Waarabu wapo, hawapo. Wahindi wapo, hawapo

KWA taarifa rasmi zilizokuwepo wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu walikuwa yapata asilimia 20 ya watu wote visiwani humo.

Neno Zanzibar lenyewe lina asili ya Kiajemi na kutokana na sababu za kihistoria, Zanzibar ina maelfu ya watu wenye asili ya Kiajemi. Zanzibar pia ina maelfu ya watu wenye asili ya Kihindi.

Cha ajabu ni kwamba, leo hii, ukitazama askari wa kawaida na wanajeshi walioko Zanzibar, hakuna hata mmoja ambaye ana asili ya Kiarabu, Kiajemi au Kihindi.

Karibu askari wote wanaovaa sare na unaopishana nao njiani na kuwaona, wote ni wana asili ya Kiafrika. Na Uafrika ninaozungumzia ni ule finyu wa kutazama rangi ya ngozi kuwa ni nyeusi.

Tanzania Bara, kwa maana ya uwiano, haina watu wengi wenye nasaba tofauti na za weusi. Lakini tuna watu wengi machotara, waarabu na wahindi.

Ndiyo sababu, huko nyuma, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), liliwahi kuwa na watu kama John Walden, Ameen Kashmiri na Zakaria Hans Poppe.

Nimeangalia JWTZ hivi sasa, na ni nina miaka mingi sijakutana na mwanajeshi Mhindi, Mwarabu, Mzungu au chotara. Wote ninaokutana nao ni wenye rangi nyeusi. Na hili liko Polisi, Magereza na kwingineko.

Wiki mbili zilizopita, nilikuwa na mjadala mrefu na mmoja wa wanajeshi wastaafu wa JWTZ. Ilikuwa inajulikana kuwa Jenerali Davis Mwamunyange alikuwa anastaafu na nafasi yake ilihitaji kuzibwa.

Tulikuwa tunajadiliana kuhusu nani na nani wanafaa kumrithi. Nilikuwa na jina moja la Mzanzibari. Yule askari akanipinga kwa kigezo kuwa “ Zanzibar haina askari wa kuweza kuongoza JWTZ”. Nikamwambia hayo ni matusi kwa Wazanzibari.

Nikamuuliza kama anamkumbuka Kanali Ali Mahfoudh ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mafunzo ya Kivita wa JWTZ. Alikuwa ni Mzanzibari na mmoja wa askari shupavu waliowahi kutokea Tanzania.

Kama Zanzibar imewahi kumtoa Ali Mahfoudh, ni matusi kusema hakuna mwanajeshi wa maana kutoka kule. Kwa bahati nzuri, kwa muktadha wa mada yangu ya leo, Mahfoudh, Mungu amrehemu huko aliko, naye alikuwa na asili ya kiarabu.

Kama tuna nia ya dhati ya kuwa taifa imara na linalosonga mbele kila kukicha, ni muhimu sana kuwa na mtazamo chanya na wazi kuhusu namna ya kuwahuisha watu kutoka kwa makundi ya walio wachache.

Ni kweli kwamba watu wasio weusi hapa Tanzania si wengi. Lakini, katika uchache wao, kama taifa, tunatakiwa kuhakikisha wanapata fursa zote za muhimu.

JWTZ na majeshi yetu yote mengine, yataendelea kuwa ya mfano endapo watakubali kubeba watu wa aina zote. Wachaga na Wamasai, Wamakonde na Wahadzabe, Wajaluo na Wanyakyusa, Wahindi na Waarabu na Wanawake na Wanaume.

Tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika duniani zimeonyesha kuwa jambo la taasisi moja kuwa na watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii inasaidia sana.

Kwa majeshi, mchanganyiko huu ni muhimu zaidi. Hii ni kwa sababu, kwa jeshi kuwa imara na nyumbulifu, ni muhimu kuwa na akili tofauti, malezi tofauti na utofauti wa mtazamo.

Kunapotokea tatizo lolote, kila mtu atakuwa na ufumbuzi tofauti kutokana na asili yake na makuzi yake. Jumla ya mawazo hayo ndiyo huifanya taasisi kuwa imara.

Wote mkiwa mnafikiri kwa namna moja, chombo mnachokiongoza kitawashinda tu. Fikiria hali moja, kama kikosi kimepotelea porini na kinaundwa na Wamasai watupu, wote watahangaika kutafuta nyama maana ndiyo chakula wanachokijua.

Lakini, kama kutakuwa na Wazaramo au makabila mengine yanayozijua vema mboga za majani, Wamasai wale wataelezwa kuwa mchicha nacho ni chakula. Na kwa namna hiyo, maisha yao yataokolewa.

Tufikiri tena tofauti. Kama tungekuwa na tabia hii ya majeshi kutojali kuhusu mjumuisho wa watu wa rangi nyingine, kwenye vyuo vikuu vyetu tungepungukiwa.

Tungemkosa Profesa Issa Shivji na Profesa Karim F. Hirji. Tungekosa kupata utaalamu wa historia wa Profesa Abdul Shareef. Lakini vyuo vikuu vina mjumuisho huu na ndiyo siri ya heshima iliyokuwa nacho Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye miaka ya 1970. Kilikuwa ni chemchem ya maarifa kutoka kote duniani.

JWTZ, Polisi na Magereza nao watanufaika zaidi kwa kufungua milango na kukaribisha wenzetu ambao ingawa hatufanani nao rangi za ngozi zetu; tunafanana kwa sababu lengo letu sote ni moja.

Wiki ijayo nitafafanua zaidi kuhusu mada hii kwa kutoa mifano ya nini kinaweza kufanyika na makosa ambayo yamefanyika hadi sasa.

One thought on “Waarabu wapo, hawapo. Wahindi wapo, hawapo”

  1. FILAN S.MGALLA says:

    JE KUNA MHINDI AU MWARABU ALIEKATALIWA KUJIUNGA NA MAJESHI YETU AU NIWAO HAWATAKI ,?? MIAKA YA NYUMA KWA WALE WALIOENDA JKT WAULIZE WALIWAHI KUKUTANA NA MWASIA ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *