Habari
Mchakato wa Katiba mpya
Wabaya waanza hujuma
Waandishi Wetu
Toleo la 234
11 Apr 2012
  • Mtandao waeneza ajenda ya udini
  • Wanasiasa wajipanga kumiliki maoni

WAKATI Mwenyekiti mteule wa Tume ya Katiba yenye jukumu la kukusanya maoni kwa ajili ya kuandika Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba, akisubiri kuapishwa sambamba na Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu (mstaafu) Augustino Ramadhani na wajumbe wengine wa tume hiyo, baadhi ya viongozi wa kisiasa wameanza ‘kuchafua hali ya hewa’, Raia Mwema limebaini.

Wanasiasa hao wameanza harakati za kutaka kuvuruga mchakato wa Katiba mpya ambao umekuwa ukisubiriwa na wananchi, wakidaiwa kujipanga kutumia mbinu mbalimbali. Mbinu hizo ni pamoja na kutaka kupandikiza hisia za udini mapema kabla hata ya mjadala husika wa Katiba mpya kuanza.

Mbali na ajenda ya udini ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonya kwamba siasa za namna hiyo zinaweza kufanywa na wanasiasa waliofilisika tu, ambao hutafuta namna ya kujihalalisha, ajenda nyingine inatajwa kuwa ni kuhakikisha maoni ya wanasiasa na vyama vyao ndiyo yanayotawala mjadala huo na hata kuingizwa kwenye Katiba mpya.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinabainisha kuwa, mitandao maalumu imekwishaanza kusukwa ambayo itakuwa ikiendeleza usimamizi wa ajenda za kuteka mjadala huru wa Katiba, hali inayoashiria kuhitajika kwa umakini wa Tume ya Katiba.

Kwa upande wa Zanzibar, juhudi zinafanyika miongoni mwa wanasiasa kupandikiza chuki dhidi ya Watanzania Bara wanaoishi huko, kinyume cha hali halisi ya muingiliano wa kimaisha wa muda mrefu kati ya Wanzanzibari na Watanzania Bara.

Inaelezwa kuwa, kwa kadiri ya kiwango cha chuki kitakavyofanikiwa kupikwa, ndivyo Wazanzibari watakavyokuwa na kasi kubwa ya kutaka kujitenga na Muungano.

Hata hivyo, bado juhudi hizo zinatajwa kukabiliana na upinzani ambao msingi wake ni namna ambavyo Wazanzibari wengi zaidi wanavyoendesha maisha yao, na hasa wale wanaoishi Tanzania Bara, hali ambayo ni tofauti na ilivyo kwa upande wa Watanzania Bara walioko Zanzibar.

Katika kile kinachoweza kutajwa kuwa ni kushindwa kuficha hisia za kutenganisha wananchi wa nchi mbili zilizoungana na kutengeneza Jamhuri ya Muungano, hivi karibuni, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Jussa Ladhu, alipendekeza katika baraza hilo kuwaondoa ‘kisheria’ watu wanaotoka Tanzania Bara kufanya kazi za kitalii na kutaka kazi hizo zifanywe na Wazanzibari wenyewe, akijaribu kujenga maudhui kuwa Watanzania Bara ni wageni kama ilivyo raia wa nchi nyingine.

Ingawa mapendekezo hayo ya Jussa yaligonga mwamba katika Baraza la Wawakilishi, lakini lawama zimeanza kujitokeza miongoni mwa Wazanzibari wanaoendesha shughuli zao za kila siku katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Wazanzibari hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini baadhi ni wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam na wengine ni  wanaomiliki maduka ya bidhaa za kawaida, ambazo kama mawazo ya Jussa yanazingatiwa, biashara ya maduka pia inaweza kufanywa na Watanzania Bara pekee.

“Viongozi na hasa hawa wanasiasa wanazungumza yale wanayotaka, wengine hata hawataki kufanya utafiti ili kujua sisi Wazanzibari tunaishi vipi huku Tanzania Bara. Kwa kweli tunaishi vizuri bila kunyoosheana vidole. Mimi ni Mzanzibari lakini naishi hapa Dar es Salaam, nimekuwa nikiishi kama raia wa Tanzania na si raia wa Zanzibar ndani ya Tanzania Bara.

“Watuache tuishi kama mwanzo bila kuanza kubaguliwa, leo hii ukianza kuwaandama Watanzania Bara waliopo Zanzibar, basi na sisi Wazanzibari tuliopo huku tutaanza kuchukiwa sasa hapo tujiulize, nani atakayekuwa ananufaika na hali hiyo?” anasema Mzanzibari mmoja ambaye ni mfanyabiashara wa vitunguu kutoka baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara na kuuza vitunguu hivyo kwa bei ya jumla sokoni Kariakoo.

Lakini wakati hayo yakitokea, muasisi wa CHADEMA, Mzee Edwin Mtei ambaye aliwahi kufanya kazi katika Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere iliyojenga umoja wa Watanzania kwa kupinga hisia za udini na ukabila, naye ameonyesha hisia zake za udini.

Mtei ambaye ingetarajiwa awe mstari wa mbele kutoongozwa kwa hisia za udini kwa angalau kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ameibuka na kukosoa Tume ya Katiba iliyoundwa na Rais Kikwete akitumia kigezo cha udini na kusisitiza kuwa, tume hiyo imekuwa na idadi kubwa ya Waislamu.

Maoni hayo ya Mtei yamekosolewa na Watanzania wengi ambao wameweka bayana kuwa jambo la kuzingatia ni uwezo wa wajumbe na si dini zao, lakini kubwa zaidi, Tume hiyo haipeleki maoni ya wajumbe wake bali inakusanya maoni ya Watanzania ambayo baadaye ni Watanzania hao hao ndio wataoyaidhinisha kwa njia ya kupiga kura.

Mtei ambaye bado ana ushawishi katika CHADEMA, akiwa ni mjumbe wa Baraza la Wazee la chama hicho, amenukuliwa akisema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, baada ya Ikulu kutoa taarifa ya majina ya wajumbe wa tume hiyo.

Hata hivyo, kutokana na kile kinachoweza kutajwa kuwa ni kuhatarisha taswira ya CHADEMA kisiasa nchini, chama hicho tayari kimetoa taarifa ya kujitenga na maoni hayo ya Mtei na kusisitiza kuwa ni “maoni yake binafsi.”

“Wakati mwingine inashangaza kuona kiongozi anapigania siasa kwa kuegemea hisia za kidini lakini ndani ya familia yake wapo watu wa dini tofauti. Mimi nilidhani kwa sababu CHADEMA walikuwa wakitaka kuandika Katiba mpya kama wangepata kura za kutosha kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010, wangefanya kazi hiyo vizuri zaidi lakini kumbe humo humo kuna hisia za udini kama hivi.

“Huu ni undumilakuwili, bahati nzuri viongozi wa aina hii hawako katika mfumo wa utawala, hawaongozi dola na kwa hiyo mawazo yao tutaendelea kuyapuuza hadi watakapotuomba radhi au wajirekebishe kabisa,” alisema mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Frank Mwenda.

Mbali na kasoro hizo zenye hisia za kibaguzi zisizowiana moja kwa moja na namna ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia mchakato wa Katiba mpya, taarifa zaidi zinaeleza kuwa, ajenda ya Zanzibar kuwa na jeshi lake la Wananchi imeanza kusukwa.

Taarifa hizo zinadaiwa kuanza kusukwa na baadhi ya wanasiasa huku ikibainika kuwa, Zanzibar kuwa na jeshi au kutokuwa na jeshi hilo kama ulivyo mfumo wa sasa ni suala lisilogusa moja kwa moja mfumo wa maisha wa sasa kati ya Wazanzibari na Watanganyika.

Kwa upande mwingine, mengi yatarajiwa kujitokeza wakati wa utoaji wa maoni kuhusu kuandika Katiba mpya, zikiwamo hisia hizo za udini, ukabila na hata maslahi binafsi ya kisiasa kwa upande wa vyama na au mwanasiasa mmoja mmoja.

Miongoni mwa yanayotarajiwa kujitokeza ni pamoja na mapendekezo ya wabunge kutoteuliwa kuwa mawaziri, na hata kuangaliwa upya kwa mfumo wa uchaguzi nchini, ili hatimaye kupatikana kwa mfumo wa uchaguzi wenye ufanisi zaidi na ambao unapunguza gharama za uendeshaji wake.

Tume iliyotangazwa na Rais inaundwa na baadhi ya watu wengine mashuhuri ambao mbali na Jaji Warioba pamoja na Jaji Mkuu mstaafu, Ramadhani, watu hao ni pamoja na aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Wengine katika orodha hiyo ya wajumbe ni Mwandishi mashuhuri wa habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Ally Salehe, pamoja na Mzee Joseph Butiku. Tume hiyo imepangiwa kukamilisha kazi ya kukusanya maoni ya Watanzania ndani ya miezi 18.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Maoni ya Wasomaji

Kwenye suala la udini Mtei amenisikitisha sana. Anataka kutufanya sisi tuliowaislam ambao ni waumini wa siasa za CDM tuanze kuamini zile propaganda zinazoenezwa na CCM kuwa ni chama cha dini fulani. Ningeomba Mtei ajiuzulu katika nafasi yake ya uzee wa chama ili kuondoa utata huu. Sisi tunajenga yeye anatoboa. Nafikiri hivi sasa CDM wampige marufuku kutoa maoni yake Publicly, yaani wamtoeshe kwenye Public forum za CDM.

