Wabunge: Tanzania ya viwanda inawezekana kweli?

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameonyesha wasiwasi wao wa kufikiwa kwa ndoto ya Rais, Dk. John Magufuli ya kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Hiyo ni baada ya Serikali kushindwa kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambayo ndio  muhimili wa uwekezaji nchini.

Wasiwasi huo unaelekezwa zaidi kwenye Wizara ya Nishati na Madini ambako upatikanaji wa gesi na umeme kwenye maeneo ya uwekezaji umekuwa ni kikwazo.

Wabunge hao walionyesha wasiwasi huo baada ya Mwenyekiti wa kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalaly Kafumu kuwasilisha taarifa ya mwaka mmoja wa utendaji wa kamati kwenye Mkutano wa sita wa Bunge la 11 ambako hofu ya kutofikiwa kwa ndoto hiyo ilitawala miongoni mwa wabunge iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa na Serikali.

Ikumbukwe kuwa Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama mwaka jana aliitaka Mifuko ya Hifadhi za Jamii kuwekeza kwenye viwanda ili kuchochea uchumi wa viwanda utakaolisaidia Taifa kukua kiuchumi na pia kuwanufaisha wanachama wa mfuko husika.

Tayari baadhi ya Mifuko hiyo imeanza kuitikia wito wa Rais Magufuli wa kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati kwa kujitokeza kufanya uwekezaji kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya sukari, chai na pamba.

Akichangia taarifa ya Kamati hiyo, Mbunge wa Mtwara vijijini  (CCM), Hawa Ghasia anasema Mpango wa kwanza wa miaka mitano wa Maendeleo ulikuwa na lengo la kuondoa vikwazo vya kimaendeleo vilivyokuwepo kipindi cha nyuma ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa umeme, kuboresha miundombinu ya reli, barabara pamoja na bandari

Mpango wa pili, ilikuwa ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na uchumi wa viwanda lakini ipo hofu ya kushindwa kufika mbali kwa sababu bado vile vikwazo vilivyokuwepo katika mpango wa kwanza vinaelekea kuendelea kuwepo kutokana na baadhi ya watu kuamua vikwazo hivyo viwepo.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, bado Serikali  haina nia ya dhati ya kuwapatia gesi au umeme kwa wanaotaka kuwekeza Mtwara na kwamba mwakani watakapokuwa wakijadili Wizara ya Viwanda na Biashara kwa maana ya kamati ya viwanda, biashara na mazingira iunganishwe na Wizara ya Nishati na Madini.

Mbunge huyo anasema walikotoka kulikuwa na changamoto ya ardhi kwa wawekezaji kwenye viwanda lakini sasa hawana tatizo kwenye ardhi wala wizara ya viwanda na biashara bali tatizo kubwa lipo upande wa Wizara ya Nishati na Madini ambapo mkoani Mtwara umeme umekuwa wa  shida huku mitambo ikiharibika kila mara.

Anasema Megawatt 18 zinazolishwa hazitoshelezi mahitaji na hawaoni mipango ya uhakika inayofanywa na Serikali ya kuhakikisha tatizo hilo linakwisha. Ndani ya Serikali wenyewe kwa wenyewe wanakwamishana, “hata vile viwanda tunavyovihisi vipo mifukoni inawezekana vinakwama kwenye Nishati,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Nishati na Madini izisaidie wizara nyingine katika kuhakikisha kwamba kama nchi imedhamiria kufikia uchumi wa viwanda, nishati kwa kiasi kikubwa itatumika hivyo wizara iamke kwani umeme unahitajika uzalishwe na kuinua uchumi wa nchi.

Hata hivyo, Mbunge huyo anaeleza kuwa, eneo ambalo Dangote amejenga kiwanda cha Saruji lina ukubwa wa hekta 17,000 huku Dangote akipewa hekta 4000 tu, hivyo ardhi kwa ajili ya uwekezaji bado ipo na haihitaji fidia.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia anasema sera ya viwanda ni zuri kinadharia, lakini utekelezaji wake ndio changamoto kubwa sana, hata Rais anapata shida kwenye utekelezaji wake kwa sababu kaikuta tu kwenye ilani.

“Tunapozungumzia Tanzania ya uchumi wa viwanda leo, lazima kujiuliza swali, hivi tulikuwa na viwanda vingapi? Tumejiuliza kwa nini viwanda vile vilikufa? Majibu yatokane na utafiti na ndio tuje na fikra ya kujenga viwanda vipya,” alisema.

Aliongeza: “Lakini tukisema tu nakuletea kiwanda leo, sidhani hata kama nchi zilizoendelea kiviwanda zilienda katika stahili hiyo. Tanzania ilikuwa na viwanda vingi Mutex, Mwatex, lakini vyote vimekufa, bila kujua aliyeviua viwanda, hivi tutaimba wimbo huu wa kuwa na Taifa la viwanda, leo, kesho na hata milele.”

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Chemba,Tanzania ina viwanda karibu 30 vya pamba lakini malighafi zinazoingia kwenye viwanda hivyo hazitoshi, pia nchi inaagiza asilimia 51 ya mafuta ya kupikia kutoka nje wakati viwanda vya mbegu za pamba ambazo zingeweza kutoa mafuta havipati malighafi ya kutosha kwa sababu kushuka kwa uzalishaji.

Kauli ya mafuta kuagizwa nje ya nchi iliungwa mkono na Mbunge wa Same Mashariki, Nanghenjwa Kaboyoka na kusema kuwa Serikali inapaswa kuboresha mazingira kuanzia ngazi ya wakulima ili kuweza kuandaa malighafi kwa ajili ya viwanda vya Tanzania.

Alisema ni muhimu kuimarishwa kwa viwanda vilivyopo sasa badala ya kufikiria kujenga vingine kwa sababu mfumo wa soko kwa sasa ni wa ushindani.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati yake, Mwenyekiti wa kamati hiyo alilieleza Bunge kuwa Serikali haikuwa na mkakati unaojitosheleza wa kutekeleza mpango wa mkakati wa kurudisha viwanda vilivyobinafsishwa.

Na hiyo anasema imetokana na kutokuwepo kwa bajeti iliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji na katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu Serikali imefanikiwa kutwaa kiwanda kimoja.

Pia  Serikali imejikita zaidi katika kujaribu kufufua viwanda kwa kuandaa utaratibu wa kuvitwaa na kuviendesha aidha kwa ubia au peke yake badala ya kujenga mazingira bora na rafiki ya uwekezaji ili kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda hivyo.

Katika taarifa hiyo ya kati ya Januari, 2016 hadi Januari 2017, Mwenyekiti, Dk. Dalaly Kafumu amesema  Serikali imeshindwa kutoa fedha zilizopitishwa na Bunge kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji.

“Kwa namna hii azma ya serikali ya kufikia nchi ya viwanda ifikapo 2025 inaweza kuwa ndoto kwani hadi kufikia robo ya pili ya mwaka wa fedha 2016/17, wizara hiyo ilikuwa haijapokea kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua hiyo inaashiria Serikali kushindwa kutekeleza azma yake,” alisema.

Kufuatia hali hiyo, Serikali imeshauriwa kutekeleza mpango wa kutoa muda wa kubadilisha biashara (grace  period) isiyozidi miaka mitatu ili wazalishaji wa viwanda wa plastiki waweza kuendelea na uzalishaji kwa muda kidogo huku wakifanya utaratibu wa kuhamia katika teknolojia rafiki kwa mazingira.

Wazalishaji wa ndani wanachangia kiasi kidogo sana cha uharibifu wa mazingira kwa kuwa mifuko mingi ya plastiki inaingizwa kutoka nje ya nchi kwa njia zisizo halali.

Serikali ilifanya maamuzi ya kupiga marufuku baadhi ya bidhaa za plastiki baada ya kufanya utafiti katika nchi ya Rwanda ambayo ni ndogo na rahisi kudhibiti mipaka yake katika uingizaji wa bidhaa haramu.

Wakati nchi ya Rwanda ikipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, nchi hiyo haikuwa na kiwanda hata kimoja kinachozalisha plastiki hivyo Serikali haina budi kujifunza kwa kuangalia nchi kubwa kama india ambayo ilijaribu kutekeleza utaratibu wa wa kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki lakini walishindwa.

Mei, mwaka jana Serikali ilitangaza kupiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji na uingizaji nchini na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kuna athari kubwa za kiuchumi kwa wazalishaji wa ndani kwa kutekeleza uamuzi wa serikali kwa haraka kwani wadau wa bidhaa za plastiki wamewekeza fedha nyingi katika viwanda.

Pia wawekezaji hao wana mikopo katika mabenki hivyo kufungwa kwa viwanda hivi kutaleta athari pia kwenye mabenki pamoja na kuondoa ajira zipatazo 60,000 kwa Watanzania.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Maswa Magharibi, Stanslaus Nyongo amesema suala la viwanda na biashara ni mtambuka linaloihitaji Serikali kupitia sekta zingine kushikamana ili kuhakikisha kuwa nchi inafika kwenye uchumi wa viwanda kama sera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyosema.

Hata hivyo, Mbunge huyo anaeleza kuwa kutopelekwa kwa fedha za miradi ya maendeleo kunakwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwani wakati Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikipelekewa shilingi bilioni 7.6 katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha  2016/17, Wizara ya Mazingira Chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira haijapewa kiasi chichote cha fedha.

Naye Mbunge wa Same Mashariki, Nanghenjwa Kaboyoka, amesema katika kufikia azma ya serikali, uzalendo zaidi unahitajika, kila wakati tumekuwa tukiangalia wawekezaji kutoka nje badala ya kuweka misingi ya kuwajengea uwezo watu wa ndani.

Akichangia, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ametofautiana na michango iliyotolewa na wabunge akieleza kuwa Serikali haina mpango wa kutwaa kiwanda na kukiendesha bali wenye viwanda wametakiwa kuhakikisha vinafanya kazi na vikishindwa vitagawiwa kwa wengine ili waviendeshe.

“Msiwaonyeshe Watanzania kwamba tuna hali mbaya, nimepewa dhamana dhamana hii Novemba 2015, hadi sasa Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili viwanda 170, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) 180, Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) viwanda 41, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) viwanda saba  na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) viwanda 1843,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *