburudishana kwa njia inayolisaidia Taifa kupiga hatua za maendeleo mbele, bila kutumbukia katika mshawasha wa kutumia uhuru huo (mpya) kwa maslahi ya wamiliki wa vyombo hivyo, wahariri na waandishi, (maslahi) ambayo yanaweza kwenda kinyume kabisa cha maslahi ya Umma na Taifa.

“ Kwangu mimi (Jenerali) utashi ni suala moja, na utashi unaweza kupatikana kwa maana ya watu wenye nia njema na nchi yao, na ambao wanajitahidi kutumia fursa mpya inayoletwa na uhuru mkubwa zaidi (kwa vyombo vya habari), katika kutenda mema kwa manufaa ya nchi yao na jamii wanamoishi.” Mwisho wa kunukuu.

Kwa kukumbusha tu, makala haya ya Jenerali, ambayo sehemu yake nimechota nukuu hii, ilikuwa ni sehemu ya mchango wake wa mawazo katika kuelekea kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayoadhimishwa kila Mei 3, ya kila mwaka.

Dunia hii ya upashanaji wa habari tuliyomo leo, ambayo Mbwambo anahimiza waandishi wake wamkosoe Rais, si kuikosoa Serikali yake, hapana. Kumkosoa moja kwa moja Rais wa nchi aliyechaguliwa na watu kwa njia ya kidemokrasia ili tu asiwe dikteta kamili (hisia tu), Jenerali aliiona na kuitilia shaka miaka 10 hivi iliyopita!

Uhuru wa habari kutoka zama za kuarifu, kuelimisha na kuburudisha hadi zama za kuchimbua na kukosoa, kuanika uozo na ufisadi bila hofu wala woga kwa chombo cha habari, lazima, lazima uzingatie miiko, maadili na misingi inayosaidia kupiga hatua za maendeleo mbele. Hilo ndilo lilikuwa angalizo la Jenerali miaka hiyo kwa miaka hii ya sasa ya kusaka fursa ya uhuru na demokrasia zaidi.

Jenerali alihofu juu ya uhuru huo mpya wa vyombo vya habari na vyombo vipya kuitumbukiza tasnia hii katika mshawasha wa kutumia uhuru mpya kwa maslahi ya wamiliki wa vyombo hivyo, wahariri na waandishi, maslahi ambayo hatimaye yanaweza kwenda kinyume kabisa na maslahi ya umma na Taifa hili.

Hakufikiria kabisa vyombo hivyo vya habari kuweza kutumika kulinda na kutetea maslahi ya wanasiasa mafisadi na au wafanyabiashara mafisadi, ambao kwa nguvu zao za fedha na vyombo hivyo wanaweza kuiyumbisha serikali iliyoko madarakani na ikibidi kuiondoa madarakani kwa kisingizio cha kuidhibiti na kujenga ukuta isivuke msitari wa udikteta poa kwenda udikiteta kamili, wakati kumbe ni ukuta unaolenga kuzuia kuingiliwa na au kuguswa maslahi yao ya kifisadi!

“Utashi ni suala moja, na utashi unaweza kupatikana kwa maana ya watu wenye nia njema na nchi yao, na ambao wanajitahidi kutumia fursa mpya inayoletwa na uhuru mkubwa zaidi (wa vyombo vya habari), katika kutenda mema kwa manufaa ya nchi yao na jamii wanamoishi.”

Je, jamii ya waandishi wa habari anayoitaja Mbwambo anayotaka iwe na utashi wa kumkosoa Rais Magufuli, yote ina nia njema na nchi yao hii? Je, anao uhakika wa asilimia zote kwamba wote hao, katika kutimiza wajibu wao wa kazi hiyo ya uandishi wanaongozwa na dhamira ya kutenda mema kwa manufaa ya nchi yao na jamii hii ya Watanzania? Somo hili la Jenerali tuliachie hapa!

Tuje kwenye hoja ya pili inayofanana na angalizo na au hofu hiyo ya Jenerali kuhusu waandishi na uandishi wa Tanzania. Mbwambo anasema alimpigia debe Magufuli katika kampeni zake za mwaka jana na kwamba hajutii hata kidogo hadi sasa kumpigia debe Magufuli, na hatimaye kumpigia kura!

Hata hivyo, pamoja na Mbwambo kusema alimpigia debe Magufuli, hatua ambayo analazimika pia kuwashuhuru wananchi walio wengi kwa kumpatia kura kiongozi huyo, hivyo kumnyima kura aliyekuwa mshindani wake, Edward Lowassa, lakini katika makala hiyo hiyo ameandika:

“Lakini nataka ieleweke kwamba nilifanya hivyo (kumpigia debe Magufuli) baada tu ya kumlinganisha na mpinzani wake Lowassa. Laiti kambi ya upinzani (Ukawa), ingeibuka na mgombea urais bora zaidi, nisingemuunga mkono Magufuli.”

Kwanini Magufuli hakuwa chaguo la Mbwambo katika uchaguzi huo wa mwaka jana? Kwanini alidhani rais bora angetokea Ukawa? Jibu analo. “Nisingemuunga mkono Magufuli kwa sababu nilimuona kuwa ana ‘viashiria’ vya kuwa full dictator asipodhibitiwa vyema. Yaani badala ya kuishia kwenye ‘udikteta poa’ ambao niliamini, na bado naamini kuwa ndiyo unaoifaa nchi yetu kwa sasa, angalau kwa awamu moja tu ya miaka mitano, bila udhibiti angekwenda mbele zaidi na kuwa dikteta kamili!”

Tafsiri ya nukuu hiyo hapo juu ya Mbwambo ni nini? Kwa maoni yangu, maneno hayo ya Mbwambo, yananipa tafsiri za maana mbili. Mosi, kwamba chaguo la CCM, Magufuli, tangu alipokuwa ameteuliwa na chama chake Julai 12/13, hakuwa amefanikiwa kumshawishi Mbwambo kama mgombea sahihi anayekidhi vigezo vya ubora vya huyo ambaye alitakiwa kuwa rais wetu kwa sasa.

Kwa hiyo, kwa sababu CCM ilishakamilisha uteuzi, na mteule huyo akawa bado si chaguo sahihi la kupigiwa debe na Mbwambo kupitia kalamu yake na safu yake kama anavyokiri mwenyewe, ni wazi mpaka hapo alikuwa akisubiria chaguo kutoka upinzani, ambaye angesimama kwa tiketi ya Ukawa. Nani huyo aliyekuwa akisubiriwa Ukawa ambaye angekuwa bora kwa Mbwambo kuliko Magufuli? Dk Wilbroad Slaa au Profesa Ibrahim Lipumba?

Julai 28, mwaka jana, Lowassa alitangazwa rasmi kujiunga na Chadema kwa sharti kuu la kuwa mgombea urais kwa teketi ya Ukawa. Baada ya hatua hiyo ya Chadema na Ukawa kumpokea Lowassa na kumtangaza kuwa mgombea mteule wa urais, Dk Slaa na Profesa Lipumba waliamua kuvikimbia vyama vyao sambamba na Ukawa kwa ujumla.

Aidha, matumaini yale ya Mbwambo ya pengine wapinzani kusimamisha mgombea bora kuliko Magufuli wa CCM, ambaye alikuwa bado anamtilia shaka kuhusu nani angemfunga gavana akiwa rais, yalitumbukia nyongo kutokana na ujio huo wa Lowassa ndani ya Ukawa, hivyo pia kutumbukiwa nyongo ya mageuzi ya kutaka mabadiliko ya mfumo wa uongozi wa nchi hii nje ya CCM.

Asiyependwa na Mbwambo alikuwa kaja Chadema na Ukawa.

Katika kisa hicho hicho cha Lowassa kuondoka CCM kwa sababu za wazi kabisa na kujiunga Chadema kwa sababu za wazi pia, sasa turejee kwenye msaada wa waandishi wa nchi hii anaoutaka Mbwambo ili kumdhibiti Magufuli.