Tatizo kubwa la wazanzibari ni kuwa na jazba na kuongozwa na watu kama jussa ambao wao wamekalia chuki. Kama wazanzibari wanataka kuwafukuza watu wenye asili ya bara, basi wazanzibari walioko bara nao warudi kwao, maana ni tit for tat. Kama kuna wabara wana shida sana ya kukaa visiwani kuna kisiwa cha mafia na visiwa vingi kwenye maziwa ya victoria na Tanganyika wanaweza kuishi humo kwa amani. Kila siku ni issue tu ya chuki dhidi ya watanganyika.......tumechoka!  Serikali ya Muungano imekaa kimya watu wanauawa, makanisa yanachomwa moto, Kikwete na serikali yake wamekaa kimya sijui wanafikiri nini? Wabara hatutaki MUUNGANO, wazanzibari mrudi kwenu!!

Ama wewe Hilal unataka kutambaza chuki yako kwa kujibanza kwa makala haya yaliyoandikwa na ”Waandishi Wetu” yenye kujaribu kuonyesha ishara ya udini na ukabila iliyoanza kujitokeza. Kutokana na maelezo yako haya mafupi na shaka kuwa wewe mwenyewe ni mbaguzi. Tena wa aina ya kibeberu. Nasema hivyo kwa sababu hiyo lugha uliyoitumia ”tit for tat”. Kwani Umoja wa Afrika Mashariki si ulibomoka pale Tanzania walipoona ianapunjwa au vile Mwalimu Nyerere alikataa kukaa pamoja na Amin. Baada ya miaka umeundwa Umoja mpya uliongezeka. Baina ya wakati wa mpito hawajafukuzana raia wa nchi yeyote.
Unajua vizuri kabla hata huo Muungano kuja maingiliano kati ya Wazanzibari na Watanganyika yalikuweko. Mara nyengine udugu wa ujirani unazidi hata ule wa damu. Eti kama kuna wabara wenye shida sana ya kukaa visiwani basi wapelekwe … kisiwa cha Mafia na maziwa ya Viktoria. Kama kuhamisha watu kutoka sehemu moja kuwapeleka sehemu nyengine ni rahisi. Basi kwa nini Watanzania wanataka suala la ardhi liwekwe upande kwanza katika Umoja wa sasa? Karibuni nimesoma mtaalamu mmoja akitoa ushauri ambao unatuhusu sisi Afrika. Anasema ni jambo la wazi kuwa baadhi ya nchi katika Afrika zimo katika ukami wa kudumu , kwa hivyo, litakuwa jambo la maana kuwapa watu hao ardhi nyengine ili waweze kuendesha maisha yao. Jee upo tayari kuwatunukia Mafia au utasema dhamana hiyo si yetu. 

eti jamani kwa ulimwengu wa teknolojia,hamna web yakuisoma katiba.kwa anaejua anuani nijulishe kwenye//www.my.opera.com ama jleonny@opera.com

Mawazo ya Mtei ni ya kweli.

 

nadhani watu wanajenga hoja ambazo hazina maslai kwa taifa letu.Mtei pumzika na wewe Jussa umefilisika kisiasa.Mnatakiwa kusaidia taifa ili liende katika mchakato wa katiba kwa amani bila chuki mbona mnaleta za kuleta??????????

Kwa wale wanaofikiri wazanzibari 10% wanaoishi Tanganyika  ndio ngao ya kuingamiza Zanzibar mumeliwa hili limefika kikomo chake kwani kura ya maoni ijayo Wazanzibari ukoloni Tanganyika basi na waTanganyika wanaotaka kukaa Zanzibar wakae hawatofukuzwa ila Watanganyika mutakaowafukuza Wazanzibari tuambieni mutatumia sheria gani ya kuwafukuza kwani watoto wao n ni Wazaliwa wa hapo na mali zai zitaandikwa mjian ya watoto wao in reality jifunzeni Egypt na Syria walipovunja Muungano  hawakufukuza rais zao same as Check and Slovak zilipokua mataifa  mawili pia waliotaka kubaki Pande wanzoishi hakuna aliewafukuza. Hii Jeuri ya kutishiana kufukuzana ni danganya toto.
Jussa ni Muwakilishi wa Wakuchaguliwa na Wananchi na Kauli zake ni za wapiga kura wake.

Wingi wa Waislam katika Tume ni kutokana na nusu ya Wanakamati kutokea Zanzibar na si vinginevyo, na hii haimaniishi chochote kwamba itaathiri mchakato wa uundwaji wa katiba. Kwanza lazima ikumbukwe kuwa hawa wanakuja kuchukua mawazo ya wananchi, hawatungi wao. Hebu tuache Kamati ifanye kazi yake. Nashukuru pia kwa kauli ya Mbowe, na nadhani Chadema wanatakiwa kukazia uzi tamko hilo la Mwenyekiti wao, watu wasije wakachukulia maneno ya Mzee Mtei kuwa ni ya chama hiki makini.

KABLA HUJATOA MAONI WASHIRIKISHE WENZAKO UJUE KAMA NI PUMBA AU MAONI YAKO YANAFAA;NAFIKISHA UJUMBE KWA MTEI.NILIKUWA NAKUKUBALI SANA LAKIN KWA HILO UMEKOSEA NA UMETUCHAFUA WANACHAMA NA WASHABIKI WA CHADEMA.

Toa maoni yako