Habari
Mwangwi wa uvuaji gamba
Wabunge 20 CCM wamtega Kikwete
Mwandishi Wetu
Toleo la 209
26 Oct 2011
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
  • Wajiandaa kujiuzulu, kutimkia upinzani

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) sasa kipo hatarini kukimbiwa na kundi la wabunge zaidi ya 20, wanaoweza kujiunga na chama kimojawapo cha upinzani na kisha kushiriki tena katika uchaguzi mdogo utakaoitishwa baada ya tukio hilo, uchunguzi wa Raia Mwema umebaini.

Hata hivyo, imebainika kuwa njia pekee ya kunusuru CCM dhidi ya hatari hiyo ni utekelezaji wa dhati wa mpango mpya wa chama hicho kujivua gamba, unaohusisha kuwaengua katika nyadhifa za uongozi ndani ya chama, vigogo wenye kasoro za kimaadili, ikiwa ni pamoja na waliopata kujiuzulu serikalini.

Katika orodha hiyo mbali na Rostam Aziz aliyekwishakujiuzulu na hivyo kujiepusha na shinikizo la kumtaka afanye hivyo, wengine ambao mara kadhaa wamewahi kutajwa katika orodha hiyo ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Kwa upande mwingine, kundi la watuhumiwa wa ufisadi limeelezwa kuendelea na mikakati ya kujisafisha huku nao wakijiandaa kujitoa CCM kumuunga mkono mmoja wao kuwania nafasi ya urais 2015 kupitia upinzani ikiwa watazuiwa kuwania ndani ya CCM.

Tayari Lowassa amejitokeza hivi karibuni kukataa kuzungumzia kuhusu kuwania urais huku akitishia waandishi wa habari watakaoendelea kumhusisha na kashfa mbalimbali ambazo hata hivyo alikataa kuzitolea majibu alipoulizwa na baadhi ya waandishi wa habari aliokutana nao Monduli, hivi karibuni.

Lowassa anatoa vitisho hivyo dhidi ya waandishi wa habari ikiwa ni takriban miaka mitatu sasa tangu alipoelezwa na iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge, apime uzito wa kashfa iliyokuwa ikimuelemea kuhusu Kampuni ya kufua umeme ya Richmond na achukue uamuzi wa kujiuzulu.

Kwa utashi wake alijiuzulu huku kukijitokeza mazingira yanayotafsirika kuwa yeye ni kati ya viongozi waliokuwa katika safu ya kushinikiza Richmond ipewe zabuni ya kufua umeme, bila kuhakiki uwezo wa kampuni hiyo.

Kujipanga kwa wabunge hao kunazidi kukiweka katika wakati mgumu chama hicho na hasa vikao vyake, kikiwamo cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambacho ndicho kilichoridhia mpango wa kujivua gamba ambao kimsingi unatafsirika kama ni mageuzi ndani ya chama hicho.

Mpango wa kujivua gamba kwa mara ya kwanza ulitambulishwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Februari mwaka huu, mjini Dodoma na kuridhiwa rasmi kwenye NEC-CCM, ambamo utekelezaji wake ulianza kwa kuvunjwa kwa iliyokuwa Kamati Kuu ya chama hicho, pamoja na iliyokuwa sekretariati, ikiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba.

Hata hivyo, uamuzi wa kuwaondoa viongozi wenye maadili yanayotiliwa shaka utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua huku kila mara ikielezwa kuwa kama wahusika watashindwa kujiuzulu wenyewe, basi watashinikizwa na chama hicho kupitia vikao vyake rasmi na wenyewe wakipambana kujiokoa.

Kutokana na chelewa chelewa hiyo na kuahirishwa mara kwa mara kwa uamuzi huo, mambo kadhaa yamekuwa yakijitokeza ambayo moja kwa moja yanahusishwa na kundi la viongozi wanaopaswa kuvuliwa nafasi zao za uongozi.

Mambo hayo ni pamoja na migogoro ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), mgogoro ambao unafukuta zaidi mkoani Arusha, kwa kumhusisha Makamu Mwenyekiti wa umoja huo ngazi ya taifa, Benno Malisa.

Vijana wanaotajwa kuhusika kwenye mgogoro huo ambao ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM, Arusha, James ole Millya na wenzake wamekuwa wakitajwa kuwa ‘vijana’ watiifu kwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye ni kati ya viongozi wanaotajwa kutakiwa kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya chama hicho, na hasa nafasi zinazowashirikisha kwenye vikao vya uamuzi kuhusu mustakabali wa chama hicho.

Haiba ya Lowassa mbele ya jamii ilizidi kuchafuka kwa kasi baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia barua yake ya kutaka kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu, kutokana na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

“Kama mkakati huu wa kufanya mageuzi ndani ya chama ikiwa ni pamoja na kuwaondoa ambao uadilifu wao ni wa kutiliwa shaka mbele ya jamii, hautafanyika, basi gharama itakayolipwa na CCM ni kubwa kiasi cha kuhatarisha zaidi uhai wake,”

“Wengine tupo tayari kujivua uanachama kuliko kuendelea kubaki humu ambamo jamii haiwezi kutuelewa kuwa tunasimamia misingi ya uadilifu au maslahi yetu binafsi. Tutaachia madaraka yote na uamuzi huo usichukuliwe kuwa ndiyo mwisho wetu wa kushiriki siasa, tutaondoka na kujiunga upande mwingine wowote na hata kugombea tena ubunge.

“Lengo ni kuhakikisha tunaitumikia jamii na kutokukubaliana kwetu na mfumo wowote unaokusudia kulinda mafisadi na ufisadi. Hadi sasa, hali halisi inathibitisha kuwa jamii inazidi kupoteza imani kwa CCM njia pekee ya kurejesha imani hii ni kufanya mageuzi ya ndani kwa kujitenga na wasio waadilifu,” alieleza mmoja wa wabunge aliyezungumzia mpango huo.

Hata hivyo, mbunge huyo kama ilivyo kwa wenzake sita ambao wamezungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kuthibitisha suala hili na kueleza kuwa wao wako zaidi ya 20 na wote kwa pamoja hawakuwa tayari majina yao kuandikwa gazeti kwa sasa.

Lakini mbali na wabunge hao, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mtandao utakaoridhia uamuzi huo ni mkubwa ndani ya CCM, ukihusisha safu ya viongozi ambao hawajapoteza imani yao ya uadilifu mbele ya umma.

Endapo wabunge hao wataondoka, CCM itaweza kuathirika zaidi katika baadhi ya mikoa ya kanda ya ziwa, kanda ya kaskazini na nyanda za juu kusini.

Hali hiyo inajitokeza wakati kikao kijacho cha NEC-CCM kikitarajiwa kufanyika mjini Dodoma mwanzoni mwa mwezi ujao, ambapo hatima ya kuwang’oa au kuwakumbatia wasio na maadili itajulikana humo, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa wale wanaotarajiwa kung’olewa kwa kukosa maadili wamekuwa wakishawishi wajumbe wa kikao hicho ili kuwatetea wasing’oke, ushawishi ambao umekuwa ukifanywa kwa kutumia nguvu ya fedha.

Kikao hicho kijacho hata hivyo kinatanguliwa na kauli mbalimbali za wana-CCM waliodhamiria chama chao kinatimiza mkakati wake wa mageuzi ya ndani. Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere.

Makongoro amenukuliwa na gazeti moja la kila wiki akisema kwamba ni lazima uamuzi wa kuwang’oa akina Lowassa na wenzake ufanyike kwa sababu kufanya hivyo ni kutekeleza uamuzi wa vikao halali vya chama na si utashi wa mtu yeyote binafsi.

Makongoro aliweka bayana kwamba hata kama Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wanafungamana na Lowassa kwa namna yoyote ile, iwe kwa urafiki au makubaliano fulani, maelewano yao hayo hayawezi kuachwa kuharibu chama hicho, kinapaswa kuendelea kuishi kwa mujibu wa misingi yake na si urafiki wa viongozi fulani.

Makongoro alifikia hatua ya kutoa kauli kali dhidi ya Kikwete akirejea kauli zinazomuweka karibu na Lowassa akisema makubaliano baina ya wanasiasa hao wanaoelezwa kuwa marafiki hayakihusu chama.

Akinukuliwa na gazeti hilo, Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, alisema jambo la msingi kwa CCM ni kutekeleza jambo la msingi na kwamba hakuna sababu ya kusikia habari za kuteteana.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Maoni ya Wasomaji

Kati ya watu hatari kwa maendeleo ya nchi hii Lowassa ni namba moja, hii inatokana na tamaa yake ya kutaka kubaki madarakani, wenzake waliojiuzuru naye akina Msabaha na karamagi hawasemi lakin yeye bado ana kinyongo akipata madaraka nadhani atafungia vyombo vyote vya habari. hafai kwa mazingira ya sasa ya nchi huru kama Tz

Mimi sifurahii gazeti lenu katu kwani mko upande wa upinzani tu You have never talked any good about your government.If I were a leader,I would have banned it.Think Safety  Guys and don't always be "ANTI" 

Ni vizuri kama kukiwa na gazeti linaloeleza ukweli wa mambo. Si kwamba raiamwema hawajui "mema" yanayofanywa. Bali wanajitahidi kuifanya government to be responsible. Nowdays the sense of responsibility is zero. So let these guys continue their good work. If you don't like it then that is too bad.

Kwa hulka ya wana Mara sio ajabu Makongoro akatekeleza hayo aliyoyasema lakini ataweza? Chama chetu hakiwezi kuwa safi kama Kikwete, Azzi na Lowassa wataendelea kuwa miongoni mwetu. Wamechangia sana hali mbaya tunayoiona CCM. Makongoro ndiye kiongozi pekee ambaye maamuzi na fikra haviongozwi na tumbo. Angalia Sitta kuonyesha kumpinga tu Kikwete mafisadi are working to expel him from the party. CCM imefikia pabaya kubadirika ni vigumu.

    Watuhumiwa wote wa ufisadi wafukuzwe ndani ya chama na serikali na hatua aliyosema Baba wa Taifa Mwal Nyerere ifuate. Wafungwe Jela, Wanapoingia wapigwe bakora 25 na wanapotoka wapate tena 25 ili wakaonyeshe wake zao, bila kuangalia cheo cha mtu au nafasi yake katika serikali inayotawala kwani hawa mafisadi wameinajisi Nchi hii

Toa maoni yako