Nimwalike na kumuomba Mbwambo, arejeshe taswira nyuma na kuvuta picha ya waandishi wa habari wa Tanzania katika kipindi kile cha Mei, mwaka jana, baada ya CCM kufungua milango na madirisha kwa makada wake kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa urais, hadi Julai 28, siku ambayo Lowassa alitangazwa kuhamia Chadema na Ukawa kwa nia ya kugombea urais.

Katika kipindi chote hicho cha kati ya Mei na hadi baada ya Julai 28, mwaka jana, cha Lowassa ndani ya Chadema, Mbwambo anaridhika na aina ile ya waandishi wa kipindi kile,  ambao ndio hao waandishi anaotaka leo wasimame imara kumkosoa, kumdhibiti na kumfunga gavana Rais Magufuli?

Waandishi hao wa kumkosoa, kumdhibiti na kumfunga gavana Rais Magufuli kwa nia njema kabisa ya kulinda na kutetea maslahi ya Umma na Taifa hili, na si wale walioko nyuma ya maslahi ya wenye ndoto zao bado za Ikulu, wakiwa bado ni wale wale ambao Mbwambo anawafahamu kwa tabia na matendo yao ya kifisadi, wapo kweli ili aweze kuwapa kazi hiyo ya kumkosoa na kumdhibiti Magufuli asivuke mstari wa udikteta? Nadhani Watanzania wanahitaji majibu ya maswali haya!

Hoja ya mwisho na hitimisho la makala haya linahusu wito wa Mbwambo katika mambo mawili. Mosi, ni kwa waandishi wa habari wa nchi hii kuungana na Watanzania wote, Bunge, vyama vya siasa, NGOs, vikundi vya kiraia, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu, katika kuhakikisha wanatimiza wajibu wao huo wa kumzuia, kumdhibiti na kumfunga gavana Magufuli asiwe dikteta kamili.

Pili, ni wito wake wa kutaka waandishi na Watanzania kurejea kwenye mkanda maarufu unaosimulia kupanda na kuanguka kwa Adolf Hitler, aliyepata kuwa mtawala na dikteta wa Ujerumani kati ya miaka ya 1930 na 1939/40.

Anaandika Mbwambo: “Kwa walioiangalia ile documentary maarufu ya BBC kuhusu Vita ya Pili ya Dunia, watakumbuka lawama zilizowaangukia waandishi wa habari wa Ujerumani wa zama hizo kwa kutowafumbua macho Wajerumani kuhusu dalili za mwanzo kabisa za udikteta wa Adolf Hitler.

“Hata pale Hitler alipoonyesha dalili za kweli za kuwa full dictator na muuaji, waandishi waliogopa kumkosoa kwa hofu ya kuwaudhi wananchi ambao walikuwa wakimpenda mno. Kwa hiyo, badala ya kumkosoa wakawa wanamsifu hata pale alipouvuka mstari wa u-benevolent dictator kuelekea kwenye udikteta kamili.”

Sina uhakika ni kwanini Mbwambo ametumia fikra mbili hizi za waandishi wetu kuungana na wanasiasa, wanaharakati na NGOs kumpinga rais wa nchi kama itatokea akawa na dalili za udikteta wa aina ya Hitler katika zama hizi za dunia ya sasa, tena katika mazingira ya Tanzania. Nahoji kwanini Mbwambo awe na fikra hizi kwa sababu sioni mfanano wala uwiano wowote wa kimazingira!

Mbwambo ni mwanataaluma ya habari asiyetia shaka yoyote juu ya taaluma yake wala weledi wake. Anajua vyema miiko na maadili ya taaluma yake hiyo kuwa havifungamani kabisa na wanasiasa wala uanaharakati. Hivi mwandishi wa habari akishaungana na wanaharakati na kugeuka kuwa mwanaharakati, huyo bado anabakia bado na sifa ya kuitwa mwandishi wa habari?

Hivi ikitokea, wanahabari wote katika nchi, wakaungana na Bunge, vyama vya siasa vya upinzani, NGO’s na vikundi vingine mbalimbali vya kiraia, wanasheria, wanaharakati wa haki za binadamu na wengine kadhaa anaowataka yeye Mbwambo kwa nia ya moja tu ya kumkosoa, kumdhibiti na kumfunga gavana Rais Magufuli, kweli Tanzania hii itatawalika tena?

Je, nikisema hapa kwamba wosia huu wa Mbwambo kwa waandishi wetu, ni sumu kali kwa ustawi wa Taifa hili, nitakuwa nimekosea? Anawahimiza waandishi wetu kufanya kama waandishi wenzao wa Misri, Libya na Tunisia, walioungana na wanasiasa na wabunge waasi, NGO’s na wanaharakati, hadi wakazifikisha nchi zao hapo zilipo leo!

Udikteta wa Hitler. Ndugu zangu, documentary za Hitler na Vita Kuu ya Dunia, wakati mwingine hazifai kurejewa kabisa katika kuzungumzia siasa za nchi hii kwa nia njema ya kujenga nchi yetu na ustawi wa demokrasia. Haileti afya katika ustawi wa siasa zetu!

Mbwambo anafahamu kwamba Hitler wa Ujerumani huyu alikuwa mwanasiasa na mwanaharakati pia aliyekuwa na chama chake alichokiasisi, akakiongoza mwenyewe hadi akafanikiwa kukiingiza Ikulu. Chama cha NAZI!

Chama hiki cha NAZI, kwa kukilinganisha na vyama vyetu vya upinzani nchini hapa na aina yao ya uongozi, Mbwambo atabaini kuwa kilikuwa ni chama cha jeshi la mtu mmoja kama vilivyo baadhi ya vyama vyetu vya upinzani nchini.

Magufuli ni Rais wa Tanzania anayetokana na uteuzi wa CCM. Tanuri alilopitia Magufuli hadi hapo alipo, linajulikana. Hivi kweli, Mbwambo anaweza akawaeleza Watanzania ufanano wowote wa kimuundo wa uongozi kati ya chama cha NAZI na CCM? Akaeleza ufanano wa uteuzi wa Magufuli na uteuzi wa Hitler, kama kweli uteuzi huo ulifanyika ndani ya chama cha NAZI?

Mbwambo anaweza akawaeleza Watanzania ni wenyeviti wangapi wa chama cha NAZI waliowahi kung’atuka wenyewe kwa hiyari yao na kuachia madaraka yao ili kupisha uongozi mwingine wa chama katika utaratibu wa kuachiana kijiti kama ilivyo kwa CCM ya tangu enzi za Mwalimu, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa Mzee Kikwete? Vipo vyama hapa nchini vinavyoweza kutuletea siku moja rais dikteta katika nchi hii, lakini si CCM kamwe! Mazingira hayo hayapo.

N nichukue fursa hii kumtoa hofu kwamba kama ambavyo wenye CCM yao waliweza kuwadhibiti mafisadi wenye fedha wasipore chama chao pamoja na Ikulu ya nchi hii mwaka jana, ndivyo pia wenye CCM hiyo watakavyomdhibiti Magufuli asivuke mstari wa kuingia kwenye udikteta kamili.

Nimtoe pia hofu kwamba kama ambavyo waandishi makini si haba wa nchi hii walivyoweza kulinda Taifa lao hili mwaka jana katika kipindi kile cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, kiasi cha kuushinda uandishi ule wa bendera fuata upepo, ndivyo pia waandishi makini hao watakavyomwezesha Magufuli kutekeleza majukumu yake kwa kasi ya udikteta poa, bila hata kuukaribia mstari wa udikteta kamili!

One thought on “Waandishi na Magufuli: Mbwambo amemwaga sumu”

  1. Simba says:

    Binafsi (inawezekana mimi mbumbu)sijaelewa kabisa ulichoandika hapo nimeisoma makala yako mara tatu ,lakini sijaambulia kitu maana  yangu sijaelewa ulikuwa unamjibu Mbwambo au ulikuwa unatoa usia kwa waandishi wasifuate usia wa Mbwambo au ulikususudia nini hasa,au ndiyo blabla zetu Za kisiasa ??

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *